Tafuta

Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa.  

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Yesu Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa

“Tokeo la Bwana, yaani Epifania” ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa Mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Wahusika wakuu wanaotajwa katika Maandiko Matakatifu ni Mamajusi kutoka Mashariki, hawa walikuwa ni wataalam wa nyota na wafasiri wa matukio mbalimbali, wanaiona nyota na kuanza kuifuatilia! Yesu!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli), Italia.

Ndugu msomaji, “Tokeo la Bwana, yaani Epifania” ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa Mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Somo letu la Injili ya leo (Mt. 2:1-12) ndiyo inayoipa Jumapili ya leo jina la “Epifania” (Tokeo la Bwana). Kwa kawaida Sherehe ya Epifania huadhimishwa Januari 6. Hata hivyo, Liturujia inaruhusu sherehe hiyo kuadhimishwa Jumapili inayokaribiana na Januari 6. Epifania ni neno la Kigiriki ambalo kwa Kiswahili ni kujifunua au kujidhihirisha. Leo Kristo “anajidhihirisha/anajifunua kwa watu wa mataifa” kwani Mamajusi hawakuwa Waisraeli bali watu wa Mataifa ya kigeni. Mamajusi walitoka “mashariki,” yaani maeneo ya ama Babilonia au Arabia au Mesopotamia kwa kadiri ya vyanzo mbalimbali. Maeneo haya waliishi watu wasio-Wayahudi, tena wengi wao walikuwa wafuasi wa dini za kipagani (dini za asili). Labda tuone kidogo juu ya Mamajusi: Mamajusi walikuwa ni wanajimu (wataalam wa mambo ya nyota). Lakini pia walikuwa na utaalamu wa kufasiri/kufafanua ndoto (na ndiyo maana Mungu atawaonya katika ndoto wasimrudie Herode). Kutokana na utaalamu wa nyota na kufasiri ndoto, watu wengi walihusisha utendaji wao wa kazi na nguvu za uchawi na hivyo hawakuheshimiwa sana katika jamii zao. Hata hivyo, Mamajusi wetu wa leo wana hadhi kubwa maana inaonekana kuwa walikuwa wafalme kutoka mashariki kulingana na dokezo tunaopata kutoka Zab. 72:10. Ingawa Maandiko Matakatifu hayasemi waziwazi idadi ya Mamajusi waliofika kwa mtoto Yesu, mapokeo ya karne nyingi yanataja kuwa walikuwa watatu kutokana na zawadi tatu walizotoa na hata wanapewa majina: Melkiori, Gaspari na Baltazari.

Mamajusi: Melkiori, Gaspari na Baltazari.
Mamajusi: Melkiori, Gaspari na Baltazari.

Hivyo, Epifania ni sherehe ambayo Bwana Wetu Yesu Kristo anajifunua/anajidhihirisha kwa “watu wa mataifa mbalimbali” kuonesha kuwa amekuja kwa ajili ya wokovu wa watu wa Mataifa yote na wala siyo kwa ajili ya Waisraeli peke yao. Tukumbuke kuwa Waisraeli walijiona wao ni taifa teule la Mungu na kuwaona wale wasio Waisraeli kuwa ni “watu wa mataifa”. Leo Kristo anajifunua kwa watu wa mataifa mengine na hivyo kuashiria kuwa Yeye amekuja kwa ajili ya wokovu wa watu wote bila kujali chimbuko lao au hadhi zao. Injili ya leo inatufundisha kuwa (1) Kristo ni mfalme ambaye anajifunua kwa wanaomtambua kuwa Yeye ni Mfalme. Mamajusi wanapofika Yerusalemu wanauliza, ‘Yupo wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Mamajusi wanakiri wazi kuwa Yesu ni Mfalme wa Wayahudi (ukweli huu utadhihirishwa tena msalabani kwenye anuani iliyogongelewa juu ya msalaba). Mamajusi walijuaje kuwa Yesu ni mfalme wa Wayahudi? Mosi, kwa kufunuliwa na Mungu (wanapata ufunuo kutoka kwa Mungu); Pili, kwa kusaidiwa na utaalamu wao wa nyota kwani watu wa nyakati hizo waliamini kuwa “kuzaliwa kwa wafalme kunaambatana na tukio fulani la kinajimu linalotokea angani”. Hivyo, walipoona tukio la nyota ya ajabu angani walifahamu kuwa mahala fulani amezaliwa mfalme. Swali la Mamajusi, “Yuko wapi… mfalme wa Wayahudi?” linadhihirisha kuwa wanamtambua Kristo kama Mfalme.

Mtoto Yesu anajifunua kama; mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga
Mtoto Yesu anajifunua kama; mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga

Je, sisi tulio watu wa mataifa (ambao kwa asili siyo Waisraeli) tunamtambua Kristo kama mfalme? Wengi wetu licha ya kubatizwa kwetu bado Kristo siyo mfalme wetu kwani tunao wafalme wengine wanaotutawala kama vile mali, kiburi, madaraka, imani potofu, rushwa, visasi, ngono, vileo, muziki, teknolojia na mengineyo. Tugeuze mioyo yetu na kumtambua Kristo kama mfalme wa maisha yetu. (2) Tunapaswa kumtafuta Kristo kwa lengo la kumsujudu. Kumtambua Kristo kama Mfalme haitoshi. Ni lazima kuwa na lengo la kumsujudu. Mamajusi walimtafuta mtoto Yesu ili wakamsujudie: “…nasi tumekuja kumsujudu”. Je, sisi tunamtafuta Kristo kwa lengo gani? Wengi wetu tunamtafuta Kristo siyo kwa nia ya kumsujudu bali kwa nia ya kutendewa miujiza, kupata utajiri wa haraka, kupata maisha mazuri, kupata umaarufu, kuondokana kabisa na matatizo yote, kupata uponyaji wa haraka wa magonjwa na mengineyo. Haya siyo malengo sahihi katika safari ya kumfuasa Kristo. Kumsujudu Kristo kunahusisha mambo makuu manne: Kumwabudu na kumsifu, Kumwomba toba, Kumshukuru na Kumpelekea maombi yetu. (3) Kristo anajifunua kwa wenye mamlaka ili nao wamtambue na kumsujudu. Ingawa Injili ya leo haisemi kuwa Mamajusi hawa walikuwa ni wafalme, tunaweza kuhitimisha kuwa walikuwa ni wafalme kwa kurejea utabiri kuhusu wafalme wanaopeleka zawadi kwa mfalme anayetawazwa kutoka Isa. 60:3,6 na Zab. 72:10. Wafalme ni watu wenye mamlaka katika himaya zao- wana vyeo na amri. Kristo anajifunua kwa wafalme ambao ni watu wenye mamlaka. Kwa unyenyekevu mkubwa wafalme hawa wanaacha mambo yote na wanamtafuta mfalme wa Wayahudi ili wamsujudu. Je, ni watu wangapi wenye vyeo na mamlaka wanamtafuta Kristo na kumtambua?

Epifania: Watu wa Mataifa kumpoea Mwana wa Mungu
Epifania: Watu wa Mataifa kumpoea Mwana wa Mungu

Mara nyingi watu wengi wenye vyeo, madaraka na mali huwa hawaoni thamani ya Mungu/kusali na mara nyingi wanatoa visingizio kuwa wana shughuli nyingi au ratiba zinawabana. Hawa wanakuwa “busy” kutafuta mali, pesa, umaarufu wa kisiasa, n.k. Kwao Kristo/Mungu si kipaumbele. Tena mbaya zaidi wanajaa kiburi na majikwezo badala ya kujishusha kama Mamajusi. Je, viongozi wanaoongoza maeneo mbalimbali duniani wanamtambua Kristo kama mfalme wao? Je, wanamsujudu Kristo? Laiti wangemtambua Kristo kama mfalme na kuwa na lengo la kumsujudu, wasingejiona kuwa wao ni miungu-watu, wasingefikiri kuwa wanaweza kila kitu wao peke yao bila kuhitaji ushauri na msaada wa wengine, wasingehalalisha utoaji mimba, wasingejinufaisha kwa migongo ya wanyonge, wasingeuana kwa sababu ya siasa au vyeo na mengineyo. (4) Wenye mamlaka huwa na hofu nyingi na hulinda mamlaka yao kwa gharama kubwa, hata ikibidi kuangamiza wapinzani wao. Injili inatueleza pia kuwa mfalme Herode “alifadhaika” aliposikia habari za mtoto mfalme kuzaliwa huko Bethlehemu ya Uyahudi. Kwa nini alifadhaika? Herode alifadhaika maana alihofu kuwa mtoto huyo atakuja kuchukua nafasi yake ya ufalme. Mtu mzima anamwogopa mtoto mchanga; Mfalme anamwogopa mtoto mdogo. Ama ajabu kweli kweli! Herode hataki kusikia habari za mfalme mwingine maana mfalme ni yeye peke yake. Tena, anatumia mdomo wake kuwalaghai Mamajusi kwa maneno matamu ili akipata habari mahali alipo mtoto akamuangamize kabisa: “mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.” Nia yake ni kumuua Yesu maana ni tishio kwa ufalme wake.

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu

Herode ni mnafiki kwani maneno yatokayo mdomoni kwake hayasadifu kulichoko moyoni mwake: mdomoni analaghai kuwa anataka kwenda kumsujudu mtoto lakini moyoni ananuia kumuua mtoto. Katika hili wengi wetu hatuna tofauti na Herode kwani “midomo yetu inatamka mambo mazuri lakini moyoni tumejaa chuki, mauaji, dhuluma, wivu, visasi na mengineyo kama hayo.” Hata wenye vyeo wengi wanafanana na Herode kwani wengi wao wanahofu sana wakiona watu wa chini yao wanapata umaarufu, sifa au kutambulika  kuzidi wao na wanadhani watachukua nafasi zao. Matokeo yake wanaanza kuwafanyia fitina na figisu wale wa chini ili kulinda vyeo vyao. Wengine wanadiriki hata kuwaua, kuwachafulia sifa zao na hata kuwazushia skendo ili kuwadhoofisha. Hiyo ni roho ya kiherode na kamwe haina tija kiroho na kimwili. (5) Tunapaswa kwenda kumsujudu Kristo/Mungu tukiwa na zawadi. Mwisho, Mamajusi walikwenda na zawadi kwa mtoto Yesu: dhahabu, uvumba na manemane. Dhahabu inaashiria kuwa Kristo ni Mfalme maana watu wa zama hizo walipaswa kutoa dhahabu kwa mfalme kama kodi/ushuru; uvumba unaashiria “ukuhani/umungu wa Kristo’ maana makuhani walihusika kuchoma ubani kwa Mungu kama ishara ya sadaka na sala zao na za watu wengine, na uvumba ulikuwa ni kwa ajili ya Mungu/miungu tu; manemane alipakwa mtu aliyekufa kwa ajili ya maandalizi ya maziko na hivyo unaashiria kifo cha Kristo. Je, tunapokwenda kumsujudu Mungu tunabeba zawadi gani? Tunamtolea Mungu nini? Hatupaswi kwenda mikono mitupu: tunapaswa kumtolea maisha yetu, nia zetu mbalimbali (ambazo zaweza kuwa katika mtindo wa Nia za Misa), majitoleo yetu ya mali au vitu, karama zetu na mengineyo. Amani ya Bwana iwe nanyi.

05 January 2024, 13:45