Tafuta

Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Mungu. Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Mungu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika IV Mwaka B wa Kanisa: Nguvu ya Neno la Kristo Yesu

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unataka ulimwengu usikie mbiu ya wokovu, ili kwa kusikia uweze kusadiki, na kwa kusadiki uweze kutumaini, na kwa kutumaini uweze kupenda. Mwenyezi Mungu anawainulia waja wake Nabii atakayekuwa ni mfano wa Musa, Mtu wa Mungu. Watu wanashangazwa na mafundisho ya Kristo Yesu na jinsi alivyokuwa na mamlaka kias kwamba, hata pepo walimtii, kielelezo cha uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya waja wake.!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Radio Vatican. Leo ni Dominika ya Nne ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Katika somo la kwanza  “Mungu anatuahidia kuwa atatuinulia nabii miongoni mwetu atakayekuwa mfano wa Musa. Katika Injili tutamsikia huyo Nabii Yesu akifika kati ya watu. Watu wameshangazwa na mafundisho yake na uweza wake umewashtua hata mashetani wanatii amri zake. Dominika hii inatawaliwa na nguvu ya Neno la Kristo, jinsi alivyo na mamlaka juu ya vyote vya mbinguni na duniani, tazama hata pepo wanamtambua na kumtii. Kama vile wayahudi walivyomshangaa Bwana Yesu, sisi nasi tunaalikwa “tumshangae” halafu tumkubali, tumpokee na kisha tumfuate, tutanufaika. “Je, na wewe unashangazwa na mafundisho ya Kristo Yesu? UFAFANUZI: Maneno tunayoyapata katika somo la kwanza (Kumb 18:15-20) kutoka kitabu cha Kumbukumbu la Torati yametimia “Bwana Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilize yeye.” linatupa namna nzuri ya kuwa wafuasi. Kwa ubatizo wetu tumefanywa manabii Mungu akitutumia kama mdomo wake. Tunapaswa kupeleka ujumbe wa Mungu kwa wenzetu, nao sharti watusikilize na kuongoka. Tusiposema, au tukisema ya kwetu ambayo Mungu hajatuagiza somo hili limeeleza kwamba tutakufa. Kumbe maneno yetu yawe kama maneno ya Mungu mwenyewe. Tutafakari kwa kawaida tunaongea maneno gani, ya Mungu? au ya kwetu wenyewe? Nionavyo, ni afadhali kidogo tukiongea ya kwetu kuliko tena kuongea ya watu wengine. Ulimwengu mamboleo unaongozwa na habari mbalimbali tena zisizo rasmi wala uthibitisho, lakina katika tasnia ya habari na mawasiliano ambayo kwa kweli ni muhimili wa nne katika kutawa jamii ya watu ukiacha mihili hii yaani serikali, bunge na mahakama. Sasa tunapozungumzia nyanja ya mawasiliano leo hii tunaona jinsi iliyo na nguvu katika ushawishi wa mambo mengi yanahusu maisha ya mwanadamu ya kila siku, namna au sanaa ya kupashana habari na taarifa ndio changamoto katika jamii ya mwanadamu wakati wote, wapo wanaotoa habari na taarifa kama njia ya mwasiliano kwa jamii, zipo taarifa zinazoogofya na  watu na kusababisha taharuki, watu kupoteza imani kwa Mungu wao na hata kwa watu wema waliowaamini. Kwasababu namna ya uwasilishaji wa habari hizo sio sahihi. Ile dhana ya kuwa manabii kusema kile tulichosikia na kufundishwa na Mungu kwa njia ya ufunuo wake kinapotoshwa na kusema yale tupendayo.

Nguvu ya Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa
Nguvu ya Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa

Katika Injili, tunamwona Yesu Kristo akianza rasmi kazi yake, Mwinjili Marko (1:21-28) anatuambia watu walimshangaa Yesu. Nasi tumewahi aidha kushangaa au kushangaashangaa. Kushangaa ni “hali ya kustaajabu baada ya kuona/kusikia jambo lisilo kawaida au ambalo halikutarajiwa, kuduwaa, kupumbazika, kutunduwaa, kuvuvuwaa”. Yesu akifundisha katika sinagogi huko Kapernaumu na ndani ya sinagogi kulikuwa na mtu mwenye pepo mchafu.Mtu huyo anaanza kulia, na anaelekeza kilio chake kwa Yesu Kristo.Wayahudi walielewa kwamba kuwa na wazimu au kutawaliwa na mawazo mabaya kulitokana na pepo wachafu. Ndivyo ambayo kila mtu aliyepagawa na pepo alitazamwa na watu. Lakini tunaona kwamba pamoja na hali yake ya kuwa na pepo wachafu, bado anamtambua Yesu Kristo kuwa ni nani.Ndiyo maana tunasikia maneno haya “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu.”  Tumeambiwa kwenye Injili kwamba, Yesu Kristo alifundisha kama mtu mwenye amri na si kama waandishi. Hii inaonekana katika kukemea pepo “Fumba kinywa umtoke.” Wale Pepo wakamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, wakamtoka. Wakashangaa wote . . . Mpendwa msikilizaji na msomaji, wa tafakari hii utakubaliana nami kuwa Katika Agano Jipya anayeshangaza kuliko wote ni Kristo. Kuzaliwa kwake tu ni kwa ajabu na kwa kushangaza kabisa, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake Bikira Maria, tena anazaliwa kwenye zizi la ng’ombe. Akiwa mtoto wa miaka 12 tu aliwashangaza wazee na walimu hekaluni kwa kuwasikiliza na kuwauliza maswali ya kiutu uzima.. Alipotuliza dhoruba wanafunzi wake walishangaa wakajiuliza “ni nani huyu hata upepo na bahari vinamtii” (Mt 8:27), alipomfufua mtoto wa mjane wa Naini “umati ulishangaa mshangao mkuu” (Mk 5:42), mafarisayo walituma watu wakamshike wakarudi bila kumkamata, walipowauliza mbona hamkuleta walijibu “tangu tuzaliwe hatujapata kuona mtu anayeongea kama yule Mgalilaya, tumeishia kushangaa tu” (Yn 7:46). Leo tumeambiwa “wakashangaa mno kwa mafundisho yake maana aliwafundisha kama mtu mwenye amri wala si kama waandishi”… mshangao unazidi wanaposhuhudia nguvu ya neno lake, jinsi pepo wanavyohaha na kuhangaika, wanavyokiri kuwa ni Mtakatifu wa Mungu wanaduwaa wakisema “ni nini hii? ni elimu mpya! maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu nao wamtii!”

Nguvu ya Neno la Mungu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina.
Nguvu ya Neno la Mungu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina.

Uweza na mamlaka ya Kristo juu ya pepo wachafu uliwashangaza. Hii ni kwa sababu watu waliwaogopa sana pepo wachafu. Waliaminika kuwa na nguvu na walileta madhara makubwa. Waliaminika kuishi baharini, jangwani na misituni. Mtu alipopagawa na pepo sura yake ilibadilika na usemi wake ukawa tofauti kabisa. Inasemekana pepo alimwezesha mtu kuwa na ujuzi na nguvu kupita kawaida. Mtu huyo aliweza kuanguka kifafa au kulia au kucheka mfululizo bila sababu. Matokeo yake yalikuwa ni ububu, ukiziwi au upofu wa muda (Mt 12:22). Ikumbukwe kuwa katika jamii ya Wayahudi, na Agano la Kale na Agano Jipya pia, Wapungaji wa pepo walitumia majani yenye harufu mbaya kuwanusisha waliopagawa, pia walitumia mboga chungu kuwalisha wagonjwa, jina la pepo mkubwa zaidi Rej. Belzebuli (Mt 12:24) na kutukana matusi makubwa ya nguoni hadi pepo anaona hapa sio kwa kukaa inabidi tu atoke. Jambo la ajabu ni hili pepo waliwapagaa hata watu wema wasio na dhambi na hivi walipopungwa wengi walishukuru sana. kwani iliwapunguzia kadhia kubwa.  Ili kubaki salama walipasika wajihadhari wasiridhike na hali yao na hivi walilazimika kukaa na Yesu na kuwa wafuasi wake wa kweli, kumruhusu Roho wa Mungu aongoze maisha yao ambapo hapo kabla shetani ndiye aliyekuwa akitawala (Mt 12:43-45). Tukiyaishi mapenzi ya Mungu pepo wachafu watakaa mbali nasi... Hakuna raha yoyote kumfuata shetani, mara zote ametuingiza katika matatizo na migogoro. Tazama alivyo mnyonge mbele ya Yesu, analalamika tu “tuna nini nawe, Yesu wa Nazareth? Je, umekuja kutuangamiza? nakutambua u nani, mtakatifu wa Mungu”, huruma sana, bado unamfuata? atakufikisha wapi? Hana lolote, anakemewa tu “fumba kinywa… umtoke”, analialia anatoka, shetani sio msaada, tuachane nae leo. Hata hivyo Ibilisi pamoja na unyonge wake, ukimpa tu nafasi lazima akughalaghaze kwenye tope fedhea na majuto na maumivu...!

Nguvu ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu
Nguvu ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu

Lengo kubwa la shetani ni kuanzisha vita na kumpinga Kristo na Kanisa lake, pamoja na yeyote anayejiita mfuasi wa Kristo. hana budi kumtegemea Roho Mtakatifu kwa kila alifanyalo. Tukiwa tumejazwa na Roho Mtakatifu, pepo wwachafu hawawezi kutusumbua. Lakini kama tutakuwa na maisha nusu nusu. Roho Mtakatifu kidogo na shetani kidogo. Hapo hatutaweza kumkimbiza Roho mwovu katika maisha yetu. Kwa baadhi yetu, maisha yametawaliwa na mtaala wa shetani. Kwa mfano: ulevi, majungu, chuki, ulafi, wivu, rushwa, mauwaji, uchu wa mali na madaraka yaliyopitiliza uunjifu wa haki za wengine. Mara kadhaa tumemruhusu atutawale kwa kule kutazamana kwetu vibaya, kukosa kwetu ushirikiano, kushindwa kuwa watu wa majitoleo, kutojisadaka kwa ajili ya wengine hasa wanyonge masikini na wenye shida. Tumezingatia yasiyo na faida na kuyaacha ya muhimu kwa maendeleo yetu kimwili na kiroho, waganga wa kienyeji wametudanganya. Bado tunateswa na imani za kishirikina na wapo wakristo waliojisajiri katika timu mbili yaani asubuhi mapka jioni ni mkristo wa kanisani, wa popote kwenye imani yake, jioni yupo kwa mganga wa kienyeji na miungu ya uongo, au jumapili kanisani ila siku za juma jumatatu-hadi jumamosi- kwa waganga na wapiga ramli  Tabia hizi zinafifisha nguvu ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Kwa sababu ya tabia hizi mbaya, watu hukosa uelewano kati yao na familia husambaratika. Hii yote ni kazi yamashetani. Mpendwa, tunaalikwa kuvaa silaha zote za Mungu ili tuweze kuzipinga hila za shetani (Waef 6:11). Kristo alimwaga damu yake ili atukomboe kutoka kwenye hila za shetani. Kristo ana uwezo wote wa kutufanya huru, tunachotakiwa kufanya ni kumpa nafasi tu. Ninawaalikeni tushangae. Sijui tutashangaaje lakini lazima tushangae, kwa kuduwaa au kwa namna unayoona inafaa kutoa mshangao na ajabio kwake kwa anayoyatenda kwetu.

Neno la Mungu linapaswa: kusomwa, kutafakarikiwa na kumwilishwa
Neno la Mungu linapaswa: kusomwa, kutafakarikiwa na kumwilishwa

Tushangae sababu Kristo yu kati yetu akiongoza maisha yetu. Ndiye Kuhani Mkuu anayetufundisha kuwa Mungu ni mmoja tu, anatufundisha uadilifu na haki, anatutangazia wokovu. Amekuja kutukomboa dhidi ya pepo wabaya, kutuondolea udhaifu na yote yanayotutesa, kutuletea amani nyumbani kwetu, kutupa afya njema tunaougua, kutupa majawabu ya changamoto za maisha yetu binafsi na ya ndugu zetu. Yesu ndiye Bwana, ni Mungu, ni Jibu. Je, unajuta kuwa kwenye wito wako iwe upadre, utawa, ndoa au kazi unayofanya? Haijalishi mnapitia njia ipi na vipindi gani, labda hali ya fedha sio nzuri, kilimo kinakataa, afya mgogoro, ajali mbalimbali, kazi haina mapato mazuri, ada za watoto ni kitendawili, tunakosa salama wa afya, nk., katika haya yote tunaweza kumruhusu pepo wa kukata tamaa, kulaumiana na kudharauliana, mwisho tunasambaratika. Haya yote ni pepo wachafu, tuwakemee kwa jina la Yesu, washindwe na walegee kabisa. Lengo, anatuambia Mt. Paulo kwenye somo II (1Kor 7:32-35), tuishi vizuri na kumtumikia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine. Tumwombe aje atusaidie, tuachane na maisha ya dhambi. Aje atamke yale maneno aliyotamka pale Kapernaumu kwa yule aliyekuwa akisumbuliwa na pepo mchafu, “Fumba kinywa umtoke” Baadaye tutakuwa na maisha ya amani na ya  kumpendeza Mungu. Kristo haonyeshi hofu wala mashaka yeyote juu ya pepo wachafu. Anayakemea na yanamtii. Yanamtoka yule mtu na anakuwa mzima tena. Cha muhimu ni kuwa huru. Tumtegemee Kristo kwa hilo. Basi siku ya leo tumwombe Kristo atukomboe kutoka kwenye gereza la hofu yamashetani wanaotawala maisha yetu.

Liturujia D4
27 January 2024, 15:26