Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwafariji9 na kuwakomboa! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumwachia Mungu nafasi ili aweze kuwafariji9 na kuwakomboa!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Mwachieni Mungu nafasi ya kuwafariji na kuwakomboa!

Majilio ni mwaliko wa kukimbilia na kuambata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayekuja kuwakomboa watu wake, kama ilivyo kwa wafiadini mbali mbali ambao katika shida na mahangaiko yao, walijiaminisha kwa faraja ya Mungu. Leo hii, faraja ni neno ambalo walimwengu wengi anasema Papa Francisko wangependa kuona linafutwa kwenye kamusi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu katika kipindi hiki cha Majilio ni mwaliko wa kukimbilia na kuambata faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha; Mungu anayekuja kuwakomboa watu wake, kama ilivyo kwa wafiadini mbali mbali ambao katika shida na mahangaiko yao, walijiaminisha kwa faraja ya Mungu. Waamini wanaalikwa kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kuwafariji! Leo hii, faraja ni neno ambalo walimwengu wangependa kuona linafutwa kwenye kamusi! Faraja kutoka kwa Mungu ni chemchemi ya amani na utulivu wa ndani!

Huu ni muhtasari wa mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 11 Desemba 2018, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya faraja, amani na utulivu wa ndani hasa wakati wa shida na mahangaiko ya ndani kama ilivyojitokeza kwa mashuhuda wa imani, walioyamimina maisha yao nchini Libya. Faraja inapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya wakristo, ingawa ni neno linalopata upinzani mkubwa katika ulimwengu mamboleo!

Mwenyezi Mungu kwa kinywa cha Nabii Isaya, anawataka viongozi kuwafariji na kuwatuliza watu wake waliovunjika na kupondeka moyo! Hii ni faraja inayoleta ukombozi na maondoleo ya dhambi na hiki ni kiini cha Habari Njema. Hivi ndivvyo alivyofanya hata Kristo Yesu ambaye aliwafariji Mitume wake kwa siku arobaini, baada ya kukumbana uso kwa uso na Fumbo la Msalaba. Lakini kwa bahati mbaya, waamini wengi wamekuwa wakimwekea Mwenyezi Mungu kizingiti, kiasi hata cha kushindwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu!

Toma, Mtume, hakuamini yale aliyoambiwa na Mitume wengine, akataka kuhakiki mwenyewe kwa kutumbukiza kidole chake kwenye Madonda Matakatifu wa Kristo Yesu! Huu ni ugonjwa wa maisha ya kiroho anasikitika kusema Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja kwa watu wanaoteseka! Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya faraja inayofyekelea mbali mizizi ya dhambi katika maisha na utume wa wakleri bila kuwasahau waamini walei ambao hawapendi kubadilika hata kidogo! Nabii Isaya anakaza kusema, tazameni thawabu yake i pamoja naye! Atalilisha kundi lake kama mchungaji, atawakusanya wanakondoo mikononi mwake na kuwachukua kifuani pake! Kwa bahati mbaya, faraja ni neno ambalo walimwengu wangependa kuona linafutwa kwenye kamusi.

Waamini wanahamasishwa kukimbilia faraja ya Mungu katika maisha yao, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Mambo ya dunia yasiwapinge waamini wanaomkimbilia Mwanaye wa pekee, ili wapate kumlaki, bali hekima yake, iwawezeshe kumshiriki Kristo Yesu! Tangu wakati wa Kanisa la Mwanzo, Wakristo walipata faraja kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hata pale walipokuwa wanakiendea kifo kama ilivyokuwa kwa Wakristo waliokuwa wanatumbukizwa kwenye tundu la wanyama wakali huko Colosseo mjini Roma, lakini wao, walikwenda kukabiliana na kifo huku wakimwimbia Mungu nyimbo za sifa na shukrani; wakakata kauli, wakijiaminisha kwa Kristo Yesu! Hivyo ndivyo walivyofanya hata mashuhuda wa imani walioyamimina maisha yao huko nchini Libya! Ni faraja inayomletea mwamini amani na utulivu wa ndani; hawa ni watu wenye mwelekeo chanya katika maisha.

Katika shida na mahangaiko, watu wengi wanahitaji kuonja faraja, amani na utulivu wa ndani: Faraja ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo waamini wanapaswa kuiomba wakati huu wanapojiandaa kuadhimisha Sherehe ya Noeli, kwani mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea na kwamba, Baba yao wa mbinguni hapendi hata mmoja wa wadogo hawa apotee. Waamini wajiandae kuadhimisha Sherehe ya Noeli wakiwa na amani na faraja kutoka kwa Mungu, hata katika hali ya dhambi. Mwenyezi Mungu yuko tayari kumtafuta mtu mmoja anayethubutu kutubu na kudiriki hata kuwaacha wale 99! Kumbe, kuna haja kwa waamini kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu anayetaka kuwakirimia faraja na amani ya ndani, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, mwamini anamfungulia lango la maisha yake!

Papa: Faraja

 

 

 

11 December 2018, 14:53
Soma yote >