Tafuta

Mama Kanisa katika masomo ya dominika hii anatupa nafasi ya kutafakari wito wetu wa kuwa watakatifu kama Mungu Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu. Mama Kanisa katika masomo ya dominika hii anatupa nafasi ya kutafakari wito wetu wa kuwa watakatifu kama Mungu Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu.   (ANSA)

Tafakari Dominika ya Pili ya Mwaka B wa Kanisa: Wito wa Utakatifu

Ni watu wanaoshuhudia unyenyekevu katika maisha, kiasi hata cha kuacha alama za mvuto na mashiko katika uekumene wa damu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wewe unaitwa kuwa mtakatifu katika maisha yako kama mtu wa ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu, mfanyakazi na mhudumu wa upendo kwa jirani zako!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 2 mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Mama Kanisa katika masomo ya dominika hii anatupa nafasi ya kutafakari wito wetu wa kuwa watakatifu kama Mungu Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12). Katika sura ya kwanza anasema, watakatifu ni watu wanaotia shime pamoja na kuwasindikiza waamini wenzao kama vyombo na mashuhuda wa imani na matumaini kama ilivyokuwa katika Agano la Kale; hata leo hii hawa ni watu wanaoweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki; watu wanaosadaka maisha yao, mashuhuda wa upendo wa Kristo na wale wanaoendelea kujitosa kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Hawa ni majirani wanaotangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku pasi na makuu. Ni watu wanaoshuhudia unyenyekevu katika maisha, kiasi hata cha kuacha alama za mvuto na mashiko katika uekumene wa damu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wewe unaitwa kuwa mtakatifu katika maisha yako kama mtu wa ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu, mfanyakazi na mhudumu wa upendo kwa jirani zako! Jambo hili linawezekana kwa kufuata maongozi yake Mungu ndiyo maana mama kanisa katika sala ya mwanzo anatuoombea akisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ndiwe unayeongoza mambo yote mbinguni na duniani. Usikilize kwa wema dua zetu sisi taifa lako, utujalie amani yako maishani mwetu”. Ni katika mukutadha huu katika wimbo wa mwanzo tunasali tukisema; “Ee Mungu, nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako, wewe Mtukufu” (Zab. 66:4).

Wito kwa wakristo wote ni kuwa watakatifu
Wito kwa wakristo wote ni kuwa watakatifu

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kwanza Samweli (1Sam 3:3b-10, 19). Somo hili linasimulia wito wa Samweli, mwamuzi wa mwisho katika Israeli. Jina Samweli maana yake ni “Niliyemwomba Bwana”. Maandiko Matakiatifu yanasimulia kuwa Hannah mama yake, mke wa pili wa Elikana alikuwa Tasa. Jambo hili lilimkosesha amani na furaha licha ya kuwa mume wake alimpenda jinsi alivyo. 1Sam 1:1-8. Basi Hannah alienda hija huko Shilloh, mbele ya Sanduku la Agano akamwomba Mungu zawadi ya mtoto wa kiume, ambaye angemtoa kuwa mtumishi hekaluni. 1 Sam 8-18. Mungu alisikiliza sala yake, akamjalia mtoto mwanaume naye akamwita jina Samweli akisema; “Nilimwomba kwa Bwana.” Akiwa na umri wa miaka 3 hivi Hannah alimtoa mwanae Samweli kwa Mungu, akamkabidhi kwa kuhani Eli ili amlee kadiri ya mpango wa Mungu 1 Sam 1: 9-19. Akiwa na umri wa miaka 12 Mungu alimtokea na kumwita. Kwa maongozi ya Eli, Samweli aliitikia sauti ya Mungu akisema; “Nena Bwana kwa kuwa Mtumishi wako anasikia.” Ndiyo maana katika kiitikio cha wimbo wa katikati tunaimba tukisema; “Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, kuyafanya mapenzi yako” (Zab: 39: 7, 8). Samweli alipoisikia na kuiitikia sauti ya Mungu, aliendelea kukua kwa kimo na busara. Mungu alikuwa pamoja naye, maana hakuacha Neno lake lidondoke chini. Somo hili linatufundisha kuwa kwa Mungu hakuna linaloshindikina. Chochote tukimuomba kwa imani atatupatia kama sisi tutakuwa waaminifu kwa neno lake na ahadi tunazozitoa kwake kama Hannah mama ya Samweli.

Wito wa Utakatifu katika Ulimwengu mamboleo
Wito wa Utakatifu katika Ulimwengu mamboleo

Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 6:13c -15b, 17-20). Katika somo hili Mtume Paulo anawaonywa Wakorintho wasiitumie miili yao kwa mambo ya kipagani. Maana mwili ni mali ya Bwana na ni hekalu la Roho Mtakatifu. Ni mwaliko wetu sisi pia kuitunza na kuiheshimu miili yetu kwa sifa na utukufu wa Mungu. Nyakati hizo za Paulo, kulikuwa na mafundisho ya Wagiriki kuwa mwili si wa maana kama roho. Ili kutunza roho makundi mawili ya namna ya kuishi yalijitokeza. Kundi la kwanza lilitilia mkazo katika kuusulubisha mwili kwa kuuchapa, kuufanyisha kazi za suluba na kuunyima chakula ili kuzima tamaa zake. Ndiyo maana katika historia ya Kanisa yaliibuka mashirika ya watawa walioitesa miili yao ili kuzipatia utakatifu roho zao. Kundi la pili lilihalalisha kila kitu kukidhi haja za mwili wakidai kuwa roho ikiwa safi, chochote kinachofanyika katika mwili hakiwezi kuiathiri. Hivyo kula na kunywa kupita kiasi na kufanya zinaa, ilionekana kuwa ni sawa. Wagiriki walijenga mahekalu ya kufanya zinaa waliyoiita ukahaba mtakatifu na kulikuwa na miungu ya zinaa ili kuwaaminishwa watu kufanya ukahaba na zinaa ni matendo matakatifu. Katika mazingira haya mtume Paulo anatoa maonyo kwa wakristo kutojihusisha na mambo haya ya kipagani akisisitiza kuwa uhuru wa Kikristo ni uhuru wa kutokutenda dhambi, na kuishi maisha safi kiroho na kimwili. Kwa ubatizo miili yetu imekuwa hekalu la Roho Mtakatifu na mwili wa fumbo la Kristo. Hivyo kufanya zinaa na makahaba ni kuudhalilisha mwili wa Kristo. Sisi ni hekalu la Roho Mtakatifu, miili yetu imewekwa wakfu kwa mambo matakatifu yamhusuyo Mungu tunapoelekea katika maisha ya utakatifu mbinguni. Tukumbuke basi dhamani yetu kuwa tumeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu. Tumepewa roho inayotia uzima wa kimungu ndani yetu. Tumepewa akili ili tuweza kupembua na kufahamu yaliyo mema na mabaya. Tumepewa utashi ili tuweza kuchagua lililo jema na kuacha yaliyo mabaya. Tumepewa mwili ili tuweze kutenda na tunatekeleza yale tuyajuayo kwa akili na kuyachagua kwa utashi wetu kadiri ya mpango wa Mungu na kuuishi wito wetu wa kuwa watakatifu kimwili na kiroho.

Utakatifu unapata fadhila: imani, matumaini na mapendo
Utakatifu unapata fadhila: imani, matumaini na mapendo

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn 1:35-42). Katika sehemu hii ya Injili Yohani Mbatizaji anawaelekeza wanafunzi wake waende kwa Yesu akiwaambia; “Tazameni mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu.” Wanafunzi wake wakamfuata Yesu naye Yesu alipowaona akawauliza “mnatafuta nini?” Wao wakamwuliza: “Mwalimu, unakaa wapi? Yesu akawaambia; “Njooni nanyi mtaona! Nao wakamfuata, wakaona anakokaa, wakakaa naye, wakajifunza kwake baadae wakawapeleka ndugu na rafiki zao kwake. Andrea alimpeleka Petro, Yohane alimpeleka Yakobo, Filipo alimpeleka Nathanaeli. Sisi nasi kwa Sakramenti ya ubatizo tumeitwa kuwa wamisionari, kuwapeleka ndugu, jamaa, na marafiki kwa Yesu kila mmoja kadiri ya wito alioitiwa na Mungu katika maisha yake. Tukumbuke kuwa ili tuweze kuufikia utakatifu kila mmoja anapaswa kuuishi kiaminifu wito aliojaliwa na Mungu na kuupokea: uwe ni wito wa kazi katika kuwahudumia wengine kwa ajili sifa na utukufu wa Mungu, au wito wa ndoa ambapo mwanamme na mwanamke wanaamua kwa makusudi kushirikiana na kwa upendo katika kutumikiana mpaka kufa, huku wakiwalea na kuwashirikisha imani yao watoto waliojaliwa na Mungu kwa upendo wao; au wito wa upadre na utawa ambapo padre au mtawa anayatolea maisha yake yote kwa ajili ya Mungu kwa kuwatumikia watu wake; au wito wa maisha ya pekee ambapo mtu anaamua kwa hiari yake, kutokuoa au kuolewa, si padre wala si mtawa, bali anaacha yote ili awe huru kuwahudumia na kuwatumikia wengine. Lakini pia wapo ambao hawajaoa wala kuolewa si kwa kupenda ila wamelazimika kuwa hivi nao wanapaswa kumshukuru Mungu kwa hali hiyo na kuishi usafi wa moyo, wakitambua kuwa wito uliomkuu kuliko yote ni wito wa sote kuwa watakatifu kama Mungu Baba yetu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Pengine si rahisi kuitambua sauti ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtoto Samweli. Na si rahisi kumtambua mwanakondoo wa Mungu anayeiondoa dhambi ya ulimwengu na kumfuata kama ilivyokuwa kwa mitume. Basi tuombe neema na Baraka za Mungu ili tuweze kuisikia na kuitambua vyema sauti yake na kufuata miito yetu kila mmoja kwa nafasi yake ili mwisho wa yote tuweze kuufikia wito wetu mkuu wa kuwa watakatifu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D2 ya Mwaka B
11 January 2024, 10:03