Tafuta

Siku ya Alhamisi Kuu, Kanisa linaadhimisha mambo makuu matatu, kuwekwa kwa; Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu - Upadre na Amri Kuu ya mapendo. Siku ya Alhamisi Kuu, Kanisa linaadhimisha mambo makuu matatu, kuwekwa kwa; Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu - Upadre na Amri Kuu ya mapendo.   (Vatican Media)

Alhamisi Kuu ni Siku ya Kuwakumbuka na Kuwaombea Mapadre! Ekaristi na Upendo

Maadhimisho ya fumbo hili Kuu la Pasaka yanaanza kwa adhimisho la Karamu ya Mwisho, kabla ya kukamatwa, kuteswa, kusulubiwa na kufa msalabani. Hili ni adhimisho Kuu moja linalodumu kwa muda wa siku tatu - Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu. Alhamisi Kuu, Kanisa linaadhimisha mambo makuu matatu, kuwekwa kwa; Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu na Amri Kuu ya mapendo. Ni Siku ya kuwaenzi Mapadre kwa huduma!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, siku ya Alhamisi Kuu. Ni siku ya kwanza kati ya siku Kuu tatu za kuadhimisha Fumbo la Wokovu wetu, Pasaka - Mateso, Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Maadhimisho ya fumbo hili Kuu la Pasaka yanaanza kwa adhimisho la Karamu ya Mwisho, mlo aliokula Yesu na Mitume wake 12, kabla ya kukamatwa, kuhukumiwa, kuteswa, kusulubiwa na kufa msalabani. Hili ni adhimisho Kuu moja linalodumu kwa muda wa siku tatu - Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu. Siku ya Alhamisi Kuu, Kanisa linaadhimisha mambo makuu matatu, kuwekwa kwa; Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu - Upadre na Amri Kuu ya mapendo. Kumbe Alhamisi Kuu ni siku ya mapadre tuwaombee na kuwaenzi kwa kuwapongeza inavyowezekana. Somo la kwanza ni la kitabu cha Kutoka (Kut 12:1-8, 11-14). Somo hili linasimulia jinsi Wayahudi walivyoadhimisha mlo wa Kipasaka, wakikumbuka kukombolewa kutoka utumwani Misri. Sherehe hii iliadhimishwa kifamilia. Baba wa nyumba ndiye aliyeongoza maadhimisho haya akielezea umuhimu na maana ya maadhimisho haya. Maandalizi ya yaliyofanyika ni pamoja na kuandaa chumba cha sherehe, mwanakondoo aliyeokwa, ishara ya Kristo mwanakondoo wa Agano jipya na milele, mikate isiyotiwa chachu ikiwakumbusha haraka yao walipoondoka Misri, mboga chungu zikiwakumbusha mateso waliyopata walipokuwa utumwani Misri na divai ya kutosha ishara ya furaha ya kukombolewa kutoka utumwa Misri. Maandalizi haya yote yanaakisi maandalizi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu aliyotuachia Bwana wetu Yesu Kristo, yanayoendelea kuadhimishwa katika Sadaka ya Misa Takatifu.

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma
Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma

Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 11:23-26). Na Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yoh. 13:1-15). Masomo haya mawili kwa pamoja yanaelezea juu ya kuwekwa kwa Ekaristi Takatifu na Daraja la Upadre katika mlo wa Kipasaka aliokula Yesu na mitume wake. Mtume Paulo anasisitiza kuwa Karamu hii inakumbusha kifo cha Yesu Kristo, tena ni amana ya karamu ya kimasiya na ya ushirika. Kila tunapokula vema karamu hiyo tunashiriki na kutangaza kifo na ufufuko wake Kristo. Ndiyo kusema tunalihuisha Agano Jipya na la milele katika maisha yetu. Hii ni kwasababu kila adhimisho la tukio katika historia ya wokovu wetu linapoadhimishwa kiliturujia lina hali mbili. Kwanza kutukumbusha yaliyotokea zamani katika historia ya ukombozi wetu. Na pili kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho na hivyo yanafanya sehemu ya maisha yetu na kutuonjesha upendo wa Mungu katika mafumbo tunayoadhimisha katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani tunapoelekea katika maisha ya umilele mbinguni. Ni katika muktadha huu tafakari hii inalenga japo kwa ufupi mambo makuu mawili: Fumbo la Ekaristi Takatifu, thamani yake na umuhimu wake katika maisha yetu ya kila siku na thamani na umuhimu wa Padre katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani. Neno Ekaristi asili yake ni lugha ya Kigiriki Eucharistein likimaanisha shukrani. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya shukrani kwa Mungu Baba kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wake. Ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo tunampokea Kristo na roho zetu kujazwa neema na kupewa amana ya uzima wa milele (KKK 1322–1323, 1409). Ekaristi Takatifu ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa. Papa Leo XIII anasema; “Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa” (Denz.3364). Kumbe bila Ekaristi Takatifu Kanisa haliwezi kuwepo, kwa sababu Ekaristi Takatifu ni Kristo mwenyewe. Ni katika Ekaristi Takatifu, ndani ya maumbo ya mkate na divai Yesu yumo mzima, mwili wake na Damu yake, ubinadamu wake na Umungu wake. Ndivyo alivyoamua Yeye kubaki na kukaa nasi katika hali hiyo, ili tuongee naye, tumueleze hali zetu, shida zetu, matatizo yetu, furaha na huzuni zetu. Basi tuipende Ekaristi Takatifu, tushiriki maadhimisho yake na kuipokea kwa kustahili.

Alhamisi kuu: Huduma ya upendo kwa watu wa Mungu
Alhamisi kuu: Huduma ya upendo kwa watu wa Mungu

Mama Kanisa anaendelea kutufundisha kuwa adhimisho la Ekaristi Takatifu ni tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu na kilele cha tendo la watu kumwabudu Yeye. Ndiyo maana katika sadaka ya Ekaristi Takatifu, Kanisa hutolea maisha ya waamini, masifu yao, mateso yao, sala zao, kazi zao na kuyaunganisha na yale ya Kristo. Kwa vile ni sadaka, Ekaristi Takatifu hutolewa kwa waamini wote, wazima na wafu, kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na kupata rehema ya Mungu. Ndiyo maana Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika hati ya Liturujia wanasema; “Kila Sadaka ya Ekaristi Takatifu inapoadhimishwa, kazi ya ukombozi wetu inafanyika kwa ukamilifu wake” (SC 2). Kumbe, Ekaristi Takatifu, hutuunganisha na Kristo, hudhoofisha nguvu ya dhambi na ni amana ya uzima wa milele.  Zaidi sana Mama Kanisa anatufundisha kuwa ni kwa njia ya adhimisho la Ekaristi Takatifu tunaungana na liturujia ya mbinguni na tunaanza kushiriki uzima wa milele (KKK 1324–1327, 1407). Hii ndiyo amana aliyotuachia Yesu Kristo siku ya Alhamisi kuu. Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu la Upadre haviwezi kutenganishwa. Bila Ekaristi Takatifu hakuna upadre wala Padre, na bila Upadre na Padre hakuna Ekaristi Takatifu, na kama hakuna Ekaristi Takatifu, hakuna Kanisa. Ni katika muktadha huu thamani na umuhimu wa Padre unakuwa wazi katika kila hatua ya maisha yetu. Upadre ni wito na anayeita ni Mungu na anayeitwa na mtu. Padre ni mwanadamu aliyetwaliwa kati ya watu, akatengwa na watu kwa mambo yamuhusuyo Mungu kwa ajili ya watu (Ebr. 5:1-4). Padre ni kuhani. Padre ni Kristo mwingine “Alter Christus.” Padre ni mwezeshaji na mtagulizi kwa mambo ya imani. Padre ni mhudumu na mtumishi wa Mungu kwa ajili ya Taifa lake.

Alhamisi Kuu ni Siku ya Kuwakumbuka na Kuwaombea Mapadre
Alhamisi Kuu ni Siku ya Kuwakumbuka na Kuwaombea Mapadre

Kumbe, Padre daima yuko na taifa la Mungu nyakati zote, kipindi cha kuzaliwa na kufa, wakati wa furaha na huzuni. Katika uchanga wetu, Padre yupo ili apate kutubatiza. Kwa uwezo aliopewa na kwa mikono yake, dhambi ya asili inaondolewa, na mbatizwa anafanywa kuwa mtoto mteule wa Mungu na wa Kanisa. Katika uchipukizi na ujana wetu, Askofu aliye Kuhani mkuu, hutupatia Sakramenti ya Kipaimara ambayo kwayo tunajazwa mapaji ya Roho Mtakatifu – hekima, akili, elimu, shauri, nguvu, ibada na uchaji wa Mungu –ili tuwe askari amini na hodari wa Kristo. Kila siku Padre hutulisha kwa Ekaristi Takatifu kwa ajili ya uzima na ustawi wa roho zetu. Tunapoanguka katika dhambi na kutubu, sauti tulivu ya Padre yenye nguvu ya Mungu inatufariji ikituambia; “Nenda na amani Mwenyezi Mungu amekusamehewa dhambi zako.” Maneno haya hawezi kuyatamka mtu yeyote isipokuwa Padre naye si kwa mamlaka yake, bali ni kwa mamlaka aliyopewa na Kristo mwenyewe kupitia mitume siku ya ufufuko wake. Zaidi sana Padre hubariki na kushuhudia makubaliano ya mume na mke wanapoahidi uaminifu mbele za Mungu na Kanisa katika sakramenti ya ndoa. Familia mpya, Kanisa la nyumbani na shule ya awali ya imani na maadili inapata baraka ya Mungu na kukua katika misingi ya imani kwa malezi elekezi ya Padre. Padre huunganisha jitihada zake na za wazazi katika kuwalea na kuwaelimisha watoto katika mambo ya imani na maadili na kuwaandaa kupokea Sakramenti. Padre hachoki, hata wakati wa ugonjwa tayari yuko karibu nasi akitupatia Mpako Mtakatifu ili kututuliza, kutuimarisha na kutuponya na udhaifu wa kimwili na kiroho. Tukifa tuna muunganiko na Kristo, kwenye mazishi yetu Padre yupo tayari kupumzisha miili yetu. Na kila siku katika Misa Takatifu husali kwa ajili ya roho za marehemu walioko toharani. Palipo na huzuni, Padre huleta furaha, pasipo na haki hutetea haki, kwa vijana huwatia moyo na kuwafundisha fadhila mbalimbali, utii, uaminifu, moyo wa uwajibikaji na heshima kwa watu na kwa Mungu. Huwakumbusha viongozi na matajiri wajibu wao wa kuwasaidia wahitaji na waajiri kulipa ujira unaostahili. Huyu ndiye Padre.

Maadhimisho ya Juma Kuu Mjini Vatican
Maadhimisho ya Juma Kuu Mjini Vatican

Lakini hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika na kukata tamaa. Ndivyo ilivyo kwa padre. Hivyo ni wajibu wa waamini kuwasaidia katika ubinadamu wao ili waweze kusimama imara katika kuwahudumia. Tuwapende mapadre, tuwaombee mapadre, tuwafariji mapadre, tuwatie moyo mapadre, ili wawe na nguvu ya kutuhudumia vizuri. Tusali kuombea miito mitakatifu katika Kanisa, ili tupate mapadre wema na waaminifu wanaojitahidi kumfuasa Kristo. Mwisho, tukumbuke kuwa, Kanisa limeweka utaratibu wa kukesha na kuabudu Ekaristi Takatifu Siku ya Alhamisi Kuu. Huu ni wasaa muhimu sana kukaa pamoja na Yesu wa Ekaristi, tukitafakari upendo wake kwetu sisi, upendo alioudhihirisha katika kujitoa kwake Sadaka msalabani na sasa yupo katika Ekaristi Takatifu. Tutumie vema muda huo kumwabudu na kumshukuru kwa zawadi ya ukombozi na tumwombe neema ya kuweza kuwa waaminifu katika maisha yetu ya kiimani na kimaadili ili mwisho wa maisha ya hapa dunia, tukafurahi naye milele yote mbinguni. Basi tumwombe Mungu Roho Mtakatifu, atuangaze na kutusaidia kuyaelewa mafumbo hayo mawili; Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Daraja Takatifu la Upadre, tuyapokee kwa moyo wa shukrani na upendo mkuu, ili tuweze kujichotea neema na baraka kutoka kwa Mungu Baba, kwa ajili ya sifa na utukufu wake na kwa ajili ya hiyo nasi tuweze kutakatifuzwa na kustahilishwa kuingia katika ufalme wake mbinguni.

Ibada ya Alhamis Kuu
27 March 2024, 15:41