Tafuta

Papa Francisko asema, ni kwa njia ya Mungu Baba Mwenyezi, Binadamu wote wanakuwa ni ndugu wamoja! Papa Francisko asema, ni kwa njia ya Mungu Baba Mwenyezi, Binadamu wote wanakuwa ni ndugu wamoja!  (Vatican Media)

Kwa Njia ya Mungu, binadamu wote wanakuwa ni ndugu wamoja

Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu, tarehe 17 Mei 2020 amewakumbuka na kuwaombea wafanyakazi wa usafi majumbani; hospitalini na barabarani. Hii ni kazi iliyofichika, lakini ni muhimu sana kwa ustawi na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia! Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakinge na kuwalinda katika huduma hii muhimu kwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hivi karibuni, Shirika la Kazi Duniani, ILO imeweka bayana kwamba bado kazi za usafi wa majumbani zinadharauliwa licha ya mchango wake mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya jamii. Hii ni ajira inayokabiliwa na nyanyaso kuanzia muda wa kazi hadi masilahi. Idadi ya wafanyakazi wa usafi majumbani inaendelea kuongezeka maradufu lakini mafao na usalama wao kazini bado ni kidogo sana! Hawani wafanyakazi wanaojisadaka kwa ajili ya kulea watoto, kutunza wazee pamoja na watu wenye ulemavu. Wafanyakazi wa usafi majumbani wakati huu wa watu kuwekwa karantini wanakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na hatari ya kukosa fursa za ajira pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha, wakati hali ya maisha ikizidi kudoda na kwamba, hili ni kundi la watu wanaoweza kuambukizwa kwa haraka ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka, tarehe 17 Mei 2020 amewakumbuka na kuwaombea wafanyakazi wa usafi majumbani; hospitalini na barabarani. Hii ni kazi iliyofichika, lakini ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia! Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakinge na kuwalinda katika huduma hii muhimu kwa jamii. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amefafanua kuhusu nafasi ya Mungu Baba anayewawezesha watoto wake hata katika tofauti zao msingi kuweza kuishi kwa amani na utulivu kama ndugu wamoja. Vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii ni dalili kwamba, hakuna upendo wa Mungu Baba unaowaunganisha watu wote kama ndugu!

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka: Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume 8: 5-8; 14-17; Somo la Pili ni Kutoka katika Waraka wa Mtume Petro kwa Watu wote 3: 15-18 na Injili na kama ilivyoandikwa na Yohane 14: 15-21. Kwa namna ya pekee, Kristo Yesu katika Injili anawaambia wafuasi wake “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui, bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu”. 

Hotuba hii kadiri ya Mwinjili Yohane anasema Baba Mtakatifu ni wosia wa Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Anatumia fursa hii kuwatuliza na kuwakirimia amani na utulivu wa ndani, kwa kuwahakikishia kwamba, kamwe hatawaacha yatima, bali atakuja kwao! Kristo Yesu anatambua machungu na adha ya kubaki yatima! Waswahili wanasema yatima hadeki kamwe! Katika ulimwengu mamboleo, kuna hisia kwamba, watu wengi wamebaki kuwa yatima, kwa kukosa kuonja uwepo wa Mungu Baba katika maisha yao. Watu wana vitu na mali nyingi lakini wanakosa ule upendo wa Mwenyezi Mungu na matokeo yake, watu wanakuza ndani mwao ile hamu ya kutaka kukutana na Mungu Baba, kama ilivyokuwa hata katika simulizi za mambo ya kale! Leo hii anasema Baba Mtakatifu, kuna hofu kubwa ya watu wengi kuishi kama yatima kwa kukosa utambulisho makini na umoja wa udugu wa kibinadamu. Katika muktadha huu, Kristo Yesu anawahakikishia wafuasi wake kwamba, atamwomba Baba yake wa mbinguni naye atawapa Msaidizi mwingine!

Huyu ni Roho wa kweli; ni Roho Mtakatifu Mfariji ambaye atawafundisha na kuwakumbusha yale mambo msingi ambayo Kristo Yesu amewafundisha alipokuwa hapa ulimwenguni. Atawasaidia na kuwaonesha njia inayokwenda kwa Baba wa mbinguni, kama alivyofundisha na kushuhudia Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Hiki ni kielelezo cha umoja na mshikamano katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Mungu Baba ni kiini cha yote. Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ametumwa na Baba wa Milele na baada ya kumaliza kazi ya ukombozi, anarejea tena kwa Baba yake wa Mbinguni.

Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, anayetoka kwa Baba na Mwana, atawafundisha na kuwakumbusha mambo msingi yanayoweza kuwapeleka kwa Mungu Baba! Ni katika uelewa huu, anasema Baba Mtakatifu Francisko, watu wa Mungu wanaweza kuishi kwa amani na utulivu wa ndani, kwa “kufyekelea mbali” dhana na mawazo ya kuishi kama watoto yatima. Vita katika uhalisia wake ni kielelezo cha dhana ya yatima katika maisha ya binadamu kwa sababu anakosekana Mungu Baba Mwenyezi, chemchemi ya amani na utulivu ndani. Mtakatifu Petro katika Somo la kwanza anawaalika wakristo kuwa tayari kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani mwao!

Wakristo watoe majibu kwa upole na hofu; kwa kuongozwa na dhamiri njema. Unyenyekevu ni fadhila inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu, anayewafundisha kuwa kweli ni watoto wa Mungu. Matusi, vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ndani ya jamii ni kielelezo cha watu kuwa yatima, kiasi hata cha kushindwa kujisikia kama ndugu wa Baba mmoja na matokeo yake ni kupoteza pia umoja na udugu wa kibinadamu! Upole, heshima na unyenyekevu ni mambo msingi yanamwonesha na kumtambulisha mtu kuwa ni sehemu ya familia kubwa ya watu wa Mungu na kwamba, wanaye Mungu Mwenyezi kama Baba yao wa mbinguni! Mwenyezi Mungu ni kiini cha umoja, upendo, udugu na mshikamano ni chemchemi ya wokovu wa binadamu, aliyemtuma Mwanaye wa pekee, ili kuja ulimwenguni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Roho Mtakatifu ni Paji la Baba na Mwana, ili kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika fadhila ya upole, unyenyekevu, amani na utulivu wa ndani! Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Roho Mtakatifu, ili aweze kuwafundisha na kuwakumbusha mambo msingi yatakayowapeleka kwa Baba yao wa Mbinguni. Huu ni mwaliko na changamoto ya kuondokana na dhana ya kubaki yatima katika utamaduni wa ulimwengu mamboleo. Roho Mtakatifu awakirimie neema na baraka ya kumtafuta na kuambatana na Mungu Baba anayewajalia watoto wake kutambua maana ya maisha na hivyo kuwawezesha tena kuwa ndugu wamoja ndani ya familia ya watu wa Mungu! Mara tu baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko amewaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, akawapatia Baraka kuu na kufunga kwa kusali Sala ya Malkia wa Mbingu, inayotumiwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka.

SALA YA MALKIA WA MBINGU

Malkia wa mbingu, furahi, Aleluya.

Kwani uliyestahili kumchukua, Aleluya.

Amefufuka alivyosema, Aleluya.

Utuombee kwa Mungu, Aleluya.

Furahi shangilia, ee Bikira Maria, Aleluya.

Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya.

TUOMBE. Ee Mungu, uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao: fanyiza, twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA MALKIA WA MBINGU KWA LUGHA YA KILATINI: Regina Caeli

Regína caeli laetáre, allelúia.

Quia quem merúisti portáre, allelúia.

Resurréxit, sicut dixit, allelúia.

Ora pro nobis Deum, allelúia.

Gaude et laetáre, Virgo María, allelúia.

Quia surréxit Dominus vere, allelúia.

Orémus: Deus, qui per resurrectiónem Filii tui Dómini nostri Iesu Christi mundum laetificáre dignátus es, praesta, quǽsumus, ut per eius Genetrícem Virginem Maríam perpétuae capiámus gáudia vitae. Per Christum Dóminum nostrum. Amen.

Papa: Ibada ya Misa Takatifu

 

 

17 May 2020, 13:28
Soma yote >