Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya pili ya Kipindi cha Majilio mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa: Itengenezeni Njia ya Bwana Apite. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya pili ya Kipindi cha Majilio mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa: Itengenezeni Njia ya Bwana Apite. 

Tafakari Dominika ya Pili Kipindi cha Majilio: Intengenezeni Njia ya Bwana Apite!

Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa. Sala, nyimbo na masomo ya dominika hii yana ujumbe wa faraja na matumaini, ujumbe unaoambatanishwa na wajibu wetu wa kuitengeneze njia ya Bwana, kuyanyoosha mapito yake ndani ya mioyo yetu ili aweze kuingia na kukaa nasi. Hii ni sauti ya mtu aliaye nyikani anayetangaza ujio wa Masisha wa Bwana, Mwaliko wa toba na wongofu wa ndani tayari kumpokea anapokuja nyoyoni mwao!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa. Sala, nyimbo na masomo ya dominika hii yana ujumbe wa faraja na matumaini, ujumbe unaoambatanishwa na wajibu wetu wa kuitengeneze njia ya Bwana, kuyanyoosha mapito yake ndani ya mioyo yetu ili aweze kuingia na kukaa nasi. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisema; “Ee Mungu Mwenyenzi Rahimu, tunakuomba mambo ya dunia yasitupinge sisi tunaomkimbilia Mwanao tupate kumlaki, bali hekima yako itufanye tumshiriki yeye”. Ni ujumbe wa maandalizi ya kuzaliwa upya Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu ili atujaze furaha mioyoni mwetu kama wimbo wa mwanzo unavyoashiria ukisema; “Enyi watu wa Sayuni, tazameni Bwana atakuja kuwaokoa mataifa; naye atawasikizisha sauti yake ya utukufu katika furaha ya mioyo yenu” (Isa. 30: 19, 30). Somo la kwanza ni la kitabu cha nabii Isaya (Isa. 40:1-5, 9-11). Somo hili ni ufunguzi wa kitabu cha pili cha Nabii Isaya. Kitabu cha kwanza kinatangaza kuchukuliwa mateka na kitabu cha pili kinatangaza kurudi nyumbani kutoka utumwani. Ndiyo maana katika somo hili Nabii Isaya anawatuliza na kuwafariji watu wake akiwatangazia kuwa utumwa wao umekwisha hivyo wajiweke tayari kwa ujio wa Mkombozi na mchungaji wao mwema atakaowarejesha katika nchi yao.

Mwanadalieni Bwana Njia ili apite
Mwanadalieni Bwana Njia ili apite

Ujumbe huu umebebwa na maneno ya faraja yasemayo; “watulizeni mioyo, watulizeni mioyo watu wangu, asema Mungu wenu. Semeni na moyo wa Yerusalemu kauambieni kwa sauti kuu ya kwamba vita vyake vimekwisha, uovu wake umeachiliwa; kwa kuwa amepokea kwa mkono wa Bwana adhabu maradufu kwa dhambi zake zote”. Ujumbe huu unawapa wajibu wa kuitengeneza nyikani njia ya Bwana, kuyanyoosha jangwani mapito yake, kuinua kila bonde na kushusha kila milima na vilima, kupanyoosha palipopotoka, na palipoparuza kupasawazisha ili utukufu wa Bwana utakapofunuliwa, wote wenye mwili wauone. Ujumbe huu unahusu matayarisho ya kiroho maana mioyo ya watu ilikuwa kama jangwa na nyika kwa sababu ya dhambi zao. Ndiyo maana tangazo linasema kuwa adhabu walioyoipokea kwa dhambi zao imeisha kwa kuwa walitambua makosa yao na dhambi zao, wakatubu na kumlilia Mungu naye akawasamehe dhambi zao na sasa anawaandaa tayari kwa kurudi katika nchi yao. Nasi tunaalikwa tuuvae moyo wa unyenyekevu na kufanya toba ya kweli ili Mungu aingie ndani mwetu na kukaa nasi kwa njia ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Mda uliokubalika ndio sasa na wakati ndio huu wa kujipatanisha na Mungu maana hatuji siku wala saa atakapomtuma mjumbe wake kutuita kwake; anaweza kukawi au kufika mapema hivyo tuwe tayari mda wote.

Yohane Mbatizaji anatangaza ujio wa Kristo Yesu
Yohane Mbatizaji anatangaza ujio wa Kristo Yesu

Somo la pili ni la Waraka wa Pili wa Mtume Petro kwa Watu Wote (2Pet.  3:8-14). Katika somo hili Mtume Petro anajibu swali hili; Kwa nini ujio wa pili wa Yesu unakawia? Jibu ni Mungu anatupa nafasi na Muda ili tujipatanishe naye ili siku atakapotuita tusiwe na lawama mbele zake. Kwa uhakika “Bwana yu aja hata kama anakawia lakini yu aja”. Lazima atatizima ahadi zake maana “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, bali huvumilia, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikirie toba. Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi, hivyo tufanye kujipatanisha naye kila wakati kwa ishini katika mwenendo wa utakatifu, tusiwe na doa, waa la aibu mbele za Bwana huku tukimsubiri kwa furaha tukitenda yatupasayo kwa busara na upendo. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk. 1:1-8). Sehemu hii ya Injili ni mwanzo kabisa mwa Injili ya Marko nayo jinsi inavyoanza ni tofauti kabisa na Injili zingine. Marko anaanza Injili yake akimnukuu Nabii Isaya akisema; Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu kama ilivyoandikwa na Nabii Isaya; “Tazama, namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako. Sauti ya mtu aliaye nyikani itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake”. Sauti hii iliayo nyikani ni ya Yohane Mbatizaji. Ujumbe wa Marko unatuambia kuwa habari njema ni hii; “Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, Mkombozi wetu, ataunda taifa jipya”. Manabii walitabiri juu ya kuja kwake Kristo; na Yohane Mbatizaji alitayarisha ujio wake kwa ubatizo wa toba, wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu, wakabatizwa katika mto Yordani, wakiziungama dhambi zao.

Andaeni Njia ya Bwana kwa Toba na Wongofu wa ndani.
Andaeni Njia ya Bwana kwa Toba na Wongofu wa ndani.

Ujumbe wa Yohane Mbatizaji katika Injili ni mwangwi wa ujumbe wa Nabii Isaya katika somo la kwanza aliyetangaza mwaliko wa kutengeneza njia ya Bwana jangwani. Yohane Mbatizaji anatangaza ujio wa Yesu Kristo yeye mwenyewe akiwa jangwani amevalia vazi la singa ya ngamia na chakula chake kikiwa ni asali na nzige nao watu wakamwendea na kubatizwa ubatizo wa toba. Nasi tunaitwa kuitengeneza njia ya bwana kwa kufanya toba maana dhambi zetu ni kama vichaka, milima, mabonde na miinuko inayotuzuia kumuona Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Hivyo kila mmoja anapaswa kujiuliza ni vichaka na visiki gani vimejaa moyoni, vinavyopaswa kukatwa na kung’olewa? Mda uliokubalika ndio sasa. Tufanye hima kujipatanisha na Mungu katika sakramenti ya kitubio ili Kristo aweze kuzaliwa upya ndani mwetu atuletee furaha na amani ya kweli katika maisha yetu. Tukifanya hivi tutaweza kuimba kwa maneno ya Baruku katika antifona ya komunio tukisema; “Ondoka, ee Yerusalemu, usimame juu; tazama uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu” (Bar. 5:4, 36). Na hivyo sala baada ya komunyo anayotuombea mama Kanisa akisema; “Ee Bwana, baada ya kutushibisha chakula cha roho, tunakuomba kwa unyenyekevu sisi tulioshiriki fumbo hili, utufundishe kuyapima kwa hekima mambo ya dunia na kuyazingatia ya mbinguni” itasikilizwa. Na wimbo wa katikati tunaoimba tukisema; “Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako, utupe wokovu wako. Na nisikie atakavyosema Bwana Mungu, maana atawambia watu wake amani. Hakika wokovu wake u karibu na wamchao, utukufu ukae katika nchi yetu. Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimebusiana. Kweli imechipuka katika nchi, Haki imechungulia kutoka mbinguni. Naam, Bwana atatoa kilicho chema, na nchi yetu itatoa mazao yake. Haki itakwenda mbele zake, nayo itazifanya hatua zake kuwa njia” (Zab.  85: 7-13), matunda yake yatadhihirika katika maisha yetu ya sasa na yale yajayo katika uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Majilio D2
05 December 2023, 14:50