Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Kwaresima ni kipindi cha kuondokana na unafiki kwa kukuza na kudumisha fadhila njema za Kikristo! Papa Francisko: Kwaresima ni kipindi cha kuondokana na unafiki kwa kukuza na kudumisha fadhila njema za Kikristo! 

Baba Mtakatifu Francisko awataka waamini kuondokana na unafiki!

Waamini wanahamasishwa kukiishi Kipindi cha Kwaresima kwa unyoofu wa moyo: kufunga na kusali; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu linalomwilishwa katika Injili na huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi, bila ya kujitafutia makuu au kupongezwa na watu. Vinginevyo, itakuwa vigumu sana kwa watu kuwatofautisha waamini pamoja na Mafarisayo na Waandishi wapenda sifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kufunga na kuitakasa saumu kwa kuwalisha wenye njaa, kuwaonesha ukarimu maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuwavika nguo walio uchi. Kwa maneno machache, Mwenyezi Mungu anawataka waamini kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha kujikita katika mambo msingi ya maisha ya kiroho! Vinginevyo, hata mfungo wa Kwaresima unaweza kuonekana kana kwamba, unafumbatwa katika mambo ya nje tu, yale yanayoonekana kwa macho!

Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa, tarehe 8 Machi 2019. Waamini wanahamasishwa kukiishi Kipindi cha Kwaresima kwa unyoofu wa moyo: kufunga na kusali; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu linalomwilishwa katika Injili na huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi, bila ya kujitafutia makuu au kupongezwa na watu. Baba Mtakatifu anasema, vinginevyo, itakuwa vigumu sana kwa watu kuwatofautisha waamini pamoja na Mafarisayo na Waandishi waliopenda kujionesha mbele ya watu!

Hiki pia kinaweza kuwa ni kishawishi cha Wakatoliki katika ulimwengu mamboleo wanaoweza kujidai kwamba, kila siku wanahudhuria Ibada ya Misa Takatifu Parokiani kwao! Na zaidi sana, wao ni wanachama wa vyama na mashirika ya kitume na wala si kama waamini wengine wasiohudhuria Ibada ya Misa Takatifu na wala si wanachama wa vyama vyovyote vile vya kitume! Wapo wapo tu! Bora siku zinakwenda! Baba Mtakatifu anawataka waamini kujivika fadhila ya unyenyekevu kwa kujitambua kwamba, mbele ya Mungu wao ni wadhambi wanaohitaji kutubu na kumwongokea Mungu! Maisha ya ndani, yaendane sawia na maisha ya nje, vinginevyo, watakuwa ni wanafiki tu unaomwilishwa katika maisha ya kiroho na kuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku, hatari kubwa!

Mwisho wa Kipindi cha Pasaka, iwe ni fursa kwa waamini kujichunguza nafsini mwao ili kuangalia ikiwa kweli yale mambo ya nje yalionekana ndiyo yale yaliyokuwa yakitoka katika undani wa maisha yao! Mwenyezi Mungu anataka kuona imani inamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Kumbe, hii ni changamoto kwa Wakatoliki wanaosimamia misingi ya ukweli, haki na uaminifu, kwa kufikiri na kutenda kama watoto wa Mungu! Wawe mstari wa mbele kukimbia dhambi na nafasi zake. Kwaresima ya Mwaka 2019, iwe ni fursa kwa waamini kuunganisha mambo msingi ya maisha ya kiroho yaliyomo katika undani wa mt una uhalisia wa maisha yanayojidhihirisha mbele ya watu. Ili kuweza kufanikisha azma hii, waamini wamwombe Mwenyezi Mungu neema ya unyenyekevu, ili kweli waweze kuwa ni kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha!

Papa: Mahubiri
08 March 2019, 15:37
Soma yote >