Tafuta

Katika Dominika hii tunawasha mshumaa wa matumaini. Katika Dominika hii tunawasha mshumaa wa matumaini.   (AFP or licensors)

Tafakari ya Dominika ya Pili Majilio Mmwaka B wa Kanisa: Hata Jangwani Kuna Njia

Hii ndio Habari Njema ya Wokovu, kwamba hata jangwani njia inawezekana. Haijalishi upo katika jangwa la aina gani ila habari njema ni kwamba njia inaweza kupatikani. Jangwani kuna ukame, kuna jua, kuna mchanga na mawe lakini njia inapatikana tu. Wewe uko katika jangwa la magonjwa, jangwa la kushuka uchumi, jangwa la misukosuko ya maisha, ndoa nk. Habari njema ni hii, njia inapatakina. Kumbe itengeneze ili Mungu aje katika jangwa lako akuokoe.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Utangulizi Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tumeingia katika Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio mwaka B. Katika Dominika hii tunawasha mshumaa wa matumaini. Haya matumaini ndio tutakayo yaona katika masomo yetu ya leo tutakayosikia hivi punde. Katika somo la kwanza Waisraeli wanapewa matumaini kuwa vita vyake vimekwisha na uovu wake umeachiliwa. Ndugu zangu utumwa hauwezi kuzoeleka. Maneno ya somo la kwanza ni faraja kubwa kwa waisraeli waliokuwa utumwani. Maneno hayo ya Nabii, kwao ni habari njema. Maneno hayo yanawatuliza mioyo ambayo imejeruhiwa sana. Katika maisha ya sasa tuna watumwa wengi sana. Kuna watu wanajihisi ni watumwa kwenye ndoa zao, Familia zao, kazini kwao, nchini kwao nk. Bila shaka wapo watu wengi sana wamejeruhiwa mioyo. Maneno haya ya Nabii Isaya yatutie moyo sasa, ya kuwa utumwa haudumu, maumivu hayadumu. Hayo yote yana mwisho tu. Mungu atakapovunja ukimya, yote yatafika mwisho. Lakini kwa namna ya pekee sana Kristo anapokuja wakati wa Noeli aje kuponya majeraha yako ya Ndoa, Familia, mahusiano, magonjwa ya mwili na roho nk. Faraja kubwa ya Waisraeli ni kwamba muda wa kurudi nyumbani umefika. Hakuna ujumbe mzuri kama huu. Baada ya kutumikishwa sana, kuteseka sana, kujeruhiwa sana, kupigwa sana sasa ni wa kutulizwa na kupata faraja. Hata wewe siku yako ikifika utasahau majeraha yote, maumivu yote pamoja na dharau yote. Hiyo siku itakuwa ni siku ya kubembelezwa, hiyo siku itakuwa wa kutulizwa moyo. Hiyo siku itakuwa kama siku ya kurudi nyumbani kwa Baba. Lakini ili kurudi nyumbani kuna kila sababu ya kutengeneza njia kwanza kama tunavyosikia katika somo la kwanza na Injili. Mara nyingi tunashindwa kutoka utumwani kwa sababu hatujatengeneza njia ya Bwana. Kila siku Mungu anatamani aje kwetu lakini tatizo kubwa bado hatujatengeeza njia. Hivyo hana sehemu ya kupitia ili aje kwetu.  Mungu mwenyewe alitengeneza njia baharini ili waisraeli waweze kutoka Misri. Sasa sisi tunatakiwa tumtengenezee njia ili aweze kuja kwetu. Leo tunaambiwa tutengeneze njia jangwani.

Majilio ni kipindi cha unyenyekevu, saburi na kiasi
Majilio ni kipindi cha unyenyekevu, saburi na kiasi

Katika masomo yetu ya leo hii ndio Habari Njema ya Wokovu, kwamba hata jangwani njia inawezekana. Haijalishi upo katika jangwa la aina gani ila habari njema ni kwamba njia inaweza kupatikani. Jangwani kuna ukame, kuna jua, kuna mchanga na mawe lakini njia inapatikana tu. Wewe uko katika jangwa la magonjwa, jangwa la kushuka uchumi, jangwa la misukosuko ya maisha, ndoa nk. Habari njema ni hii, njia inapatakina. Kumbe itengeneze ili Mungu aje katika jangwa lako akuokoe. Pili, Mabonde yanatakiwa kuinuliwa. Mabonde ni dhambi zetu za kutotimiza wajibu. Kumbe unaposhindwa kutimiza wajibu unatengeneza bonde katika maisha yako. Unapokosa kumsaidia maskini, unaposhindwa kuwajali na kuwasikiliza wanao hitaji msaada wako unatengeneza mabonde katika ukristo wako.  Leo hesabu mabonde yako, ni mangapi? Leo unaalikwa kuyafukia kwa sababuyanamzuia Kristo kuja kwako. Kristo anaweza kuja kwako hata sasa, tatizo ni hilo bonde ambalo hujalifukia. Pili kuna milima mingi sana katika maisha yetu.  Milima nayo ni kiburi na majivuno yanayotufanya tujiinue kama milima mbele ya watu wengine. Yesu anatutaka tuisambaratishe milima hiyo, tukawe wanyenyekevu kama Yohane mbatizaji. Hata alipoona watu wanazidi kuja kubatizwa hakutaka kujiinua sana na kujiona wa maana kuliko Yesu. Katika somo la Injlli yeye mwenyewe kwa unyenyekevu mkubwa anasema, "Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinana na kulegeza gidamu ya viatu vyake." Alijua mipaka yake. Na wewe jua mipaka yako. Leo usivuke mipaka yako. Yohane anajitambua kabisa kuwa hawezi kushika nafasi ya Kristo hata mara moja na hivyo hakuvuka mipaka. Hata kwenye Familia, acheni kuvuka mipaka. Baba ni kichwa, wamama msivuke mipaka. Vijana msivuke mipaka na kujitakia mambo makubwa ambayo sio saizi yenu. Jueni mipaka yenu kwani Yohane mbatizaji ni mfano kwetu leo, hata pale watu walipoongezeka na labda kufikiri kuwa yeye ni masiha, hakuvuka mipaka na kujiona yeye ni Masiha.  Tena yeye kuna sehemu alisema, "mimi nipungue wewe uongezeke." Kama ni wewe au mimi, je, tungeweza kujishusha kiasi hicho?  Wengine wakipewa karama fulani kama kuombea, kuhubiri, karama ya uponyaji na kadhalika mara nyingi wanashindwa kuwa wanyenyekevu.

Mtengenezeeni Bwana Njia ili azaliwe kati yenu
Mtengenezeeni Bwana Njia ili azaliwe kati yenu

Wengine wakipanda cheo au kusoma sana wanatunyima usingizi walivyo wasumbufu. Kuna wakati tunatakiwa kuangalia nyuma, tunapoona mafanikio yetu tuseme, ni Mungu tu. Wewe umesoma kwa sababu ni Mungu tu, umeolewa kwa sababu ni Mungu tu, umepanda cheo kwa sababu ni Mungu tu. Ndugu zangu tujifunze kuwa wanyenyekevu kama Yohane Mbatizaji. Yohane alibatiza ubatizo wa toba na hii ndio iliyokuwa namna moja ya kuwafanya watu watengeneze njia zao. Kristo anakuja kwetu krismasi hii, kila mmoja ajiulize njia yangu iko tayari? Je ina kona za ujanja, ina mabonde ya kutotimiza wajibu, ina vilima vya kiburi? Leo tunaambiwa tunyoshe. Kuna watu wanapindisha ukweli, leo tunaalikwa kunyoosha.  Tutengeneze njia safi na kumsubiri Kristo aje kwetu kwa wakati wake. Hatujui atakuja lini ila kazi yetu ni kutengeneza njia na kumsubiri.  Katika somo la pili wakristo wa kwanza walimngoja Bwana sana. Waliamini Kristo atarudi upesi sana. Sasa walipoona hajarudi, wakaanza kuwa na mashaka. Hapo ndipo petro anapofafanua katika somo la pili kuwa, kwa Mungu siku moja ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja.  Saa ya Mungu ni tofauti na ya Binadamu. Mungu huwa anakuja kwa wakati wake na kwa wakati unaofaa na hasa unaokufaa wewe. Kuna Wakati tunaona Mungu amekawia sana, alitakiwa kuja jana, alitakiwa kuja leo saa nane lakini hajafika. Kuna wakati tunaona kama ni muongo, lakini ukweli ni kwamba, kama hajafika, wakati wake haujafika.  Kazi yetu ni moja tu, nayo ni kumngoja Bwana. Kuna wakati Mungu huwa anachelewa kuja ili atupe nafasi zaidi ya kujiandaa. Nafasi ya kusawasisha milima na kufukia mabonde yetu. Kipindi cha majilio basi ni muda tuliopewa wa kufukia mabonde na kushusha vilima tulivyo navyo katika maisha yetu. Basi tutumie fursa hii vizuri. Nakutakia DOMINIKA njema ya kufukia mabonde na kushusha vilima.

Liturujia D2 Majilio
08 December 2023, 16:05