Tafuta

Dominika ya Matawi, ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu. Dominika ya Matawi, ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu.  (Vatican Media)

Dominika ya Matawi Mwaka B wa Kanisa: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu

Dominika ya Matawi, ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Matawi ni ishara ya ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya dhambi na mauti. Kumbe, Kanisa linaadhimisha Siku ile Yesu alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe na pili huu ni mwanzo wa mateso, kifo na ufufuko.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji, Dominika ya Matawi, ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Liturujia ya Dominika ya Matawi mahali pote duniani kadiri ya Mapokea na mafundisho ya Kanisa kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, liturujia inaanza na maandamano kuelekea Kanisani kwa shangwe, tukimshangilia Yesu Kristo, Masiha, Mfalme wetu na Mwokozi wetu, anayeingia Yerusalemu kutukomboa kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Katika kufanya hivyo, tunaungana na kumwungama Kristo, aliyeteseka, kufa na kufufuka kwa ajili yetu sisi. Tunaonesha imani na matumaini yetu kwake, kama wafuasi wake.  Tangu Jumatano ya Majivu, tumekuwa tukifanya bidii ya kurekebisha mienendo yetu mibaya ili kujiweka katika hali njema, na kujipatanisha na Mungu.Majuma yote hayo yamepita na hatimaye tunalianza Juma Kuu. Matawi yanayobebwa na waamini wote washiriki wa adhimisho la dominika hii ya mateso leo ni ishara ya ushindi wa Yesu dhidi ya dhambi na kifo. Tumeshangilia kuwa Kristo anakwenda kushinda dhambi na mauti. Kama vile Watoto wa Mayahudi walimshangilia kama sisi leo wakiamini kuwa ndiye Mfalme waliyemngoja. Matawi haya tukayaweke nyumbani na vyumbani kwetu tukijua kuwa ni visakramenti na hivyo yatukumbushe daima fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Siku 6 kabla ya Pasaka ya wayahudi, watoto walimlaki Bwana kwa shangwe, watu walitandika nguo wakatupa maua na kumpungia matawi ya mizeituni wakiimba “hosanna Mwana wa Daudi”. Yeye mwenyewe alikuwa mtulivu, mtumishi wa Bwana kadiri ya Isaya kwenye Somo la Kwanza amekaza uso wake kama gumegume kuelekea Yerusalemu kutupigania sote ile hadhi tuliyoipoteza kwa uasi wa Adamu KRISTO ni Adam mpya.

Matawi ni alama ya Kristo Mshinda dhidi ya dhambi na mauti
Matawi ni alama ya Kristo Mshinda dhidi ya dhambi na mauti

UFAFANUZI: Leo tunaadhimisha matukio mawili ya msingi katika historia ya ukombozi wetu. La kwanza ni kuingia kwa shangwe kwa Yesu Yerusalemu, jambo ambalo nasi tumeshiriki leo. La pili ni mwanzo wa mateso ya Yesu Kristo huko Yerusalemu, jambo ambalo tunatafakari kwa undani ndani ya Juma hili Kuu, na kuhitimisha kwa kuadhimisha kifo na ufufuko wake Kristo. Haya ni matukio mawili yanayokinzana hasa katika fikra zetu za kibinadamu, lakini kadri ya mpango wa Mungu wa ukombozi yanaendana kabisa, na ndivyo ilivyotakiwa na inavyotakiwa yaadhimishwe ili utukufu wa Mungu udhihilike dhidi ya shetani, dhambi na mauti, kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.  masomo ya leo pamoja na historia ya mateso ya Yesu, tuliyosikia leo yanatualika tutafakari kwa kina mateso ya Yesu, yanayodhirisha ubinadamu wake. Yesu alitungwa mimba tumboni mwa Mama Bikira Maria, akazaliwa na kukua kama sisi. Na baadaye aliumizwa na kuteseka kama sisi tuesekavyo katika shida na taabu za maisha. Ila aliteseka na anaendelea kuteseka zaidi yetu kutokana na dhambi, kiburi na ukaidi wetu. Lakini pia upande wa pili, Umungu wake unadhihilishwa kwa kutungwa kwake tumboni mwa Mama Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, miujiza yake mikubwa, muunganiko wake na Baba na Roho Mtakatifu katika utume wake, na hasa katika mateso na kifo chake msalabani. Zaidi sana Umungu wake unadhihirika katika kushinda kifo na mauti kwa kufufuka kwake. Yesu alikuja ulimwenguni, akimtii Baba, ili kutufungulia njia ya kwenda mbinguni, kutufanya wana wa Mungu, katufunulia upendo, huruma na msamaha wa Mungu kwa mateso na kifo chake Msalabani.

Dominika ya Matawi, Mwanzo wa Juma kuu, Mjini Vatican
Dominika ya Matawi, Mwanzo wa Juma kuu, Mjini Vatican

Tukio hili la Bwana wetu Yesu Kristo kuingia kwa shangwe linaambatana na furaha ya watu waliochukua matawi na kutandika nguo zao huku wakimtangaza Kristo Yesu kwamba ndiye Masiha. Walichukua matawi kama ishara ya ushindi na matumaini kwa Masiha. Na mtindo huu wa kushangilia haukuwa mara ya kwanza, waliwahi kumshangilia mfalme Antioko baada ya kulikomboa hekalu kutoka kwenye unajisi wake, walimpongeza na kumshangilia kwa shangwe, nderemo wakibeba matawi huku wakiimba zaburi, (rejea 2Mak 10:7). Katika Agano la Kale matawi yalikuwa ishara ya uzuri na ushindi. Yalichorwa kwenye sarafu na majengo ya serikali. Mfalme Suleiman aliyachora kwenye kuta na kwenye milango ya hekalu (1Fal 6:29) na halafu mwishoni mwa nyakati wote watafurahi mbele ya kiti cha enzi wakiwa na matawi ya mitende mikononi (Ufu 7:9). Nyakati hizi matawi yanatukumbusha ukuu wa Mungu katika Kristo, yanatupa tafakari ya sadaka ya Yesu msalabani, yanatuhamasisha kumsifu na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya ukombozi na kutazamia kwa hamu ujio wake wa Pili. Lakini kuingia kwa utukufu kwake Bwana wetu Yesu Kristo ilikuwa ni kutimia kwa utabiri wa nabii Zekaria “Furahi sana ee binti Sayuni, piga kelele ee binti Yerusalemu! Tazama mfalme wako anakuja kwako. Ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mnyenyekevu amepanda punda, naam, mwana punda, mtoto wa punda” (Zek.9:9).    Kundi hili linalomshangilia Yesu ni la wanyonge, watu toka mashambani, watu duni, wenye kipato cha chini; watu hawa duni wanafanya mji wote wa Yerusalemu utikisike kwa kelele za shangwe na hivyo kuamsha hasira za wakuu wa Makuhani, Mafarisayo na Waandishi. Haya yote yalipelekea kuanza kwa mikakati ya kumkamata Yesu usiku uleule. Swali ni, Kwa nini wanamkamata Yesu usiku na kutoa hukumu upesi? Hivyo tunapata jibu kuwa, Makuhani na mafarisayo wanafanya mambo haya yote usiku wakiogopa kundi lile la watu duni, wa mashambani wanaomwamini Yesu kwamba ni mfalme na Masiha, wasije wakawakasirikia na kufanya mapinduzi. Hata leo tunashuhudia mahali pengi duniani hasa nchi zinazoendelea katika vyombo vya kutoa haki mintarafu mahakama, haki za wanyonge na wasio na pesa zinapindishwa hakuna wa kuwatetea wala kuwa semea, leo tunaalikwa kuwa sauti ya mnyonge na maaskini awe wa kiroho au kimwili. Hivyo mahakama zote za kijamii na za kikanisa zinapaswa kutoa haki zikiongonzwa na huruma na ukweli. 

Matawi ni kisakramenti, yatunzwe kwa heshima.
Matawi ni kisakramenti, yatunzwe kwa heshima.

Kwa Myahudi ilikuwa ni kashifa kubwa kusikia mfalme anateswa, anapigwa na kufanyiwa yote haya. Ndiyo maana, wengi walikata tamaa na kumwona Yesu kama mtu wa kawaida. Wanawaza iweje mfalme ateswe! Tendo hilo linashusha imani yao kwake. Ukisimliwa kirahisi rahisi huwezi kuonja maumivu aliyoyapata. Jaribu kufikiri maumivu tunayoyapata unapodungwa sindano kama tiba. HOSANNA HOSANNA tunayoimba leo imuelekee Kristo kwani juma hii anakwenda kuyapa maana maisha yetu na kuyafanya mapya, anakwenda kutupa zawadi ya maisha yake, ya mwili wake, ya damu yake, zawadi ya upendo wake. Tupokee upendo huo kwa unyenyekevu kisha nasi pia tumpe zawadi ya nafsi zetu, ya maisha yetu, tumpe Mungu muda wetu, sala zetu, tena tuunganike na Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa ajili yetu. Kama Wayahudi walivyotandaza nguo zao Yesu akapita juu yake nasi tutandaze miguuni pa Yesu maisha yetu, tujitandaze wenyewe kwa mkao wa kuabudu na kushukuru. Tusitandaze nguo na matawi yasiyo na uhai, yenye kuchakaa bali tujiweke wenyewe miguuni pa Kristo, tutabarikiwa. Tunapoimba “Hosanna Mwana wa Daudi” tukumbatie mambo 3: mosi tushikilie Injili, Habari Njema inayotukutanisha na Kristo na hivi tunapata kumjua na kulisikiliza neno lake. Pili, tukumbatie Msalaba wake kwani katika huo tunajipatia alama ya upendo wake kwetu alipoamua kwa hiyari kufa juu yake kwa ajili yetu. Na tatu, tuwe ushuhuda kamili, mashahidi wa imani kwa matendo ya kimapendo. Maisha yetu ya imani ni safari isiyoweza kuepuka mateso. Pamoja na hayo, tukumbuke kuwa Mungu hatuletei mateso bali huweza kuruhusu mateso fulani yatupate ili atupatie mazuri zaidi iwapo tutakuwa na imani. Uvumilivu na kuyapokea mateso yetu kwa imani kubwa ndiyo dawa ya kuyakabili mateso hayo.

Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.
Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.

Tunahitaji amani katika biashara, masomo, kazi na katika nyumba zetu hasa zile ambazo wahusika wake wanaishi maisha ya Simba na Swala katika maana ya kuviziana ili kuumbuana, wanaishi mradi siku zinapita, na laiti ingetolewa ruhusa ya kuamua upya kila mtu angalichukua njia yake; baba kivyake, mama kivyake, watoto kivyao, kwa watawala nao wangejua maumiu ya watawaliwa pale wanapokuwa wamechokwa kwa kutotimiza wajibu na ahadi zao walizotoa kabla ya kupewa dhamana sehemu nyingi raia huwakana watawala kuwataka waachie ngazi, na hata hufikia maanadamano ya shinikizo sio kama yale aliyopata Yesu Mwana wa Mungu, inapofika katika  anguko la hivi huwa kubwa na kuipata tena amani huwa ngumu kabisa. Ikiwa tutasafiri kwa Punda kama Yesu japo ni polepole lakini tutaepuka ajali. Tutaimba HOSANNA kwa utulivu. Tusipotumia usafiri wa Yesu ajali ni dhahiri. Ajali ya kwanza ni kuvunjika moyo wa kusali, hii mbaya kabisa. Ajali ya Pili ni kuitoroka meza ya Bwana, kutopokea sakramenti kwa sababu yoyote ni kumkosa Yesu moyoni, ajali hii ni mbaya afadhali ugongwe na treni. Ajali ya Tatu kutosoma Maandiko Matakatifu na kujikosesha fursa ya kukutana na Kristo na kumsikia katika neno lake hilo adhimu. Ajali ya Nne ni kuishi bila sala, ukavu wa maisha ya kiroho kwa kujiamini kupita kiasi na kutojali ulinzi wa Mungu. Bado ipo ajali ya Tano nayo ni kuchelewa Kanisani kwa sababu za kawaida sana kama vile kuchelewa kuamka, kwa sababu ya nyingi. Tunaposafiria Punda wa Yesu tunaepuka ajali ya Sita ambayo ni kumwacha Mungu na kuabudu miungu mali, fedha, watu, kazi, vitu na kutojali. Mkristo epuka ajali ya Saba maishani mwako ambayo ni kuvunja amri za Mungu, kukosa upendo kwake na kwa jirani yako, kuendekeza ugomvi na migogoro na kushindwa kusamehe majeraha. Katika ajali hizi suluhu ni moja, kusafiri kwa usafiri wa Kristo, naam, mwanapunda mtoto wa punda. Mpendwa katika Kristo, kujua thamani ya mateso kutupe uvumilivu, ustahimilivu na ujasiri wa kuyapokea mateso mbalimbali tunayokumbana nayo na kwa hayo, tuimarishwe zaidi katika imani yetu. Tukiwa na mtazamo huu wa mateso, kamwe mateso hayatakuwa kikwazo kwa imani yetu.

Dominika ya Matawi
23 March 2024, 09:22