Tafuta

Kipindi cha Kwaresima ni safari inayokazia Sakramenti ya Ubatizo mlango wa Sakramenti za Kanisa; Kufunga na Kusali pamoja na kujikita katika tabia njema au matendo ya huruma. Kipindi cha Kwaresima ni safari inayokazia Sakramenti ya Ubatizo mlango wa Sakramenti za Kanisa; Kufunga na Kusali pamoja na kujikita katika tabia njema au matendo ya huruma.  (© JUGO MEDIA)

Kipindi cha Kwaresima: Safari ya Ubatizo, Kufunga na Tabia Njema

Kipindi cha Kwaresima ni hija ya Siku arobaini inayojikita katika Ubatizo, Kufunga, Kusali na Tabia Njema. Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Kufunga ni mtima wa sala na huruma ni uhai wake. Kufunga na kufanya matendo ya huruma ni chanda na pete, ili kuweza kuwa makini kusikiliza shida na mahangaiko ya wengine. Kufunga kunamsaidia mwamini kuepuka dhambi na nafasi zake.

Na Padre Stefano Kaombe, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kati ya vipindi muhimu kabisa vya kiliturujia katika Kanisa n ikipindi cha Kwaresima, wengi wetu tuna kumbukumbu nyingi kuhusiana na kipindi hiki, hasa kaidadini ya kupakwa majivu siku ya Jumatano ya Majivu, Njia ya Msalaba kila Ijumaa, kufunga, kutopiga kinanda na ala zingine wakati wa kuimba na hasa utajiri mkubwa wa nyimbo za kipindi hiki. Katika makala haya Padre Stefano Kaombe, kutoka Parokia ya Roho Mtakatifu, Kitunda, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, anafanya tafakari ya kina kuhusu: Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Kufunga ni mtima wa sala na huruma ni uhai wake. Kufunga na kufanya matendo ya huruma ni chanda na pete, ili kuweza kuwa makini kusikiliza shida na mahangaiko ya wengine. Kufunga kunamsaidia mwamini kuepuka dhambi na nafasi zake. Sakramenti ya Ubatizo ambayo kimsingi ni mlango wa Sakramenti zingine zote, Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa Hekalu la Roho Mtakatifu (KKK 1263).

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha

Kufunga kunamsaidia mwamini kuepuka dhambi na nafasi zake, ili kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu kama inavyojidhihirisha katika Maandiko Matakatifu. Kufunga kunaiwezesha roho ya mtu kumgeukia Mungu anayeangalia yale yaliyofichika kwenye moyo wa mwanadamu na kumkirimia kadiri ya mapenzi yake. Huu ni mwaliko kwa mwamini kujiachilia na kujiaminisha kwa huruma ya Mungu. Kufunga ni tendo ambalo limekuwepo tangu kwenye Kanisa la Mwanzo. Kufunga ni mtima wa sala na huruma ni uhai wake. Kufunga na kufanya matendo ya huruma ni chanda na pete, ili kuweza kuwa makini kusikiliza shida na mahangaiko ya wengine. Kwa sasa watu wengi wanaanza kupoteza maana ya kufunga kiroho kwa kutoa mwenelekeo wa kutafuta mali na urembo. Kufunga ni tiba inayomwezesha mwamini kujikatalia mambo yote yanayokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu na kujitoa kwa ajili ya kuwasaidia jirani. Ni kufisha tabia ya uchoyo na ubinafsi na kufungua hazina ya moyo kwa Mungu na jirani, kama njia ya kutekeleza muhtasari wa Injili ya upendo unaofumbatwa katika amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Kufunga kuna mwezesha mwamini kudumisha umoja katika utu wake mzima: mwili na roho, kwa kumjengea uwezo wa kupinga dhambi na hatimaye kukuza uhusiano wa dhati na Kristo Yesu, ili kujipatia msamaha wa dhambi kadiri ya mapenzi ya Mungu mwenyewe. Kujikatalia chakula ambacho kinatoa lishe kwa mwili wa mwanadamu ni kufungua masikio ya moyo kusikiliza Neno la Mungu linalo okoa. Kufunga na kusali kunasaidia kuzima kiu ya ndani ya maisha ya mwanadamu: yaani njaa na kiu ya Mungu. Kufunga kunamwezesha mwamini kufungua macho ili kuyaangalia mateso na mahangaiko ya jirani zake, ili kuwaonjesha kwa kuwamegea huruma kama alivyofanya yule Msamaria mwema kwa kuwapatia nafasi wageni kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha ya waamini.

Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha mahusiano mema na Kristo Yesu
Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha mahusiano mema na Kristo Yesu

Utu ni hali ya binadamu ya kuwa na kutenda kadiri ya hadhi yake kama alivyoumbwa na Mungu. Katika Maandiko Matakatifu, Mtakatifu Paulo anatualika kuvaa utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli (rej. Efe 4:24). Mwanadamu ana utu wa nje na utu wa ndani, utu wa kimwili na utu wa kiroho. Kwa maneno mengine mwanadamu anaweza kuwa na utu wa kale na utu mpya. Utu wa kale ni utu wa asili yaani utu ambao mtu anaurithi kutoka kwa wazazi wake (dhambi ya asili). Aidha, ni utu ambao mtu alijifunza au alifundishwa lakini ukiwa ni utaratibu ulio kinyume na wokovu wa Mungu katika Kristo Yesu. Tunachotakiwa kufanya juu ya utu wa kale ni kuusulubisha ili utu huo ubatilike (Rej. Rum 6:5-14). Kibiblia, Utu mpya ni matokeo ya mabadiliko ya utu wa kale. Rej. Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, 2023.

Kwaresima ni wakati wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu
Kwaresima ni wakati wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu

Ubatizo: Kipindi chote cha Kwaresima, ni kipindi cha maandalizi ya Ubatizo, kwa wakatekumeni kuingizwa katika imani na sisi tuliokwisha kubatizwa kurudia ahadi zetu za ubatizo siku ya Kesha la Pasaka, kilele cha maandalizi haya yote. Maandalizi haya ya karibu ya wakatekumeni tunayaona katika Dominika za Kwaresima kwa uwazi: Dominika I wanateuliwa, Dominika III, wanafanyiwa ‘takaso’ la kwanza, Dominika IV, wanafanyiwa ‘takaso’ la pili na Dominika V wanafanyiwa ‘takaso’ la tatu. Kuna uhusiano mahususi kati ya Jumatano ya Majivu tunapofungua mlango wa Kipindi cha Kwaresima na Kesha la Pasaka, tunapoadhimisha kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kupakwa majivu ni ishara ya kifo, kwani Maandiko Matakatifu yanaweka wazi kabisa, Mungu alimwambia Adamu: “Kwa kuwa wewe ni uvumbi, nawe utarudi katika uvumbi” (Mwz 3:19). Laana hii ya kupotea katika uvumbi, Bwana wetu Yesu Kristo anaibadirisha kwa sadaka yake Msalabani na siku ya Pasaka, anaupatia ulimwengu zawadi ya hali ya utukufu wa ufufuko wake. Ndio hija yetu hapa duniani, tutoke katika vumbi, katika kiza tuelekee katika utukufu, ndio maana katika Kesha la Pasaka tunaanza na kaidadini ya mwanga, tutembee maisha yetu yote katika nuru ya ufufuko. Katika kipindi cha Kwaresima, tuwaombee wakatekumeni wajiandae vyema kuipokea imani ya Kristo Mfufuka. Kwa wabatizwa, ni wakati wa kuketi na kutafakari safari yetu: ninaikumbuka hata tu siku yangu ya ubatizo? Je, hija yangu hapa duniani ni yenye unyoofu, tunatembea katika mwanga wa Kristo? Je, vazi jeupe tulilopewa siku ya Ubatizo wetu linang’aa kwa uadilifu au hata tu silijui hata linipolitupa? Mafuta ya wakatekumeni na ya Krisma ya Wokovu tuliyopakwa siku hiyo bado yanafanya nafsi zetu kuendelea kuwa laini na kung’aa kwa utakatifu na ukarimu? Midomo yetu na masikio yetu inasikia na kutangaza Habari Njema ya Kristo Mfufuka?

Kwaresima: Ubatizo, Sala, Kufunga na Tabia Njema
Kwaresima: Ubatizo, Sala, Kufunga na Tabia Njema

b). Kanisa limeruhusu desturi ya kufunga, inaisisitiza na nyakati nyingine imeiagiza: Funga siku ya Jumatano ya Majivu… Mwalimu wa Kanisa wa Malaika Tomaso wa Akwino anatuambia kwamba tunafunga kutokana na malengo matatu: “Kwanza, ili tuweze kutiisha hatamu (kutiisha) tamaa za mwili… Pili, tunakimbilia kufunga ili kwamba akili zetu kwa uhuru ziweze kutaamali mambo ya mbinguni… Tatu ilikufanya malipizi ya dhambi zetu…” Mtakatifu Basili Mkuu yeye naye alithibitisha umuhimu wa kufunga kwa ajili ya kujilinda dhidi ya nguvu za kishetani, anatuambia: “Kufunga ni silaha ya kujilinda dhidi ya mashetani. Malaika wetu walinzi wanakuwa wako tayari kukaa na wale ambao wamesafisha roho zao kwa kufunga.” Katekisimu ya Kanisa Katoliki, KKK inatuelezea juu ya umuhimu wa kufunga, mosi kwa ajili ya toba ya ndani 1434, inataja kipindi cha Kwaresima na hasa kila Ijumaa yake kuwa ni nyakati nzito za toba 1438. Pili, tunafuata mfano wa Yesu ambaye alienda jangwani kwa siku arobaini kufunga 534-40, soma Mk 1:13. Padre Thomas Kinkead katika andiko lake juu ya ufafanuzi wa KKK aliandika “Tukumbuke kwamba ni miili yetu ndiyo inayotuingiza katika dhambi, hivyo, kama tunauadhibu mwili kwa kufunga na kujitesa, tunafanya malipizi ya dhambi zetu, hivyo Mungu anafuta sehemu ya adhabu yetu ya muda kwa mfungo wetu huo. Papa Leo Mkuu katika mwaka 461 kwa hekima alitoa ushauri kwamba kufunga ni njia na si lengo lenyewe. Kwa wale ambao hawawezi kufunga kwa dhati kabisa, kwa hekima alishauri, “Kila tunachokiacha kwa kufunga kitolewe kama msaada kwa maskini.” Kuacha kufunga, hata kwa sababu stahiki za afya, hakumsameheshi mtu kuacha kutimiza agizo la kila mmoja wetu la kufanya toba (soma Lk 13:3 “Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo”). Tunapaswa kusema kwamba hatupati thawabu kwa kufanya malipizi, hata kama ni makali hivyo, kama tupo katika hali ya dhambi ya mauti. Kuwa katika hali ya neema ni muhimu sana ili kupata thawabu kwa kufunga.

Kwaresima ni kipindi chenye kumbukumbu nyingi katika maisha
Kwaresima ni kipindi chenye kumbukumbu nyingi katika maisha

Kujifunza kile ambacho tumekipoteza ni hatua ya kwanza katika kugundua upya urithi wetu. Kwa namna gani tufunge kama Wakatoliki? Zamani, kufunga kulikuwa ni muhimu kwa maisha ya kikatoliki kama vile ilivyo kwa Misa ya Dominika. Karibu theluthi moja ya siku katika mwaka zilikuwa ni siku za kufunga na 2/3 ya siku zilikuwa za kujikatalia. Si siku zote za kujikatalia zilikuwa siku za kufunga, lakini siku zote za kufunga zilikuwa pia ni siku za kujikatalia. Kila mmoja wetu anapaswa kuwasha moto wa kuishi Misa, uchaji na desturi njema za Kikatoliki ili jiwe kwa jiwe, tofali kwa tofali tuujenge ufalme wa Kristo. Mtakatifu Fruktuoso, Askofu mtakatifu wa Taragon huko Hispania, wakati wa madhulumu ya Mfalme Valeriano katika mwaka 259, alichukuliwa msobe msobe kwenda kuuawa siku ya Ijumaa saa nne asubuhi. Alipopewa maji anywe aliyakataa, kwani muda wake wa kumaliza mfungo wake ulikuwa haujafika. Mtakatifu huyu japokuwa alikuwa amechoka sana kutokana na mateso ya gerezani na alikuwa na hitaji la kuwa na nguvu ili aweze kuvumilia maumivu yake ya mwisho, lakini alibaki kuwa thabiti: “Niko katika funga, hivyo nakataa kunywa maji, haijafika saa kenda; hata kifo chenyewe hakiwezi kunilazimisha mimi kuvunja funga yangu.” Huu ndio aina ya uchaji tunaopaswa kuuonesha katika mfungo wetu wa Kwaresima, katika kutii amri ya Kanisa… Unapofunga jiulize, Je, funga yangu hii ni ya toba, najutia udhaifu na upotovu wangu? Je, funga hii inafanya nijue shida na mahangaiko ya wasio nacho, hivyo kujitambulisha nao? Je, funga hii inanifanya niwe mkarimu zaidi kwa wengine, kwa utayari wangu wa kuwa karibu na na kuwasaidia kwa kadiri ya uwezo wangu? Funga yangu hii inanipa ushujaa wa kumkataa shetani na anasa zake zote? Je, funga yangu inanisaidia kuing’oa kabisa mizizi ya dhambi katika nafsi yangu?

Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu
Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu

c. Kipindi cha Kwaresima kinapaswa kutawaliwa na tabia njema, kwa kila mtu na kila familia. Tabia hii tuzipande kwenye udongo mzuri wa nafsi zetu, tuzimwagilie kwa maji ya ubatizo, tuzipalilie kwa toba na wongofu wa ndani ili mwisho Bwana wetu Yesu Kristo atujalie zawadi ya uzima wa milele. Ni tabia za kikwaresima, lakini hasa zinapaswa kuendelea kuwa tabia zetu njema za kila siku, maisha yetu yote. Kwaresima hii itujengee stamina na uwezo wa kuendelea daima na tabia hizi. Si kila mmoja anaweza kuziishi zote, inategemea, uwezo, mazingira na hali yake. Zile unazoziweza au unayoiweza iishi kishujaa, watu wakutambulishe kwa tabia hiyo. Mfano mzuri ni Familia Takatifu, wao walikuwa na tabia njema tambulishi ya familia yao, wao kila mwaka walikuwa wanaenda Yerusalemu kwenye sikukuu, hii ilikuwa ndio desturi yao (soma Lk 2:41f). Hapa tunataja desturi njema mbalimbali bila kuzingatia uzito wake: 1. Angalau siku moja kwa juma, iweke kwa mlo wa kibiblia au wa kitamaduni, achana na vyakula vya viwandani: dafu badala ya soda, muhogo badala ya mkate, ugali au ndizi badala ya baga au piza.

Ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia
Ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia

2. Bidii katika kazi, wajibika pale ulipo, usisubiri kusukumwa, tumtazame na tumwige Mtakatifu Yosefu, “mfano wa watu wa kazi.” 3. Chagua changamoto ya kimazingira. Acha kiyoyozi, maji ya baridi, panda mti, usitupe tupe hovyo chupa za plastiki na uchafu. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa kinara wa kutunza ikolojia yetu. Kwaresima hii boresha mazingira yako. 4. Funga, hata siku moja kwa juma, mf Ijumaa au kupunguza mlo, kuacha aina fulani ya chakula, mf kitimoto! Acha pombe! Huu ni wakati mzuri wa kujikatalia vile visivyo vya lazima, mf kwenda saloni! 5. Jifunze historia za watakatifu. Wafundishe watoto wako mambo ya ajabu yaliyofanywa nao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hata wewe leo, binafsi au na familia yako yote mwaweza kuwa watakatifu. Familia ya Josef na Wiktoria Umma na watoto wao wote saba kutangazwa kwao kuwa wote ni watakatifu kutokana na kifodini chao wakati wa Vita Kuu II ya Dunia, kwa kuwahifadhi Wayahudi dhidi ya Wanazi, ni mfano kwetu kuwa nasi sote twaweza kushikana pamoja kama familia na kuwa watakatifu. 6. Jifunze neno moja au mawili ya Kilatini katika juma, na hasa kile cha Misa, iwe Kyrie eleison au Pater Noster! 7. Jijengee desturi ya kujisomea Maandiko. Kumbuka maneno ya Mtakatifu Yeronimo: “Kutojua Maandiko ni kutomjua Kristo.” Kamwe hatuwezi kuwa “wakristo,” kama hatuchukui juhudi binafsi za kujisomea, kutafakari na kuweka katika matendo Neno la Mungu. 8. Jitolee, maisha yana shughuli nyingi na ni kukimbizana na muda na pesa. Saa yako moja kwa ajili ya wengine ina maana sana, kuwasaidia wahitaji, kujenga urafiki mpya. 9. Kama u mzazi, fuatilia malezi ya watoto wako: Je, wanafanya vizuri shuleni? Je, jirani wanasema nini juu yao, kweli wanapendwa na Mungu na jirani kama alivyokuwa mtoto Yesu? 10. Kuwa na kitabu chako cha sala ambao umezitunga mwenyewe kwa matumizi yako binafsi. Kumbukumbu kubwa ya pale ulipohitaji uongozi au msaada, nyakati za furaha au huzuni. Leo hii tuna sala mbalimbali maarufu, sala ya Mt. Inyasi, ni kwa kuwa kuna watu walikaa chini na kuandika fikra na tafakari zao. 11. Kuwa na moyo wa shukrani. Hakika asiye na moyo wa shukrani, si mfuasi wa Kristo. Mbele yao uwepo wema au ubaya, joto au baridi, urafiki au uadui, kusifika au kulaaniwa, uwe na shukrani. 12. Ni wakati wa sakramenti zaidi, hasa Ekaristi na Kitubio. Kwaresima hii isipite bila kwenda kuungama, aidha, usibaki tu kushiriki Misa siku za Dominika, jiongeze katikati ya juma pia.

Kwaresima ni kipindi cha sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu
Kwaresima ni kipindi cha sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu

13. Rozari ya familia, hapa na pale vikwazo, ila msonge mbele, wafundishe wanafamilia. Wahenga walituambia “Nani kama mama?” Vivyo hivyo, nasi kuwa karibu na mateso ya Yesu, kujua ukuu wa sadaka yake kwetu, tunapaswa kukaa miguuni mwa Mama Bikira Maria na kujifunza toka kwake, kutafakari pamoja naye kama watoto watii na wema. 14. Sali zaidi, weka muda maalum, pahala pa sala. Sala nikuzungumza na Mungu, huwezi kumpenda mtu bila kuwa na mawasiliano naye. Tujenge mawasiliano thabiti na Mungu kwa njia ya sala. 15. Sikiliza nyimbo za dini. Ni sehemu muhimu ya imani yetu, zenyewe zinasaidia kutuinua na kumtazama na kumsikiliza Mungu. Nyimbodini ni muhimili muhimu katika maisha yetu ya kiroho, tuwe na huzuni au furaha, bado utupa tumaini kuu la msaada wa Mungu na faraja yake. Kipindi hiki cha Kwaresima, ziwe kama kivuli chetu, popote tutembeapo, kuchota neema au kusambaza neema. 16. Tembea kwa miguu mapema asubuhi tafakari juma lililopita au lijalo. Mshukuru Mungu kwa mema yote, shukrani itakupa nguvu mpya, hewa safi ya kiroho katika mapafu yako. 17. Wahi Kanisani. Huu ni ugonjwa sugu. Hakika kama wewe ni mmoja wa “manunda” wa kuchelewa Kanisani, kama utafanikiwa angalau tu kuung’oa mzizi pori na ukorofi huu wa uchelewaji, utakuwa umepiga hatua kubwa mbele kuwa karibu na Kristo. 18. Zima mitandao ya kijamii, angalau saa moja kwa jioni moja kwa juma. Jisomee, andika sala, kaa na familia kwa masimulizi matakatifu. Haya ni machache katika hija yetu ya maisha ya kiroho, ila kila mmoja kwa neema ya Mungu ana uwezo wa kujijenga kiroho kwa kuwa na tabia njema. Tabia hii unapaswa kuianza leo, kamwe usingoje kesho, kwani kesho ni ya mchimba kaburi. Kama utajikubali kuwa wewe ni mavumbi, kwa hakika hakuna chochote kitakachoweza kukuzuia usiwe karibu na Kristo, shuhuda wa ukweli huu ni Mtakatifu Paulo Mtume:  Ni nani atakayetutenganisha na upendo wa Kristo? Je, ni dhiki, au ni shida au adha au njaa au uchi au hatari au upanga? Lakini katika mambo hayo yote tunashinda na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo wala wenye uwezo. Wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakiwezi kukutenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu (Rum 8:35ff). Kwaresima njema.

Na Padre Steno Kaombe, Parokia ya Roho Mtakatifu: Kitunda, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Jumatano ya Majivu 2024.

Kipindi cha Kwaresima
15 February 2024, 11:12