Tafuta

“Amin, amin, nawambia: Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yn. 12:24). “Amin, amin, nawambia: Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yn. 12:24).  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tano Kwaresima Mwaka B: Saa ya Yesu

Tumekaribia kuadhimisha kilele cha Fumbo la wokovu wetu yaani Pasaka ya Bwana. Kilele hicho kinaashiria “saa ya yake kutimia kama tutakavyosikia siku ya ijumaa kuu yametimia” ambapo mwanadamu anafanywa huru apate kuabudu anarudishiwa uhuru na hadhi ya kuwa mwana mpendwa wa Mungu kama alivyo Kristo ndivyo anavyojitoa kama mbegu inayokufa kisha kuchipua tena kwa kutoa mazao mengi ndivyo na sisi tuliowengi tunazaliwa katika kifo cha Kristo Yesu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGALIZI: Leo ni Dominika ya 5 ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka B wa Kanisa. Ni kipindi tunapoalikwa kutafakari kwa kina juu ya mwendo wetu wa maisha kama wafuasi wa Kristo; ni kwa kiasi gani tumebaki kuwa waaminifu katika amri na maagizo yake. Tunapokaribia kusherehekea sikukuu ya Pasaka, nawaalika tutafakari juu ya maneno haya mazito ya Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo yanayoonesha upendo wa kujisadaka kwaajili ya mwingine tumesikia sehemu ya maneno ya Injli ya leo “Amin, amin, nawambia: Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yn. 12:24). Tumekaribia kuadhimisha kilele cha Fumbo la wokovu wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Bwan wetu. Kilele hicho kinaashiria “saa ya yake kutimia kama tutakavyosikia siku ya ijumaa kuu yametimia” ambapo mwanadamu anafanywa huru apate kuabudu anarudishiwa uhuru na hadhi ya kuwa mwana mpendwa wa Mungu kama alivyo Kristo Bwana na mwalimu wetu ndivyo anavyojitoa kama mbegu inayokufa kisha kuchipua na kuwa hai kwa kutoa mazao mengi ndivyo na sisi tuliowengi tunazaliwa katika kifo cha kristo kwa kufanywa upya na kuwa wana saw ana yeye “katika roho na kweli.”

Saa ya Kristo Yesu: Mateso, Kifo na Ufufuko wake kwa wafu.
Saa ya Kristo Yesu: Mateso, Kifo na Ufufuko wake kwa wafu.

UFAFANUZI: Tufe kama mbegu ardhini ili tuzae matunda, namna gani? Nabii Yeremia katika Somo la Kwanza: (Yer 31:31-34) anatufundisha kuwa Agano hilo ni tofauti na la Kale. Mwanadamu alishindwa kulishika sababu Sheria ya Mungu iliandikwa kwenye mawe na si moyoni mwa watu na ikafungiwa kwenye Sanduku la Agano, ikanyumbuliwa hadi kufika sheria 613 na kuwa mzigo usiobebeka hata wenye uwezo wa kukariri iliwapa shida hasa katika matendo hata kumbukumbu. Watu waliambiwa tu “fanya… usifanye!” kujua ni jambo moja kutenda ni jambo jingine, tunajua mazuri mengi lakini hatuyatendi (kama mwanazuoni wa Kiyunani Sokratesi anavyowataadhalisha wanafunzi wake). Tuipokee sheria na maagizo ya Mungu kama sehemu ya maisha na si kama mzigo usiobebeka. Ahadi alizoahidiwa Abraham na vizazi vyake tangu zamani zinatuhusu sisi pia na sheria ya Musa inawahusu mataifa yote katika Yesu Kristo Bwana wetu ndio AMRI YA UPENDO KWA MUNGU NA JIRANI. Mwanzoni mwa Injili (Yn. 12:20-33.) tumesikia kuhusu Wayunani waliofika Yerusalemu kumwabudu Mungu wa kweli wa Israeli. Na baada ya kuwa wameshuhudia na kuvutiwa na utukufu na mashangilio aliyoyapata Yesu alipoingia Yerusalemu. ili tuelewe vizuri ujumbe anaotuletea Yesu kupitia mfano huu, ni lazima tujue desturi ya wayahudi katika shughuli ya kupanda mbegu za ngano. Tukirejea mfano maarufu wa “mpanzi” (Mt. 13:18-23), wayahudi walikuwa wanatawanya mbegu shambani ndipo wanalima. Kulima kulikuwa ni tendo la kufukia mbegu ili ife ardhini na kuchipua upya. Namna hii ya upandaji mbegu ni tofauti na utaratibu wetu ambapo sisi tunaanza kulima na kasha kusia mbegu.

Pasaka ni kilele cha Fumbo la Ukombozi
Pasaka ni kilele cha Fumbo la Ukombozi

Chembe ya ngano “inayokufa ili kuzaa sana” ni Yesu Mwenyewe anayejitoa afe ili kuzaa mazao ya ukombozi. Kifo cha Yesu ni udhihirisho wa upendo usio na mipaka na ambao hakuna kanuni yoyote ya kimahesabu wala ya kifizikia inayoweza kuukokotoa wala mzani unaoweza kuupima. Mmoja anafikia kilele cha ukomavu pale anapofaulu KUPENDA hadi kuutoa uhai wake kwa ajili ya ndugu zake (Yn 10:11). Mkulima anafanya nini akiwa na nafaka kidogo na anaogopa isiibiwe? Anaweza kuificha bado ikaliwa na wadudu au ikaoza, au anaweza kuikaanga na kuila na hapo hatabakiwa na kitu. Njia nzuri ni kujikaza na kuizika ardhini na kuiacha ife ili impatie mazao zaidi, ndiyo busara ya kilimo. Tufe kama mbegu ardhini ili tuzae matunda, namna gani? Mpendwa msikilizaji na msomaji ili mbegu yoyote ile (iwe ya ngano, mahindi, maharage, maparachichi au maboga) iote na baadae kutoa mazao mazuri na kwa wingi, ni lazima ikauke vizuri, ifukiwe ardhini, ioze, ipasuke na kupoteza kabisa umbo lake la awali, yaani ife. Ni kiini tu cha mbegu kinachotakiwa kwa ajili ya kuotesha mmea mpya. Lakini magamba ya nje si kama kwamba hayafai, bali kazi yake ni kukilinda kiini kile kisiharibiwe na wadudu na hali mbaya ya hewa, kabla ya kufika muda wa kuotesha. Hivyo ndivyo tufanyavyo kila mwaka tunapopanda mbegu zetu ili tupate mazao na mavuno mapya, mazuri na ya kutosha. La sivyo, hatutapata chochote na tutakufa kwa njaa.

Mbegu inayokufa ndiyo inayoota na kuzaa matunda.
Mbegu inayokufa ndiyo inayoota na kuzaa matunda.

Kufa kama chembe ya ngano na kumea na kuzaa sana” ni kumakinika katika kazi tuliyopata kwa ubatizo ya KUENEZA UFALME WA MUNGU DUNIANI. Ili kutimiza wajibu huu sharti tuzikwe kama ngano, yaani tujitahidi kwa moyo, nguvu na akili KUMPENDA MUNGU NA JIRANI. Jambo hili linapita katika njia ngumu kiroho na kimwili, Mungu mwema na atuimarishe. kuishi fadhila za busara, haki, uhodari na kiasi... amani, uwazi, ukweli na uelewano, tukichukuliana, kuvumiliana na kuonyana kindugu katika udhaifu wetu kama watoto wa baba na mama mmoja, kaka na dada za Yesu. kufanya mabadiliko. Yesu anasema “…mbegu isipokufa hukaa hali hiyohiyo peke yake…” hapa panadai uongofu na kukubali kuwa wapya. Yesu anajifananisha na chembe (mbegu) ya ngano, akitaka kueleza ukweli huu kwamba, ili amtukuze Baba na kuwakomboa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi, ni lazima ateswe, afe, azikwe na hatimaye, afufuke katika wafu, ili kutuletea sisi uzima wa roho. Hivyo, Yesu alipoteza thamani ya mwili wake na heshima ya kibinadamu pale msalabani ili autukuze na kuuhuisha uzima wa kimungu katika roho zetu kwa ushindi wa ufufuko. Tujifunze haya katika maisha ya kila siku kutokana na ujumbe wa masomo ya leo. Ili kuwaleta wengi zaidi kwa Kristo. Ulimwengu unatusubiri tuuhudumie; ni ulimwengu uliojeruhiwa, una hali mbaya, upo kichwa chini miguu juu. Tupo msituni tunashindana daima (The Law of the Jungle: struggle for survival, survival of the fittest), mwenye nguvu ndiye anayeishi akijipambanua kama mnyama kwa mwanadamu mwenzake (homo homini lupus est). Ulimwengu wetu unaahidi mambo mengi yanayoonekana mazuri na ya kuvutia kwa nje lakini kinyume chake unatuletea matatizo na kuharibu jamii.

Wokovu wetu umetundikwa juu ya Msalaba
Wokovu wetu umetundikwa juu ya Msalaba

Sisi sote, tuliowafuasi wake Kristo, tumekombolewa na Kristo kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Sisi pia ni mbegu za ngano zinazotakiwa zife katika dhambi na kuotesha utakatifu. Kwa sakramenti ya ubatizo tumekufa na Kristo katika dhambi na mauti, na kufufuka naye katika uzima wa roho. Tufe katika mwili ili tuishi katika roho.” Miili yetu inafanana na sehemu ya nje ya mbegu na roho zetu zinafanana na kiini cha mbegu. Mwili wa mwanadamu kibilia unawakilisha: umbile na viungo vyote vya binadamu; kikao cha vionjo na tamaa za mtu; udhaifu wote wa mtu; udogo wa mtu mbele ya Mungu. Lakini roho kibiblia ina maana ya uzima wa kimungu katika mtu; ni chanzo cha imani na utakaso wetu; ni nguvu ya maisha adilifu; ni mwungano wa ndani kabisa wa mtu na Mungu. Tuyaogope na kuyakwepa yote yanayoweza kutufisha mwili na roho. Tusiishi kwa kuongozwa na vionjo na mvuto wa kimwili. Tusijisifie na kufurahia kubaki katika udhaifu wetu. Tuyaache maisha ya kawaida na ya kale yaliyojaa maovu, hasa katika kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima, tunapojitahidi kufanya mabadiliko chanya ya maisha yetu. Tutafakari na kujiuliza kila mmoja wetu ndani ya nafsi yake kwamba je, kuna dhambi, kikwazo au kilema chochote kinachodhoofisha au kinachofisha uhusiano wake na Mungu na jirani zake? Kama bado hatujaviondoa tujongee kwenye kiti cha kitubio, tutubu na kuungama, ili tutakapoadhimisha sherehe za Pasaka, tufufuke na Kristo tukiwa na maisha mapya kiroho, tukihusiana vema na Mungu na jirani zetu.

Jiandaeni Kusherehekea Pasaka ya Bwana
Jiandaeni Kusherehekea Pasaka ya Bwana

Leo hii tunaishi katika ulimwengu wenye mifumo mingi tena haribifu, mifumo inayoua umoja na mshikamano wa familia na kampeni kubwa ya kuua hofu ya Mungu kwa watu wake. Ni ulimwengu unaochukia mema na kumchukia Kristo sababu daima anazionya na kuziangaza dhamiri ya mwanadamu, anausuta moyo wake na tamaa zake mbaya. Je, mwamini mwenzangu upo tayari kuhubiri Injili katika mazingira hayo? Tusijipende na kujihurumia mno sababu “yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza, naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele” (Yn 12:25), kwa imani yanawezekana... Tumtumikie Mungu katika huduma naye Baba atatuheshimu na atakapokuwapo Kristo ndipo na sisi tutakapokuwapo. Wapendwa, sisi tu viumbe dhaifu, na mara nyingi tunayumbishwa katika imani yetu kwa Kristo na tunatengana naye kwa sababu ya udhaifu wetu wa kimwili. Tumuombe Mwenyezi Mungu atujalie neema na nguvu ya kutimiza haya yote. Yaani, “kujitoa kufa kama ngano ili kuzaa matunda” kwa kuwa waaminifu kwa Agano letu na Mungu, kushika ahadi za Ubatizo, kutimiza mapenzi ya Mungu kwa moyo laini na mnyenyekevu, kuishi maisha ya fadhila na kuzielekeza nafsi zetu katika mabadiliko ya kweli. Hapo tutaunda jamii mpya ya amani, ustawi, umoja, usawa na mshikamano kwa njia ya Kristo Bwana wetu. tutiwe nguvu ya kuushinda udhaifu wetu wa kimwili kwa kusali, kufunga na kuwasaidia wasiojiweza kwa sadaka na majitoleo yetu.

Liturujia D5 Kwaresima
15 March 2024, 11:13