Tafuta

Vatican News
Papa Francisko aonya kuhusu upagani mamboleo unaowanyemelea Wakristo! Papa Francisko aonya kuhusu upagani mamboleo unaowanyemelea Wakristo!  (ANSA)

Papa Francisko aonya kuhusu upagani mamboleo!

Watu wengi wanaishi kadiri wanavyotaka kwa kuuweka Ukristo wao pembezoni! Ni watu wa maneno kibao, lakini matendo kiduchu! Kwa hakika, hawa ni sawa na maji na mafuta kwani kamwe hayawezi kuchanganyika. Huu ndio utamaduni wa upagani mamboleo unaowafanya Wakristo kuishi kama wapagani! Baada ya mambo yote haya Kristo Yesu atakuja kwa nguvu na utukufu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anapokaribia kufunga Mwaka wa Liturujia ya Kanisa anaendelea kuwatafakarisha watoto wake kuhusu Mambo ya Mwisho wa Nyakati kwa kuonesha misigano kati ya uharibifu na matumaini; ushindi na kushindwa na hivi ndivyo itakavyokuwa Siku ile ya Mwisho, Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Ufunuo wa Yohane, linaonesha kuporomoka kwa mji wa Babeli alama ya ulimwengu mamboleo unaojikita katika fahari, mwenekano wa nje, hali ya kujiamini kupita kiasi, nguvu na mamlaka ya dunia hii. Mwinjili Luka, anagusia kuhusu hukumu na uharibifu wa mji Mtakatifu wa Yerusalemu, kielelezo cha hasira ya Mwenyezi Mungu!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 29 Novemba 2018 wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Kuanguka na kusambaratika kwa mji wa Babeli ni kielelezo cha ushindi wa Mwenyezi Mungu na ufunuo wa ukweli dhidi ya mji ambao uligeuka kuwa ni maskani ya mashetani, ngome ya roho chafu, pango la ndege wenye kuchukiza, nyumba ya uasherati na ulevi! Zote hizi ni dalili za kukengeuka na kwamba, sherehe zote zilizokuwa zikifanyika mjini humo badala ya kuwa ni kielelezo cha furaha, ziligeuka kuwa chanzo cha uharibifu na mmong’onyoko wa kimaadili na kamwe sauti za furaha na nderemo hazitaweza kusikika tena, wala mwanga wake kuonekana, kwani huu ni utamaduni wa watu waliokengeuka na kutopea katika maovu anasema Baba Mtakatifu Francisko! Hakutakuwepo tena na wanandoa, ambao nyakati zile walikuwa wengi kibao, lakini bila ya kuwa na upendo wa dhati ndiyo maana Mwenyezi Mungu anaamua kuingilia kati, ili kukomesha maovu haya kwenye uso wa dunia!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Yerusalemu mji Mtakatifu, ulifungua malango yake kwa wapagani na kuanza kuporomoka, kiasi hata cha kukosa uaminifu, upendo wa dhati kwa Mwenyezi Mungu na Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu na matokeo yake, mji wa Yerusalemu ukasiginwa kama “mbegu za ufuta” na wapagani na hivyo kukiona cha mtema kuni kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo hali inayojitokeza hata katika maisha ya Wakristo katika ulimwengu mamboleo, kwani wamezamia upagani mamboleo, kwa kuvutwa na kumezwa na malimwengu kama ilivyokuwa kwenye mji wa Babeli na Yerusalemu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, watu wengi wanaishi kadiri wanavyotaka kwa kuuweka Ukristo wao pembezoni! Ni watu wa maneno kibao, lakini matendo kiduchu! Kwa hakika, hawa ni sawa na maji na mafuta kwani kamwe hayawezi kuchanganyika. Huu ndio utamaduni wa upagani mamboleo unaowafanya Wakristo kuishi kama wapagani! Baada ya mambo yote haya ya mwisho wa nyakati, Kristo Yesu atakuja kwa nguvu na utukufu na wale walioalikwa kwenye Karamu ya Mwanakondoo, watafurahi na kushangilia, watampatia sifa na utukufu Mwanakondoo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, wale wanaomtumaini Mungu watapata wokovu na mavazi yao yatasafishwa kwenye Damu ya Mwanakondoo, kielelezo cha matumaini yanayokoa kwani matumaini ni nguvu ya wachamungu. Hii ni changamoto ambayo waamini wanapaswa kuomba nguvu na msaada kutoka kwa Roho Mtakatifu. Matumaini yawe ni dira na mwongozo wa maisha ya wafuasi wa Kristo na kamwe wasikubali kumezwa na upagani mamboleo, kwani huko watakiona cha mtema kuni!

Papa: Upagani mamboleo

 

29 November 2018, 14:26
Soma yote >