Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika kipindi hiki cha Majilio kujivika fadhila ya unyenyekevu. Papa Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika kipindi hiki cha Majilio kujivika fadhila ya unyenyekevu.  (ANSA)

Papa Francisko: Kipindi cha Majilio: Jivikeni fadhila ya unyenyekevu

Kwa njia ya unyenyekevu, Mwenyezi Mungu amewafunuliwa waja wake: huruma, upendo, wema na ukuu wake. Unyenyekevu wa moyo kamwe usiwafanye waamini kujitafuta na kujifungia katika ubinafsi wao, bali wawe tayari kuthubutu, kwa kujiachilia chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Majilio ni kipindi muafaka cha kutafakari kuhusu: Ufunuo wa Mungu na kazi ya ukombozi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Francisko Xsaveri, Mtume wa Uinjilishaji nchini India na msimamizi wa shughuli za kitume duniani. Mama Kanisa anatumwa ulimwenguni kutangaza Injili ya Furaha inayomkirimia mwanadamu amani, utulivu na furaha ya ndani. Watu wana kiu ya amani itakayoletwa na Masiha. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, amekazia umuhimu wa unyenyekevu wa moyo unaopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya unyenyekevu, Mwenyezi Mungu amewafunuliwa waja wake: huruma, upendo, wema na ukuu wake. Unyenyekevu wa moyo kamwe usiwafanye waamini kujitafuta na kujifungia katika ubinafsi wao, bali wawe tayari kuthubutu, kwa kujiachilia chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu. Katika kipindi hiki cha Majilio, Liturujia ya Neno la Mungu inawasaidia waamini kutafakari kuhusu: Ufunuo wa Mungu na kazi ya ukombozi.

Mwenyezi Mungu amejifunua katika hali ya unyenyekevu kinyume kabisa na wakuu wa Mataifa kama ilivyoshuhudiwa na Kristo Yesu wakati wa majaribu yake Jangwani, kabla ya kuanza utume na maisha yake ya hadhara, Shetani, Ibilisi alijitambulisha kuwa ni mweza wa yote, mwenye miliki wa falme zote za ulimwengu, lakini mambo ni kinyume katika maisha ya Yesu ambaye ni chipukizi kutoka katika shina la Yese. Injili Takatifu inafafanua kuhusu unyenyekevu wa Kristo Yesu ambaye kwa hekima na busara ya Kimungu amefunuliwa kwa maskini na wanyonge. Huu ni mwaliko kwa waamini kwenda Pangoni ili kushuhudia unyenyekevu wa Mungu ulivyofunuliwa kwa njia ya Mtoto Yesu. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kikristo kutafuta na kuambata unyenyekevu katika maisha yake. Ufalme wa Mungu unachipua na kuchanua katika hali ya unyenyekevu na wala hakuna sababu ya kutumia nguvu ili “kujimwambafai”. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga na kudumisha unyenyekevu wa moyo ili kumpatia nafasi Roho Mtakatifu kuja na kufanya makazi yake.

Kamwe, Roho Mtakatifu hawezi kukaa katika nyoyo za watu wenye kiburi na majivuno. Wanataalimungu wanakumbushwa kwamba, taalimungu inaandikwa kwa kupiga magoti na kujinyenyekesha! Viongozi wa Kanisa hawana budi kujenga na kudumisha fadhila ya unyenyekevu katika maisha na utume wao. Huu pia ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu bila ubaguzi wowote ule! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, fadhila ya unyenyekevu isiwafanye Wakristo kujitafuta na hatimaye kujifungia katika ubinafsi wao. Bali kwa njia ya unyenyekevu wawe na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Katika changamoto mamboleo, waamini wanapaswa kusimama imara na kamwe wasitishwe na mawimbi makubwa yavumayo, bali watambue kwamba, Mwenyezi Mungu amejifunua kwa watu wake katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu. Sala, toba na wongofu wa ndani, viwasaidie waamini kukuza na kudumisha fadhila ya unyenyekevu, tayari kumtolea Mungu sifa ya utukufu na shukrani.

Baba Mtakatifu anasema, katika maisha na utume wake, anapenda sana kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto wadogo, kwani wao wanazungumza ukweli wa mambo ulivyo bila kuzunguka mbuyu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu fadhila ya unyenyekevu, ili waweze kutambua udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, ili kwa njia ya nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu waweze kuwa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao.

Papa: Ufunuo

 

03 December 2019, 15:35
Soma yote >