Tafuta

Kuwa mwanamke na kusherehekea siku ya wanawake duniani ni ungamo la imani awali ya yote kwa Mungu aliye Muumbaji,ambaye kwake sote tumefanyika na kuitwa kike au wa kiume! Kuwa mwanamke na kusherehekea siku ya wanawake duniani ni ungamo la imani awali ya yote kwa Mungu aliye Muumbaji,ambaye kwake sote tumefanyika na kuitwa kike au wa kiume! 

Siku ya Wanawake2024:Mwanamke ni mpango na mapenzi ya Mungu!Mwanamke sio ajali!

Leo ni Siku ya Wanawake duniani.Wito wetu wa kwanza na wa awali ni kuwa wanadamu!Ni kuwa vkadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu kwetu!Ndicho wanachokiadhimisha wanawake leo hii duniani kote!Ni tafakari ya Padre Mkude katika fursa ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani 2024 akichambua mwanadamu kama Imago Dei.

Padre Mkude Gaston na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake  tarehe 8 Machi 2024 inayoongozwa na kauli mbiu: “Wekeza katika wanawake. Kuharakisha maendeleo ya kijamii”, Umoja wa Mataifa unataka kuakisi mwaka huu juu ya utambuzi wa mafanikio ya wanawake, bila kujali utaifa, kabila, dini, utamaduni, lugha, hali ya kiuchumi au mwelekeo wa kisiasa. Lakini pia mbali na hiyo inawezekana kujikita na sehemu nyingine ya tafakari kama ambayo inaletwa na Padre Gastone Mkude. Katika makala hii, Padre Mkude anapenda kujikita juu ya “Ungamo la imani.” Je ni nini anataka kutueleza?

Wanawake Duniani wanaungana kadhimisha siku ya wanawake duniani
Wanawake Duniani wanaungana kadhimisha siku ya wanawake duniani

Kwanza naomba tuungane sote kuwatakia kila lenye heri na baraka tele kutoka kwa Maulana Muumbaji wa ulimwengu mzima! Ni leo wanawake wanaungama kwa kukiri jinsi na vile Muumba amewafinyanga kwa namna ya ajabu na kuwaita kwa kuwafanya kuwa wanawake! Kuwa vile na jinsi ya ajabu kama wanawake! Kuwa mwanamke kama vile kuwa mwanaume ni wito wa Muumba kwa mwanadamu na viumbe vingine vyote!  Ni wito wa Mungu kwa mwanadamu! Kuwa mwanamke na kusherehekea siku hii ya wanawake duniani ni ungamo la imani awali ya yote! Sio ungamo la dini, kwani leo nisingependa tuzungumzie dini bali ni imani, narudia ni ungamo la imani kwa Mungu aliye Muumbaji, ambaye kwake sote tumefanyika na kuitwa kuwa aidha wa kike au wa kiume!

Kwa kila anayeamini katika Mungu, la kwanza linalotujia hata katika misaafu yetu ni kuwa sisi ni viumbe, hatujajiumba kwani tunaamini tumetoka kwake Maulana , aliye Muumbaji wetu sote! Leo wanawake ulimwenguni kote wanakiri imani, wanakiri na kuona fahari sio vile wanavyotaka au kupenda au uchaguzi wao bali wanaona fahari jinsi Mungu alivyowatunuku na kuwaita kuwa jinsi vile walivyo, kuwa ni wanawake! Ndio ni fahari na furaha yao kwa jinsi vile Mungu amewaleta duniani kwa kuwafanya kuwa wanawake! Wito wetu wa kwanza na wa awali ni kuwa wanadamu! Ni kuwa vile kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu kwetu! Na ndicho hicho wanachokiadhimisha wanawake leo duniani kote!

Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke
Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke

Mwanamke na mwanaume aliwafanya! Aliwaumba, aliwafinyanga kwa jinsi na namna ya ajabu kabisa! Ni leo kila mwanamke anayejitambua anaona fahari kuwa vile Muumba wake alivyopanga tangu milele yote! Mwanamke ni mpango na mapenzi ya Mungu! Mwanamke sio ajali! Mwanamke ni sura na mfano wa Mungu! Mwanamke sio nusu mwanadamu, ni (waw) ya kutoka ubavu wa mwanaume! Ndiye kiumbe ambaye anapata (waw) ya Mungu aliye muumbaji, na mwanadamu yule wa kwanza yaani Adamu! Ni kiumbe ambaye mara baada ya uumbaji anaonekana kwa mshangao mbele ya Mungu na hata kwa mwanadamu mwenzake, yaani Adamu! Ndio kadiri ya Maandiko anapata zile (waw) mbili!

Mwanamke ni wito wa pekee kutoka kwa Mungu, ndio anaitwa kuwa vile na jinsi ile ya Mungu mwenyewe! Mwanamke hivyo sio mwanadamu wa daraja la pili au duni kamwe, kwani Mungu ametuumba sisi sote kuwa sawa kwani sote tunabeba sura na mfano wa Muumba wetu (Imago Dei). Mbele ya Mungu sisi sote ni wana na watoto wake wapendwa sana tena sana! Kila mmoja wetu ni mpango na mapenzi ya Muumba wetu! Kila mwanamke ni wa thamani sawa kwani kila mmoja anabeba chapa ya Mungu! Kama vile pesa zinavyobeba chapa, basi mwanadamu akiwemo mwanamke anabeba chapa ile ya sura na mfano wa Mungu. Mwanamke ni (Imago Dei!). Ni sura na mfano wa Mungu, aliyeumbwa kwa namna na jinsi ya ajabu! Mwanamke ni wa thamani sio tu machoni mwa Mungu bali hata mbele ya uumbaji mzima! Ni mwanamke pekee anayepokea (waw) zile mbili!

Siku ya wanawake duniani 2024
Siku ya wanawake duniani 2024

Kwa nini nasema haya yote? Ni nini kimenifanya leo niamke na yote haya? Labda kwa wengine ni upotezaji tu wa muda! Yawezekana kabisa kwani kila mmoja anaweza kuona jinsi vile anavyotaka na kuweza kuuona ulimwengu wetu wa leo! Tunaishi nyakati zenye mitazamo ya kifalsafa ya aina na namna nyingi kabisa! Lakini kama ilivyokuwa kwa mwanadamu yule wa mwanzo, dhambi na kosa lile la mwanzo ndilo lile lile tunalolitenda hata katika nyakati zetu za leo! Niniarudia kuwa mwanamke au kuwa mwanaume ni ungamo la imani! Ni kukubali kuwa sisi sote ni viumbe, hivyo tunatoka kwa Muumba wetu, yaani Mungu mwenyewe. Kukiri jinsia ni kukiri kuwa tu viumbe kwa namna na jinsi ya Mungu, hivyo hatujajiumba na jinsia zetu sio maamuzi yetu bali ni mapenzi ya Mungu kwetu, ni mpango na mapenzi ya Muumba wetu wa milele yote! Mmoja amefanyika kuwa mwanamke au mwanaume, sio kwa matashi na uchaguzi wetu bali ni mapenzi ya Mungu!

Hatutaki au tuna mashaka katika mapenzi ya Mungu kuwa vile tulivyo? Labda tuna wasiwasi na kutofurahishwa na jinsi vile Mungu ametuumba? Yawezekana tukawa na maswali mengi vichwani na akilini mwetu! Kwa kila mwenye imani, kwa kila anayemkiri Mungu kuwa ni Muumbaji wa ulimwengu mzima! Hakika huyo anakiri kuwa mapenzi ya Mungu kwetu ni mema na mazuri, kwani kila alichoumba Mungu amekiona kuwa ni kizuri na chema sana machoni pake! Kutaka au kupendelea kuwa vinginevyo ni kumkosoa Mungu kama Muumbaji wetu, ni kutaka kuchukua nafasi ya Muumbaji kwani ni kutaka kujiumba sisi wenyewe! Ni kosa lile lile la mwanadamu wa kwanza. Ni mwanadamu anataka kupora nafasi ya Muumbaji wake. Ni mwanadamu anataka kujiumba yeye mwenyewe kwa namna na jinsi yake!

Siku ya wanawake duniani
Siku ya wanawake duniani

Na ndio  inaitwa (gender ideology) yaani Itikadi ya kijinsia  inayoimbwa na kupigiwa upatu katika ulimwengu wa leo! Ndio sera ya kumpinga Mungu, ya kutokumkiri Mungu kama Muumbaji wetu aliyetuumba sisi sote kwa namna na jinsi ya ajabu kabisa. Ndio tunaishi nyakati za mwanadamu kutaka kuwa Mungu, kutaka kuwa Muumbaji, kutaka kuwa vile anataka kuwa! Ni nyakati za usaliti na uasi mkuu! Ndio kutaka kuwa na kuenenda sio tena kadiri ya Uumbaji wa Mungu bali kwa kutaka kujiumba sisi wenyewe kadiri ya mapenzi na matashi yetu wanadamu! Ni nyakati za kutaka kuwa na jinsia tunazoamua sisi, kwa kuwa mwanadamu anataka kuwa mungu wa _small letter m_ ! Ni nyakati kengefu! Ni mwanadamu amekengeuka, kwani hataki tena kuwa kiumbe mbele ya Muumba wake!

Sikukuu ya wanawake duniani ni ungamo la imani kwa Mungu aliye Muumbaji wa kila mwanadamu, lakini hasa leo wanawake wanaona fahari na kuutangazia ulimwengu mzima ukweli huu wa imani kuu (Kerygma). Leo wanawake wanabeba bango la tangazo kuu la Uumbaji wa Mungu kwa jinsi na namna ile ya ajabu kabisa walivyo! Ni tangazo la wao kuona fahari uumbaji wa Mungu kuwa wameumbwa na kuitwa kuwa wanawake! Uanamke ni uuumbaji wenye wito nyuma yake! Mwanamke ameumbwa kuwa mwanamke na ndani mwake amebeba hazina na lulu ya thamani kuu kadiri ya mapenzi yake Muumbaji wetu!

Tuwapongeze Wanawake
Tuwapongeze Wanawake

Tuungane na wanawake wote duniani leo kuwatakia kila jema na baraka la kuona fahari na kuwa vile Muumbaji wetu amewafanya na kuwaita kuwa! Kuwa mwanamke ni uumbaji, ni wito wa Muumba wetu! Mwanamke sio mwanadamu wa daraja la pili bali ni namna na jinsi ya Mungu katika kukamilisha utukufu wa uumbaji wake! Siku takatifu na njema kwa kila mwanamke anayekiri kuwa yeye ni kiumbe kwa namna na jinsi ya Mungu mwenyewe aliye Muumbaji wa ulimwengu mzima.

Siku ya Wanawake duniani:Mpango wa Mungu kwa Mwanadamu ni upi?
08 March 2024, 15:54