Tafuta

Masomo ya Dominika hii yanatuelekeza namna ya kukutana na kumtambua Kristo Yesu Mfufuka: Katika Neno na Katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu Masomo ya Dominika hii yanatuelekeza namna ya kukutana na kumtambua Kristo Yesu Mfufuka: Katika Neno na Katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tatu Pasaka Mwaka B: Utambulisho wa Yesu: Neno na Kuumega Mkate

Masomo yanatuelekeza namna ya kukutana na kumtambua Kristo Mfufuka katika adhimisho la sadaka ya Misa Takatifu kwa kusikiliza Neno lake na katika kuumega mkate. Sharti ni kuwa katika hali ya neema ya utakaso, kuwa bila dhambi. Kumbe, tunapaswa kujitakasa kwa kuziungama na kuzikiri dhambi zetu kabla ya kuijongea meza ya Bwana. Hii ndiyo zawadi kuu ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Sakramenti ya Upatanisho, kurudishiwa hadhi ya wana wa Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya tatu ya Kipindi cha Pasaka Mwaka B. Masomo ya Dominika hii yanatuelekeza namna ya kukutana na kumtambua Kristo Yesu Mfufuka katika adhimisho la sadaka ya Misa Takatifu kwa kusikiliza Neno lake na katika kuumega mkate. Sharti ni kuwa katika hali ya neema ya utakaso, kuwa bila dhambi. Kumbe, tunapaswa kujitakasa kwa kuziungama na kuzikiri dhambi zetu kabla ya kuijongea meza ya Bwana. Hii ndiyo zawadi kuu ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Sakramenti ya Upatanisho, kurudishiwa hadhi ya wana wa Mungu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha siku zote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafurahi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wako, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo.3:3-15,17-19). Somo hili ni mawaidha ya Mtume Petro kwa Wayahudi akiwaasa watubu dhambi zao ili wanaweze kusamehewa na kuokoka ingawa walimwua Yesu kwa kumtundika msalabani. Maana kwa kifo na ufufuko wake, Yesu ametupatanisha na Mungu Baba na kutufungulia mlango wa kwenda mbingu. Mtume Petro kwa ujasiri anawaambia waziwazi akisema; “Yesu ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji. Mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.” Kwa maneno haya, mioyo yao ilichomwa. Wakajiona kuwa wakosaji mno. Petro aliwafariji na kuwapa matumaini mapya akiwaambia; “Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Basi, tubuni, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe.”

Utambulisho wa Kristo Mfufuka: Neno na Ekaristi Takatifu
Utambulisho wa Kristo Mfufuka: Neno na Ekaristi Takatifu

Ni mwaliko kwetu sote wa kujirudi kila tunapotenda dhambi, kutubu, na kurejea kwa Kristo, kwa kufanya toba ya kweli, naye atazifuta dhambi zetu na kutusamehe na kutujaza furaha na amani tele mioyoni mwetu. Ndiyo maana zaburi ya wimbo wa mwanzo inatuambia hivi; “Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote, imbeni utukufu wa jina lake. Tukuzeni sifa zake, aleluya” (Zab. 66:1-2). Na katika wimbo wa katikati tunaimba kwa matumaini kwa maneno haya; “Bwana, utuinulie nuru ya uso wako. Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo. Umenifanyizia nafasi wakati wa shida; unifadhili na kuisikia sala yangu. Basi jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa; Bwana atasikia nimwitapo. Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema? Bwana, utuinulie nuru ya uso wako. Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, Bwana, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama (Zab. 4:1, 3, 6, 8). Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Yohane kwa Watu Wote (1Yoh. 2:1-5). Somo hili linatufundisha kuwa kumjua Mungu ndio kushika amri zake na katika kuzishika amri za Mungu, upendo wake unakamilika ndani mwetu. Sisi tulio wafuasi wa Kristo, tupaswa kuenenda katika nuru ya Mungu kwa kujitenga na dhambi. Na kama tukitenda dhambi, basi, tumkimbilie mara moja Yesu aliye Mwokozi na Mpatanishi wetu kwa Baba. Mtume Yohane anasisistiza jambo hili akisema; “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwokozi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu…na za ulimwengu wote.” Tuikimbilie basi kila mara sakramenti ya kitubio, kujipatanisha na Mungu Baba yetu.

Utambulisho wa Kristo Mfufuka: Neno la Mungu
Utambulisho wa Kristo Mfufuka: Neno la Mungu

Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 24:35-48). Sehemu hii ya Injili inaanzia pale Wanafunzi wa Emmau waliporejea Yerusalemu na jinsi walivyomtambua Yesu mfufuka katika kuumega mkate. Yesu mwenyewe anawaeleza na kuwahakikishia Mitume juu ya kifo na ufufuko wake, jinsi walivyotabiri na kuagua manabii. Kisha anawatuma waende duniani kote kuhubiri na kuushuhudia ufufuko wake. Yesu mfufuka ni Mungu na mtu naye anawafariji na kuwapa matumaini mitume wake akiwadhihirishia hali yake ya kibinadamu akiwaambia; “Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni shikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo…Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia; Mna chakula chochote? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akabariki, akala mbele yao.” Akawakumbusha torati na maandiko ya manabii yanayosema kuwa Kristo atateswa lakini atafufuka, Mataifa yatahubiriwa habari zake nao watamwamini. Kwa jina la Kristo, toba na ondoleo la dhambi ni kwa wote wanaomwamini. Hili ndilo tunda la fumbo la Pasaka; Msamaha wa dhambi kwa wote. Haijalishi ukubwa wa dhambi. Kinachohitajika ni kufanya toba ya kweli na kuungama. Kumbe upendo wa fumbo la pasaka unadhihirishwa katika sakramenti ya Upatatanisho. Hapa watu wote wanaonja upendo, huruma na msamaha wa dhambi na kupatanishwa na Mungu Baba.

Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate
Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate

Kwa mateso, kifo na Ufufuko wa Kristo tumekombolewa, sote ni wana na warithi wa uzima wa milele. Lakini inafaa tukumbuke maneno ya Mtakatifu Augustino kwamba; “Mungu aliyetuumba pasipo sisi kupenda, hawezi kutukomboa pasipo sisi kupenda.” Tunaalikwa kupokea zawadi ya wokovu, kwa kuishi ndani ya Kristo kwa kulisoma Neno lake kwa moyo wa sala na ibada, kwa kupokea vyema Sakramenti, kwa kuzishika na kuziishi Amri na maagizo ya Mungu, kwa kushika maagano na viapo vyetu vya ubatizo kwa upendo, uaminifu, na uvumilivu. Kila mmoja atambue nafasi yake katika mpango wa Mungu; wazazi, watoto, vijana na hata wazee. Upendo wa Kristo ukitubidisha ili siku moja nasi tuweze kustahilishwa kuupokea uzima wa milele mbinguni. Uzima wa milele mbinguni ndilo tunachokitumainia. Tumaini hili mama Kanisa anatukumbusha kila mara anaposali na kutuombea. Katika sala ya mwanzo mama Kanisa anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha siku zote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafurahi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wako, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi”. Na katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana tunakuomba uzipokee dhabihu za Kanisa lako linalofanya shangwe. Na kama ulivyolifanya lifurahi sana sasa, ulijalie pia furaha ya milele”. Na anahitimisha katika sala baada ya komunyo akisali; “Ee Bwana, tunakuomba utuangalie kwa wema sisi taifa lako. Utujalie tufufuke na miili mitukufu, sisi ambao umependa kutufanya wapya kwa mafumbo haya ya milele.” Tujiweka basi chini ya Kristo Mfufuko ili siku moja tukashiriki naye huu uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 3 Pasaka Mwaka B
09 April 2024, 14:58