Tafuta

2024.03.12 Tanzania: Askofu Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga akabidhi msaada wa Magodoro kwa ajili ya wafungwa wa Magereza ya Kayanga, Karagwe Tanzania. 2024.03.12 Tanzania: Askofu Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga akabidhi msaada wa Magodoro kwa ajili ya wafungwa wa Magereza ya Kayanga, Karagwe Tanzania. 

Tanzania:Askofu Rweyongeza atoa msaada wa magodoro kwa wafungwa,Kayanga!

“Kanisa lina haki ya kuwahudumia wafungwa kiroho na kimwili kwa kuwapelekea mahitaji msingi kama vyakula na malazi pia kuwahudumia kiroho kwa kuwatembelea, kusali pamoja nao pia kuwapelekea vifaa vya kiroho kama Biblia na Rozari Takatifu.”Haya yalisemwa na Askofu Rweyongeza wa jimbo la Kayanga,Tanzania wakati wa kukabidhi magodoro 100 kwa ajili ya Wafungwa Wilayani Karagwe,Tanzaia Machi 11,2024.

Dativa Tuluhungwa,Patrick Tibanga-Bukoba na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Kipindi cha Kwaresima ambacho tumefikia Dominika ya IV ya Kwaresima bado tunakumbushwa mchakato wa hija ya Siku Arobaini inayojikita mizizi katika Ubatizo, kufunga, kusali na kuwa na tabia njema hasa inayojionesha kwa matendo yetu mema  kwa wahitaji. Katika ubatizo wetu ambao ni Sakramenti inatuingiza ndani ya ukristo wa kweli kwa kushiriki kuwa wa Kristo na Ndugu wa Kristo. Na ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu  zetu ambazo tulizirithi tangu Adamu na Eva. Kipindi cha Kwaresima ni  muhimu hasa kufunga, sala na huruma ya uhai wetu na kwa ajili ya wengine. Katika kufunga ndipo tunajigundua udhaifu na kuwa na moyo wa upendo hasa kuweza kufanya matendo ya huruma kwa ajili ya  wahitaji. Hizi ni ishara rahisi na muhimu katika maisha yetu ya kila siku na hasa katika vipindi vikuu ambavyo mama Kanisa anatujalia. Ishara hizi haziwezi kukosekana ili kuwa makini kwa kusikiliza kilio, shida na mahangaiko ya wengine. Ni watu wangapi wanateseka katika Ulimwengu huu? Ni Vituo vingapi vya wahitaji kuanzia na Watoto yatima, wagonjwa mahospitalini, vituo vya kutunza wazee, walemavu, vipofu na hatimaye katika magereza zote , kike kiume na vijana? Yesu Mwenyewe alisema: “Nilikuwa Uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kinitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kinitembelea… “Mt 25, 36-40).

Askofu Rweyongeza akikabidhi magodoro
Askofu Rweyongeza akikabidhi magodoro

Kumbe basi katika muktadha wa kipindi hiki cha Kwaresima Askofu Almachius Vincent Rweyongeza, wa Jimbo Katoliki la Kayanga nchini Tanzania, alitoa msaada wa zaidi ya magodoro 100 kama sehemu ya matendo ya huruma kwa ajili ya wafungwa wa Gereza la Kayanga, Wilayani Karagwe nchini Tanzania Jumatatu tarehe 11 Machi 2024. Katika afla ya kukabidhi msaada huo Askofu Rweyongeza alisema kuwa: “Upendo kwa wafungwa ni ishara ya Ukristo kamili pia kuuishi Upendo wa Yesu Kristo alioonesha kwa wanadamu. Kanisa lina haki ya kuwahudumia wafungwa kiroho na kimwili kwa kuwapelekea mahitaji msingi kama vyakula na malazi pia kuwahudumia kiroho kwa kuwatembelea, kusali pamoja  nao pia kuwapelekea vifaa vya kiroho kama Biblia na Rozari Takatifu.” Askofu Rweyongeza kwa namna hiyo alitoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema kutumia vema kipindi cha mfungo huu wa Kwaresima kwa kuwatembelea na kuwajali wafungwa ambao wanahitaji zaidi huduma za kiroho na kimwili.

Afande Masalu ashukuru Askofu Rweyongeza kwa ukarimu

Waliopokea msada huo  ni viongozi wakuu wa Gereza la Kayanga Wilayani Karagwe, Tanzania, ambapo  kwa niaba ya wote, neno kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Wafungwa, Afande John Masalu alisema jinsi ambavyo wamekuwa na changamoto ya malazi kwa muda mrefu na kwa njia hiyo alimshukuru Askofu Rweyongeza kwa “kuonesha moyo wa ukarimu na moyo wa kujitoa kwa wafungwa.”

Afande Masalu,Mkuu wa Magereza ya Kayanga Karagwe akimshukuru Askofu wa Kayanga
Afande Masalu,Mkuu wa Magereza ya Kayanga Karagwe akimshukuru Askofu wa Kayanga

Ndugu msomaji, ikumbukwe kwamba hali za magereza duniani kote ni mbaya sana. Wafungwa wanahitaji msaada wa hali na mali katika maisha yao, yawe ya kiroho na kimwili. Wafungwa na hata wafanyakazi wao, wote kwa pamoja wanahitaji kusindikizwa kwa msada, kutembelewa na kuzungumza. Haijalishi ni wafungwa kwa sababu, Yesu hakuja kwa ajili ya wenye afya bali kwa wagojwa ili wapate kutubu. Kwa njia hiyo mimi na wewe tunao wajibu kweli wa kuwatembelea, kuwasindikiza katika maisha yao.

Askofu A. Rweyongeza atoa msaada wa magodoro kwa wafungwa wa Kayanga-Karagwe Tanzania
12 March 2024, 16:36