Tafuta

Asubuhi ya maisha ya kiroho na ya wito ni kipindi cha kujenga na kuweka misingi. Mchana huwa si muda mzuri sana katika wito na maisha ya kiroho mchana sio kipindi rahisi kwani kina changamoto zake. Asubuhi ya maisha ya kiroho na ya wito ni kipindi cha kujenga na kuweka misingi. Mchana huwa si muda mzuri sana katika wito na maisha ya kiroho mchana sio kipindi rahisi kwani kina changamoto zake. 

Asubuhi, Mchana na Jioni ya Maisha ya Wito wa Kila Mkristo! Uzoefu wa Abrahamu

Asubuhi ya maisha ya kiroho na ya wito ni kipindi cha kujenga na kuweka misingi. Katika wito na maisha ya kiroho mchana sio kipindi rahisi. Mababa wa Kanisa wanakiita kipindi cha uchovu na anayeleta uchovu ni yule anayeitwa “pepo wa mchana.” Jioni ya wito ni kipindi cha ukomavu. Ndipo hapa unaanza kuingia ukomavu wa maisha, ukomavu wa kichungaji, wa wito na vyote hivi vinajionesha katika namna ya maisha na katika uzito wa mang’amuzi ambayo mtu anayafanya.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Asubuhi ya maisha ya wito huendana endana na muda wa ujana au hatua za mwanzo za malezi au za utume. Ni kipindi kizuri kinachosheheni matumaini makubwa ya baadaye kama vile tu siku inapoanza mtu akiwa na matumaini na mipango mbalimbali. Asubuhi ya maisha ya kiroho na ya wito ni kipindi cha kujenga na kuweka misingi. Mchana huwa si muda mzuri sana katika wito na maisha ya kiroho mchana sio kipindi rahisi. Mababa wa Kanisa wanakiita kipindi cha uchovu na anayeleta uchovu ni yule anayeitwa “pepo wa mchana.” Jioni ya wito ni kipindi cha ukomavu. Ndipo hapa unaanza kuingia ukomavu wa maisha, ukomavu wa kichungaji, wa wito na vyote hivi vinajionesha katika namna ya maisha na katika uzito wa mang’amuzi ambayo mtu anayafanya. Huu ni muhtasari wa tafakari ya Kipindi cha Kwaresima iliyotolewa na Padre William Bahitwa kwa Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, JWWI, Dominika tarehe 25 Februari 2024 kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Paulo, kilichoko mjini Roma. Maisha ya kiroho ni safari. Yana mwanzo wake, yana hatua na vituo vyake mbalimbali na yana lengo lake ambalo ni kuishi vema hapa duniani na kufikia utimilifu wa maisha kwa Mungu mwenyewe. Mababa wa maisha ya kiroho wameyafananisha na nyakati za siku (asubuhi, mchana na jioni) Thomas Halik (Mwandishi wa Kitabu “Pomeriggio del cristianes imo”) amechambua historia ya ukristo: asubuhi inaendana na kipindi cha mwanzo cha uinjilishaji, mchana na kipindi cha changamoto na jioni kipindi cha ukomavu.  Tukiingia katika maisha ya kiroho na hasa safari ya wito, mchanganuo huo una ukweli wake. Asubuhi ya maisha ya wito huendana endana na muda wa ujana au hatua za mwanzo za malezi au za utume. Ni kipindi kizuri na kilichojaa matumaini makubwa ya baadaye kama vile tu siku inapoanza mtu akiwa na matumaini na mipango mbalimbali. Asubuhi ya maisha ya kiroho na ya wito ni kipindi cha kujenga na kuweka misingi.

Asubuhi ya maisha na wito ni muda wa kujenga msingi
Asubuhi ya maisha na wito ni muda wa kujenga msingi

Mchana huwa si muda mzuri sana katika wito na maisha ya kiroho mchana sio kipindi rahisi. Mababa wa Kanisa wanakiita kipindi cha uchovu na anayeleta uchovu ni yule anayeitwa “pepo wa mchana” – “demon of the midday; il demone di mezzogiorno.” Papa Francisco ametumia pia msemo huu katika katekesi yake ya wiki iliyopita aliyoitoa siku ya jumatano ya majivu. Ni kipindi ambacho anaanza kuchoka. Ile hamasa aliyokuwa nayo asubuhi inaanza kupungua, matumaini hali kadhalika, anaanza kuona vitu kuwa ni vya kawaida tu n.k. Mtu akivuka kipindi hicho anaingia jioni katika kipindi cha jioni ya wito na ya maisha ya kiroho. Jioni ya wito ni kipindi cha ukomavu. Ndipo hapa unaanza kuingia ukomavu wa maisha, ukomavu wa kichungaji, wa wito na vyote hivi vinajionesha katika namna ya maisha na katika uzito wa mang’amuzi ambayo mtu anayafanya. Lakini pia jioni hii inaweza kuwa ni wakati mbaya. Tunasikia mara kwa mara watu wanasema “huyu mzee anazeeka vibaya.” Unakuwa ni wakati wa kukata tamaa kwa sababu labda mtu anaona yale matumaini aliyoanza nayo hayapo tena na hayawezi kutimia. Anaangalia nyuma anapata hasira na kuanza kulaumu watu, kulaumu taasisi n.k na kwa kifupi mtu anaanza kuwa mchungu na mwenye hasira. Katika tafakari yetu ya leo ninawaalika tuipitie safari yetu ya wito katika mchanganuo huo, tukiongozwa lakini na maisha ya Babu yetu wa Imani: Abraham.

Mchana si muda mzuri wa maisha na wito; kuna uchovu!
Mchana si muda mzuri wa maisha na wito; kuna uchovu!

ASUBUHI YA ABRAHAM: Somo: Mwanzo 12: 1-9. Kifungu hiki kinaelezea wito wa Abraham. Abraham, mwenye umri wa miska 75 anapokea wito kutoka kwa Mungu mwenyewe, “Toka katika nchi yako, na jamas zako na nyumba ya baba yak, under mpaka nchi nitakayokuonesha… Basi Abraham akaenda (akatoka). Hapa hatuelezwi mengi kutusu Abraham, ila tukirudi nyuma katika sura ya 11 kuanzia aya ya 28 Tunaona kuwa Abahamu alikuwa akiishi maisha ya kawaida kabisa kati ya ndugu zake. Wito unafungua ukurasa mpya katika maisha yake. Kutoka maisha ya kukaa kwa utulivu mahali pamoja, Abraham anakuwa mtu wa kuhama hama. Lile neno “toka” linakuwa ndio ufafanuzi wa maisha atakayoishi. Pamoja na hayo yote, Abraham anapokea wito wake kwa utayari mkubwa. Anaambiwa “toka” naye anaondoka. Na hapa ndipo, katika Maandiko Matakatifu, inapozaliwa imani. Tefsiri ya kiyahudi inatumia mzizi ule ule wa neno “lek - wayyelek”: ndiyo kusema “toka - akatoka”, “nenda – akaenda.” Abraham anakuwa ni wa kwanza kuitikia namna ile ile ambavyo Mungu amemtaka. Na biyo ndiyo imani: kuwa tayari kuitikia moja kwa moja na kwa namna ile ile ambayo sauti ya Mungu imekutaka. Abraham anakuwa Baba wa Imani na anafungulia mlango wa watu kujenga mahusiano mapya na Mungu kwa njia ya imani, yaani kuitikia kuyatekeleza mapenzi ya Mungu. Abraham anapokea wito wake bila kuhoji. Anaupokea bila kuchelewa na bila kusita. Anaondoka asijue anakokwenda, anachojua ni kimoja tu kwamba ameitwa na yeye ana imani na yule aliyemwita na ana imani na kile alichoitiwa. Hii ndiyo asubuhi ya Abraham. Tunaweza kuielezea kama asubuhi yenye ari ya kuteleleza kilicho mbele, asubuhi yenye kupokea bila kufikiria nia mbaya upande wa pili, asubuhi njema.

Asubuhi ya maisha ya wito ni kipindi cha ujana! Wakati wa kupiga suti!
Asubuhi ya maisha ya wito ni kipindi cha ujana! Wakati wa kupiga suti!

ASUBUHI YETU: Asubuhi ya Abraham itusaidie na sisi kuitazama asubuhi yetu. Na hapa ingependeza kila mmoja akajikumbusha historia ya imani yake na hasa historia ya wito wake. Asubuhi ilikuwaje? Au ikoje? Asubuhi ya miaka ya seminarini au katika nyumba za kitawa. Asubuhi ya utume baada tu ya upadrisho au kuweka nadhiri. Ile hamu kubwa sana ya kuwa Padre au kuwa mtawa, yaani mtu hakuambii kitu: ni wewe na kanisani, kanisani na wewe. Ni wewe na konventi, konventi na wewe. Kipindi hicho, kila kitu ni kizuri na kinavutia. Asubuhi ya upadrisho ndio usiseme! Kila mmoja ana historia yake. Historia zetu tofauti tofauti zinaunganishwa na hamasa. Asubuhi ya malezi, asubuhi ya wito ni asubuhi iliyojaa hamasa na matumaini makubwa. Zipo pia asubuhi zenye giza, pale ambapo mwanzo unakuwa hauleleweki. Maswali yanakuwa mengi kuliko majibu n.k. Lakini hata katika asubuhi za namna hiyo matumaini kuwa jua litachomoza na giza litaondoka ni makubwa. Matumaini hayo ndiyo huchochea hamasa na hutupa nguvu ya kuendelea. Tuwapo asubuhi ya maisha yetu ya wito, Kanisa halituachi tu twende mbele kwa nguvu ya hamasa tuliyonayo. Linatusaidia kukiishi kipindi hicho katika kujiunda. Maelekezo msingi linayotoa katika nyaraka za malezi kama vile: “Optatam Totius” na “Vita consacrata,” zote hizo huzungumzia kitu kinachoitwa “Malezi Fungamani”. Haya ni malezi yanayojumuisha malezi ya kiutu, ya kiroho, ya kiakili na ya kichungaji. Ni kipindi ambacho kinatusaidia kujenga misingi itakayotuwezesha kuyaishi na kuyatekeleza matakwa na madai ya wito wetu. Na msingi hauji tu kwa sababu vitu vya msingi tunavielewa. Unakuja hasa kwa sababu vitu vya msingi tunaviishi, yaani polepole tumevifanya kuwa sehemu ya maisha yetu. Silabasi ya masomo na malezi yetu ukiiangalia vizuri unaweza kuimaliza kwa muda mfupi sana. Lakini tunaambiwa hapana, ruhusu muda upite. Na wakati huohuo tunajengewa mzunguko katika ratiba; ratiba ya siku, ratiba ya wiki, ratiba ya mwezi, ratiba ya mwaka n.k. Tunapofika Roma pia tuna asubuhi yetu. Ukiachilia mbali changamoto ya lugha, ya hali ya hewa, ya kukimbiia mabasi; asubuhi ni nzuri na imejaa furaha na matumaini.

Ukifika Roma kuna changamoto zake pia na wala maisha si maji kwa glasi
Ukifika Roma kuna changamoto zake pia na wala maisha si maji kwa glasi

MCHANA WA ABRAHAM: Somo I: Mwanzo 12:10-20. Nini kinatokea? Inatokea njaa. Abraham analazimika kwenda Misri ili kutafuta chakula. Kitendo cha kwenda Misri atakuja kukirudia Yakobo, pale atakapotuma wanawe kwenda huko kutafuta chakula. Kama tunavyofahamu, huko wanamkuta Yosefu waliyemuuza na unakuwa ni mwanzo wa familia nzima ya Yakobo kuhamia huko moja kwa moja. Familia Takatifu pia illikimbilia Misri ili kujiokoa kutoka kwa Herode. Anachokifanya Abraham kinakuwa ni kitu cha ajabu kidogo. Anakuwa kama mtu ambaye ule wito hana tena. Ule wito ambao ulimtoa katika mazingira yake, ukamuunganisha kwa namna ya pekee na Mungu kwa njia ya ahadi mbalimbali ni kama haupo tena. Abraham anakumbwa na hofu kubwa na katika hofu yake hiyo anajiona peke yake, Mungu hayupo. Hofu ya Abraham inatokana na nini? Anaogopa kuuwawa kwa sababu Sarai mkewe ni mzuri. Anachoamua ni kumwambia Sarai asiseme kuwa Abraham ni mmewe bali aseme ni kaka yake. Abraham anamruhusu mkewe achukuliwe na Farao kama mke ili tu yeye aweze kupona. Ili kuokoa maisha yake, Abraham anakuwa tayari kumkana mkewe, anakuwa tayari kudanganya na mbaya zaidi anakuwa tayari kumuuza mkewe kwa Farao ili kujiokoa. Iko wapi hamasa aliyokuwa nayo katika wito, yako wapi matumaini yake, iko wapi imani yake? Hii inatukumbusha matukio mengine mawili: Simulizi la ndama wa dhahabu: Kutoka 32, 1-6 wako jangwani, Musa kiongozi wao hayupo, wanaamua kujitafutia usalama wao wenyewe nje na bila ya Mungu. Simulizi la Petro kumkana Yesu: Luka 22, 54-60 Petro ili kujiokoa anamkana Yesu, anawakana wenzake na anamalizia kwa kuikana hata asili yake (identity). Somo II: Mwanzo 16, 1-4. Tukirudi kwa Abraham, tukio lingine tunaliona Mwanzo 16, 1-4. Abraham anaona Mungu amemdanganya kupata mtoto. Mungu yule yule aliyemtokea akampa wito, akambariki na kumpa ahadi, ndiyo huyo huyo Abraham anayeona amemdanganya na kwamba hatapata tena mtoto. Anapokea ushauri wa Sarai, anazaa na mjakazi wake Hajiri.

Mchana ni kipindi cha uchovu na hali ya kujikatia tamaa
Mchana ni kipindi cha uchovu na hali ya kujikatia tamaa

MCHANA WETU: Kutoka katika mchana wa Abraham, tuuangalie na sisi mchana wa maisha yetu ya wito. Mchana wetu, kama ulivyokuwa mchana wa Abraham, unachochewa na kutawaliwa na matatizo. Kuna vitu vinaingia katika safari yetu ya wito vinakausha uhai wake. Ile hamasa inapotea, nguvu zinapungua na ladha inaanza nayo kupungua. Seminari au malezini ulipoingia ukapaona ni mbinguni panageuka kuwa jehanam; mapadre wenzako, watawa wenzako wanakuwa ndio wapinzani wakubwa; askofu ambaye mwanzoni alikuwa ni kila kitu unaanza kumtoa kasoro - ndogondogo na zingine kubwa kubwa. Na hata unapojiangalia mwenyewe, ni kama unaona mambo hayaendi. Utagunduaje uko katika hatua hii? Papa Francisko, kwenye hiyo Katekesi niliyoitaja mwanzoni, amezungumza juu ya kilema cha uvivu. Na yeye mwenyewe alisema neno hilo Uvivu kimsingi halielezei vizuri sana kilema hicho kwa sababu uvivu ni matokeo ya kilema hicho na sio chanzo. Chanzo chake ni kile kinachoitwa kwa kiitaliano accidia. Katekisimu ya Kanisa Katoliki kwa Lugha ya Kiswahili imetumia neno “Utepetevu.” Papa anasema, kwa anayekumbwa na utepetevu huu, maisha hupoteza maana, sala hugeuka kuwa mzigo. (ule mchapo nadhani mnaufahamu, wa yule mmonaki ambaye maisha yake ya sala yalianza kushuka kwa kasi. Ikafika wakati sala ya kula ndiyo ikawa sala yake ya kwanza ya siku. Hali ilivyozidi kuwa mbaya, sala hiyo ya kula ikawa ndiyo sala pekee ya siku. Baadaye, akaacha kabisa hata kuisali. Hapo ndipo akaanza kuangalia sahani ya chakula chake mezani haelewi. Anaona chakula kibaya kama makapi. Wamonaki wengine wakawa wanamwambia mbona chakula hiki hiki ndio umekila kwa zaidi ya mika 20 hapa utawani). Ladha ya sala ilipotea, ladha ya chakula ikapotea pia.

Mtu akivuka kipindi cha mchana anaingia kipindi cha jioni cha maisha ya wito.
Mtu akivuka kipindi cha mchana anaingia kipindi cha jioni cha maisha ya wito.

Papa Francisko anaendelea kusema kuwa mtu mwenye “accidia” utepetevu haweki tena juhudi katika lolote. Hata kama ujanani au hapo mwanzo alikuwa na juhudi na bidii za kufanya mambo, anajitolea huku na kule, juhudi zote hizo zinaonekana hazina maana. Anakata tamaa. Anakuwa ni kama mtu ambaye tayari ameshakufa lakini bado anaishi. Nini kinatufikisha hapo? Kama ilivyokuwa kwa Abraham, mchana wa wito wetu huathiriwa na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali zinazotukumba (Crisis). Ukiuangalia mchana kama umri wa kati, hapo ndipo utasikia pia changamoto za umri wa kati. Matatizo yapo na yanaweza kumkumba yeyote. Matatizo haya yanaweza kuwa yametoka ndani mwetu lakini pia yanaweza kuwa yametoka nje hasa katika vitu ambavyo hatuna uwezo navyo kwa mfano ugonjwa. Kwa bahati mbaya watu huwa tunaweka juhudi kubwa kuepuka matatizo tunasahau kujiandaa pia kwa namna ya kuyatatua au kuyakabili pale yanapotokea. Matatizo yanayotokana na sisi yanaweza kusababishwa na vitu tunavyoweza kuviita “viporo vya asubuhi yetu” yaani mapungufu katika kile kipindi cha kujenga misingi au kipindi cha mwanzo cha utume. Wakati mwingine kuna vitu mtu ameanza kuvipalilia asubuhi, au pia kuvipunguza kimoja kimoja. Vitu hivi vinapokua vinaweza kugeuka kuwa kitanzi kwetu. Yapo pia matatizo yanaweza kutukumba kutoka nje. Unaweza kuja ugonjwa unakubadilisha kabisa mfumo wa maisha. Tatizo lingine kubwa linalotukumba kutoka nje ni kule kuwa mhanga wa mazingira (victim of the circumstances): mfano: ubaguzi wa rangi, wa utaifa, wa ukabila, wa kipato n.k katika jumuiya; kueleweka vibaya na kuwekewa “lebo” - mkorofi, mbishi, hawezi chochote, hana moyo wa shirika n.k. Ni kwa namna gani tunaweza kuuishi mchana wa maisha yetu ya wito? Viporo vya asubuhi hivyo vinatuhitaji kurudi kwenye njia tuliyoipoteza. Ndiyo kurudi kukubali kujifunza na kujijengea mazoea yanayokoleza maisha ya wito na kuyarudishia ladha.

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani: Rudi!
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani: Rudi!

Toba na wongofu wa ndani; Kurudi ndio neno ambalo kipindi hiki cha Kwaresima linalitumia kutualika kutubu, kuongoka na kumrudia Mungu. Kurudi ni kubadili njia, kurudi ni kukubali kuwa umekosa shabaha. Papa Francisko amegusia kitu kimoja cha pekee sana ambacho anapendekeza kinaweza kusaidia kuikabili hali hii ya “pepo wa mchana katika wito.” Anaiita “uvumilivu wa imani” - pazienza della fede. Katika hali ngumu inayoweza kuukumba mchana wa wito wetu, uvumilivu wa namna hii unahitajika. Huu sio ule uvumilivu wa kusema “sina cha kufanya, ninasubiri litakalotokea na litokee.” Sio uvumilivu wa namna hiyo. Ni uvumilivu wa imani, yaani katika kuvumilia hali isiyoeleweka, imani inakuambia Mungu yupo. Mungu yupo na wewe. Mungu yupo na wewe akuokoe. Uvumilivu wa imani ndio unaotusaidia kuvishinda vile Vilema sugu, kuzishinda zile dhambi sugu na zile hali ambazo hazieleweki wala hazielezeki. Uvumilivu wa imani Ndio unaokupa ujasiri wa kukiambia kilema chako “wewe kilema wewe, nitese tu sasa hivi Ila jua kuna siku ntakushinda na hutaniangusha tena.” Ndio unaokupa ujasiri kuiambia dhambi inayokutesa mara kwa mara “wewe Dhambi wewe nitese tu, siku zako zinahesabika. Iko siku nitasimama na sitaanguka tena” uvumilivu wa imani unakusaidia kuona upande mzuri wa maisha yako na hasa unakusaidia kuona Mungu hajakuacha. Mtakatifu Yohane wa Msalaba aliongea juu ya kipindi cha giza la roho. Kipindi ambacho ni kama Mungu amejificha, haonekani lakini ni kipindi ambacho roho inatakaswa inapendelea kupiga hatua kumuelekea Mungu. Nilishangaa sana niliposikia kuwa Mama Teresa, kwa miaka mingi aliishi kipindi hiki cha ukimya wa Mungu. Alipokuwa walikuta katika maandishi yake anaeleza kuwa kwa muda mrefu alikuwa haonji ile ladha ya sala. Pamoja na hayo alisali sana, alitafakari sana hasa nyakati za asubuhi na alipotoka hapo aliendelea kwa furaha na utume wake kana kwamba hana ugumu katika maisha yake binafsi ya kiroho.

Tunahitaji uvumilivu wa imani
Tunahitaji uvumilivu wa imani

JIONI YA ABRAHAM: Masomo: Mwanzo 13: 8-12 Abraham na Lutu wanatengana. Abraham anatambua umuhimu wa kutunza mahusiano mazuri na ndugu yake. Anatambua kuwa amani ni ya muhimu zaidi huenda hata kuliko kulinda himaya yae na mifugo wake. Zaidi ya hayo anampa Lutu nafasi ya kwanza kuchagua eneo la kwenda yeye na mifugo yake. Yohane Krisostom anasema Lutu alichagua kulingana na tamaa zake, Abraham akachagua kulingana na uadilifu wake. Mwanzo 14: 8-16. Abraham anaunda Jeshi kwenda kumwokoa Lutu. Mwanzo 18: 20-32 Abraham anautetea mji wa Sodoma usiharibiwe. Abraham, mtu mmoja tu, mwadilifu anakuwa ile nguzo imara anayoizungumzia Mt. Ambrose, nguvo ambayo moja tu ina uwezo wa kusimama mbele ya Mungu kutetea nchi nzima. Mwanzo 22: 1-18 Abraham anakuwa tayari kumtoa sadaka mwanae Isaka. Vifungu hivi vichache kati ya vingi vinavyomwonesha Abraham aliyekomaa. Jioni yake ni jioni ya mtu mwenye busara, mwenye mang’amuzi na ni mtu aliyetulia. JIONI YETU: Jioni yetu ni wakati wa ukomavu; ukomavu wa imani, ukomavu wa wito, ukomavu wa maisha ya kitawa, ukomavu wa kichungaji n.k. Ukomavu huu unaweza kuendana na muda au umri lakini si mara zote huwa hivyo. Tunaambiwa kuwa “kukua ni matokeo ya muda” lakini “kukomaa ni mpaka mtu aamue.” Jioni ya maisha ni pale mtu anapofika mahali akakubali kwamba yote aliyopitia katika maisha yamemfundisha. Na kukubali huku kunaendana na kuchukua sasa hayo mafundisho ambayo maisha yamekupatia. Mambo tunayopitia, yawe ni mambo chanya au mambo hasi hutupa uzoefu na hutujenga. Hutuondoa katika ile nadharia ya maisha na hutuingiza katika uhalisia wa maisha (Ebr 5:1-3 Yesu, Kuhani mkuu mwenye kuwachukulia watu kwa sababu na yeye alijaribiwa).

Jioni yetu ni wakati wa ukomavu wa kiimani, kichungaji na maisha ya kiroho
Jioni yetu ni wakati wa ukomavu wa kiimani, kichungaji na maisha ya kiroho

Namnukuu Amedeo Cencini: “Kama maisha yangu, kama wito wangu ni wito wa Mungu - na kweli ndivyo ilivyo- basi hakuna dakika ambayo Mungu huyu anayeita atasinzia au atajisahau asiyaangalie maisha yako na asiuangalie wito wako.” Pamoja na kujifunza kutokana na uzoefu tulioupata, Amedeo Cencini anaongeza kitu kimoja muhimu sana. Anaalika kuikubali historia yetu. Kuikubali historia ya familia tunakotoka, kuikubali historia yetu binafsi, kuikubali historia ya wito na utume n.k. Kuna matukio tunapitia yanatuachia makovu. Makovu hayo si lazima uhangaike kuyafuta. Makovu sio kidonda. Ulishafanya Kazi ya kutibu kidonda, kimepona, basi. Songa mbele. “Kuikubali historia ni ule mchakato wa kutambua kuwa katika yale tuliyopitia kuna mkono wa Mungu unaoumba upya. Mkono huu wakati mwingine unaonekana, wakati mwingine hauonekani lakini upo” na anamalizia kwa kusema matukio katika maisha huongea, hulitambua hilo yule tu aliye tayari kuyasikiliza maisha (Amedeo Cencini, L’albero della vita, 128). HITIMISHO: Hatua tulizozipitia ni hatua elekezi tu zenye lengo la kuchokoza tafakari pana juu ya   hali ya maisha yetu ya wito pamoja na mabadiliko yake. Zinaweza kwenda kwa namna tulivyoziona, zinaweza kwenda mbele na kurudi nyuma na inawezekana zikawa na taswira tofauti kadiri ya mtu na mtu na kadiri ya mazingira. Pamoja na yote hayo, ni hatua zinazotuonesha kuwa wito wetu ni safari na tangu siku ile Mungu anapotuita safari inaanza bila kusimama. Agizo lenyewe la Kristo ni “Enendeni”. Sasa, kama hakuna kusimama yanabaki mambo mawili tu; au kuna kusonga mbele au kuna kurudi nyuma. Hatua hizi ambazo tumezitafakari zinaingia hapo ili kutusaidia tuzidi kusonga mbele katika safari yetu ya wito. Mungu aliyetuita yupo macho na ni yeye anayetuongoza daima. Hatuko peke yetu. Nimalizie kwa kunukuu yale maneno ya Mtume Paulo kwa Wafilipi, 1:6. Haya ni maneno ambayo Kanisa hutuambia siku ya kufunga nadhiri na siku ya kupewa daraja Takatifu. Kanisa hutuambia maneno hayo likiyaamini na hapo hapo likisali na kutuombea ili yatimie katika maisha ya utume wetu. Nami ninathubutu kuyarudia maneno hayo nikimwambia kila mmoja aliye hapa: “Yeye aliyeianzisha kazi njema moyoni mwako, aikamilishe hata siku ya Kristo Yesu.” Amina. Tumsifu Yesu Kristo.

Maisha na Wito
27 February 2024, 16:52