Tafuta

Ilikuwa ni tarehe 21 Februari 1998 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteua Askofu mkuu Polycarp Pengo kuwa ni Kardinali na hatimaye akamsimika, takribani miaka 26 iliyopita. Ilikuwa ni tarehe 21 Februari 1998 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteua Askofu mkuu Polycarp Pengo kuwa ni Kardinali na hatimaye akamsimika, takribani miaka 26 iliyopita.  

Kardinali Pengo Azindua Shule ya Awali ya Kardinali Pengo: Malezi na Makuzi ya Watoto

Kimsingi hii ndiyo dhamana na jukumu ambalo Shirika la Masista la Dada Wadogo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, Jimbo kuu la Dar es Salam waliyojitwaliwa kwa kuzindua Shule ya Awali ya Kardinali Pengo: “Cardinal Pengo Nursery School”, tarehe 23 Februari 2024, wakati wa Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Polycarp, Askofu na mfiadini. Shule hii ya awali imejengwa katika Parokia ya Mtakatifu Maria De Mattias, Mivumoni, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Na Daniel A. Ling’wentu, - Dar Es Salaam.

Malezi ni matendo yote yanayofanywa na wazazi, walezi na jamii kwa lengo la kumlea, kumkuza, kumlinda na kumwendeleza mtoto kimwili, kiakili, kijamii, kihisia, kiutu na kimaadili ili hatimaye aweze kuishi, kukua vizuri na kukubalika na jamii. Ili mtoto aweze kukua katika misingi hiyo muhimu yapo mambo muhimu ambayo wazazi wanapaswa kuyazingatia wakati wote wa malezi na makuzi. Mambo hayo ni pamoja na: Afya bora, anahitaji kupatiwa kinga zote dhidi ya maradhi ya kuambukiza kwa njia ya chanjo na kupatiwa tiba mara anapougua. Mazingira yanayomzunguka mtoto hayana budi kuwa katika hali ya usafi na usalama wakati wote. Mazingira hayo ni pamoja na mahali anapolala, sehemu anazochezea, mavazi na vyombo anavyotumia. Ili mtoto aweze kukua vizuri kimwili na kiakili anahitaji chakula bora au mlo kamili. Ni muhimu mtoto aliye na umri chini ya miaka mitano apate milo isiyopungua mitano kwa siku na yenye virutubisho vya kutosha. Uchangamshi ni matendo au mwelekeo unaooneshwa na mzazi au mlezi kwa mtoto kwa lengo la kuchochea ukuaji na maendeleo ya mtoto kimwili, kiakili, kimaono, kihisia, kiutu na kimaadili ambapo uchangamshi wa mtoto huanza tangu akiwa tumboni kwa mama na kuendelezwa baada ya kuzaliwa. Uchangamshi katika kipindi hiki huchangiwa kwa kiwango kikubwa na hali ya afya ya mama. Hivyo malezi na uchangamshi wa awali kwa mtoto unatakiwa uanze mara mimba inapotunga. Uangalizi unajumuisha vitendo vitakavyowezesha kuhakikisha kuwa mtoto yuko katika hali ya usalama ili kulinda uhai na maendeleo ya mtoto. Vitendo hivyo vinajumuisha kumpatia mtoto mahitaji muhimu kama vile chakula chenye virutubisho vyote, chanjo dhidi ya magonjwa na tiba mara anapougua, ulinzi na usalama, kumpakata, kuzungumza naye na kucheza nae. Hivyo inashauriwa kuwa ni vyema mtoto apewe uangalizi wa kutosha ili kumwepusha na ajali na mazingira hatarishi yatakayopelekea kuathiri afya yake, kupata ajali au kufanyiwa vitendo viovu kinyume cha kanuni maadili na utu wema.

Shule ya Awali ya Kardinali Pengo, Mivumoni, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Shule ya Awali ya Kardinali Pengo, Mivumoni, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Majirani na jamii inayomzunguka mtoto vina mchango katika malezi na makuzi ya mtoto. Ukuaji na maendeleo mazuri ya mtoto yanachagizwa na mahusiano mazuri na watoto wenzake, walimu wake na watu wengine wanaomzunguka. Kimsingi hii ndiyo dhamana na jukumu ambalo Shirika la Masista la Dada Wadogo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, Jimbo kuu la Dar es Salam waliyojitwaliwa kwa kuzindua Shule ya Awali ya Kardinali Pengo: “Cardinal Pengo Nursery School”, tarehe 23 Februari 2024, wakati wa Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Polycarp, Askofu na mfiadini. Shule hii ya awali imejengwa katika Parokia ya Mtakatifu Maria De Mattias, Mivumoni, Jimbo kuu la Dar es Salaam na iko chini ya uongozi wa Padre Edwin Kigomba.  Ilikuwa ni tarehe 21 Februari 1998 Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteua Askofu mkuu Polycarp Pengo kuwa ni Kardinali na hatimaye akamsimika, takribani miaka 26 iliyopita. Hii ndiyo historia inayoandikwa na “Shule ya Awali ya Kardinali Pengo”, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Hili ni tukio ambalo katika mahubiri yake, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam amelikumbuka. Amelishukuru Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Francisko, Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kumuenzi, alipokuwa anafanya pia kumbukizi la Mtakatifu Polycarp.

Kardinali Pengo anawashukuru Wadada Wadogo, Jimbo kuu la Dar Es Salaam
Kardinali Pengo anawashukuru Wadada Wadogo, Jimbo kuu la Dar Es Salaam

Kardinali Pengo amesema kwamba, Mtakatifu Paulo VI wakati fulani aliwahi kusema kwamba, alitamani kurudia utoto, ili kuweza kujifunza thamani na maana ya shule ya familia. Kimsingi, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kardinali Pengo amesema, kuna mabadiliko makubwa kati ya shule za awali, enzi yake na hizi zinazojengwa kwa wakati huu. Anamwomba Mwenyezi Mungu apokee jitihada na gharama zote zilizowekwa ili kuwaandalia watoto mazingira bora ya kusomea. Amewaalika wale waliohudhuria tukio hili, kuwakumbuka na kuwaombea wale wote watakaopewa dhamana ya kusimamia mahali hapa, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ari na moyo mkuu. Imekuwa ni fursa ya kuliombea Kanisa katika ujumla wake. Amelishukuru na kulipongeza Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Francisko, Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa heshima waliotumtunukia mahali hapa na Mungu Mwenyezi awe pamoja nao: Leo, Kesho na Hata Milele. Kwa upande wake, Sr. Doreen Bella Mwakaliku, Mhudumu mkuu wa Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, Jimbo kuu la Dar es Salaam kama sehemu ya utekelezaji wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” kwa kupanda miti.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote
Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote

Baba Mtakatifu Francisko anaonekana kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi, kwa kuimba utenzi wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia na kwa kukazia umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina mapana, jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiikolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pamoja na mambo mengine kuung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

Kardinali Pengo
28 February 2024, 14:32