Tafuta

Wanafunzi Wakatoliki kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania wanaadhimisha Kongamano la 15 la Kitaifa, Jimbo kuu la Mwanza, 2023. Wanafunzi Wakatoliki kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania wanaadhimisha Kongamano la 15 la Kitaifa, Jimbo kuu la Mwanza, 2023. 

Kongamano la 15 la Kitaifa la Wanafunzi Wakatoliki Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu, 2023

Wanafunzi Wakatoliki kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania wanaadhimisha Kongamano la 15 la Kitaifa linalofanyika Kitaifa katika Jimbo Kuu Katoliki Mwanza kuanzia tarehe 26 Desemba hadi tarehe 30 Desemba 2023 wakiongozwa na mada kuu “Kijana, Familia na Uumbaji.” Mada nyingine ni: Nafasi ya kijana katika kuthamini, kutunza uumbaji na kujithamini; uwekaji wa akiba ni msingi wa uchumi bora na maendeleo; Uwajibikaji ni wajibu wa Kikristo!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, - Jimbo Kuu Katoliki Mwanza, Tanzania

Ubora wa elimu unapimwa kwa kuangalia thamani yake katika maisha na uwezo wa kuanzisha utamaduni mpya unaowashirikisha watu wengi zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa wito kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kutoka katika sekta ya utamaduni, sayansi, sanaa na michezo na wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii kushiriki katika Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” kwa njia ya ushuhuda na kazi zao. Wasaidie kuhamasisha tunu msingi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani; uzuri, wema, ukarimu na udugu wa kibinadamu. Kila mtu ajitahidi kuwajibika, ili kuendeleza mchakato wa mageuzi; ili kuganga na kuponya ulimwengu huu ambao umejeruhiwa vibaya; kila mmoja, akijitahidi kuwa ni Msamaria mwema, anayeguswa na mahangaiko ya wengine, badala ya kuchochea chuki na uhasama kati ya jamii ya binadamu. Huu ni mfumo wa elimu wenye mwono mpana na wenye uwezo wa kuwashirikisha wote ili kutoa majibu yatakayosaidia kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ulimwengu mamboleo unawahitaji watu watakaojenga na kudumisha amani na utulivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mtu binafsi, anawajibika kutoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa mfumo mpya wa elimu: utu na heshima ya binadamu, ili hatimaye, kila mtu aweze kuonesha: uzuri na upekee wake; uwezo wa kuhusiana na kufungamana na wengine katika hali na mazingira yanayowazunguka, ili kuondokana na utamaduni wa chuki na uhasama ambao kimsingi umepitwa na wakati. Huu ni muda wa kusikiliza na kujibu kilio cha watoto na vijana wanaorithishwa tunu msingi, uelewa na ufahamu, ili kwa pamoja waweze kujenga leo na kesho inayosimikwa katika haki, amani na maisha bora zaidi.

Kongamano la 15 la Kitaifa la wanafunzi wakatoliki vyuo vikuu, 2023
Kongamano la 15 la Kitaifa la wanafunzi wakatoliki vyuo vikuu, 2023

Wakati huo huo, Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu katika barua yake ijulikanayo kama “The Presence of the Church in the University and in University Culture” yaani “Uwepo wa Kanisa katika Chuo Kikuu na katika Utamaduni wa Chuo Kikuu” iliyotolewa Mei 22, 1994 inasema, “Uwepo wa Wakatoliki katika Chuo Kikuu ni matumaini kwa Kanisa.” Hata hivyo, barua hiyo hiyo inatazama changamoto kubwa iliyopo vyuoni kwa kusema, “Walimu wengi na wanafunzi huchukulia imani yao kuwa jambo la kibinafsi, au hawaoni athari za maisha yao ya chuo kikuu juu ya uwepo wao wa kikristo. Uwepo wao katika Chuo Kikuu inaonekana kama mabano katika maisha yao ya imani. Baadhi, miongoni mwao hata makuhani au watawa, kwa jina la uhuru wa chuo kikuu, huenda mbali bila hata ya kuacha ushuhuda wowote wa wazi wa imani yao. Wengine hutumia uhuru huu kueneza mafundisho kinyume na mafundisho ya Kanisa.”

Mada kuu: Kijana, Familia na UUmbaji
Mada kuu: Kijana, Familia na UUmbaji

Katika juhudi za kuitatua changamoto hii, Kanisa Katoliki nchini Tanzania limeendelea kuwatazama kwa upekee wanafunzi Wakaoliki katika vyuo na taasisi nyingine za elimu ya juu kwa kujitahidi kuwapatia fursa za kuwajenga kiimani ili waweze kweli kuwa mashuhuda imara wa imani katika vyuo walivyoko. Ni katika muktadha huu Wanafunzi Wakatoliki kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania wanaadhimisha Kongamano la 15 la Kitaifa la Wanafunzi Wakatoliki wa Vyuo Vikuu kupitia umoja wao ujulikanao kama “Tanzania Movement of Catholic Students” (TMCS) linalofanyika Kitaifa katika Jimbo Kuu Katoliki Mwanza katika Shule ya Wasichana ya Loreto kuanzia Desemba 26 hadi Desemba 30, 2023. Wakiongozwa na mada kuu “Kijana, Familia na Uumbaji.” Mada nyingine ni pamoja na “Nafasi ya Kijana katika Kuthamini, Kutunza Uumbaji na Kujitambua,” “Uwekaji wa Akiba ni Msingi wa Uchumi Bora na Maendeleo,” “Uwajibikaji ni Wajibu wa Kikristo: Mfano wa Familia Takatifu” Pamoja na “Kuushuhudia Ukatoliki Kiaminifu katika Mazingira ya Usasa.” Miongoni mwa wawezeshaji katika kongamano hili ni pamoja na: Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Askofu Simon Masondole wa Jimbo Katoliki Bunda, Askofu Methodius Kilaini, Askofu Msaidizi na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Bukoba pamoja na Profesa Padre Aidan Msafiri.

Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote
Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote

Naye Mhashamu Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara wakati wa mahubiri katika Misa ya Ufunguzi wa Kongamano hilo, Desemba 27, 2023 katika Sikukuu ya Mt. Yohane Mtume na Mwinjili, amewataka Wanafunzi Wakatoliki kutoka vyuo mbalimbali Tanzania kukataa kwa nguvu vitendo vya ushoga na usagaji. Askofu Niwemugizi amesema wazi kuwa mafundisho ya Kanisa Katoliki hayajabadilika kuhusu ndoa na ya kwamba kutoka katika ufunuo wa Maandiko Matakatifu miungano ya mume na mume ni haramu na ya kwamba fundisho hilo haliwezi kubadilika hata kama watu wangetamani namna gani. Ameongeza kusema kuwa Mungu hakuwa mjinga alipoumba Adamu na Eva. Askofu Nimemugizi anasisitiza kuwa ushoga unapingana na kazi ya uumbaji aliyoweka Mungu katika mpango wa ndoa. Amewasihi vijana Wanafunzi Wakatoliki walioko vyuoni kujifunza kusema hapana kwa lolote linalowaelekeza kuingia katika ubaya, lolote linalopingana na mapenzi ya Mungu. Askofu Niwemugizi ametoa tahadhari kuwa mambo ya ushoga na usagaji yanaendelea hata nchini Tanzania kwani wapo watu wanaotumia mahitaji ya wengine, hasa mahitaji ya pesa, kupenyeza ushoga na usagaji. Anasisitiza akisema, “tupo katika nyakati za kuchanganyikiwa, za kuvurugukiwa na hivyo tunamhitaji zaidi Kristo Yesu sasa ili kutuongoza tena, kutufunua macho ili kutoka katika giza linalousakama ulimwengu. Vijana wanapaswa kuujua ukweli, kuukubali ukweli na kuuishi na kuushuhudia ukweli, amesisitiza Askofu Niwemugizi. Kongamango la 15 la Kitaifa la Wanafunzi Wakatoliki kutoka Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu linahudhuriwa na washiriki 1,450 toka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki Tanzania pamoja na wageni waalikwa kutoka Kenya na Zimbabwe huku pia likihudhuriwa na Mheshimiwa Patrobas Katambi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kongamano hili litadumu kwa muda wa siku 5 hadi litakapofungwa rasmi tarehe 30 Desemba 2023.

Kongamano vijana 2023
28 December 2023, 14:51