Tafuta

Migogoro nchini Msumbiji: zaidi ya watoto 60,000 wamekimbia wimbi jipya la vurugu katika majimbo ya eneo la Cabo Delgado. Migogoro nchini Msumbiji: zaidi ya watoto 60,000 wamekimbia wimbi jipya la vurugu katika majimbo ya eneo la Cabo Delgado.  (AFP or licensors)

Msumbiji:zaidi ya watoto 61,000 wanalazimika kuacha makazi yao huko Cabo Delgado

Shirika la Save the Children linasema zaidi ya watoto 61,000 wanalazimika kuacha makazi yaohuko Cabo Delgado kutokana na mashambulizi mapya.huo ni uhamisho mkubwa zaidi katika miezi 18 iliyopita.Shirika linatoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa mzozo huu ili watoto waweze kuishi maisha ya amani na kurejea shuleni.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, zaidi ya watoto 61,000 wamekimbia wimbi jipya la vurugu katika Mkoa wa Cabo Delgado nchini Msumbiji. Kama ilivyoripotiwa na Shirika la kimataifa la Save the Children ambalo limekuwa likipambania kuokoa wasichana na wavulana na kuwahakikishia maisha ya baadaye kwa zaidi ya miaka 100, katika taarifa yao tarehe 6 Machi 2024 inabainisha kwamba hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya watoto waliolazimishwa kuacha nyumba zao kwa muda mfupi kama huo. Mapigano mengi makali kati ya makundi yenye silaha na vikosi vya usalama yameripotiwa katika wilaya za Macomia, Chiure, Mecufi, Metuge, Mocímboa da Praia, Quissanga, Muidumbe na Ibo na ghasia za mara kwa mara katika mkoa wa kaskazini na kusababisha zaidi ya watu 99,313 kuhama makazi yao, watoto 61,492 ambao wamekimbia makazi yao kati ya  tarehe 22 Desemba2023  na 3 Machi 2014.

Kila siku ni kufungasha na kukimbia nchini Msumbiji
Kila siku ni kufungasha na kukimbia nchini Msumbiji

Mzozo wa Cabo Delgado, ambao sasa ni mwaka wa saba usio na mwisho, umekuwa na athari mbaya kwa maisha ya wanadamu. Kuna ripoti zinazoendelea kutolewa kuhusu kukatwa vichwa na utekaji nyara, huku watoto wengi wakiwa miongoni mwa waathiriwa. Hadi sasa, mapigano hayo tayari yamewafanya watu 540,000 kuyahama makazi yao, ambapo zaidi ya nusu yao ni watoto wadogo. Kuongezeka kwa ghasia hizo kunakuja baada ya kipindi cha utulivu kidogo huku mashambulizi yakikithiri katika baadhi ya maeneo katika sehemu ya kaskazini ya mkoa huo. Katika mwaka 2023 karibu watu 600,000 wamerejea hatua kwa hatua katika vitongoji vyao vya asili katika jaribio la kurejesha maisha ya kawaida, ingawa kutokana na ghasia za mara kwa mara, baadhi ya watu waliohama makazi yao wameendelea kutokea katika baadhi ya wilaya hizi.

Kuna haja ya kuchukua hatua za haraka kuzuia hali mbaya

Katika wilaya ya Chiúre, mashambulizi ya hivi karibuni huko Mazeze na Ocua,  ambayo hadi hivi karibuni yalikuwa kimbilio salama kwa watu waliokimbia makazi yao  yamechomwa moto kadhaa,  nyumba, soko, kituo cha afya na kanisa. Uharibifu wa miundombinu ya kiraia na ya umma unatishia kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana katika kuhamisha watoto na familia zao kwenye nyumba na shule. Kutokana na hali hii mbaya, Shirika la Save the Children linatoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuwalinda watoto na kuakisi kwamba wimbi hili la ukatili ni shambulio jipya dhidi ya elimu kwani huko Cabo Delgado, zaidi ya shule 100 zilifungwa katika wilaya 6, zikiwemo shule nyingine 17 za Nampula, na kuathiri takriban wasichana 71,000 na wavulana.

Watu wengin wanaishi katika makambi ya wakimbizi huko Cabo Delgado
Watu wengin wanaishi katika makambi ya wakimbizi huko Cabo Delgado

“Kuna watoto ambao sasa wana umri wa miaka saba na wangependa kwenda shule kwa mara ya kwanza mwaka huu 2024  lakini wanakimbia kuokoa maisha yao. Watoto hawa hawajawahi kujua maisha bila vita na kwa bahati mbaya ni wa kizazi kinachokua cha watoto ambao utoto wao unapotea kutoka mikononi mwao." Alisema hayo Brechtje van Lith, Mkurugenzi wa Save the Children nchini Msumbiji. “Wimbi la hivi majuzi la mapigano na mashambulizi linawakilisha kurudi nyuma kwa juhudi za kujenga upya maisha ya watoto na familia huko Cabo Delgado. Tunataka kukomeshwa mara moja kwa mzozo huu ili watoto waweze kuishi maisha kwa amani na kurudi shuleni.” Alihitimisha Brechtje van Lith.

Huduma isiyoisha ya Save the Children - Okoa Watoto

Save the Children na washirika wake wanawaweka watoto wadogo katika shule katika jumuiya zinazowapokea, huku wakihakikisha usambazaji wa vifaa vya shule kwa wanafunzi na walimu. Katika baadhi ya jumuiya, mahema yameanzishwa ili kuunda nafasi za muda wa kujifunza. Shirika hutoa huduma za usaidizi wa kisaikolojia na kijamii kwa watoto na walezi wao na hutambua watoto ambao hawajazindikizwa na waliotenganishwa kwa ajili ya utafutaji wa familia na kuunganishwa tena. Huko Cabo Delgado, Shirika na waendeshaji wengi, hata hivyo, wanajikuta wakikabiliwa na matatizo makubwa katika kupata ufadhili wa kutosha ili kukabiliana na mahitaji yaliyopo ya kibinadamu. Shirika la Save the Children ni mojawapo ya mashirika makuu yaliyojitolea kushughulikia mgogoro wa Cabo Delgado na mwaka 2023 tayari umefikia watu 381,773, ikiwa ni pamoja na karibu watoto 259,676. Wakimbizi wa ndani, jumuiya zinazowapokea na familia zimesaidiwa kwa misaada na bidhaa za kuokoa maisha, kuhakikisha watoto na familia zao wanapata ulinzi, elimu, afya, lishe, njia za kujikimu, maji, usafi wa mazingira na usafi, pamoja na mipango ya kibinadamu na kujenga amani. Shirika la Save the Children linatekeleza afua katika wilaya za Pemba, Metuge, Chiure, Montepuez, Mueda na Palma, Macomia, Quissanga na Mocímboa ya Praia.

Kampeni ya “Ungeokoa Nini?”

Watoto waliokimbia makazi wa Capo Delgado ni sehemu ya watoto zaidi ya milioni 50 waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na sababu mbalimbali, kuanzia mabadiliko ya tabianchi hadi mafuriko, ukame na, zaidi ya yote, kutokana na migogoro ni idadi ya juu zaidi katika historia. Shirika la Save the Children hufanya kazi kila siku ili kuwapa wasichana na wavulana wanaopata hali hii, hasa kutokana na migogoro, usaidizi wa haraka na wa muda mrefu. Ndiyo maana lilianzisha kampeni yenye kichwa: “Ungeokoa nini?” Inahitajika kuzingatia matokeo makubwa ya vita dhidi ya watoto wadogo na kualika kutafakari juu ya changamoto zinazowapata watoto wanaotoka katika maeneo yenye migogoro. Watoto katika nchi zilizo kwenye vita hupoteza kila kitu: wanasesere wao, nyumba zao, jamii zao, usalama wao. Ulimwengu wao wote. Pamoja na kampeni ya “Ungeokoa nini?”, Save the Children inaalika kila mtu kujibu swali hili: “Ungeokoa nini ikiwa ungelazimishwa kuacha nyumba yako kwa sababu ya vita?” Lakini vita vinapozuka kuna mengi zaidi ambayo haiwezekani kuokoa: usalama, mapato, mahali pa kucheza, kucheka na kujifunza, mtu wa kupigania haki za wale waliolazimika kukimbia. Kuwalinda na kuhakikisha wana kila kitu wanachohitaji ndiyo asili katika utume wa Shirika la Save the Children- Saidia  watoto.

06 March 2024, 12:00