Tafuta

Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe.  

Fumbo la Utatu Mtakatifu Ni Msingi wa Imani na Maisha ya Kikristo

Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe; ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza. Hili ni fundisho la kweli ya imani. Imani Katoliki ndiyo hii: Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, nyingine ya Mwana na nyingine ya Roho Mtakatifu, ni umungu mmoja!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu katika Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kipindi cha cha Pasaka kimehitishwa kwa Sherehe Pentekoste. Tuko kipindi cha kawaida cha mwaka wa kiliturujia. Hivyo sherehe hii ya Utatu Mtakatifu tunaiadhimisha jumapili ya 8 kipindi cha kawaida na Jumapili ya 9 tutaadhimisha  Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Hii ni kwa sababu tulipofika juma la 6 kipindi cha kawaida tulianza kipindi cha kwaresima siku 40, majuma 5, na baadae Juma Kuu lilifunguliwa kwa dominika ya matawi kikifuatiwa na kipindi cha Pasaka majuma 7. Kumbe masomo ya jumapili ya 7, 8 na 9 kipindi cha kawaida mwaka B, 2024, hatutayatafakari kwa sababu masomo ya sherehe hizi yanachukua nafasi yao. Mababa wa Kanisa wanasema, Fumbo la Utatu Mtakatifu sana ndilo Fumbo la Msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Ni Fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Kwa hivyo ni chemchemi ya mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangaza. Hili ni fundisho la kweli ya imani. Imani Katoliki ndiyo hii: Tunamwabudu Mungu Mmoja katika Utatu na Utatu katika Umoja, bila kuchanganya nafsi, wala kutenganisha uwamo; kwani ni Nafsi ya Baba, nyingine ya Mwana na nyingine ya Roho Mtakatifu, ni umungu mmoja, wa Baba, na wa Mwana na wa Roho Mtakatifu; utukufu ulio sawa, ukuu wa pamoja wa milele. Rej. KKK 222-266. Utatu Mtakatifu ni Fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu, Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Kwa Utatu Mtakatifu tunafunuliwa upendo, wema, ukuu, mamlaka na huruma ya Mungu katika Nafsi hizi tatu. Ndiyo maana wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya sherehe hii unasema wazi; “Asifiwe Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu; kwa sababu ametufanyizia huruma yake.”

Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani ya Kanisa
Fumbo la Utatu Mtakatifu kiini cha imani ya Kanisa

Hili ni fumbo la imani kuwa hizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili na imani tu, yaelewa. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anakiri kuwa Mungu ndiye anayetufunulia hili fumbo na anazidi kumuomba atujalie ufahamu wake zaidi akisali; “Ee Mungu Baba, uliwafumbulia watu fumbo lako la ajabu, hapo ulipompeleka Neno wako na Roho Mtakatifu ulimwenguni. Utujalie kuutambua utukufu wa Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli na kuabudu Umoja wa Mungu katika enzi ya fahari yake”. Ni katika Utatu Mtakatifu ndimo tunamopata ufupisho na simulizi la asili yetu tangu kuumbwa hata ukombozi kwa njia ya Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu, ndimo zinamolala sala zetu na matumaini yetu kufikia utimilifu wa upendo kwa kuungana na Mungu aliye asili ya upendo. Somo la kwanza ni la kitabu cha Kumbukumbu la Torati (4:32-34, 39-40). Katika somo hili Musa anataja matendo makuu ya Mungu aliyolitendea taifa lake teule, Israeli. Hivyo anawakumbusha watu wake wawe waaminifu kwa Mungu wao. Maana Yeye ndiye aliyewatoa utumwani Misri na kuwaongoza katika nchi ya Ahadi. Aliwatoa katika tope la dhambi nakuwatakasa, hivyo wasirudie tena matapishi ya dhambi kwa kuabudu sanamu. Bali wazishike amri zake ili wapate kufanikiwa wao na watoto wao. Ni katika muktadha huu mzaburi alipotafakari makuu ya Bwana aliimba maneno haya ya wimbo wa katikati akisema; “Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao. Kwa kuwa neno la Bwana ni adili, na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu. Bwana huzipenda haki na hukumu, nchi imejaa fadhili za Bwana. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake. Maana Yeye alisema, ikawa; Na yeye aliamuru, ikasimama. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, wazingojeao fadhili zake; Yeye huwaponya nafsi zao na mauti; Na kuwahuisha wakati wa njaa.  Nafsi zetu zinamngoja Bwana, Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi. Kama vile tulivyokungoja Wewe (Zab. 33:4-6, 9, 13, 18, 20, 22).

Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Imani katika Mungu mmoja Nafsi
Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Imani katika Mungu mmoja Nafsi

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (8:14-17). Katika somo hili mtume Paulo anatueleza kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu Baba. Sisi tunaweza kuwa na haki ya kumwita Mungu “Aba” yaani Baba, tukikubali kuongozwa na Roho Mtakatifu anayekamilisha siri ya wokovu wetu. Hivi wokovu wetu ni mapato ya kazi ya Nafsi zote Tatu za Mungu mmoja. Mtume Paulo anasisitiza hivi; “Kila mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu, huyo ndiye mtoto wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithi pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye”. Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (28:16-20). Sehemu hii ya Injili inahusu maagizo ya Yesu kwa wanafunzi wake kuihubiri Injili kwa mataifa yote, kuwafundisha watu mafundisho yake na kuwabatiza katika Utatu Mtakatifu wakisema; “kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Na kwamba yeye yupo pamoja nao siku zote, hata ukamilifu wa dahari. Tunaona kuwa masomo haya yote hayafafanui waziwazi Fumbo la Utatu Mtakatifu. Lakini kwa pamoja yanadhihirisha uwepo na ukuu wake katika maisha yetu. Ni wazi, kwa kuwa maadhimisho ya Sadaka ya Misa Takatifu, sakramenti na sala zingine zote daima zinaanza na kumalizika kwa ishara ya msalaba huku tukitamaka maneno haya: “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Maneno haya hutamkwa wakati wa ubatizo, wakati wa Kipaimara na wakati wa sakramenti ya kitubio Padre anapomwondolea mtu dhambi zake akisema: “Nami nakuondolea dhambi zako, kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho mtakatifu.” Hutumika wakati wanandoa wanapoadhimisha sakramenti ya ndoa kwa kuvikana pete kila mmoja anahitimisha ahadi zake kwa mwenzake akisema; “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Hata kwenye mazishi maneno haya yanatumika kwa namna moja au nyingine tunaposema; “Uandikwe ishara ya Msalaba wa Mkombozi wetu”. Katika hii sala rahisi hivi ya ishara ya Msalaba, tunakiri kile tunachokiamini kwa kirefu katika Kanuni ya Imani katika sehemu kuu tatu tukisema: “Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, mwumba wa mbingu na Dunia… Nasadiki kwa Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu…Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima…”. Tunasadiki kwa sababu siri ya fumbo la Utatu Mtakatifu ni fumbo la Imani na hivyo kwa akili za kibindamu, hatuwezi kulielewa fumbo hili maana linapita uwezo wa ufahamu wetu.

Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.
Roho Mtakatifu ni mhimili wa uinjilishaji, maisha na utume wa Kanisa.

Mtakatifu Augustino wa Hippo, Mwana Falsafa na Mtaalimungu mkubwa katika Kanisa, baada ya kuongoka kwake, alihangaika sana ili aweze kulielewa kwa ufasaha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Masimulizi yanasema kuwa, siku moja akiwa anatembea ufukweni mwa bahari akitafakari juu ya Fumbo hili, alimwona mtoto mdogo akichimba shimo dogo, kisha akawa anachukua maji kwa kikombe kidogo kutoka baharini na kuyamwaga katika hilo shimo dogo alilolichimba. Augustino alimtazama kwa mda akifanya hivyo, kisha akamwendea na kumwuliza: “Unafanya nini wewe mtoto? Naye akamjibu: Ninataka kuihamishia bahari katika hili shimo”. Augustino akamhoji, unafikiri unaweza kutimiza hamu yako ya kuihamishia bahari katika shimo hili dogo hivi? Haiwezekani! Bahari ni kubwa mno na hili ni shimo dogo tu. Mtoto huyo akatabasamu, kisha akamwambia, hilo ndilo unalolifanya Baba Askofu. Mungu ni zaidi ya bahari. Akili yako ni ndogo kuliko hivi kuweza kuelewa ukuu wa Mungu. Kamwe hutaweza kuelewa fumbo la Utatu Mtakatifu. Akatoweka. Mtakatifu Augustino akafikia hitimisho na kusema inatupasa kusadiki kwa sababu Mungu ametufunulia. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala utangulizi ya sherehe hii anasali akisema; “Mungu mwenyezi wa milele, Wewe pamoja na Mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa nafsi, ila katika Utatu wa umungu mmoja. Mambo tunayoyasadiki juu ya utukufu wako, kwa sababu ya ufunuo wako, twayasadiki pia juu ya Mwanao na juu ya Roho Mtakatifu pasipo tofauti ya kutengana. Nasi tunapoungama Umungu wa kweli na wa milele, tunaabudu nafsi zilizo mbalimbali za Mungu mmoja zenye utukufu ulio sawa.”

Sherehe ya Utatu Mtakatifu ni Siku pia ya Watoto Ulimwenguni
Sherehe ya Utatu Mtakatifu ni Siku pia ya Watoto Ulimwenguni

Mtakatifu Thomaso wa Akwino aliyejaliwa uelewa mkubwa na wa hali ya juu wa mambo yamhusuyo Mungu katika wimbo wake wa kuabudu Ekaristi Takatifu anasema; “waficha Umungu msalabani, na ubinadamu altareni, mafahamu yangu yadanganya yanapokuona na kugusa, nami nasadiki bila haya. Mtume Paulo naye anasema: “Basi, sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtumpu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. Maandiko yasema, nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Lakini sisi tunayo akili ya Kristo” (1Kor.2:13-16). Thomaso wa Akwino anashauri kwamba: “ukikutana na lolote ambalo hulielewi ama katika Biblia au katika mafundisho ya Kanisa usiseme mambo haya hayaeleweki au yamekosewa bali useme akili zangu ni ndogo kuelewa ukweli huu.” Fanya juhudi kuelewa utakavyoweza. Yatakayokushinda inamisha kichwa mpaka nchi na kusema pamoja na mtakatifu Hipoliti kuwa; “Nasadiki kwa kuwa sina uwezo wa kueleza” (Nasadiki kwa kuwa ni upuuzi). Jambo muhimu la kujifunza kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kuishi kwa umoja, ushirikiano, uelewano, amani na upendo. Licha ya kuwa mama Kanisa anatufundisha kuwa Mungu Baba ametuumba, Mungu Mwana ametukomboa na Mungu Roho mtakatifu anatupa uzima. Lakini Mungu Baba alipokuwa anaumba alifanya hivyo kwa njia ya Mwana na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ni Bwana Mleta Uzima atokaye kwa Baba na Mwana.
Roho Mtakatifu ni Bwana Mleta Uzima atokaye kwa Baba na Mwana.

Katika Injili ya Yohane tunasoma hivi; “Hapo mwanzo kulikuwa Neno naye Neno alikuwa kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika” (Yn.1:1). Mungu Mwana alifanya kazi ya ukombozi kwa mamlaka ya Mungu Baba na kwa nguvu ya Mungu Roho Mtakatifu. Yesu mwenyewe alisema wazi kuwa; “wakati unakuja, tena umekwishafika, ambapo ninyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yangu yu pamoja nami’ (Yn.16:32). Naye Mungu Roho Mtakatifu anatupa uzima na kututakasa kwa nguvu na mamlaka kutoka kwa Mungu Baba na Mungu Mwana. Nasi tuishi na tufanye kazi kwa ushirika tukifuata mfano wa Utatu Mtakatifu. Hili linawezekana tukiomba “neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu vikae nasi kama Mtume Paulo alivyowaombea Wakorinto katika hitimisho la waraka wake wa pili. Lengo likiwa ni kuponya mpasuko uliokuwepo kati yao. Hivyo aliwasihi waishi kwa umoja na mapendo kama familia ya Mungu. Basi tuzingatie wosia huu wa mtume Paulo: “Hatimaye ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi katika Utatu Mtakatifu. Salimianeni kwa busu takatifu” (2Kor 13:11-14).

Utatu Mtakatifu
22 May 2024, 12:04