Cerca

Vatican News
Injili ya huduma, wema, ukarimu na upendo inapaswa kumwilishwa kila siku katika hija ya maisha ya waamini! Injili ya huduma, wema, ukarimu na upendo inapaswa kumwilishwa kila siku katika hija ya maisha ya waamini!  (ANSA)

Papa Francisko. Ukarimu unapaswa kumwilishwa katika matendo ya kila siku!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kufanya hija ya ukarimu katika maisha yao, kwa kuanzia katika familia zao, ili kugawana na wengine, hata kile kidogo walicho nacho na kwamba, ulaji wa kutisha ni hatari sana kwa moyo wa ukarimu, ni ugonjwa wa akili, lakini ukarimu unawajengea watu furaha ya kweli, moyo mkuu na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Toa kwa moyo wa ukarimu, upendo na shukrani; toa katika hali ya sadaka na ukamilifu hata kama machoni pa watu kinaonekana kuwa kidogo namna gani. Namna hii ya kujitoa inadhihirisha upendo na imani thabiti katika Mungu mpaji na kujitegemeza katika fadhila zake dhidi ya tabia ya uchoyo na ulaji wa kupindukia! Ukarimu unafumbatwa katika nia njema, kwa kuzingatia maadili na haki na kwamba, ukarimu unajikita katika haki na uadilifu kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 26 Novemba 2018 wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kwa kina na mapana kuhusu ukarimu wao kwa maskini, ili kusikiliza na kujibu kilio cha akina Lazaro maskini wa nyakati hizi. Kristo Yesu katika mafundisho yake, mara nyingi ametoa upendeleo wa pekee kwa maskini na kuonya juu ya utajiri unaoweza kuwa ni kikwazo cha kuingia katika ufalme wa Mungu, kwani nyuma ya pazia la utajiri wakati mwingine kuna mkono wa Shetani! Yesu anaonya kwamba si rahisi sana kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja, ni vigumu kumtumikia Mungu na kuambata utajiri!

Baba Mtakatifu katika tafakari yake mintarafu Injili ya Luka 21: 1-4 anasema Yesu alimpongeza yule mwanamke mjane na maskini aliyetoa zaidi kuliko wote, maana matajiri walitoa sadaka mali iliyowazidi, bali mwanamke yule katika umaskini wake, ametia vyote alivyokuwa navyo kwani alijiaminisha na kumtumainia Mwenyezi Mungu! Kiini cha sehemu hii ya Injili ni kuonesha ukarimu kwa maskini na wahitaji zaidi! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna umati mkubwa sana wa watoto wanaoteseka na kufa kwa njaa na utapiamlo wa kutisha; wengine wanapoteza maisha kwa kukosa tiba na dawa muafaka. Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kutafakari jinsi ya kuwasaidia watoto kama hawa hata ikiwa ni katika kiwango kidogo sana, wathubutu kutenda kama alivyofanya yule mwanamke mjane.

Ukarimu unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku! Wale wenye masanduku ya nguo na viatu, wajitahidi kuwagawia maskini na wahitaji wanaowazunguka, hii ni sehemu ya kumwilisha Injili ya ukarimu kwa jirani! Ukarimu uwasaidie waamini kushirikishana na wengine utajiri ambao Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha yao, pengine bila hata mastahili yao. Kuna watu hata leo hii wanaendelea kutoa zaka na sadaka kwa ajili ya kuwasaidia maskini na watu wasiojiweza! Hawa ni wale wanaoendelea kutenda miujiza kwa kujinyima hata kile kidogo walichonacho!

Ukarimu ni dawa dhidi ya "uchoyo na mkono wa birika"! Ugonjwa wa ulaji wa kupindukia, unaendelea kusambaa kama moto wa mabua sehemu mbali mbali za dunia. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kujinyima, ili kujisadaka kwa ajili ya maskini, hali ambayo inawasaidia wengi kuona wema, huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya waja wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya ukarimu katika maisha yao, kwa kuanzia katika familia zao, ili kugawana na wengine, hata kile kidogo walicho nacho na kwamba, ulaji wa kutisha ni hatari sana kwa moyo wa ukarimu, ni ugonjwa wa akili, lakini ukarimu unawajengea watu furaha ya kweli, moyo mkuu na utu wema.

Papa: Ukarimu

 

 

 

26 November 2018, 13:33
Soma yote >