Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuwaombea madaktari na wauguzi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka na kuwaombea madaktari na wauguzi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. 

Virusi vya Corona: Papa Francisko awaombea Madaktari na Wauguzi

Papa Francisko ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi wote katika sekta ya afya na hasa zaidi wanaotekeleza dhamana na utume wao huko Bergamo, Brescia na Cremona. Kutokana na kipeo cha maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID, wafanyakazi hawa wameendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu walioathirika kwa Corona nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya Kaskazini mwa Italia wanaendelea kupukutika kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hawa wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa kama mashuhuda wa huduma ya upendo kwa jirani zao hasa katika kipindi hiki kigumu, kila mtu anapohofia usalama wa maisha yake. Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 20 Machi 2020 ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi wote katika sekta ya afya na hasa zaidi wanaotekeleza dhamana na utume wao huko Bergamo, Brescia na Cremona. Kutokana na kipeo cha maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID, wafanyakazi hawa wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wengi wao kwa sasa wamekata tamaa ya maisha.

Baba Mtakatifu amewaombea pia viongozi wa Serikali ili waendelee kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika kipindi hiki kigumu. Madaktari, wauguzi, watu wa kujitolea pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali ni watu muhimu sana kwa wakati huu, kwani wanaiwezesha jamii kusonga mbele kwa imani na matumaini! Hawa ni walinzi wanaosadaka maisha yao kwa jili ya jirani zao. Katika mahangaiko ya ndani, waamini wanahimizwa kugundua uwepo wa Mwenyezi Mungu ambaye ni Baba mwema, tayari kumuungamia dhambi zao, ikiwa kama hawatapata nafasi ya kwenda kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, yaani, Sakramenti ya Upatanisho.

Baba Mtakatifu amezama zaidi katika Liturujia ya Neno la Mungu, Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Nabii Hosea: 14:2-9 na Injili kutoka Mk.12:28-34. Waamini wajitahidi kujenga utamaduni wa kuzungumza na Mwenyezi Mungu kama Baba mwema na kamwe wasimwogope na kumwona kama Hakimu katili. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo; daima yuko tayari kusamehe na kusahau kama inavyojionesha katika sehemu ya Injili ya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu. Huyu ni Baba aliyekuwa anamsubiria Mwana mpotevu ili aweze kurejea nyumbani! Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kurejea nyumbani kwa Baba, ili kuonja, huruma, upendo na msamaha wake wa daima. Mwenyezi Mungu anataka kuwaganga na kuwaponya wale wote wanaotubu na kumwongokea! Kwaresima ni fursa kwa waamini kurejea nyumbani kwa Baba mwenye huruma, ili aweze kuwaosha, kuwatakasa na kuwasamehe dhambi zao.

Kwaresima iwe ni fursa ya kukimbilia daima huruma ya Mungu katika maisha. Yamekuwa ni mazoea ya waamini wengi, kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao wakati wa maandalizi ya Sherehe za Pasaka! Lakini kutokana na hali na mazingira ya wakati huu, nchi nyingi zinapambana dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19! Kumbe, pengine haitakuwa rahisi sana kuweza kupata Mapadre wa kuwaungamisha. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawashauri waamini kumuungamia Mungu dhambi zao katika ukweli na uwazi; na kuwa tayari kuomba neema ya toba na wongofu wa ndani pamoja na kusali Sala ya Kutubu. Waamini wakipata nafasi ya kuungama, itawabidi kwenda kuungama mbele ya Padre. Hii ni njia moja wapo ya kupokea msamaha kutoka kwa Mungu pale ambapo kuna shida ya kupata Mapadre wa kuungamisha. Kwa njia hii, Mwenyezi Mungu atawasafisha na kuwa weupe pe, kuliko theluji.

Baba Mtakatifu amehitimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kuwapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema baraka ya Ekaristi Takatifu na kuwaomba kupokea Ekaristi Takatifu kwa tamaa! Baba Mtakatifu amesali mbele ya Ekaristi Takatifu, kwa kuomba msamaha wa dhambi na kumwabudu Kristo Yesu katika maumbo ya mkate na divai. Amemwomba Yesu wa Ekaristi aweze kuingia katika undani wa maisha yao, hata kama ni wadhaifu na wadhambi. Anatumaini kwamba, iko siku wataweza kumpokea Yesu wa Ekaristi, watakapokutana naye mubashara. Upendo wake, uenee katika maisha waja wake, kwa sasa na wakati wa kufa kwao. Amemalizia kwa kusema, Yesu nina kuamini, nina kutumainia na kukupenda!

Papa: Misa Madaktari
20 March 2020, 15:12
Soma yote >