Tafuta

Kauli mbiu ya Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ni “Mimi ni BWANA Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri kutoka utumwani" (Kut 20:2). Kauli mbiu ya Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ni “Mimi ni BWANA Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri kutoka utumwani" (Kut 20:2). 

Dominika ya Kwanza Kwaresima Mwaka B: Toba Na Wongofu wa Ndani

Kipindi hiki cha Kwaresima kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa usemao: “Mimi ni BWANA Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri kutoka utumwani" (Kut 20:2). Huu ni muhutasari wa amri kumi za Mungu, zilizopokewa na Musa juu ya Mlima Sinai. Huu ni muda wa kufunga na kusali; kusoma, kutafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika matendo adili na matakatifu ni wakati wa kujikita katika Injili ya huruma na upendo!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Leo ni Dominika ya kwanza ya kipindi cha Kwaresima cha Mwaka B, Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Kwaresima ni neno lenye asili ya lugha ya Kilatini, na maana yake ni “Arobaini” kwa hiyo, Kwaresima yadumu siku arobaini. Kama tulivyopigiwa mbiu Jumatano ya majivu juu ya safari ya siku arobani za kufanya metanoia ya kweli tukiongozwa na kristo mteseka. Tunaendelea kuhimizwa kurarua mioyo yetu katika dhana ya kutubu na kuimini injili ndiyo Neno la Mungu aliyetwa mwili akakaa kwetu nasi tukawa na uzima, sasa baada ya dosari hizo tunaitwa tena ili tujirekebishe katika ufuasi wetu. Kipindi hiki cha Kwaresima kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa usemao: “Mimi ni BWANA Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri kutoka utumwani" (Kut 20:2). Huu ni muhutasari wa amri kumi za Mungu, zilizopokewa na Musa juu ya Mlima Sinai. Watu wanajua vizuri kile ambacho Mungu anazungumzia: uzoefu wa utumwa bado umechapishwa katika mwili wao. Anapokea maneno kumi jangwani kama njia ya uhuru wa kuchagua kufata au kukaidi. Tunaziita "amri," huu ni msisitizo wa wazi wa nguvu ya upendo ambayo kwayo Mungu huwaelimisha watu wake. Kwa kweli, ni wito wa nguvu kwa utashi na uhuru wa wanadamu kuitikia.

Huu ni mwaliko wa kuingia katika jango la maisha yako.
Huu ni mwaliko wa kuingia katika jango la maisha yako.

Ufafanuzi: Katika somo la kwanza ( Mwa 9:8-15) tunasikia masimulizi ya tukio la janga la kiasi yaani mafuriko makubwa mintarafu gharika, kama vile Nuhu alivyokaa ndani ya safina siku arobaini kabla ya kupewa agano na Mungu la kutoharibu tena ulimwengu kwa Gharika Kuu, au Gharika la Nuhu. Kama vile Yesu alivyofunga siku arobaini jangwani kabla ya kuanza kazi yake; basi nasi tunapata nafasi ya siku arobaini za kuyachunguza maisha yetu kwa kufanya toba, kusali na kufunga, na kutenda matendo mema. Siku arobaini maana yake ni siku za kutosha. Arobaini ni namba ya ukamilifu. Hali hii haishii katika tukio moja la mahangaiko, kwa sababu inakomaa katika safari kurudi nchi ya ahadi. Kama vile Israeli bado ina Misri ndani yake jangwani, vivyo hivyo leo watu wa Mungu hubeba ndani yao vifungo vya ukandamizaji ambavyo lazima wachague kuachana navyo. Tunatambua hili wakati tunakosa tumaini na kutangatanga katika maisha kama vile katika nchi ya ukiwa, bila nchi ya ahadi ya kujitahidi kuifikia. Kwaresima ni wakati wa neema ambao inakuwa ni safari ya jangwani, katika maisha ya uongofu, kama nabii Hosea anavyotangaza - mahali pa upendo wa kwanza (taz. Mungu anawaelimisha watu wake ili waweze kutoka utumwani mwao na kupata uzoefu wa kupita kutoka kifo hadi uzima (Anakazia Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2024.)

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha

Mwaliko tunaoupata katika Injili ya leo ni huu: “tubuni na kuiamini Injili”. Kwa nini tutubu na kuiamini Injili? Kwa sababu wito wetu wa msingi ni kufika mbinguni kwa Baba. Hatuwezi kufika mbinguni kwa Baba bila kutubu na kuiamini Injili. Tunayo miito mingi sana katika Kanisa letu; wito wa ndoa, wito wa utawa, wito wa upadre na mambo mengine, lakini wito wetu msingi ni kuwa watakatifu na kuishi na Mungu milele mbinguni. Tunaweza kujiuliza swali: Tunawezaje kufika huko mbinguni kwa Baba? Injili tuliyoisikia leo, imetupatia jibu: ili tuweze kufika mbinguni ni lazima tutubu na kuiamini Injili. Yesu katika Injili ya leo anaanza kutuhubiria Habari Njema kwa kutuambia, “Tubuni na Kuiamini Injili”. Ili Kwaresima yetu iwe thabiti, hatua ya kwanza ni kutaka kuona ukweli. Wakati Bwana alipomvuta Musa kwenye kichaka cha moto na kuzungumza naye, mara moja alijifunua kama Mungu ambaye anaona na, zaidi ya yote, anasikia Yesu anatambua hali yetu ya dhambi na anatutaka tusimame kila tunapoanguka. Pili Yesu anatutaka tuiamini injili. Tuiamini injili inapotuambia Yesu ndiye njia, ukweli na uzima, mtu hawezi kwenda kwa Baba ila kwa njia yake (Yoh.14:6). Tuiamini injili inayotuambia mapadre wamepewa uwezo wa kumfungia mtu duniani akafungiwa na mbinguni na uwezo wa kumfungulia mtu duniani akafunguliwa na mbinguni (Yoh.20:21-23). Tuiamini injili inayotuambia yule atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokoka (Mt 24:13).  Ukweli huu umejidhihirisha katika masomo yote matatu tuliyoyasikia leo. Katika somo la kwanza Nuhu na familia yake wanaokolewa na gharika kwa sababu  walitubu na kuamini maneno ya Mungu.

Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu
Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu

Somo la Pili (1Pet 3,18-22) linatuambia maji yaleyale yaliyowaangamiza wenye dhambi wakati wa Nuhu, sasa ndiyo yanayotuokoa sisi kwa ubatizo. Kwaresima ni wakati wa kutenda mema na  kuacha mabaya . Kutulia katika sala, kupokea Neno la Mungu, na kupumzika kama Msamaria, mbele ya ndugu yake aliyejeruhiwa. Upendo wa Mungu na jirani ni upendo mmoja. Kuwa na miungu mingine ni kuacha upendo mbele ya Mungu, katika mwili wa jirani yake mteseka. Kwa sababu hii, sala, sadaka na kufunga sio mazoezi matatu huru tu, lakini ni harakati moja ya uwazi, ya kuondoa: nje na sanamu zinazotuweka, mbali na vifungo vinavyotufunga hasa upendo Ndugu zangu wapendwa, fundisho la kwanza kabisa la Katekisimu, linasema; “Tupo duniani ili tumtumikie Mungu, tumpende na mwisho tufike kwake mbinguni” Kumtumikia Mungu ni kuishi kadiri ya matakwa yake; yaani kuzishika amri, hasa amri kuu ya mapendo. Tuwapende wenzetu, tuwapende wagonjwa, yatima, wazee na wenye shida mbalimbali, hasa wale wanaobaguliwa na kuonewa kwa ajili ya ulemavu wao wa viungo na ngozi tuwasaidie. Huku ndiko kuiamini injili ya Kristo. Kipindi cha Kwaresima ni kipindi muhimu sana kwetu sisi Wakristo. Ni kipindi ambacho tunaonja huruma kuu ya Mungu anayetuita tushiriki uzima wa milele licha ya udhaifu na dhambi tulizo nazo kwa sharti rahisi kabisa: kutubu na kuiamini Injili. Wapendwa, Mungu anapendezwa sana na unyenyekevu wetu pale tunapotambua makosa yetu na kuyaungama. Kutoungama dhambi ni kiburi na majivuno tu ya mtu. Ingelikuwa heri leo msikie sauti yake, msiifanye migumu mioyo yenu (Zab. 95:8). 

Kwaresima ni kipindi cha sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu
Kwaresima ni kipindi cha sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu

Tubuni na kuiamini Injili. Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha kufunga na kusali. Unaposali kwa unyenyekevu unaongea na Mungu. Nikuambieni, hakuna furaha anayoweza kuipata mwanadamu inayopita furaha aipatayo anapoongea na Mungu ambaye ndiye uzima wake, furaha yake na vyote alivyo navyo. Tulio wengi hatujui siri ya furaha hii, hatuitumii nafasi hii adimu na ndiyo maana tuna huzuni mpaka tunazeeka kabla ya wakati. Mungu tunamwona kama kitu cha ziada kwetu. Si ajabu utamsikia mtu akisema “Mimi huwa nasahau kusali kila siku” lakini mtu huyohuyo hajawahi kusahau kula, kuvaa au hata kupiga mswaki tu. Maana yake, kwake kupiga mswaki kuna umuhimu zaidi ya Mungu. Kila mmoja ajiulize amemdhihaki Mungu namna hii mara ngapi? Mpenda msikilizaji na msomaji kumbuka kuwa Yesu aliyashinda majaribu ya shetani kwa kufunga na kusali. Hata sisi tutambue kuwa kamwe hatuwezi kumshinda shetani bila silaha hizi, muhimu tunapofunga na kusali kipindi hiki cha Kwaresima, tusali na kuomba mambo yafuatayo; umoja wa Kanisa, umoja wa WaKristo, amani ya dunia, upendo katika familia, bidii katika kazi, maelewano na maridhiano, ndani ya Kanisa, Ukristo na Dini nyingine, moyo wa toba, uvumilivu katika mateso taifa na taifa, watawala na wwatawaliwa na mambo mengine.Lakini Yesu Kristo ambaye ndiye Simba wa Yuda anatuambia; “Mimi nimeushinda ulimwengu na wala msifadhaike”. Wa kutupigania tunaye, yule asiyeshindwa kamwe. Wajibu wetu sisi ni kumwomba. Ndiyo maana nawaombeni kila mmoja wetu amwombe Mungu amwondoe huyu shetani anayetugawanya hata sisi Wakristo.

Mungu akaweka Agano na Binadamu baada ya Gharika Kuu
Mungu akaweka Agano na Binadamu baada ya Gharika Kuu

Tuombeane mema sisi kwa sisi, tupendane sisi kwa sisi, ili watu wajue kuwa sisi ni wanafunzi wa Yesu. Mtume Yakobo anatuambia hatuna kitu kwa sababu hatuombi, na hata tukiomba twaomba vibaya ndiyo maana hatupati (Yak.4:2). Tupo wengi tunaokwenda makanisani kuwaombea wengine mabaya yawezekana hata wewe unayesikiliza na kusoma tafakari hii ni mhanga mkubwa wa kilema hiki cha chuki na wivu kwa wengine sasa wokovu umekufikia badili tabia na mitazamo yako isiyo na afya ya roho, akili mwili na hata kijamii katik kuhusiana. Jambo hili halifai kabisa machoni pa Mungu. Omba sala ni ombi jema daima! Lenye ukarimu pia kwa wengine sio kwaajili yako tu Tuombeane mema na rehema daima! Basi tuombe neema ya Mungu itusaidie hasa katika kipindi hiki muhimu, tujaliwe unyenyekevu wa kutubu makosa yetu na kuiamini Habari Njema ya wokovu tuwe dhaifu katika kumtegemea Mungu na tuwe waoga katika kutenda dhambi na kama tunanguka tuinuke mara na haraka kwenda kwenye kitubio na upatanisho ili tuwe na amani na Mungu wetu na jirani zetu.

Liturujia ya Kwaresima D1
16 February 2024, 08:58