Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Pasaka: Walimtambua Kristo Yesu kwa kuumega mkate na kwa ufafanuzi wa Neno la Mungu chachu ya mabadiliko katika maisha. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Pasaka: Walimtambua Kristo Yesu kwa kuumega mkate na kwa ufafanuzi wa Neno la Mungu chachu ya mabadiliko katika maisha.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tatu ya Pasaka Mwaka B: Neno na Ekaristi Chachu ya Upya wa Maisha

Ikumbukwe kwamba: Ukuu na nguvu ya Mungu havijioneshi kwa nguvu, vitisho na mamlaka, bali katika upendo, msamaha na maisha tele! Wanafunzi walimtambua Yesu kwa kuumega mkate, katika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, changamoto na mwaliko wa kuvunjilia mbali mambo yote yanayofisha macho yao na hivyo kuufanya moyo wao kushindwa kuvunjilia mbali mawazo mgando na maamuzi mbele, kwa hakika watashindwa kuufahamu Uso wa Mungu!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji Tunaendela na wimbo wetu amefufuka kweli aleluya Kufufuka kwa Yesu kuwe sababu ya kufanya mabadiliko katika maisha yetu, yaani kutoka maisha ya dhambi kwenda maisha ya utakatifu. Bila kufanya hivyo ufufuko wa Yesu hautatusaidia kupata utakatifu, bali utabaki kuwa kumbukumbu tu, na siyo kama tukio hai na halisi kwetu kiroho na kimwili. Suala la ufufuko sio jambo dogo au jepesi, akitokea mtu ambaye tuna hakika alikufa na tumemzika wenyewe hatutapenda jambo hilo hata kidogo, tutamuogopa na kumkimbia, tutamuitia police na hatutakaa nae kwa amani. Ugumu huo waliupata pia wanafunzi wa Kristo na waliona kabisa kwamba haiwezekani mtu waliyemshuhudia kuuawa msalabani na mazishi yake awe ni mzima tena, hawakuamini. Ni kweli hayupo aliyefufuka kwa hakika isipokuwa Kristo, amekuwa wa kwanza kutoka kwa wafu, na kwa ufufuko huo wote tumepata uzima, Kanisa limepata kazi na wanadamu wamezawadiwa tumaini jipya. Alipowatokea wanafunzi wake aliwahoji “mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Hebu nitazameni, nishikenishikeni, jamani ni mimi mwenyewe, sio pepo, sio roho, hivyo havina nyama wala mifupa. Kama vile haitoshi anakula samaki mbele yao na wanafunzi wanapofunguliwa akili zao na kuelewa maandiko ya torati ya Musa, manabii na zaburi, mashaka yanaisha na furaha inatawala.

Waliwatambua kwa kuumega Mkate
Waliwatambua kwa kuumega Mkate

UFAFANUZI: Mpendwa katika Kristo, kubadilika ni kutoka katika hali fulani kwenda katika hali nyingine, na haya mabadiliko yaweza kuwa chanya au tendo la hasi. Mmoja anapotoka katika hali mbaya na kwenda katika hali njema, mabadiliko haya ni chanya na kinyume chake ni mabadiliko hasi. Mabadiliko ambayo mimi nayahusianisha na ufufuko ni mabadiliko chanya yaani kutoka mazingira/hali ya dhambi na kuingia katika hali ya neema na zaidi sana kuishi maisha ya utakatifu. Katika somo la kwanza (Mdo. 3:13-15,17-19) tumesikia kuwa mtume Petro anawaambia wayahudi kuwa, kwa njia ya kutubu wanaweza kuokoka ingawa walimwua Yesu Mkombozi wetu. Hivyo Petro aliwataka Wayahudi wafanye toba na kufanya mabadiliko chanya katika maisha yao ili wasamehewe dhambi zao wapate kuurithi uzima wa mileleDaima Kristo mfufuka hajulikani mwanzoni, Maria Magdalene alimfananisha na mtunza bustani, wafuasi 2 wa Emau walimchukulia kama msafiri tu, mitume walidhani roho/pepo/mzuka... ametambulikana baadaye anapowakumbusha maandiko matakatifu yaliyomuhusu na katika kuumega mkate. Imani juu ya ufufuko si hadithi ya kubuni, bali ni dhahiri kwamba Kristo yu hai kama alivyokuwa mwanzo, ana mwili wa utukufu wenye mifupa, nyama na damu, anayeongea na kula na watu. Ni Masiha, ukamilifu wa Agano la Kale anayeangaza akili za wanadamu na kuwafafanulia maandiko matakatifu, yupo kati yetu, anaishi ndani ya mioyo yetu. Swali hili “mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu?” linatuhusu pia. Inawezekana maisha yetu yameghubikwa na wimbi la mashaka na mfadhaiko kiasi cha kuitikisa imani yetu na kuujaribu utashi wetu. Kama watu tuliofunuliwa tunaalikwa kuondoa mashaka na kujaa furaha ya Pasaka na kuwashirikisha wenzetu. Tunapowashirikishana Yesu anajifunua zaidi kwetu, “ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko”, hili linahusisha kuwatafuta waliorejea nyuma na kuwaleta kwa Yesu. Kuja Kanisani peke yetu ilhali wale wanaotuzunguka tumewaacha mtaani ni mbali na ushuhuda wa Pasaka. Kuwa mashahidi sio kuwatishia watu moto wa milele bali ni kuwa tayari kumjibu kwa ufasaha kila anayetuuliza juu ya matumaini tuliyo nayo kwa upole na heshima.

Walitambulikana kwa kuumega Mkate
Walitambulikana kwa kuumega Mkate

Somo la pili (1Yoh. 2:1-5) linaeleza kuwa kumjua Mungu ndio kushika na kutenda kadiri mapenzi yake na hasa amri yake ya mapendo. Imani yetu kwa Mungu lazima ionekane katika mfano wa maisha yetu mema. Iwapo tunasema kuwa tunamjua Mungu na hatu yafanyi mapenzi yake, tujue kuwa sisi ni waongo na kweli haimo ndani mwetu. Tutafakari kwa kiasi gani tumefanikiwa kumjua Mungu kwa njia ya kushika maagizo yake? Kama hatujafanikiwa yatupasa leo kufanya mabadiliko kutoka maisha hayo ya dhambi na kuishi maisha ya utakatifu ili tung’ae kama Yesu mfufuka bila kuwa na mashaka.  Kutokuwa na mashaka na kuishi kama tunaoamini ufufuko ni kuwagusa watu na amani ya Kristo mfufuka. Tutaweza kufanya hivi kwa namna tunavyoishi. Mungu ametujalia uwezo wa kuzungumza, basi maongezi yetu yawe ya Kikristo, tusiongee uongo, tusiwazushie wenzetu, tusieneze udhaifu wao, tusijione wakamilifu. Katika mazungumzo tuzingatie walau mambo 5: unazungumza nini? Unamzungumzia nani? Unazungumza namna gani? Unazungumza muda gani? Na unazungumzia wapi? Ukitaka kuzungumza mambo mabaya, hiyo ndio hamu yako ya leo, na kwamba chakula hakiwezi kushuka na usingizi hautakuja hadi leo hii uongee mabaya basi nenda mtoni, kayaseme yote kwa makelele upendavyo. Utakayoyasema hayatasikika kwa yeyote, yatachukuliwa na maji na wewe utapata nafuu moyoni mwako, ukitoka mtoni kula chakula chako ulale usingizi, kimyaa. Kinyume chake ukiongea mabaya mbele ya wenzio, au kilabuni au ofisini au mbele ya kamera za video sio tu utakuwa unatawanya neno baya bali pia hilo litabaki limetunzwa maktaba kwa vizazi vijavyo na historia itakuwa tayari kukuhukumu.

Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate
Walimtambua Kristo Yesu Mfufuka kwa Kuumega Mkate

Watu wasio na mashaka wanapendana. Ili kupenda kweli ni lazima kujisadaka, “kusudi sadaka yoyote iwe halisi ni lazima igharamiwe, ni lazima iume tena ni lazima tujitoe haswa. Tunda la sadaka ni sala, tunda la sala ni imani, tunda la imani ni upendo, tunda la upendo ni huduma na tunda la huduma ni amani” (Anasema MT Mama Teresa wa Klkuta). Faida nyingine ya upendo ni heshima, “nanyi wanaume katika kuishi na wake zenu muwatendee kwa heshima” (1Pet 3:7) na “mke anapaswa kumuheshimu mumewe” (Efe 5:30). Msifadhaike, msione shaka bali jitahidini kuushinda ulimwengu kwa kuuishi. Katika Injili ya leo, (Lk 24:35-48.) Yesu anawashangaa wafuasi wake wanaoshindwa kuamini ufufuko wake. Hivyo anachukua jukumu la kuwahahakikishia kuwa yeye sio roho, bali ni Yesu mfufuka kwa kuwaonesha majeraha yake na kwa kula kipande cha samaki. Yesu anafanya hivyo ili waweze kubadilika kutoka masikitiko kwenda kwenye hali ya furaha, unyonge na woga kwenda kwenye hali ya ujasiri, kutoka kutoamini hadi hali ya kuamini, ili waweze kuwa mashahidi wa ufufuko wake, na wawe wahubiri wa toba na ondoleo la dhambi kwa mataifa yote. Upendo wenye heshima ulio ni kitu cha bure lakini chenye thamani. Unayemuheshimu utamsikiliza na utamlinda. Ukifanikiwa kumwaibisha jirani yako tambua umefeli somo la heshima, unaishi kwa mashaka na mfadhaiko. Baba na amuheshimu mama, mama na amuheshimu mama, wazazi na watoto na waheshimiane, wakubwa na wadogo, matajiri na fukara, wenye vyeo na waongozwa na waheshimiane.

Neno la Mungu liwe ni chachu ya mabadiliko katika maisha
Neno la Mungu liwe ni chachu ya mabadiliko katika maisha

Mara nyingi tunashindwa kufanya mabadiliko kwa sababu, mosi kuogopa kujitolea katika kufanya mabadiliko na pili, daima tunaadhimisha Ufufuko wa Bwana kama kumbukumbu tu, na siyo kama tukio hai na halisi kwetu kiroho na kimwili. Hebu tumtazame mmoja mwenye miaka 60,40,30,20 na kila mmoja ameadhimisha Pasaka kadiri ya umri wake.  Je ni Pasaka za mtindo na aina gani Ulizoadhimisha? Ingekuwa ni kufanya mabadiliko chanya angekuwa ameacha vilema vingi kadiri ya umri wake. Wengi tuko hapa ambao hatukufanya maazimio ya kufanya mabadiliko yoyote wakati wa kwaresma hashakuhm si matusi hawa nachelea kusema Nyani ni walewale ila msitu ni mpya na hivi tulikuwa tunasubiri tuadhimishe Pasaka kama kumbukumbu tu! Lakini bado hatujachelewa kufanya mabadiliko. Tututumie kipindi hiki cha Pasaka kuacha vilema vyetu. Kufanya mabadiliko si kazi rahisi, ni sadaka, wala si ‘lele mama’ bali ni kazi, jasho na mateso. Kwani katika kufanya mabadiliko tutakumbana na vikwazo vingi, wakati mwingine unaweza kufanya mabadiliko kutoka uvivu katika sala na kuwa mtu wa sala na hali ya kitume na kuwajibika kwa uaminifu katika majukumu yako lakini utapewa dhihaka na wengine watakuita Baba wa roho au mama wa roho nk, Au ukaambiwa walikuwepo wenzako waliojidai kuwa wema kama wewe lakini walishindwa vibaya, na wewe tunakutazamia kupata kuona mbio za sakafuni. Usipokuwa imara katika imani unaweza kurudia matopeni ulikotoka. Hivyo mabadiliko ni sadaka, hivyo tufanye bidii bila kukata tama kubadili maisha yetu kuelekea utakatifu. Hofu, mashaka na mfadhaiko wetu vitakoma tukiwa watu tunaosali na kumtegemea Mungu katika kila jambo. Mkristo mwenzangu busara itakulinda, hekima itakuhifadhi, bidii itakuongezea maarifa, maombi yatakusogeza karibu na Mungu na ukarimu utakufanya ukumbukwe siku zote, usiyumbe, usirudi nyuma, usikate tamaa, usipoteze matumaini, jipe moyo usonge mbele kwani Yesu aliyefufuka yupo pamoja nawe kukusaidia, kwa nguvu zetu hatuwezi kufanya mabadiliko ya maisha yetu kutoka hali ya dhambi kwenda maisha ya utakatifu. Basi, tumwombe Mwenyezi Mungu ili neema zitokanazo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ziendelee kufanya kazi ya mabadiliko ndani mwetu na hatimaye tushiriki matunda ya utukufu yatokanayo na kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.  Amina.

Liturujia D3 ya Pasaka Mwaka B
13 April 2024, 08:25