Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya Kwaresima Mwaka B wa Kanisa. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya Kwaresima Mwaka B wa Kanisa.  (ANSA)

Tafakari Dominika ya Kwanza Ya Kwaresima Mwaka B: Agano Jipya Na la Milele

Kiini cha ujumbe wa masomo ya Dominika yaKkwanza ya Kipindi cha Kwaresima umejika katika dhana ya Agano jipya na la milele alilofanya Mungu na wanadamu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Agano hili jipya ni utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa jamii ya wanadamu ya tangu Agano la Kale, Faraja, amani na matumaini kwa Wakristo wanaoteseka na kudhulumiwa; mapambano ya maisha ya kiroho kwa kujikita katika kufunga, kusali, kutafakari na matendo ya huruma.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya Kwaresima Mwaka B wa Kanisa. Ni siku ya 5 ya kipindi hiki cha siku arobaini za majiundo ya kiroho kwa kufunga, kusali, kulisoma, kutafakari na kuliishi Neno la Mungu kwa kutenda matendo ya huruma ili kujenga muungano na Mungu wetu mtakatifu kwa kumwilisha ndani mwetu Amri Kuu ya mapendo. Msisitizo mkuu wa kipindi hiki ni kujikubali kuwa sisi ni jumuiya ya wakosaji tunaohitaji kufanya toba na kutakaswa kwa huruma na upendo wa Mungu. Naye Mungu anatuahidi katika wimbo wa mwanzo akisema; “Ataniita nami nitamwitikia; nitamwokoa na kumtukuza; kwa siku nyingi nitamshibisha” (Zab. 91:15-16). Huu ndio upendo na huruma kuu ya Mungu inayojithihirisha kwetu kwa njia ya Yesu Kristo. Ni katika tumaini hili, Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, utujalie tuzidi kuifahamu siri ya Kristo na kupata manufaa yake katika mwenendo wetu mwema kwa mfungo wa Kwaresima wa kila mwaka.” Kiini cha ujumbe wa masomo ya Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima umejika katika dhana ya Agano jipya na la milele alilofanya Mungu na wanadamu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Agano hili jipya ni utimilifu wa ahadi ya Mungu kwa jamii ya wanadamu ya tangu Agano la Kale. Somo la kwanza ni la kitabu cha mwanzo (Mwa. 9:8-15). Nalo linatueleza jinsi Mungu alivyofanya Agano na Nuhu pamoja na wanae baada ya gharika kuu. Itakumbukwa kuwa gharika kuu ilikuwa adhabu ya haki kwa watu kwa dhambi zao. Mungu akijua udhaifu wa wanadamu na kwa huruma yake kuu na upendo wake, anaweka Agano la kutokuangamiza viumbe alivyoviumba yeye kwa njia ya gharika. Ishara ya Agano hili ni upinde wa mvua. Mzaburi alipotafakari upendo huu na huruma ya Mungu aliimba zaburi ambayo ni wimbo wa katikati unaosema; “Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, kwao walishikao Agano lake na shuhuda zake. Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako, uniongoze katika kweli yako, na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu. Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, maana zimekuwako tokea zamani. Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. Bwana yu mwema na mwenye adili, kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia zake. Wenye upole atawafundisha njia yake” (Zab. 25:4-10). Kazi kwetu ni kusikiliza mafundisho ya Mungu na kuyaishi kwa wokovu wetu.

Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga
Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 3:18-22). Katika som hilii, Mtume Petro anawafariji na kuwatuliza, akiwatia moyo na kuwapa matumaini waamini wakristo waliokuwa wanadhulumiwa na kuteswa kwa ajili ya imani yako kwa Kristo. Mtume Petro anawaasa wavumilie mateso wakifuata mfano wa Kristo alivyovumilia hata akafa msalabani kwa ajili ya wokovu wao. Nasi tunakumbushwa kuwa tunafaidi matunda ya Agano hili jipya na la milele kwa njia ya sakramenti ya ubatizo. Maji ya ubatizo ni kinyume na maji ya wakati wa gharika ambayo yaliangamiza uhai. Maji haya yanakuwa chanzo cha uhai kwetu na uthibisho wa ahadi ambayo Mungu alimwahidia Nuhu kuwa hatamdhuru tena mwanadamu na viumbe vingine kwa maji. Kama vile maji ya gharika yalivyowaangamiza wadhambi, ndivyo maji ya ubatizo yanavyomwangamiza shetani na mitego yake na kutufanya sisi washindi dhidi ya dhambi na mauti. Ndiyo maana kwa ubatizo Mungu alipendezwa nasi, kwa sababu tulikiri kumkataa shetani na fahari zake zote. Tukiwa na imani hiyo tuna uhakika wa wokovu wetu ndani ya Kristo. Hivyo yatupasa kuvumilia taabu, mahangaiko na mateso yanayotokana na imani yetu kwa ajili ya wokovu wetu wenyewe. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk. 1:12-15). Sehemu hii ya Injili inatueleza jinsi Yesu baada ya ubatizo wake alivyoongozwa na Roho Mtakatifu mpaka jangwani. Na huko alipambana na mwovu shetani na kuvishinda vishawishi vyake. Baada ya hapo, Yohane Mbatizaji alipotiwa gerezani, Yesu akaanza kutangaza habari njema ya wokovu. Ujumbe wake mahususi ni huu; “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.” Kumbe, ushindi wa Yesu juu ya shetani ni kuusimika ufalme wa Mungu. Sisi tunakuwa wana wa ufalme huu na kujazwa nguvu ya Roho Mtakatifu kwa Sakramenti ya ubatizo ili kupambana na shetani. Ndiyo maana Mtume Paulo anatuambia; “Tulipobatiza tuliungana na kifo chake Kristo, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya” (Rum.6:4). Kumbe tunaona kuwa Agano la Mungu na mwandamu katika Agano la Kale, utimilifu wake ni katika Agano jipya na milele kwa njia ya Mwanae wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo. Nasi tunashirikishwa matunda ya Agano hili kwa njia ya ubatizo. Kwa Ubatizo sisi tumekuwa wadau wa Agano hili Jipya, kwani tumeshiriki katika kile kiapo cha kushiriki mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.

Kwa Ubatizo mwamini anazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu
Kwa Ubatizo mwamini anazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu

Agano hili Jipya na la milele, sio Agano kati ya Mungu na mtu binafsi au na kundi la watu, bali ni Agano kati ya Mungu na jamii yote ya wanadamu. Agano hili linathibitishwa kwa njia ya ubatizo nalo limeidhinishwa mioyoni mwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Agano hili linaratibishwa na Yesu Kristo Mwana wa Mungu kwa Damu yake na siyo ya wanyama kama katika Agano la kale. Agano hili Jipya linatufanya kuwa wana wa Mungu na warithi wa uzima wa milele pamoja na Kristo. Agano hili lilitangazwa na Manabii, likaratibishwa na kuadhimishwa na Kristo, jioni kabla ya kifo chake katika karamu ya mwisho alipochukua Mkate na kuugeuza kuwa Mwili wake na Divai kuwa Damu yake, iliyomwagika kwa ajili ya wengi, kwa maondoleo ya dhambi na wokovu wa wote watakaompokea na kumwamini. Na kila inapoadhimishwa Sadaka ya Misa Takatifu nasi kupokea Ekaristi Takatifu, Agano hili jipya na la milele linahuishwa kwani Ekaristi Takatifu ni ukumbusho wa Agano hili Jipya. Katika kipindi hiki cha Kwaresima Mama Kanisa anatukumbusha tena na tena kuzihuisha na kuziishi ahadi tulizoweka katika Agano hili kwa njia ya Ubatizo kwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kutenda matendo ya huruma kwa upendo. Tunaalikwa kuzishika na kuziishi Amri za Mungu ili kujenga mahusiano mema na Mungu na jirani zetu. Utimilifu wa amri hizi ni Upendo kwa Mungu na Jirani. Maana Maandiko Matakatifu yanatuambia: Msiwiwe na deni lingine isipokuwa deni la kupendana. Kule kusema usizini, usiibe, usiue, usitamani mwanamke au mwanaume asiye wako, usiseme uongo; haya yote hupata ukamilifu wake katika amri ya mapendo kwani pendo halimfanyii jirani neno baya. Basi kila mmoja na aishi vyema ahadi za ubatizo katika wito aliouchagua. Wanandoa tunzeni maagano yenu ya ndoa, mdumishe maisha ya familia, Kanisa la nyumbani, shule ya sala na maadili mema. Watawa na mapadre tutunze maagano ya miito yetu mitakatifu. Tuishi kadiri ya miito yetu tukimfuata Kristo aliye Njia, Ukweli na Uzima. Na wengine ambao bado hamjachagua aina ya maisha, ishiri kiamifu mkitafakari vizuri ili mfanye maamuzi yaliyo mema.

Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha
Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha

Tukifanya hivyo, tutajiandaa vyema kuvishinda vishawishi vya yule mwovu shetani, na kusherehekea kwa furaha na amani fumbo la ukombozi wetu, yaani Pasaka, kama utangulizi wa dominika hii unavyosema; “Yeye, Kristu Bwana wetu, alifunga chakula siku arobaini, akaonyesha ubora wa namna hiyo ya kufanya kitubio. Amewaepusha watu wote na hila za nyoka wa kale na kutufundisha kuishinda chachu ya uovu. Nasi tunapoadhimisha fumbo la Pasaka kwa mioyo safi, utujalie hatimaye tuifikie pasaka ya milele”. Na hili ndilo tumaini letu ndiyo maana Mama Kanisa anapohitimisha adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu katika dominika hii anatuombea akisema; “Ee Bwana, sisi tumekula mkate wa mbinguni unaolisha imani, unaoleta tumaini, na kuzidisha mapendo. Tunakuomba utuwezeshe kumtamani yeye aliye Mkate hai wa kweli, tuweze kuishi kwa kila neno litokalo katika kinywa chako”. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 1 Kwaresima
Dominika 1 Kwaresima
14 February 2024, 15:02