Tafuta

Katika Nchi ya Haiti kila mmoja anatafuta mahali pa kukimbilia . Katika Nchi ya Haiti kila mmoja anatafuta mahali pa kukimbilia . 

Haiti:Watawa Saba wa Jumuiya ya Madelaine na Ndugu wa Moyo Mtakatifu wameachiliwa

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Haiti watawa 7 wa Jumuiya mbali mbali za Haiti wameachiliwa huru.Dominika 10 Machi 2024,Papa alitoa wito kwa maombi ya wakazi wa Haiti."Ninafuatilia kwa wasiwasi na uchungu kuhusu mgogoro mkubwa unaoathiri Haiti na matukio ya vurugu ambayo yametokea katika siku za hivi karibuni.Niko karibu na Kanisa na watu wapendwa wa Haiti,ambao wamekuwa wakipitia mateso mengi kwa miaka mingi."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Watawa watatu wa Shirika la Mtakatifu Joseph wa Cluny waliotekwa nyara siku ya Jumanne tarehe 5 Machi 2024 kutoka katika kituo cha watoto yatima cha La Madeleine wameachiliwa huru. Kulingana na Baraza la Watawa la Haiti, kikundi cha majambazi wenye silaha walikuwa wamechukua mateka watawa kutoka Croix-des-Bouquets. Zaidi ya hayo, vyombo vya habari vya nchini humo viliripoti Dominika tarehe 10 Machi kwamba wanne 4 kati ya Watawa sita wa Shirika la Ndugu wa Moyo Mtakatifu waliachiliwa lakini hakuna habari yeyote  kutoka kwa Polisi wa Kitaifa wa Haiti (PNH). Watawa hao sita walitekwa nyara mnamo tarehe 23 Februari 2024 walipokuwa wakielekea katika utume wao wa shule ya Yohane wa XXIII huko Port auPrince, katika wilaya ya Bicentenaire. Mnamo tarehe 18 Februari iliyopita Askofu André Dumas, wa Anse-à-Veau Miragoâne, alijeruhiwa vibaya katika mlipuko huko Port au Prince. Hakuna genge lililodai kuhusika na shambulio hilo dhidi ya Askofu huyo, ambaye pia ni makamu wa rais wa Baraza la Maaskofu wa Haiti (CEH) na Polisi Kitaifa PNH haijafuatilia wahusika wake. Hivi sasa Askofu  Dumas alilazwa katika hospitali ya Florida na anaendelea kupata nafuu.

Matukio ya utekaji nyara yamekithiri

Mnamo Januari Askofu alijitoa kama mateka badala ya watawa sita wa Shirika la  Mtakatifu Anne, waliotekwa nyara huko Port-au-Prince, ambao Papa Francisko pia alitoa ombi lake la kuachiliwa kwao. Makamu wa rais wa CEH amekuwa akikosoa na kupambana dhidi ya magenge ya wahalifu yanayofanya kazi nchini Haiti, hasa dhidi ya uhalifu wa utekaji nyara, ambao aliufafanua kuwa tabia isiyo ya kibinadamu na ya kudharauliwa. Vile vile mwito mkali  pia kwa tabaka la kisiasa la Haiti ambalo anauliza kila mara kuachana na ubinafsi ili kuondokana na mzozo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii ambao unaikumba nchi ya Kisiwa Kikubwa cha Carribien.

Wito wa Papa Francisko kwa ajili ya Haiti

Hivi karibuni Askofu  Dumas alikuwa ametoa wito wa mabadiliko ya amani ya mamlaka, kwamba jamii imezimwa na hofu na hii ni ishara ya kushindwa.  Na katika sala ya Malaika wa Bwana Tarehe 10 Machi 2024, Papa Francisko, akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume mara baada ya tafakari miongoni mwa miito yake kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, alitoa wito kwa maombi kwa ajili ya wakazi wa Haiti. "Ninafuatilia kwa wasiwasi na uchungu mgogoro mkubwa unaoathiri Haiti na matukio ya vurugu ambayo yametokea katika siku za hivi karibuni - alisema Papa. "Niko karibu na Kanisa na watu wapendwa wa Haiti, ambao wamekuwa wakipitia mateso mengi kwa miaka mingi. Ninawaalika kusali, kwa maombezi ya Mama Yetu wa Msaada wa Daima ili kila aina ya vurugu zikome na kila mtu atoe mchango wake katika kuongeza amani na upatanisho nchini, kwa kuungwa mkono upya na jumuiya ya kimataifa."

11 March 2024, 11:50