Tafuta

Ujumbe wa Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa: Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani Ujumbe wa Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa: Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Yesu Mchungaji Mwema: Wajumbe wa Matumaini Na Amani

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu watu walioko safarini mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mwaka wa sala kwa ajili ya Jubilei 2025.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Nne ya Kipindi cha Pasaka mwaka B. Maadhimisho ya Kiliturujia ya dominika hii yanaanza kwa wimbo wa mwanzo kwa maneno haya; “Nchi imejaa fadhili za Bwana. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, aleluya” (Zab. 33:5-6). Ni Dominika ya mchungaji mwema. Yesu Kristo ndiye Mchungaji wetu mwema anayetuongoza kuelekea kwenye malisho mema na ya milele huko mbinguni. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea sisi wanawe akisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo wako wanyonge tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa.” Na katika sala baada ya komunio anahitimisha akisali; “Ee Mchungaji mwema, ututazame kwa mapendo sisi kundi lako. Upende kutuweka katika malisho ya milele sisi kondoo wako uliotukomboa kwa damu takatifu ya Mwanao.” Ni siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa unanogeshwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Baba Mtakatifu anafafanua kuhusu watu walioko safarini mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Sala kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 anasema sala ndiyo nguvu na ufunguo wa malango ya matumaini.

Mahujaji wa matumaini na amani
Mahujaji wa matumaini na amani

Waamini ni mahujaji wa matumaini na wajenzi wa amani na kwamba, lengo kuu la safari ya maisha ni kuishi kwa haki, amani na upendo na kwamba, lengo na wito ni kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; umoja, amani na udugu. Kila mwamini ajitahidi kugundua wito wake sahihi katika Kanisa na Ulimwengu, kwa kuwa hujaji matumaini na wajenzi wa amani. Ni siku ya kumwomba Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake kama alivyoagiza Yesu mwenyewe.  “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke wafanyakazi katika shamba lake” (Mt 9:37, Lk 10: 2). Ni siku ya kumwomba Mungu awaite vijana wengi kuwa wafanyakazi katika shamba lake. Ni siku ya kutafakari na kuona namna tunavyoweza kuwasaidia vijana walioonesha moyo wa kutaka kuwa mapadre na watawa, ili waweze kuendelea kuisikiliza na kuijua vyema sauti ya Kristo mchunguji mwema, waifuate na kukua katika miito hiyo mitakatifu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unasema kuwa; Tumeitwa kupanda matumaini na kujenga jumuiya ya Amani.”

Mashuhuda wa matumaini na wajenzi wa amani
Mashuhuda wa matumaini na wajenzi wa amani

Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 4:8-12). Somo hili linatueleza habari za Petro na Yohana kupelekwa mbele ya baraza la wayahudi kwa sababu ya kumhubiri Kristo mfufuka. Petro kwa ujasiri, akijaa Roho Mtakatifu anashuhudia mbele yao bila kuogopa kuwa Yesu waliyemkana na kumwua amefufuka, na kwa jina lake, mitume wanaponya wagonjwa, na kwa njia yake tu, sote tutaokoka, wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inapata maana. Yesu ndiye “Jiwe walilolikataa waashi, Naye amekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu.” Ndiyo maana mzaburi anatuasa kwanza kumtumainia Mungu na sio wanadamu maana Yeye ni muweza wa yote akisema; “Ni heri kumkimbilia Bwana, kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia Bwana, kuliko kuwatumainia wakuu”. Tukiweka matumaini yetu kwa Mungu daima tutakuwa salama. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo huu wa katikati anatuasa tumshukuru Mungu kwa wema wake kwetu akisema; “Aleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Nitakushukuru kwa maana umenijibu, nawe umekuwa wokovu wangu. Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana. Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru, ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele” (Zab. 117: 1, 8-9, 21-23, 26, 28-29).

Vijana ni mashuhuda wa matumaini na wajenzi wa amani duniani
Vijana ni mashuhuda wa matumaini na wajenzi wa amani duniani

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa watu wote (1Yn. 3:1-2). Somo hili linatufafanulia ukweli huu kuwa; Sababu ya mapendo yake, Mungu amemtuma Mwanae ili atufanye kuwa watoto wake. Kwa hiyo yatupasa kuishi kama watoto wa Mungu ili mwishowe tuweze kumwona Mungu Baba yetu mbinguni uso kwa uso. Ndivyo anavyotuandikia Yohane akisema; “Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo.” Licha ya kuwa hakuna anayejua tutakavyokuwa hapo baadae baada ya kifo, Yohane anatupa matumaini haya kuwa; “Atakapodhihirishwa Yesu, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.” Na hili ndilo tumaini letu linalotufanya tuishi tukiwa tumeungana naye. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (10:11-18). Sehemu hii ya Injili ndiyo imebeba dhamira na kiini cha ujumbe wa dominika hii ikitueleza uhusiano uliopo kati yetu sisi waamini tuliobatizwa na kumkubali Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu! Uhusiano huu ni kama wa Mchungaji na Kondoo. Yesu ndiye mchungaji mwema, anayeutoa uhai wake kwa ajili yetu sisi. Yesu mchungaji wetu mwema anatupenda, anatujua, anatufahamu na kutujali kama mchungaji anavyowapenda na kuwajali kondoo wake. Yesu anamjua kila mbatizwa kwa Jina lake, mahitaji yake, madhaifu yake, matatizo na changamoto zake, magonjwa na tiba ayohitaji kadiri ya majeraha yaliyosababishwa na dhambi. Kristo mchungaji mwema anatulisha sote kwa Neno lake na kwa mwili na damu yake. Anatuponywa kwa sakramenti ya Upatanisho, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu tunafanywa kuwa askari hodari wanaoufahamu na kuulinda ukweli unaookoa. Naye anatuongoza kuelekea nchi ya ahadi, Yerusalemu Mpya, Mbinguni, tukawe warithi wa uzima wa milele pamoja naye. Ni wajibu wetu kumfahamu Kristo mchungaji wetu mwema, kuitambua sauti yake ili kila anapotuita tunapokuwa tumepotea, tuweza kuisikia, kuisikiliza na kuifuata kwani ndiyo inayotupeleka katika uzima wa milele.

Kristo Yesu ni Mchungaji mwema
Kristo Yesu ni Mchungaji mwema

Kama tulivyosema mwanzoni, ni dominika ya kuombea miito. Basi tuhitimishe tafakari ya dominika hii kwa kusali sala ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwa sala ya Papa Benedikto XVI. Tuombe: “Ee Baba, uamshe ndani ya waamini wako, Miito mitakatifu ya Upadre na Utawa, ili kuimarisha Imani na kulinda uzuri wa kumbukumbu ya mwanao Yesu Kristo, kwa njia ya kueneza neno lake, na kutoa sakramenti ambazo hufanya upya Waamini wako. Utupe watumishi watakatifu kujongea altare yako, ambao ni waangalifu, na wenye kuheshimu Ekaristi Takatifu, kama zawadi kubwa ya Yesu kukomboa ulimwengu. Kwa huruma yako uite watumishi, ambao kwa njia ya sakramenti ya kitubio, wataeneza furaha yako ya msamaha kwa watu. Ee Baba ulijalie Kanisa lako lipokee kwa furaha Roho ya Mwanao, na kuwa waaminifu kwa mafundisho yake. Kanisa lako litunze miito ya wale walioitwa kwa maisha ya wakfu ya Upadre na Utawa. Uwaimarishe Maaskofu, Mapadre, Mashemasi na Watawa wote wa kike na wa kiume, waliojitoa kwa maisha ya wakfu. Pia uwaimarishe wote waliobatizwa kwa Jina la Kristo, ili wawe waaminifu katika Utume kwa huduma ya kutangaza Enjili. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana Wetu. Amina.” Bikira Maria Malkia wa Mitume, Utuombee. Tumsifu Yesu Kristo.

D4 ya Pasaka Mwaka B
20 April 2024, 10:47