Tafuta

Idadi ya watanzania waliofariki kwenye mafuriko pamoja na maporomoko ya udongo hadi kufikia Alhamisi tarehe 7 Desemba 2023 ilikuwa ni watu 69, Idadi ya watanzania waliofariki kwenye mafuriko pamoja na maporomoko ya udongo hadi kufikia Alhamisi tarehe 7 Desemba 2023 ilikuwa ni watu 69,  

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Maafa ya Hanang, Manyara!

Taarifa inaonesha kwamba, hadi kufikia Alhamisi tarehe 7 Desemba 2023 ilikuwa ni watu 69, majeruhi ni watu 116, wagonjwa waliolazwa hospitalini ni 90 na kwamba, kaya 1,150 zimeathirika kwa mafuriko na maporomoko ya ardhi. Kwa ujumla watu 5,600 wameathirika kutokana na maporomoko ya udongo yaliyotokea wilayani Hanang, mkoani Manyara, Dominika tarehe 3 Desemba 2023. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetuma salam za rambirambi kwa waathirika.

Na Padre Cyril Tluwaycy, Mbulu na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Idadi ya watanzania waliofariki kwenye mafuriko pamoja na maporomoko ya udongo hadi kufikia Alhamisi tarehe 7 Desemba 2023 ilikuwa ni watu 69, majeruhi ni watu 116, wagonjwa waliolazwa hospitalini ni 90 na kwamba, kaya 1,150 zimeathirika na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi. Kwa ujumla watu 5,600 wameathirika kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyotokea wilayani Hanang, mkoani Manyara, Dominika tarehe 3 Desemba 2023. Serikali ya Tanzania imesema kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang mkoani Manyara, ambayo ilikuwa ina miamba dhohofu iliyonyonya maji ndio chanzo cha maporomoko yaliyoleta maafa katika eneo hilo la Hanang mkoani Manyara. Sehemu iliyonyonya maji ilizua mgandamizo na sehemu ya Mlima ikashindwa kuhimili mgandamizo huo na hivyo kusababisha kumeguka kwa sehemu hiyo na kutengeneza tope ambalo ndilo lilianza kuporomoka kufuata mkondo wa mto Jorodom uliozoa mawe na miti na kushambulia makazi ya binadamu yaliyokuwa pembezoni mwa mto huo. Hayo yamebainishwa na Msemaji mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.

Watu waliofariki duniani maafa ya Hanang wamefikia 69
Watu waliofariki duniani maafa ya Hanang wamefikia 69

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC ametuma salam za rambirambi kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania pamoja na familia ya Mungu nchini Tanzania kufuatia mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara. Haya ni maafa makubwa na yakutisha na kwamba, Kanisa linapenda kuonesha uwepo wake na mshikamano na wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya makubwa na kwamba, maafa haya yanamguso wa kimazingira na hivyo isingekuwa rahisi kuepukika hapo kwa papo. Maafa haya yamesababisha vifo vingi, upotevu na uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu pamoja na usumbufu mkubwa kwa watu. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaishukuru Serikali kwa hatua za dharura zilizochukuliwa; vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watu wote waliojituma sana katika kushughulikia uokoaji wa haraka na wa dharura wa watu walioathirika pamoja na wote waliotoa huduma mbalimbali katika maafa haya. Baraza linatoa pole na kuwatia moyo wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya kamwe wasikate tamaa pamoja na kuwasihi watanzania kuendelea kuonesha moyo wa ukarimu kwa waathirika wa maafa haya. Iwe ni fursa ya kuendelea kumwamini Mungu anayewapenda na kuwawazia mema.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania latuma salam za rambirambi
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania latuma salam za rambirambi

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anawaalika watanzania kumwomba Mungu daima ili awalinde na kuwaepusha na hatari. Awaangazie akili zao ili waweze kutambua kwa wakati hatari zinazowakabili, awakirimie ujasiri wa kuchukua hatua za tahadhari zinazostahili dhidi ya maafa na majanga yote yanayoweza kuwakabili. Watanzania walipokee janga hili kwa moyo wa ujasiri, waendelee kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kitaifa kadiri inavyowezekana. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linawaombea majeruhi uponyaji kamili na wa haraka. Linawaombea marehemu waliofikwa na umauti kutokana na maafa haya ili wapate pumziko la amani kwa Mwenyezi Mungu. Maaskofu wanaoiombea Tanzania usalama wa kimazingira na kijamii. Watanzania waendelee kushikamana na hatimaye, Mungu apende kuibariki Tanzania.

Maporomoko ya udongo Hanang mkoani Manyara yamesababisha maafa
Maporomoko ya udongo Hanang mkoani Manyara yamesababisha maafa

Wakati huo huo, Askofu Anton Gasper Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu amesema kwamba, Kanisa linaungana na litaendelea kushikamana na wananchi waliokumbwa na maafa ya mafuriko pamoja na maporomoko ya udongo kufuatia mvua kubwa zilizonyeesha usiku wa kuamkia tarehe 3 Desemba 2023. Jimbo Katoliki la Mbulu litaendelea kutoa ushirikiano hasa katika huduma za kibinadamu katika kuwasaidia wahanga wa mafuko haya. Askofu ameendelea kuhimiza sala na dua kwa wale waliotangulia mbele za haki, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele. Askofu Anton Gasper Lagwen amemwomba Mwenyezi Mungu apende kubariki juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali katika mchakato wa kuokoa maisha ya watu waliokumbwa na maafa haya. Anamwomba Mungu aweze kuwapatia nguvu watanzania ili waweze kuupokea msiba huu kwa imani na matumaini. Nalo Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Tanzania, Caritas Tanzania, linawaalika watanzania kutangaza na kushuhudia Injili ya Msamaria mwema bila kujali dini, kabila, rangi au itikadi ya mtu. Rej. Lk 10: 25-37. Idara ya Caritas Tanzania ambacho ni chombo cha huduma cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tangu zamani kimekuwa mstari wa mbele katika hutoaji wa huduma kwa watu wenye shida na majanga mbalimbali katika maisha.

Maaskofu Hanang
07 December 2023, 14:44