Tafuta

Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu “Kaeni katika Neno langu” Yn 8:31. Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu “Kaeni katika Neno langu” Yn 8:31.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya V ya Neno la Mungu: Kaeni Katika Neno Langu: Ufahamu wa Neno la Mungu

Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo wa Kristo Yesu inayomwilishwa katika maisha halisi. Na Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu “Kaeni katika Neno langu” Yn 8:31. Ufahamu!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji, leo Mama Kanisa Mtakatifu anaadhimisha Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa waamini wote, kama anayotualika Baba Mtakatifu Francisko katika waraka wake wa kitume wa tarehe 30/09/2019 uitwao Appeluit llis” Kutangazwa rasmi na Kuitenga Dominika ya tatu katika mwaka wa kiliturujia kwa ajili ya Neno la Mungu lengo ni kuliwezesha Kanisa zima kupata utambuzi mpya jinsi Bwana Mfufuka anavyotufungulia  hazina ya Neno lake na kutuwezesha kutangaza utajiri huo mkubwa kwa ulimwengu. “Aliwafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” (Lk 24:45). Kitendo hicho ni kati ya vitendo vya mwisho alivyovitenda Bwana mfufuka, kabla ya kupaa kwake mbinguni. Alionekana kwa wanafunzi wake walipokuwa wamekusanyika pamoja, akamega mkate pamoja nao, akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko Matakatifu. Kwa watu wale waliokuwa wameshikwa na hofu na kukata tamaa, alifunua maana ya fumbo la Pasaka: yaani kwamba, kadiri ya mpango wa milele wa Mungu Baba, Yesu alipaswa kuteswa na kufufuka kutoka katika wafu ili awajalie watu wote uongofu na msamaha wa dhambi (taz. Lk. 24:26.46-47); pia aliahidi kumpeleka Roho Mtakatifu atakayewapa nguvu ya kuwa mashahidi wa Fumbo hili la wokovu (taz. Lk 24:49). Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee katika uhusiano wa dhati kati ya Bwana Yesu Mfufuka, jumuiya ya waamini na Maandiko Matakatifu. Bila ya Bwana Yesu anayetuangaza, haiwezekani kabisa tuelewe kwa kina Maandiko Matakatifu; lakini pia ni kweli kinyume chake: yaani, bila ya Maandiko Matakatifu haiwezekani kuelewa matukio ya utume wake Yesu na wa Kanisa lake ulimwenguni. Ndiyo maana Mt. Hieronimo aliweza kuandika: “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo” (In Is., Utangulizi: PL 24,17). Kumbe, Dominika ya Neno la Mungu ni matunda ya Maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu.

Dominika ya V ya Neno la Mungu: Kaeni katika Neno langu Yn 8:31
Dominika ya V ya Neno la Mungu: Kaeni katika Neno langu Yn 8:31

Dominika ya Neno la Mungu ni kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kulishuhudia Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo wa Kristo Yesu inayomwilishwa katika maisha halisi. Na Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu “Kaeni katika Neno langu” Yn 8:31. Hapa tunakumbushwa mafundisho ya Mtakatifu Ephraim “Ee Bwana nani aweza kuutambua utajiri hata wa neno lako moja?” Kuna mambo mengi tusiyoweza kuyaelewa kuliko yale tunayopata kuyaelewa. Tupo kama wenye kiu tunakunywa kutoka kwenye chemchemi. Neno lako lina utajiri mwingi hasa kwa wale wanaopata utaalamu wa kulisoma na kutenga muda wa kulielewa. Bwana amelipatia neno lake uzuri wa pekee ili yeyote anayepata kulisoma afaidi uzuri huo na kuutafakari. Ameficha katika neno lake utajiri wote ili kila mmoja aupate utajiri huo kwa namna anavyoutafakari uzuri huo adhimu. Mawazo haya yanajitokeza katika masomo ya leo hasa katika Injili Kristo mwenyewe akidhihirisha hili kabla ya kuanza utume wako, alitoa mwaliko wa kuelewa Neno la Mungu ambaye kwa kweli ndiye huyu aliyetwa mwili akakaa kwetu ili tuwe na uzima tele, anasema “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini Injili”, ili kuanzisha ufalme huo anawaita watakaomsaidia na kuwafanya wavuvi wa watu, nao bila kusita wanaacha yote wanamfuata. Nao wakaziacha nyavu zao wakamfuata.

Dominika ya Neno la Mungu: Siku ya Wasomaji wa Neno la Mungu
Dominika ya Neno la Mungu: Siku ya Wasomaji wa Neno la Mungu

Ufafanuzi: Dominika hii ya Neno la Mungu ni muda muafaka katika  tunahimizwa kuimarisha ushirika wetu na Wayahudi na kuombea umoja wa wakristo. Hili si jambo la ghafla au bahati nasibu: tunapoadhimisha Dominika ya Neno la Mungu tunaona thamani ya kiukemene kwakuwa Maandiko Matakatifu huonesha kwa wale wanaopata kusikiliza njia ya haki na umoja thabiti. Katika somo la kwanza Nabii Yona anaonesha ubinafsi na ubaguzi katika maisha ya mwanadamu aliyekaukiwa na neno la Mungu litialo uzima na taa ya kutuongoza tunaona mwanzoni hakupenda kuona Waninawi wanaongoka vile hawakuwa ndugu zake. Anakimbilia Tarshishi ambako ni upande mwingine kabisa, lakini baada ya majanga mengi na misukosuko ya upepo, dhoruba za baharini na kumezwa na nyangumi siku 3 analazimika kuacha yote, kwanza anaelewa maana ya neno la Mungu na kuitika wito huo wa kuwaongoa Waninawi na Mungu anawasamehe (Yon 3:1-5, 10). Ni kama nabii Yona amewavua kutoka bahari/ziwa la dhambi na kuwaleta mpaka  bandari ya salama. Maandiko matakatifu ua Biblia haiwezi kuwa urithi wa wachache, kwamba mkusanyo wote wa vitabu hivi uwe ni kwa ajili ya wateule wachache. Ni kwa ajili ya wote walioitwa kuusikiliza ujumbe wake na kuuthibitisha kwa maneno yake. Kunaweza kuwepo tabia ya kujimilikisha Maandiko Matakatifu kwa kuyafungia tu kwa sehemu fulani au kuchagua makundi baadhi. Haiwezi kuwa hivyo kamwe. Biblia ni kitabu cha watu wa Bwana ambao kwa kusikiliza hutoka katika mkanganyiko na mgawanyiko na kuelekea katika amani. Neno la Mungu huwaunganisha waamini na kuwafanya kuwa kitu kimoja. Huu ni mwaliko kwa maisha ya jumuiya nzima ya waamini, katika mwanga wa kimisonari mwenye mwangwi wa kisinodi wa ushirika, ushiriki na umisionari kwa kila kiumbe, Suala la kutafakari Neno la Mungu katika maisha ya jumuiya ni utaratibu wa kawaida hasa katika jumuiya za maisha ya wakfu na ya kitume kwani daima huwa ni sehemu ya utaratibu na kanuni katika nyumba zao na sehemu zao za kitume.

Neno la Mungu ni taa na dira ya maisha ya waamini.
Neno la Mungu ni taa na dira ya maisha ya waamini.

Ndugu mpendwa dominika hii ni fursa ya kuhimiza kusoma na kutafakari hazina zilizomo ndani ya Neno la Mungu, hasa kwa nchi za misioni kwa upekee katika jumuiya ndogondogo za Kikristo kipekee barani Afrika katika umoja wa nchi za AMECEA wanaadhimisha jubilei ya miaka 50 ya kuanzishwa wa jumuiya ndogondogo za Kikristo ambayo imeonyesha kuleta matunda wazi kwa kukuza imani, ni muda sasa kwa kila jumuiya na kaya zake kujikita na kuendeleza utamaduni natabia ya kusoma na kutafakari Neno la Mungu pamoja na kupandikiza mbegu hii kwa vijana na watoto, kwani daima ndio tumaini la kanisa na jamii nzima ya binadamu. Katika injili tumesikia “Nifuateni nami nitawafanya wavuvi wa watu” ni maneno yanayoashiria wito wa kumfuata na kumtumikia Mungu kila siku, “kwa hiyo nawasihi mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa kwa unyenyekevu wote na upole…(Efe 4:1-6)” Kwa vile samaki walikuwa muhimu uvuvi ulikuwa kati ya kazi muhimu za uchumi ukifanyika kaskazini kwenye Ziwa Galilaya na pia mto Yordani. Upande wa kusini kuna bahari iliyokufa isiyo na viumbe hai sababu ya chumvi kali ya maji yake, wito wa kuvua watu unahusisha kazi zetu za kila siku kama Uandisi, biashara, ujasiliamali, ualimu, udaktari, ufugaji, kilimo nk inafaa tuheshimu miito ya kila mmoja wetu na tusiwapangie watoto wetu aina ya maisha ya baadae tuwahimize na kuwaonesha umuhimu pia wa kuwa wahudumu wa Neno la Mungu kwa miito ya upadre na utawa. Pamoja na hayo wito wa maisha katika Mungu unahusisha kumfuata Kristo na kuziishi amri za Mungu, kuuishi upendo wa kindugu yaani kupendana bila masharti, kutenda haki na usawa. Kumfuata Kristo ni kupigania ukweli, kuishi mapenzi ya Mungu, sala, toba na kuishi kama watoto wa Mungu. Tusichoke kutumia muda kusali na kutafakari neno, ili liweze kupokeleka “sio kama neno la mwanadamu bali kama lilivyo neno la Mungu” (1 Thess 2:13).

Dominika ya Neno la Mungu kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu.
Dominika ya Neno la Mungu kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu.

Maandiko Matatifu kifo na ufufuko wake haviwezi kueleweka kikamilifu. Hii ndio sababu moja kati ya maungamo ya imani ya zamani kusisitiza “Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kadiri ya maandiko na alizikwa na kwamba alifufuka siku ya tatu kadiri ya maandiko, na alimtokea Kefa” (1 Kor 15:3-5). Kwa kuwa kila sehemu ya Maandiko Matakatifu yanamzungumzia Kristo; tunaweza kuamini kuwa kifo na ufufuko wake sio mfano bali historia ya kweli, nani kiini cha imani ya Mitume. Kristo anapotuita anajua kuwa maisha ya haki na adili sio rahisi hasa nyakati hizi, zetu, ndio maana anafananisha kumfuata Yeye na kazi ya uvuvi ambayo sio rahisi hata kidogo japo siku hizi sehemu chache wanatumia teknolojia . Mosi, baharini au ziwani kuna hatari za papa, nyangumi, mamba, dhoruba/mawimbi, mvua, baridi na pia wayahudi waliamini bahari ni makao ya mashetani... Mvuvi anapaswa kuwa ziwani usiku ili kutega nyavu na kujihimu sana kuangalia kama kuna chochote. Kuna kipindi wavuvi hupotea baharini wasijue nchi kavu ni wapi. Akina Petro waliwahi kesha ziwani bila kupata kitu (Lk 5:5). Kwa hiyo wavuvi wanapaswa kuwa mashujaa, jasiri, hodari, wasioogopa hatari za ziwani/baharini.. Tunapobatizwa tunaanza maisha ya kumfuata Mungu na lazima tutapambana na hatari mbalimbali katika kazi hiyo. Hata wapendwa wetu wanaweza kuwa vikwazo katika kuuishi Ukristo wetu vizuri kwa kutushauri mambo mabaya, kutunyima misaada ya kibinadamu, kutukosesha amani kwa kusababisha malumbano, ugomvi baina ya wanafamilia na wanandugu, uminywaji wa demokrasia na haki za binadamu, rushwa, ubadhirifu, tofauti kati ya maskini na tajiri, ujinga, maradhi, ushirikina kama na mambo kama hayo. Hivyo, Maandiko Matakatifu na Sakramenti havitenganishwi. Sakramenti zinapoongozwa na Neno la Mungu, zinakuwa lengo dhahiri la mpango ambao kwao Kristo anafungua akili na mioyo kuikabili kazi yake ya wokovu. “Mara wakaziacha nyavu zao wakamfuata” Je, tupo tayari kuacha nyavu zetu? Ndio nyumba, ndugu, mali, watoto, baba na yote tuliyonayo na kumfuata Kristo? Mitume waliacha bila kusita wakamfuata japo hawakumjua vizuri, sisi tumefundishwa hivyo tunamjua kuwa ni Mwana wa Mungu, Je, tunamfuata inavyotakiwa? tunamwamini? Basi na tuwe watulivu kwani “ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana na kumngojea kwa utulivu” (Omb 3:26). Ndugu una shida gani? Acha nyavu zako, yaani yote yanayokufunga umfuate Kristo, umngoje kwa utulivu, naye atafanya. Huna haja ya kung’ang’ania nyavu za zamani… nyavu za kukata tamaa, za kuachia ndoto zako za maisha, za kujisikia vibaya, za kujiadhibu mwenyewe, za kujitesa mwenyewe, za kuharakisha maisha, za ulalamishi na manung’uniko, za kuishi maisha bandia ya mtandaoni, za kujiona hupendwi… na mengine mengi, acha nyavu hizo leo, mfuate Kristo Yesu!

Liturujia D3 Neno
19 January 2024, 17:20