Tafuta

Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso yake, mateso ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso yake, mateso ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa mateso, kifo na ufufuko wake.  (Vatican Media)

Dominika ya Matawi: Mwanzo wa Juma Kuu: Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa

Dominika ya Matawi: Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso yake ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Kwa dominika hii Kanisa linaingia katika Juma Kuu. Linaitwa Juma Kuu kwa sababu ndani yake yanatendeka mafumbo ya wokovu wetu ambayo ni makubwa kuliko mafumbo mengine yoyote tunayoadhimisha kwa mwaka mzima wa Kiliturujia, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko uletao uzima wa milele.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi, mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa. Dominika hii tunaadhimisha dominika ya Matawi. Tunaadhimisha tukio la Yesu kuingia Yerusalemu ili kuyakabili mateso yake, mateso ambayo yameuletea ulimwengu ukombozi kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Kwa dominika hii Kanisa linaingia katika Juma Kuu. Linaitwa Juma Kuu kwa sababu ndani yake yanatendeka mafumbo ya wokovu wetu ambayo ni makubwa kuliko mafumbo mengine yoyote tunayoadhimisha kwa mwaka mzima wa Kiliturujia, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko uletao uzima wa milele. Dominika hii ina hali kuu mbili - furaha na huzuni. Hali ya furaha tunaionja katika sehemu ya kwanza ya ibada ya siku hii tunapoadhimisha kumbukumbu ya Yesu kuingia kwa shangwe Yerusalemu. Watu waliomlaki walikuwa na matawi ya mitende mikononi wakiimba nyimbo za furaha wakisema: “Hosana, mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli: Hosana juu mbinguni (Mt. 21:9). Mama Kanisa anatualika kufanya maandamano ya amani kwa shangwe na furaha tukiwa na matawi mikononi, ishara ya kuingia Yerusalemu mpya yaani mbinguni. Ndiyo maana sala ya kuyabariki matawi yanayotumika inasema hivi: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, uyatakase matawi haya kwa baraka yako. Nasi tunaomfuata Kristo Mfalme kwa shangwe, utujalie tufike Yerusalemu ya milele kwa jina lake”. Baada ya sala hii, matawi hunyunyiziwa maji ya baraka wakati huo watu wakiwa kimya wakitafakari matendo makuu ya Mungu.

Dominika ya Matawi, Mwanzo wa Juma kuu
Dominika ya Matawi, Mwanzo wa Juma kuu

Kabla ya kuanza maandamano, Injili inayosimulia Yesu kuingia kwa shangwe la Kimasiha Yerusalemu, inasomwa. Katika mwaka B wa kiliturujia, inasomwa Injili ya Marko 11:1-10 au Yohane 12:12-16. Baada ya injili kusomwa, yanafuata mahubiri mafupi. Baada ya mahubiri, maandamano yanayopambwa kwa nyimbo za shangwe na furaha za kumsifu Mungu kwa matendo makuu aliyotundea kwa njia ya Yesu Kristo, yanaanza kuelekea kanisani. Katika maandamano haya mtumishi wa chetezo hutangulia mbele akiwa amechukua chetezo chenye kufuka moshi. Nyuma yake anafuata mtumishi mwenye kuchukua msalaba uliopambwa, kati ya watumishi wawili wenye kuchukua mishumaa inayowaka. Kisha anafuata Padre na watumishi wengine, na mwisho wanakuja waamini, wote wakiwa na matawi wakiimba kwa shangwe. Yesu anatuonya kuwa tusipoimba kwa shangwe na kushangilia kwa furaha au tukinyamaza, “mawe yatapiga kelele.” Sehemu ya pili ya ibada ya siku hii ni kukumbuka Mateso ya Yesu Kristo yanayotuingiza katika Jumaa Kuu la kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, ndiyo Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Ndiyo maana Mama Kanisa hachoki kutueleza mapato ya mateso ya Yesu; ushindi dhidi ya dhambi na mauti, unaodhihirishwa na utukufu wa ufufuko. Ndivyo sala ya mwanzo inavyoweka wazi ukweli huu ikisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulitaka Mwokozi wetu atwae mwili na kuteswa msalabani ili wanadamu wapate kufuata mfano wa unyenyekevu wake. Utujalie kwa wema wako tuweze kuwa na uvumilivu kama yeye, na kustahili kuishi mateso ya Yesu Kristo ambayo tunaweza kuyafahamu vizuri tu, tukiyatazama pamoja na ufufuko wake.” Hivyo liturujia ya adhimisho hili imejaa mwanga wa Pasaka ikitudhihirishia kuwa Kristo si mshindwa bali ni mshindi.

Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana
Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 50:4-7). Somo hili linatupa nafasi ya kunatafakari utabiri wa Mtumishi wa Mungu aliye mwaminifu katika kazi yake. Yeye haogopi mateso, bali anayakabili. Kwa uaminifu wake, Mungu alimpa uwezo ili aweze kuwafundisha na kuwapa matumaini waliovunjika moyo. Kwa usikivu wake, Mungu alimwamsha asubuhi baada ya asubuhi, alizibua sikio lake apate kusikia Neno lake, alimpa nguvu na uvumilivu dhidi ya watesi wake. Mtumishi huyu, hakuficha uso wake asipate fedheha na kutemewa mate. Bali aliwatolea watesi wake mgongo wake walipomchapa mijeledi na walipomng’oa ndevu mashavuni mwake, hakuficha uso wake. Kwa matumaini alimlilia Mungu amuokoea kama wimbo wa katikati unavyoimba; “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Wote wanionao hunicheka sana. Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao; Husema: Alimtegemea Bwana na amponye; Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Kwa maana mbwa wamenizunguka; kusanyiko la waovu wamenisonga; wamenizua mikono na miguu, naweza kuihesabu mifupa yangu yote. Wanagawanya nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura. Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, katikati ya kusanyiko nitakusifu. Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni. Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni (Zab. 22:7-8; 16-17a; 18-19; 22-20). Nasi tukiwa katika taabu na mahangaiko, tuweke matumaini yetu yote kwa Mungu hakimu mwenye haki.

Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.
Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Flp 2:6-11). Katika somo hili tunaona na kuonja matunda ya utii, unyenyekevu na uvumilivu wa Yesu Kristo, mtumishi mwaminifu wa Mungu. Itakumbukwa kuwa dhambi na mauti viliingia katika historia ya mwanadamu kwa kosa la mwanadamu kukosa utii kwa Mungu. Kwa utii wa Kristo, dhambi na mauti vimeangamizwa. Kwa kutotii kwa Adamu na Eva tulitengwa na Mungu, kwa kutii kwake Kristo tumeunganishwa na Mungu. Nasi tunapaswa kutii amri za Mungu na za Kanisa. Kutii mafundisho ya Kanisa, kuwatii na kuwasikiliza viongozi wa Kanisa kwani; asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Tukubali kutii kuwa sisi kwa asili tu binadamu, lakini tusiung’ang’anie kwa nguvu ubinadamu wetu, bali tuuachilie, tujitwalie hali ya kimungu ili tukaishi milele yote mbinguni na Mungu Baba yetu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk 14:1-15:47). Nayo inasimulia mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, ndiyo kiini cha sehemu ya pili ya maadhimisho ya siku hii. Kawaida siku ya Dominika ya Matawi na Ijumaa kuu, injili inasomwa pasipo mishumaa wala chetezo na bila utangulizi wala ishara ya msalaba. Injili husomwa na shemasi baada ya kuomba na kupokea baraka ya Askofu au Padre. Na kama hakuna shemasi, husomwa na Padre. Lakini pia ili kuipanda liturujia ya siku hii, injili huweza kusomwa na walei kwa kuimbwa. Muhimu na kuzingatia, sehemu ya Kristo, lazima isomwe au kuimbwa na Padre. Bwana wetu Yesu Kristo, alikamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali. Tukumbuke daima kusali katika maisha yetu ya kila siku. Bila kosa alihukumiwa kifo kama utangulizi wa siku hii unavyokiri; “Kristo Bwana wetu, Yeye, ingawa hakuwa na kosa, alikubali kuteswa na kuhukumiwa pasipo haki kwa ajili ya wakosefu”. Alibebeshwa msalaba kuelekea Golgota kusulubiwa. Ni safari ya mateso makali; Alifanyiwa dhihaka, alivuliwa nguo, akatemewa mate na kutukanwa, akavika taji ya miiba na kupigwa mijeledi. Mwisho alisulubiwa na hatimaye kufa kifo cha aibu msalabani ili sisi tupate wokovu. Ndiyo Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea hivi; “Ee Bwana, utujalie rehema yako kwa ajili ya mateso ya Mwanao wa Pekee. Basi ingawa hatustahili kitu kwa matendo yetu, tuipate rehema yako kwa ajili ya sadaka hii kubwa”. Nayo sala ya utangulizi inatilia mkazo kusema; “Amefuta dhambi zetu kwa kifo chake na kutufanya wenye haki kwa ufufuko wake.”

Dominika ya Matawi: Matawi ya Mitendo kielelezo cha ushindi
Dominika ya Matawi: Matawi ya Mitendo kielelezo cha ushindi

Ni kweli maana kifo chake kilikuwa cha pekee sana; dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili. Nao walioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema; hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Askari alipomchoma ubavu kwa mkuki, ilitoka damu na maji, chemichemi za Sakramenti za Kanisa. Hii inatufunulia ukweli kuwa, hakuna utukufu pasipo mateso, wala Pasaka bila Ijumaa kuu. Ndiyo maana Mama Kanisa anatuhimiza kuvumilia mateso tuyapatayo katika kuikiri na kuishuhudia imani yetu, kwani yanatustahilisha kuingia katika ufalme wa mbinguni kama tukiyapokea kwa imani na bila manung`uniko. Lakini, mateso yatokanayo na dhambi zetu wenyewe au kwa kutokutimiza nyajibu zetu, hayatuletei wokovu. Bali yatatupeleka kwenye moto wa milele, tusiyapokiri, kuyangama na kuamua kuyaacha na kutoyarudia. Katika simulizi la mateso ya Yesu, umati wa watu walipiga makelele wakisema: Asulubishwe! Asulubishwe! Nasi kwa mawazo, maneno na matendo yetu maovu, tunatoa mlio na makelele hayo hayo: Msulubishe! Msulubishe! Petro alijaribu kupambana na ubaya kwa upanga. Je, sisi hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za giza kwa ubanga wa giza; maseng’enyo, malumbano, mapigano, visasi na fitina? Huku ndiko kusema katika makundi ya watu; Msulubishe! Msulubishe! Mwondoshe! Mwondoshe! Tukumbuke kuwa Kristo alipambana na kumshinda shetani si kwa upanga wala vitisho. Bali kwa uvumilivu wake, kwa unyenyekevu wake, kwa upole wake na kwa utii wake kwa Mungu Baba. Nasi hatupaswi kumpigania Kristo kwa upanga, bali kwa ushuhuda wa maneno na matendo mema. Hata tunaposikia; Hatumjui mtu huyu! Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Msulubishe! Tusikate tamaa au kukwazika na kurudi nyuma. Bali tuweke tumaini letu lote kwa Mungu. Katika Juma Kuu tunalolianza, tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii, tujipatanishe na Mungu ili tuweze kufurahia siku ya Pasaka tukingojea kwa matumaini kuifikia Pasaka ya milele Mbinguni kama anavyotuombea Mama Kanisa katika sala baada ya komunyo akisema; “Ee Bwana, sisi tulioshiba mapaji yako matakatifu umetupa tumaini la kupata hayo tunayoamini kwa ajili ya kifo cha Mwanao. Tunakusihi, hapo atakapofufuka utufikishe huko tuendako”. Hili ndilo tumaini letu kuu na hii ndiyo hamu yetu, kufika mbinguni.

Dominika ya Matawi

 

20 March 2024, 11:38