Dkt. Philip Isdor Mpango Akemea Matumizi Mabaya ya Mitandao ya Kijamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango. tarehe 10 Desemba 2023, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio ameshiriki Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege, Jimbo kuu la Dodoma. Ibada hiyo imeongozwa na Padre Dionis Paskal Safari. Amepata fursa ya kusalimiana na waamini Parokiani hapo, takribani mwezi mmoja bila ya kuonekana hadharani.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, Makamu wa Rais amewaasa watanzania kutumia vema mitandao ya kijamii. Amesema matumizi yasiofaa ya mitandao ya kijamii yamekuwa yakiumiza watu wengi hivyo yampasa kila mmoja kutumia vema pamoja na kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu.
Makamu wa Rais amewashukuru waamini hao kwa kuendelea kumwombea ili aweze kutekeleza vema majukumu yake. “Asanteni sana kwa kuniombea. Yamesemwa mengi si ndio? Na wengine wanasema mimi ni mzuka” amesema Dk Mpango. Amesema kwa takribani mwezi mmoja ambao hakuwa masikioni wala machoni mwa wengi ni kwa sababu alikuwa nje ya nchi kwa ajili ya shughuli maalumu. “Wengine wanasema mzee amakata moto. Bado kabisa, kazi ambayo Mungu amenituma kufanya sijaimaliza. Wakati utakapofika nitarejea kwa Muumba wangu.” alisema Dakta Mpango huku akishukuru wote waliomwombea.