Tafuta

Malaika wanaimba “Gloria in excensis Deo”, yaani “Utukufu juu mbinguni duniani kuwe na amani kwa wote wenye mapenzi mema.” Malaika wanaimba “Gloria in excensis Deo”, yaani “Utukufu juu mbinguni duniani kuwe na amani kwa wote wenye mapenzi mema.”   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sherehe ya Noeli Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu Ni Mfalme wa Haki na Amani

Malaika wanaimba: “Utukufu juu mbinguni duniani kuwe na amani kwa wote wenye mapenzi mema.” Ni furaha kuu kwa kuwa Nuru kuu imewazukia na giza limeondolewa; uUe umbali ulioletwa na dhambi ya kale sasa umefutwa naye Mungu amekuja ili kuziunganisha mbingu na nchi, Mungu na wanadamu katika Mwanaye aliyezaliwa, Sherehe ya Noeli ni wakati Sahihi ambapo watu wengi na dini mbalimbali hasa wakristo kote duniani, wanasherehekea Noeli ya Bwana.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, leo ni Sherehe kubwa, siku ambapo watu wa kila kabila, rangi, taifa, na lugha, watu wa kila bara, wa mijini na vijijini (urbi et orbi), wakubwa kwa wadogo, wake kwa waume; wote wanashangilia, Malaika wanaimba “Gloria in excensis Deo”, yaani “Utukufu juu mbinguni duniani kuwe na amani kwa wote wenye mapenzi mema.” Ni furaha kuu kwa kuwa Nuru kuu imewazukia na giza limeondolewa, ni furaha kwa sababu ule umbali ulioletwa na dhambi ya kale sasa umefutwa naye Mungu amekuja ili kututafuta kaziunganisha mbingu na nchi, Mungu na wanadamu katika Mwanaye aliyezaliwa, Sherehe ya Noeli ni wakati Sahihi ambapo watu wengi na dini mbalimbali hasa wakristo kote duniani, wanasherehekea Siku ya kuzaliwa Bwana Yesu Kristo katika fumbo la umwilisho.Ni vema kukumbuka kwamba hatusherekei na kuadhimisha tarehe bali ni tukio la kuzaliwa Bwana Yesu.Waswahili wanasema “mgeni njoo mwenyeji apone”, hakika ni kweli. UFAFANUZI: Tukio la kuzaliwa Bwana Yesu Kristo katika kipindi cha Noeli linaanzisha safari rasmi ukombozi wa sisi wanadamu kiroho, kimwili na kimaisha kiujumla. Yesu ni mgeni wetu rasmi anayekuja kututembelea. Tujiulize mgeni huyu amesukumwa na nini kuja kwetu na ametuletea nini?  Noeli ni Sherehe ya Mapendo na amani. Tumkaribishe Yesu mgeni wetu ili azaliwe kwetu na kuyabadilisha maisha yetu, Je, umemkaribisha mgeni. Au huna taarifa yoyote? Katika somo la kwanza, Nabii Isaya anatuambia kuwa “Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki.” Huyu ndiye Yesu mfalme wa amani na mgeni wetu rasmi katika kipindi hiki cha Noeli.

Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, amani duniani
Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, amani duniani

Leo Neno wa Mungu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele, Mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa kweli ameutwaa ubinadamu kama ilivyotabiriwa, ameshuka duniani katika mwili na kukaa kati yetu. Amekuja kufanya nini? Amekuja ili afe (Anasema mwenye heri askofu mkuu Fultoni. Sheen) na kwa kifo hicho sisi tuupate uzima tena tuwe nao tele. Huyu Mtoto ndiye Mwana pekee wa Baba, ni Mungu na mtu pia, ni Mkombozi, ni Mfalme, ni Bwana, ndiye Mwana wa Bikira Maria, katika Yeye vitu vyote hujimudu na kuwa na uhai, wala pasipo Yeye hakuna chochote kile kilichofanyika, ndiye utimilifu wa neema na ni katika Yeye Agano la Mungu na watu wake linatimia na ni katika Yeye Agano la awali (Abraham, Musa, Daudi) linakuwa la Kale (zamani) na Yeye anakuwa Agano Jipya na la Milele. Vivyo katika somo la pili, tunasikia kwamba “Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu.” Yesu ambaye anazaliwa leo ni chapa ya Mungu ambaye tangu kuanguka kwetu dhambini anatutafuta kutukomboa. Manabii walitabiri zamani na sasa waliyotabiri yanakamilishwa na kuzaliwa kwa Yesu.Yesu kwa kuzaliwa kwake anatuonyesha upendo mkubwa kwetu,anatufundisha unyenyekevu na mwisho anatutunukia zawadi ya amani ambayo ni lulu adimu inayotafutwa na kila mmoja wetu.

Watu wameouona utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi
Watu wameouona utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi

Mpendwa, mwenye sifa hizo ndiye aliyezaliwa leo, nasi tumeuona utukufu wake, tunapaswa kumtambua na kumuelekea, basi twendeni Betlehemu, tukamuone mtoto na mama, tuwasalimie huko, tuwape na zawadi zetu. Pongezi za pekee na za dhati zimwendee Binti wa pekee wa Nazareti yaani Bikira Maria kwa “kumvika nguo za kitoto na kumlaza walau mahali pa kulishia ng’ombe”, tunamshukuru mama huyu kwa kumruhusu Mkombozi mkuu kama huyu azaliwe ili dunia nzima iokolewe. Hii ni kutokana na ukweli kuwa leo hii kutokana na utamaduni wa kifo, kupigiwa kampeni na kushangliwa baadhi ya akina dada na akina mama wengi duniani kote hawana amani, furaha namatumaini ya Maisha yao kwa sababu mara zote wanasikia sauti na mwangi katika dhamiri na akili zao, au ndotoni sauti za watoto wachanga zikilalamika, “mama mama, mbona uliniua? Kwa nini hukuniacha nizaliwe? Kwa nini umenitupa kwenye choo, au kwenye jalala ndani? Ona mama, ningekuwa mkubwa sasa hivi na hakika ningekusaidia katika mahangaiko yako, lakini wewe hukuniacha nizaliwe, umeniua kabla ya kuzaliwa, umenitupa baada ya kunizaa, umeniharibu kwa umekatisha uhai na haki yangu nisione uso wa dunia ukatili usioelezeka.

Kristo Yesu ni Mfalme wa haki na amani
Kristo Yesu ni Mfalme wa haki na amani

Tumbo lako limekuwa siyo tumbo tena linaalobeba uhai bali ni sawa chumba cha kuhifadhia maiti “mortuary’s” hii ni habari ya huzuni, kama Maria katika mazingira magumu aliyokuwa nayo angetoa mimba, halafu ukombozi wetu ungetoka wapi? Kila mmoja ana fungu lake naye Mungu ana mpango na kila mtoto anayezaliwa uso wa dunia, kwa nini tunawaua? Mimi/wewe siyo chanzo cha uhai, haki ya kuwaangamiza tunaitoa wapi? Je, aibu ya mimba, hofu ya shule na masomo, urembo na umaridadi, mfumo wa Maisha na usasa, urafiki, talaka, mume, ndugu na mengine mengi, Je, hayo yote ni sawa na uhai wa mwanadamu? Kumbuka kuwa watoto wanaouawa hivi ni malaika wa Mungu, wengine wangekuwa madaktari bingwa, wahandisi, marais, mapadre na watawa wema, hapana, hapana ndugu zanguni, hii haiwezekani, na katika hili hakuna urafiki hakuna undugu, asante sana Mama Maria hakika izazi vyoteitaendelea kukuita mbarikiwa. Pia katika Injili, Matayo anaonyesha namna ya unasaba auuhusiano wa Mungu kuwa mwanadamu kwa kuzaliwa na mwanadamu kama wazaliwayo wanadamu wengine kinachomtofautisha ni kuwa yeye anazaliwa kwa uwezo wa roho mtatifu kutoka tumbo la bikila Maria na kupewa jina  “ Emanuel yaani Mungu pamoja nasi” huu ni udhihilisho wa mpango wa Mungu tangu awali, kuwa alipanga kumkomboa mtu kutoka utumwa wa dhambi n ana kumweka katika uhuru wa kuwa mwana pamoja namwanae wa pekee ndio nafsi ya pili ya Mungu katika utatu mtakatifu. hapo mwanzo alikuwapo neno, naye neno alikuwako kwa Mungu, naye neno alikuwa Mungu.Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.”

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu

Yesu anatuletea uzima mpya kwa kutupatanisha na Mungu wetu. Dhambi inatukosesha amani na Mungu na inatuweka mbali naye. Sasa tuangalie huyu mgeni wetu Yesu amesukumwa na nini kuja hapa duniani kwa safari ndefu hii kutoka mbuinguni? kama tunayokumbushwa mara nyingi na amafundisho ya mama kanisa kutoka katika katekismu kuwa Mungu amaetuumba kwa malengo haya, tumjue, tumpende, tumtumikie, na hatimae tufike mbinguni alipo.  Tumpe nafasi Mtoto Yesu azaliwe kwetu leo hii, tumkaribishe, awe mgeni wetu tunapokula, awe msikilizaji wa mazungumzo yetu, achangie mawazo katika mipango yetu nasi tutabarikiwa. Katika Maisha: Ni vema kutambua kwamba Noeli ni sikukuu kubwa sana kwetu tunapoaadhimisha fumbo la umwilisho yaani Mungu kuzaliwa kwetu kama mwanadamu.Yatupasa kuwa watu wenye upendo katika mawazo,maneno na matendo yetu ili tumshuhudie mtoto Yesu.Mtoto Yesu ni zawadi iliyo kuu zaidi ambayo Mungu aliizawadia dunia,dunia hii ndogo sana inayopotea katika anga kuu kati ya mamilioni ya nyota,lakini iliyoteuliwa na kuchaguliwa,hadi kuwa maskani ya kweli ya Mungu aliyejifanya mtu.Noeli inapaza sauti kwetu kwanba Mungu anatupenda,Mungu ni upendo. Tunavyokumbuka pia kuzaliwa kwa Bwana Yesu,tutafakari kwa kina na mapana suala tete la amani na jinsi ya kuipata. Amani ni hazina iliyositirika ambayo tunaitafuta kwa udi na uvumba.Basi tujifunze kuwa na amani na Mungu wetu,amani ndani yetu na amani na wenzetu.Hili linawezekana tu kama tukijibidisha kushika imani yetu kikamilifu,kuwa thabiti katika kutimiza mapenzi ya Mungu na kutochoka kutenda mema kwa watu wote,katika hali zote na mazingira yote.Mtoto yesu ni shule ya upendo na amani ya kweli. Ni vema kutilia mkazo jambo hili hasa tunaposherekea sikukuu ya kuzaliwa Bwana kwamba mtu mtakatifu afurahi kwa kuwa anaikaribia taji ya ushindi; mtu mwenye dhambi, yeye naye afurahi kwa kuwa anasamehewa dhambi zake; na mpagani sharti afurahi kwa kuwa anaitwa kupewa uzima na mgeni wetu rasmi Yesu Kristo. Na pia tuunganike pamoja na Malaika kumshangilia Yesu aliyezaliwa huku tukiimba “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni”na kwa sauti tutangaze “Amani duniani kwa watu waliopendezwa nao.” Sasa tumshangilie kwa nderemo, vifijo na chereko mtoto Yesu anayekuja kwetu kwa mapendo kutuletea zawadi kemkem ya amani. Tuwe na sikukuu njema ya Krismas yenye baraka tele na neema lukuki. Heri ya Sherehe ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Aleluya!

Sherehe Noeli 2023

 

23 December 2023, 15:39