Tafuta

Uingereza:Papa aunga mkono wimbo wa“Hear Angels Cry”

Papa alituma Ujumbe kwa Kardinali Vincent Nichol,Askofu Mkuu wa Westmister katika kuunga mkono mpango wa Wimbo wa Noeli kwa ajili ya Bethlelemu.“Katika Noeli hii,wimbo wa Bethlehemu uweze kuhamasisha mshikamano,upatanisho na amani katika Nchi Takatifu.”

Na Angella Rwezaula, - Vatican

Hakutakuwa na mti wa Noeli au sherehe za kiutamaduni mahali pa kuzaliwa kwa Yesu Kristo mwaka huu katika kujibu maelfu ya waliouawa katika vita katika Nchi Takatifu. Badala yake, msisitizo  katika Kanisa la Kuzaliwa kwa Bwana na katika Uwanja wa Kanisa hilo huko Bethlehemu utakuwa katika kuombea amani.

Sikia Malaika Wakilia

“Katikati ya vifusi na magofu, sauti ya uchungu inainuka kutangaza kwamba mwanga wa matumaini utaendelea kuwepo katika mji mdogo wa Ukingo wa Magharibi ambapo historia ya Noeli ilifunuliwa.” Kwa njia hiyo Youstina Safar, mkazi wa Bethlehemu na mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Bethlehemu, ameshirikiana na bendi ya Ooberfuse ya mjini London kutoa ujumbe huo mzito kupitia wimbo wao wa Noeli, “Hear Angels Cry”, yaani: “Sikia Kilio cha Malaika”. “Wimbo huo unaendana na imani kuwa na matumaini ya maisha bora ya baadaye, yaliyozaliwa katika mioyo ya wanadamu.”

Uungwaji mkono wa Papa

Baba Mtakatifu, Papa Francisko, katika muktadha huo, sio tu kwamba amesikia kuhusu wimbo huo, bali ametuma ujumbe kwa Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu, Katoliki wa Uingereza na Walles akiupongeza kwa kutoa kipaumbele katika  “umuhimu mkuu wa jiji ambalo Yesu Kristo alizaliwa  na kukulia.”  Katika Ujumbe wake uliotiwa saini na Kardinali  Pietro Parolin, Katibu wa Vatican unabainisha  kwamba  “Nchi Takatifu ni mahali palipokuwa nyumbani kwa Yesu, Mfalme wa Amani, na kuitwa mahali pa kukutana, mazungumzo na matumaini kwa wote,” kwa njia hiyo “matumaini yake ni kuwa wimbo huo utawatia moyo watu wengi  katika Noeli hii ili kusali kwa ajili ya kushamiri kwa mshikamano wa kidugu, upatanisho na amani katika Nchi Takatifu.”

Sikiliza

Unaweza kutazama wimbo wa “Sikia Malaika Wakilia” kupitia  YouTube. Wimbo huu pia unatiririshwa kwenye Spotify na Apple Music. Unaweza pia kuunga mkono juhudi za kuchangisha pesa kwa wanaoteseka katika Nchi Takatifu kwa kununua wimbo huo kupitia Amazon.

Matumaini ya Youstina Safar

Mwimbaji Youstina Safar anatumaini kuwa wimbo wa Hear Angels Cry utatoa nuru gizani: “Katikati ya kukata tamaa, wimbo wetu wa Hear Angels Cry unasimama kama ushuhuda wa roho ya kudumu ya matumaini katika mji wa Bethlehemu. Ingawa maonesho ya kiutamaduni ya Noeli  yanaweza kufifia mwaka huu kwa ukumbusho wa maisha yaliyopotea huko Gaza, sauti zetu zinaungana kuthibitisha kwamba matumaini hayataingia gizani kamwe.” Alisema.

Cherrie Anderson

Kwa upande wa Cherrie Anderson, kutoka bendi ya Ooberfuse, alisema: “Tulipoanzisha mpango huu wa muziki mwezi wa Juni, hatukutarajia kamwe kukataliwa katika maonesho ya Noeli  huko Bethlehemu. Taa zenye mwanga hafifu katika Uwanja wa Madhabahu zinawaheshimu wale waliopoteza maisha katika Nchi Takatifu. Wimbo wa Sikia Malaika Wakilia unajumuisha ujumbe wa Yesu wa upendo, unaoenea hata katika hali ya kutokuwa na tumaini. Mapato yote kutoka katika wimbo huo yatanufaisha moja kwa moja wale wanaoteseka huko Gaza, hasa watoto wanaounda upya vipande vya maisha yao.”

Mshirika, John Handal

Na kama mshirika katika mpango huo, John Handal, mtayarishaji wa muziki kutoka Bethlehem, na mmiliki wa RJ Music, amefanya jukumu muhimu katika kuleta ushirikiano wa uhai huu. Kujitolea kwake katika mpango huo kunaonesha maono ya pamoja ya kutumia muziki kama mwanga wa matumaini na uponyaji katika eneo hili. “Ni heshima kuwa sehemu ya mpango unaovuka mipaka na kuwaleta pamoja wasanii kutoka Bethlehem na London,”alisema. “Hear Angels Cry ni ushuhuda wa nguvu ya kudumu ya muziki kuwasilisha ujumbe wa amani na uthabiti.

Sikiliza Malaika wakilia ni ombi la moyoni

Sikiliza Malaika Wakilia si wimbo tu bali ni ombi la kutoka moyoni kwa ajili ya umoja, huruma, na nguvu ya kudumu ya tumaini, hata katika hali ngumu zaidi. Noeli hii, duniani inaalika kujumuika katika ujumbe huu wa mshikamano na msaada kwa wale walioathirika na mapambano yanayoendelea katika Nchi Takatifu. Marafiki wa Nchi Takatifu.

Kusaidia Nchi Takatifu

Mapato kutoka katika wimbo huo yatakwenda kwa Maraki wa Nchi Takatifu, shirika la Upendo la  Uingereza ambalo  pia imesajiliwa  huko Palestina. Kupitia ofisi yake huko Bethlehem, iko mahali pazuri  pa kupata msaada wa dharura, wa kibinafsi kwa familia zinazohitaji sana huko Gaza na Ukingo wa Magharibi na itahakikisha wanaohitaji zaidi wanasaidiwa haraka na mapato kutoka katika wimbo.  

Ujumbe wa Kristo ni nuru

Ujumbe wa Kristo umekuwa nuru, kiroho na kimatendo, kupitia kazi ya taasisi nyingi za Kikristo katika eneo hilo kwa maelfu ya miaka. Jumuiya na taasisi hizi zinamfuata Yesu ambapo alitembea na kuwapenda jirani zao kwa kutoa hospitali, shule bora, vyuo vikuu na huduma za kijamii katika maeneo ya Palestina. Ikiwa ungependa kutoa mchango moja kwa moja ili kusaidia kazi ya Marafiki wa Nchi Takatifu,(   Friends of the Holy Land,) tafadhali tembelea tovuti yake ili kufanya hivyo kwa usalama. Ujumbe wa Papa:https://www.cbcew.org.uk/wp-content/uploads/sites/3/2023/12/Pope-Msg-Bethlehem-Song.pdf

Na kwa maelezo zaidi  katika makala ya Kanisa katoli  la Uingereza na Walles unaweza kubonyeza hapa: https://www.cbcew.org.uk/pope-prays-bethlehem-song-can-inspire-solidarity-reconciliation-and-peace-in-the-holy-land-this-christmas/

Papa apongeza wimbo wa Hear Angels Cry
11 December 2023, 10:27