Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Upendo wa kweli unamwilishwa katika huruma kwa jirani! Papa Francisko: Upendo wa kweli unamwilishwa katika huruma kwa jirani!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Upendo wa dhati unamwilishwa katika huruma!

Baba Mtakatifu ameendelea kukita mahubiri yake katika fadhila ya upendo kama ambavyo Mtakatifu Yohane anavyokaza kusema, upendo unatoka kwa Mungu na unakita mizizi yake katika imani, changamoto na mwaliko kwa waamini kupendana kwa dhati, kama Mwenyezi Mungu alivyowapenda wao hata akamtuma Mwanaye wa pekee, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu aliguswa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wanamwendea, akawahurumia kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, akawafundisha na hatimaye, akafanya muujiza wa kugeuza mikate mitano na samaki wawili, akawalisha watu zaidi ya elfu tano waliokuwa jangwani wanamsikiliza! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 8 Januari 2019 amesema, Kristo Yesu alikuwa wa kwanza kuonesha upendo na huruma, lakini, wakati mwingine hata kwa waamini wanaoonekana kuwa watu wema pengine wanashindwa kung’amua mahitaji na mahangaiko ya jirani zao.

Hii inatokana na sababu kwamba, watu wa namna hii, upendo wa Mungu bado haujakita mizizi yake katika nyoyo zao! Katika Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amemkumbuka na kumwombea Marehemu Askofu mkuu Giorgio Zur, aliyefariki usiku wa kuamkia tarehe 8 Januari 2019 na alikuwa anaishi kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha. Marehemu Askofu mkuu Zur amewahi kuwa Balozi wa Vatican nchini Austria. Baba Mtakatifu ameendelea kukita mahubiri yake katika fadhila ya upendo kama ambavyo Mtakatifu Yohane anavyokaza kusema, upendo unatoka kwa Mungu na unakita mizizi yake katika imani, changamoto na mwaliko kwa waamini kupendana kwa dhati, kama Mwenyezi Mungu alivyowapenda wao hata akamtuma Mwanaye wa pekee, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa!

Lakini, inasikitisha kuona kwamba, binadamu bado hajaweza kujifunza kupenda kwa dhati na hatimaye, kuutolea ushuhuda upendo huo, kama alivyofanya Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, ili Kristo Yesu, aweze kuwakomboa watu kutoka katika dimbwi la dhambi na mauti; awakirimie uelewa mpya wa maisha, ili kuwapyaisha na kuwaumba tena upya katika mwanga wa huruma na upendo. Kristo Yesu alifanya muujiza wa kugeuza mikate mitano na samaki wawili ili kuwalisha watu zaidi ya elfu tano, kwa sababu alikuwa na huruma na upendo kwa waja wake.

Kristo Yesu aliguswa na mahangaiko yao, kiasi kwamba, hakuweza kuwageuzia kisogo na kuwaacha waende zao wakiwa na njaa na kiu! Upendo wa kweli unafumbatwa katika huruma kwa jirani! Yesu anawafundisha waja wake kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na mapendo; mambo yanayomwilishwa katika huduma ya Injili ya upendo: kiroho na kimwili. Huu ni muujiza uliotendwa jangwani, alasiri, wakati Mitume walikuwa wameanza kuchanganyikiwa kuhusu umati mkubwa wa watu, kiasi cha kutaka kuwageuzia kisogo!

Ile mikate mitano na samaki wawili, walikuwa wamemwachia Yesu; kwani wao, kipaumbele cha kwanza kilikuwa kwa Kristo Yesu na wala si kwa umati mkubwa uliokuwa mbele yao; hawakuwa na huruma na wala hawakufahamu jinsi ya kupenda kadiri ya vigezo vya Mwalimu wao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hapa Yesu, anawageuzia kibao na kutaka Mitume wake, waupatie umati ule wote chakula, huo ukawa ni mwanzo wa mapambano kati ya huruma ya Kristo Yesu na mwelekeo wao wa kutojali mahangaiko ya watu waliokuwa mbele yao; hali ambayo inaendelea kujirudia katika historia ya maisha ya mwanadamu hadi leo hii, mwaliko wa kuingia katika upendo wa Mungu, ili kuweza kuumwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu.

Kuna umati mkubwa wa maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, ambao watu waliokula na kushiba wanawapita bila hata ya kuwatupia jicho, hizi ni dalili za utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani, kama walivyofanya Mitume wa Yesu. Kinyume cha upendo ni hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Papa Francisko anasema, hii si chuki, bali ni tabia ya kutojali shida za wengine. Waamini wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu daima amekuwa wa kwanza kuonesha huruma na upendo kwa waja wake, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaponya na tabia ya utandawazi wa kutojali shida na mahangaiko ya wengine. Mwishoni, Baba Mtakatifu amemtumia salam na matashi mema Kiko Argùello, muasisi wa Chama cha Kitume cha Njia ya Ukatekumeni mpya anayeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 80 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu anamshukuru kwa ari na moyo mkuu katika kulitumikia Kanisa la Kristo!

Papa: Huruma

 

08 January 2019, 14:07
Soma yote >