Tafuta

Kesha yaPasaka ni usiku Mtakatifu, uliopamba kwa nuru na mwanga wa mshumaa ambao sifa zake zinatangazwa katika kupigwa kwa Mbiu ya Pasaka. Kesha yaPasaka ni usiku Mtakatifu, uliopamba kwa nuru na mwanga wa mshumaa ambao sifa zake zinatangazwa katika kupigwa kwa Mbiu ya Pasaka.  (Vatican Media)

Jumamosi Kuu Mkesha wa Pasaka: Mama Wa Mikesha Yote ya Kanisa

Ni mkesha wa usiku mtakatifu, Mama Kanisa na wanae anapoadhimisha kilele cha fumbo la ukombozi wetu – ufufuko wa Yesu Kristo. Ni usiku ule inapopigwa mbiu ya Pasaka, kutujulisha ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Ni usiku ule ambapo Kristo Yesu alikata minyororo ya mauti, akatoka kuzimu ameshinda mauti. Kanisa halichoki kutueleza maana ya usiku huu kwamba ni usiku wa kutoka katika hali ya upotevu na kuingia katika hali ya uzima wa Kimungu. Kesha Kuu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu mkesha wa Pasaka. Ni mkesha wa usiku mtakatifu, Mama Kanisa na wanae anapoadhimisha kilele cha fumbo la ukombozi wetu – ufufuko wa Yesu Kristo. Ni usiku ule inapopigwa mbiu ya Pasaka, kutujulisha ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Ni usiku ule ambapo Kristo Yesu alikata minyororo ya mauti, akatoka kuzimu ameshinda mauti. Kanisa halichoki kutueleza maana ya usiku huu kwamba ni usiku wa kutoka katika hali ya upotevu na kuingia katika hali ya uzima wa Kimungu. Sisi tuliokufa katika dhambi, tunafufuka katika Kristo pamoja naye. Hivyo, Kanisa linatualika wanawe, tukeshe na kusali pamoja, ili kuadhimisha Pasaka ya Bwana kwa kusikiliza neno lake na kuyatukuza mafumbo yake, kwa tumaini la kushiriki naye shangwe milele yote mbinguni. Maadhimisho ya Mkesha huu yamegawanyika katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ni Liturujia ya Mwanga inayopambwa kwa kuwashwa mshumaa wa Pasaka na kupigwa kwa mbiu ya Pasaka, tukiyakumbuka na kuyatafakari maajabu Mungu aliyolitendea taifa lake teule tangu mwanzo. Pili ni Liturujia ya neno yenye masomo tisa yanayosimulizia historia ya mwanadamu tangu kuumbwa kwa ulimwengu mpaka ukombozi wake kwa njia ya Yesu Kristo. Tatu ni adhimisho la Sakramenti ya ubatizo wa wakatekumeni, ishara ya ukamilifu wa Agano jipya na la milele. Na nne Kanisa pamoja na wanachama wapya waliozaliwa katika vijilia hii linakula kwa furaha chakula alicholiandalia Bwana taifa lake kwa kufa na kufufuka kwake, ndiyo kuumega mkate, Ekaristi Takatifu. Katika liturujia ya Neno katika kesha hili ambalo ni Mama wa mikesha yote, Mama Kanisa ametuwekea masomo kenda ili kutafakari kwa kina fumbo la ukombozi wetu; saba ya Agano la Kale na mawili ya Agano Jipya (Waraka na Injili). Baada ya kupigwa mbiu takatifu, Padre anawaalika waamini kulisikiliza Neno la Mungu kwa makini ili kulijua vyema fumbo la ukombozi wetu tangu matayarisho yake katika Agano la kale na utimilifu wake katika Agano jipya na la milele akisema; “Tumeingia katika kesha la Pasaka, sasa tusikilize neno la Mungu kwa moyo mtulivu. Tuwaze jinsi Mungu alivyolikomboa taifa lake wakati ulipowadia, na mwishowe akamtuma kwetu Mwanawe awe Mkombozi. Tumwombe Mungu wetu aifanikishe hii kazi ya wokovu wakati huu wa Pasaka, ili nasi tupate ukombozi kamili”. Masomo haya ni ya kusikiliza kwa makini, ili kulitambua na kuliishi vyema fumbo hili la ukombozi wetu.

Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka
Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka

Somo la kwanza la kitabu cha mwanzo (Mw.1:1-2:2) ni simulizi la uumbaji. Somo hili linatufundisha kuwa asili na chanzo cha mwanadamu ni Mungu katika Utatu Mtakatifu. Katika viumbe vyote vilivyoumbwa (Mw.1-2), ni mwanadamu peke yake ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mw.1:26-27) ili amjue, ampende, amtumikie na mwisho afike kwake mbinguni. Mungu kabla ya kumuumba mwanadamu aliviumba vitu vingine vyote (Mw1:1-25) kama maandalizi ya mazingira ya kuishi mwanadamu. Baada ya kumwumba mwanadamu alimkabidhi vyote ili avitiishe na kuvitawala (Mw. 1:28), akampa na ruhusa ya kuvitumia vyote (Mw.1:29-30) na kula matunda ya miti yote (Mw. 2:16). Lakini kwa sharti moja tu, asile matunda ya mti wa katikati (Mw. 2:17). Maana yake jukumu la lipi ni jema na lipi ni baya sio jukumu lake mwanadamu bali la Mungu. Lakini ikawa ni kinyume chake. Mwanadamu alikaidi maagizo ya Mungu, akataka kuwa sawa na Mungu, akaamua lipi liwe jema na lipi liwe baya, akala alichokatazwa (Mw.3:6-7). Kwa kosa la kutotii amri na maagizo ya Mungu dhambi iliingia duniani. Mungu akawaadhibu kwa kosa lao la kutotii maagizo yake (Mw. 3:14-19). Baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva kukaidi maagizo na amri za Mungu, walipoteza neema ya utakaso, sura na mfano wa Mungu ndani mwao na mahusiano mazuri na Mungu yakatoweka kwasababu ya kiburi na ukaidi. Ndipo taabu, mahangaiko na mateso yakamwandama mwanadamu kwa kujitenga kwake na Muumba wake. Maana walichokipoteza Adamu na Eva kilipotea kwa binadamu wote kwani ubinadamu wote ulikuwa tayari kwao. Lakini Mungu kwa upendo wake na kwa huruma yake hakumwacha mwanadamu apotee na kuangamia kabisa. Kwa nyakati mbalimbali na tofauti, mara nyingi na kwa namna nyingi na njia mbalimbali, Mungu nyakati zote amefanya juhudi kubwa kumrudisha kwake mwanadamu aliyejitenga kwa ukaidi wake (Ebr.1:1-4).

Liturujia ya Mwanga
Liturujia ya Mwanga

Kwanza aliwaangamiza kwa gharika wakati wa Nuhu (Mw. 6:1-9:29). Baada ya gharika alimteua na kumwita Ibrahimu kuwa Baba wa Imani na kufanya naye Agano. Katika somo la pili la mkesha wa Pasaka Mungu anaijaribu imani ya Ibrahimu kwa kumtaka amtoe kafara mwanae Isaka (Mwa.22:1-18). Mungu akaliteua taifa la Israeli, si kwasababu ya ubora wake bali kwa mpango na makusudi yake akalifanya kuwa taifa teule litakalompokea Mwokozi wa ulimwengu. Kila walipokosea, aliwaadhibu kwa kuwapelekwa utumwani na walipotubu makosa yao, aliwasamehe na kuwarudisha katika nchi yao. Kwanza aliwapeleka utumwani Misri, akawatoa kwa mkono wa Musa kwa akawavusha bahari ya shamu (Kut. 14:15 –15:1). Ndilo somo la tatu la mkesha wa Pasaka. Akafanya nao Agano na kuwapa Amri kumi ziwe mwongozo wa maisha yao (Kut. 19:3-24:8). Ukaidi wa mwanadamu uliendelea. Mungu akawatuma waamuzi, wakaja pia wafalme na manabii wakati wa utumwa wa Babeli – somo 4 (Isaya 54:5-14), somo 5 (Isaya 55:1-11), somo 6 (Baruku 3:9-15, 32-4:4), na somo la 7 (Ezekieli 36:16-17a, 18-28). Nao walipotambua makosa yao, wakatubu, wakamlilia Mungu. Yeye aliwasamehe na kuwarudisha katika nchi yao kwa mkono wa mfalme Koreshi wa uajemi. Lakini hata hivyo, waliendelea kuwa na moyo mgumu kama binadamu wengine. Kwa ukaidi wao, waliwatenda jeuri waliotumwa na Mungu na wengine kuwaua kabisa. Nabii Isaya akatabiri ujio wa masiha, mtumishi wa Mungu, mwana pekee wa Mungu, mpatanishi wetu na Mungu. Aliyezaliwa na Bikira Maria muda ulipotimia.

Liturujia ya Neno la Mungu
Liturujia ya Neno la Mungu

Baadae Mungu alimtambulisha siku ya Ubatizo wake mtoni Yordani (Mk.1:9-10) na alipogeuka sura mlimani Tabor kuwa ndiye Mwanaye mpendwa tumsikilize Yeye (Mk.9:2-10). Huyu ndiye Kristo ambaye kwa dhambi zetu aliyeteswa mateso mengi, alimpigwa mijeledi (Yn. 19:1), akamvika taji ya miiba kichwani (Yn.19:2,5), akampigwa makofi (Yn. 19:3), akamtemea mate, akiwa amechoka kabisa yuko hoi, akambebeshwa msalaba mzito kwenda kusulibishwa (Yn19:17). Alipoanguka kwa udhaifu wa kimwili, alimpigwa bila huruma. Hatimaye akamtundika juu ya msalaba kwa kumpigilia misumari kama mhalifu katikati ya wahalifu (Yn. 19:18). Alipoona kiu alipewa siki badala ya maji (Yn. 19: 28-30). Alipokufa hawakuamini, wakaona haitoshi wakamtoboa ubavu wake kwa mkuki ikatoka damu na maji (Yn.19:34), ndizo chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. Kwa jina lake tumebatizwa, somo 8 la mkesha (Rm.6:3-11 -). Watu wema wakazimka (Yn 19:38-40), siku ya tatu akafufuka. Ili kuthibitisha ufufuko wake aliwatokea wengi katika wanafunzi wake (Yn. 20) akianza na wanawake (Lk 24:1-12 – Injili ya mkesha wa vijilia vya Pasaka). Hivi ndivyo lilivyo fumbo la ukombozi wetu kwa mhutasari. Ufufuko wa Yesu Kristo, ni ukweli kabisa wa imani yetu. Imani tunayoisadiki na kuiishi kama msingi wa jumuiya ya kwanza ya Kikristo. Ufufuko wa Yesu ni ishara ya matumaini, ni nguvu katika safari yetu ya maisha ya kiroho. Ufufuko wa Yesu Kristo ni uthibitisho mkubwa kabisa wa Umungu wake. Ufufuko wa Yesu Kristo ni utimilifu wa fumbo la wokovu wetu. Tumekombelewa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Kifo na ufufuko wake havitenganishwi, ingawa hayo ni matukio mawili ya kihistoria. Ni kwa ufufuko, safari ya kwenda mbinguni kwa Baba ilikamilika. Kumbe ufufuko ni ishara ya kupokelewa kwa sadaka ya Yesu Kristo na Mungu Baba.

Sakramenti ya Ubatizo
Sakramenti ya Ubatizo

Pasaka ni mabadiliko. Neno Pasaka asili yake ni lugha ya Kiebrania “Pesach, Passover” kwa Kiingereza, ikimaanisha kupita juu. Pasaka ni sikukuu kubwa katika liturujia ya mwaka ya wayahudi wakikumbuka Siku ambapo Malaika wa Bwana alipita juu ya nyumba zao alipowapiga wazaliwa wa kwanza wa Wamisri na kuwaua ili Farao awaachie wawe huru (Kut.12:1-30). Hii ndiyo siku ambapo waisraeli walitoka utumwani Misri wakaanza maisha mapya kama watu huru. Kwetu sisi Pasaka ni mabadiliko ya kiroho kutoka katika utumwa wa dhambi, utumwa wa shetani na kuwa watu huru. Ni Mabadiliko kutoka katika maisha ya zamani, kwenda maisha mapya. Basi tusibaki katika maisha ya zamani tubadilike, tuuvue utu wa kale na tuuvae utu mpya.  Kesha la Pasaka ni usiku Mtakatifu, uliopamba kwa nuru na mwanga wa Mshumaa wa Pasaka ambao sifa zake zinatangazwa katika kupigwa kwa mbiu. Mshumaa huu unakuwepo katikati yetu ukitumulika na kutuangazia nuru ya kweli ndiye Kristo mfufuka. Ni usiku wa kuutangazia ulimwengu kuwa Kristo amefufuka yu hai. Ni usiku wa kuepuka nafasi za dhambi. Ni usiku wa upendo. Ni usiku wa furaha na amani. Ni usiku wa kumcha Mungu. Ni usiku wa kwenda mbio kuutangazia ulimwengu kuwa Kristo amefufuka kweli kweli aleluya na tunaweza kumwona na kumtambua katika kuumega mkate chakula cha kiroho katika safari ya kuelekea mbinguni huko aliko Yeye Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Tumsifu Yesu Kristo!

Kesha la Pasaka
30 March 2024, 10:23