Tafuta

Ni sherehe kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani. Ni sherehe kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani. 

Sherehe ya Noeli Mwaka B wa Kanisa: Misa ya Mchana: Neno wa Mungu Akatwaa Mwili

Noeli ni sherehe ya Umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa mwanadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo; “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu” (Isa.9:6). Hii ni sherehe ya imani, matumaini na mapendo thabiti.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya neno la Mungu katika ya Liturujia ya Neno la Mungu Misa ya mchana Sherehe ya Noeli. Ni sherehe ya Umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, kuwa mwanadamu na kukaa kwetu. Ni sherehe kuzaliwa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu, Emmanueli, Mungu pamoja nasi, Mfalme wa Amani kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo; “Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu” (Isa.9:6). Naye Mama Kanisa katika sala mwanzo anatuombea akisema; “Ee Mungu, ulimweka mwanadamu katika cheo cha ajabu, na tena ukamtengeneza upya kwa namna ya ajabu zaidi. Tunakuomba utujalie kushiriki umungu wake, yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu.” Kazi ya mfalme ni kutawala na kuongoza. Kristo amekuja kutawala maisha yetu na kutuongoza kwa Mungu. Amekuja kuanzisha utawala wa Mungu duniani; utawala wa haki na amani, umoja na upendo. Ni Mungu aliyetwaa sura, umbo na mwili wa kibinadamu na kuzaliwa kati yetu kama mtoto mchanga. Kuzaliwa kwake ni mwanzo wa utimilifu wa ukombozi wetu kutimia, na nuru kuushukia ulimwengu. Nuru hii inamwangazia kila anayeipokea ili aweze kuona njia ya kwenda Mbinguni kwa Mungu Baba, maana kila anayeipokea Nuru hii, kwake huondolewa giza la dhambi. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:7-10). Somo hili limegawinyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni wasifu wa mjumbe wa Mungu anayewantangazia watu amani; “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima miguu yake aletaye habari njema. Yeye aitangazaye amani, aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki! Sauti ya walinzi wako! Wanapaza sauti zao, wanaimba pamoja; Maana wataona jicho kwa jicho, jinsi Bwana arejeavyo Sayuni” (Isa. 52:7-8).

Kristo amezaliwa ili kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini
Kristo amezaliwa ili kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini

Ni ahadi ya kuwarudisha kutoka utumwani. Ni ujumbe wa matumaini kuwa amani imefika, vita sasa vimekwisha, utumwa umekwisha. Utumwa huu ni mfano wa hali ya dhambi, na ukombozi huo ni mfano wa ukombozi wa mataifa yote kutoka dhambini. Sehemu ya pili ni mwaliko wa watu kufurahi ambapo Nabii anawaambia; “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa. Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, ameukomboa Yerusalemu. Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu macho pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia, zitauona wokovu wa Mungu wetu” (Isa. 52:9-10). Ujumbe huu ni utabiri wa ukombozi wa watu wote kutoka utumwa wa dhambi. Nasi tunafurahia kuupata kwa kuzaliwa kwake Yesu Kristo wokovu wetu kama tunavyoimba katika wimbo wa katikati tukisema; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. Bwana ameufunua wokovu wake, machoni pa mataifa amedhihirisha haki yake. Amezikumbuka rehema zake, na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni Bwana, nchi yote, inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za zaburi. Kwa panda na sauti ya baragumu, shangilieni mbele za Mfalme, Bwana” (Zab. 98:1-6). Somo la Pili ni la Waraka kwa Waebrania (Ebr. 1:1-6). Somo hili liweka wazi kuwa utabiri wa kale umetimia katika Yesu Kristo. Katika yeye utukufu wa Mungu umefunuliwa na ni katika yeye tu Mungu anaongea nasi katika nyakati hizi zetu. Tunasoma hivi; “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwanaye, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu….Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu.” Kumbe mtoto Yesu ni chapa ya Mungu. Na tukitaka kumuona Mungu, tumuangalie mtoto Yesu kwa macho ya imani, na tukitaka tumpokee Mungu katika maisha yetu, tumpokee mtoto Yesu.

Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo
Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo

Injili ni kama ilivyoandikwa na Injili ya Yohane (Yn 1:1-18). Licha ya kuwa Injili zote nne zinasimilia habari zake Bwana wetu Yesu Kristo, kila Mwinjili ana namna yake ya kuanza na kumalizia katika kuandika. Marko, yeye anaanza kwa kuandika habari za Yesu kuanza kuhubiri na hajishughulishi kabisa na habari ya kuzaliwa kwake. Mathayo na Luka licha ya kuwa wote wanaanza kwa habari za fumbo la umwilisho - Neno wa Mungu kutwaa mwili – kuzaliwa kwake Yesu, kila mmoja naye ana namna yake ya kuanza. Mathayo anaanza kwa kueleza ukoo wa Yesu kuanzia kwa Ibrahimu mpaka kwa Yosefu wa ukoo wa Daudi. Luka kwa upande wake licha ya kuwa anaweka wazi kuwa Yesu amezaliwa katika ukoo wa Daudi, msisitizo wake uko katika nafasi ya Bikira Maria katika historia ya ukombozi wetu. Yohane kwa upande wake anaanza kwa kutuonyesha nini kilikuwepo hapo mwanzo wa uumbaji, na nani walihusika katika uumbaji. Hapa tunafahamishwa kuwa Yesu ni Neno wa Mungu naye tangu mwanzo alikuwa Mungu kama anavyoandika Paulo katika waraka wake kwa wafilipi akisema; “Yesu kwa asili alikuwa daima Mungu, lakini hakufikiri kwamba kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kung’ang’ania kwa nguvu, bali kwa hiyari yake mwenyewe aliachilia hayo yote akajitwalia hali ya mtumishi akawa sawa na wanadamu, akaonekana kama wanadamu” (Flp. 2:6-7). Lengo ni kumkomboa mwanadamu toka utumwa wa dhambi na mauti. Kumbe, Noeli ni sherehe ya matumaini kwa wanaokandamizwa na dhambi, wasiojua mema na mabaya, mafisadi, makahaba, wezi, wakimbizi, mateka wa vita, wanaodhulumiwa haki zao, yatima, wajane, maskini, na walemavu. Hawa ndio “wanaokwenda katika giza na kukaa katika nchi ya uvuli wa mauti”. Hawa ndio wanaotamani kuona Nuru inawaangazia.

Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na nuru ya Mataifa

Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake kuhusu Maendeleo ya watu, “Populorum Progressio”,  wa 26 Machi 1967 anasema; “Ni wajibu wa Kanisa likishirikiana na serikali na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha hawa watu wanapata ukombozi, na kurudishiwa hadhi yao.” Kwa maana hiyo Kanisa linaendeleza kazi ya Kristo ya kumkomboa mwanadamu kiroho, kimwili, kiakili na kijamii ili awe karibu zaidi na Mungu aliye asili ya hadhi na heshima yake. Naye Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” katika sura ya tano anaisisitiza kuwa; Serikali za dunia zenye umakini na siasa safi zinapaswa kushirikiana na Kanisa katika kuondoa na kutokomeza ujinga, umaskini, maradhi na kuleta maendeleo, ili kuhakikisha kuwa mwanadamu anatibiwa na kupona kimwili na  kiroho kwa kuzingatia utu, haki msingi za kibinadamu na baada ya maisha yake hapa duniani aurithi uzima wa milele. Serikali inapaswa kuhakikisha nchi inatiririka maziwa na asali ili watu wake waishi kwa furaha na amani. Kanisa linamhakikishia huyu mtu kuwa furaha hii itakamilishwa katika uzima wa milele. Na wakati mtu huyu duni akitibiwa na kuhudumiwa anaendelea kuheshimiwa katika hali zote akiwa mchanga, mdogo, kijana, mzee, kikongwe, mdhambi, masikini au tajiri, mjinga au msomi, anabaki na hadhi na heshima yake kama binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Hivyo serikali inapaswa kumlinda kila mmoja kwa kuzingatia katiba, sheria na itikadi zilizowekwa kwa usawa. Kama tulivyokuwa tunaimba wakati wa majilio, “Dondokeni enyi mbingu toka juu, na mawingu yammwage mwenye haki, nchi ifunguke na kumtoa Mwokozi”. Mbingu zimeshafunguka na mawingu yameshammwaga mwenye haki na nchi imekwishafunguka kumtuoa mwokozi ndiye Kristo Yesu. Basi, tuifungue mioyo yetu tumpokee Yeye aliye Nuru iliyokuja ulimwenguni, ituangaze katika njia ya kwenda mbinguni kama mama Kanisa anavyotuombea katika sala baada ya komunyo akisema; “Ee Mungu mwenye huruma, tunaomba huyo Mwokozi wa dunia aliyezaliwa akatufanya watoto wako, atujalie pia uzima wa milele”. Nawatakieni heri na baraka za kuzaliwa mtoto Yesu. Tumsifu Yesu Kristo.

Noeli Mchana Ok
23 December 2023, 15:07