Askofu Berardi amebariki masalia ya Areta na kuwekwa Kanisa Kuu la Mama Yetu wa Arabia
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Askofu Aldo Berardi, O.SS.T, Msimamizi wa Kitume wa Uarabuni Kaskazini, alihubiri kwa waamini zaidi ya elfu moja waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa Dominika tarehe 10 Desemba 2023, wakati wa kutabaruku Kanisa Kuu la Awali huko Bahrein ambalo linaitwa Mama Yetu wa Uarabuni, na Kadinali Luis Antonio Tagle, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji. Katika Mahubiri ya Askofu Berardi alisema “Kanisa Kuu sio Parokia. Ni mahali pa Kiroho, pa kukaribishwa, mahali ambapo tunaweza kupata mtu aliye tayari kutusikiliza. Sisi ni hekalu la kweli kwa sababu, ibada ya kuabudu ya ukweli inafanyika moyoni. Unapokuja kwenye Kanisa Kuu,” aliongeza Askofu Berardi wakati wa mahubiri, “lazima ujisikie uko nyumbani. Hapa unaweza kuomba na kutafakari. Watu huja kanisani ili kujipata wenyewe, na kujisikia amani.”
Katika Misa hiyo kuu iliadhimishwa na maaskofu na mapadre kumi na wawili wa Vikariati ya Kitume. Liturujia ilianza na maandamano ya kundi la waamini waliokabidhi baadhi ya masalia matakatifu kwa Askofu Berardi, ambapo likiwemo lile la Mtakatifu Areta, aliyeuawa kishahidi katika Ghuba ya Uarabuni pamoja na wenzake katika mauaji ya mwaka 523 BK. Askofu Berardi pia alipewa masalia ya Mtakatifu Yohane De Matha, mwanzilishi wa Shirika la Mapadre wa Utatu (huko Kaskazini mwa Arabia) na Mtakatifu Josephine Bakhita, aliyeachiliwa kutoka utumwani na kisha kubatizwa. Masalia hayo yalibarikiwa na Askofu na kuwekwa ndani ya madhabahu na Msimamizi wa Kanisa Kuu, Padre Saji Thomas(Ofm Cap). Wakati wa Liturujia ya Ekaristi takatifu Msimamizi wa Kitume, akifuatana na mapadre na wahudumu walei, waliweka wakfu misalaba iliyobandikwa kwenye kuta ndani ya Kanisa Kuu. Kwa maelezo Askofu alioneza kusema kuwa: “Mahali panakuwa patakatifu kwa sababu pamewekwa wakfu, lakini sisi tumewekwa wakfu kama Wakristo.” Liturujia ya Ekaristi ilisindikizwa na kwaya ya Kanisa Kuu na kundi kubwa la watumishi wa altareni ambap waliotoa huduma yao kwa umakini na uangalifu mkubwa.
Kuhusiana na Jubilee ya miaka 1500 tangu kuuawa kwa Aretas na wafia dini wenzake imani inaaendelea kuadhimishwa ambapo kumbukumbu yao ya kiliturujia iliadhimishwa kunako tarehe 24 Oktoba 2023. Matukio hayo kiukweli yaliashiria mapito ya Jumuiya ya Kikristo ya Kikatoliki ya Vikariati ya Kitume ya Kaskazini mwa Arabia hasa mnamo tarehe hiyo ambapo Parokia zote za Kanisa Katoliki la Vikariate ya Kitume ya Kaskazini mwa Arabia iliadhimisha misa takatifu kwa ajili ya sikukuu ya kiliturujia ya kuuawa kwa Mtakatifu Areta. Askofu Aldo Berardi, wa Shirika la Maoadre wa Utatu Mtakatifu na wa Watumwa (O.SS.T.), alishirikisha furaha hiyo kwa Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari Fides kuwa maandalizi yalikuwa ni tukio hilo muhimu linaloadhimisha kumbukumbu ya miaka 1500 ya kifo cha kishahidi cha Mtakatifu Areta (523), pamoja na takriban Wakristo elfu 4 Waarabu kutoka mji wa kale wa Najran, kusini mwa Arabia, ambapo sasa Saudi Arabia. "Kwenye makanisa ya Vicariate ambayo ni pamoja na Bahrain, Kuwait, Qatar na Saudi Arabia, hakuna alama za kidini au alama, ni marufuku isipokuwa Bahrain - alielezea Askofu Berardi, Msimamizi wa Kitume wa Kaskazini mwa Arabia. Niliweka msalaba mkubwa kwenye Kanisa Kuu jipya kuonesha kwamba ni kanisa. Kanisa kuu liko nje ya jiji na, ili kuruhusu waamini kulifikia, njia maalum ya basi imeanzishwa kamili na ishara ni Kanisa kuu” alisisitiza Askofu Berardi.
Katika Vicariate ya Kaskazini kuna nchi nne zenye ukweli mbili tofauti. Katika nchi zilizoidhinishwa, kama vile Kuwait, Bahrain na Qatar, kuna makanisa na mapadre, lakini kuna ukosefu wa nafasi na walipenda kujenga zaidi. Bahrain ndiyo iliyo wazi zaidi kati ya nne, wakati nyingine tatu bado ni chache sana. Askofu Berardi pia alitaja juu ya elimu kuwa huko Bahrain kuna shule ya Moyo Mtakatifu, iliyopo kwa zaidi ya miaka 70, inayosimamiwa na watawa wa Kitume wa Karmeli wa India wenye watoto elfu mbili. Na sasa shule ina kampasi kubwa.
Kuhusu tukio jingine lililohusisha Jumuiya ya Kikatoliki ya Vikariati ya Kitume, Askofu alitaja ufunguzi wa Mlango Mtakatifu wa Kanisa kuu la Familia Takatifu nchini Kuwait. Mnamo tarehe 29 Septemba 2023 iliyopita waliadhimisha ufunguzi wa Mlango Mtakatifu katika Kanisa kuu la Kuwait ambapo waamini wote wa jumuiya za parokia walishiriki sala na kuimba nyimbo maalum" alisema Askofu Berardi kuhusiana na maadhimisho hayo ambayo yeye mwenyewe aliongoza pamoja na makuhani wengine wa Vikarieti. Kwa mujibu wake alieleza kuwa “Kuwait inaonekana kuendelea kurudi nyuma, hakuna utulivu wa kisiasa, uhuru unazidi kuwa mdogo. Sisi pia tunapitia mambo mengi kwa sababu yametuwekea masharti mapya. Yote ni ngumu, sheria zinabadilika kila wakati, hata watu wenye msimamo mkali wameingia.
Askofu alisema "Tunazo parokia nne: kanisa kuu la zamani la Familia Takatifu, kanisa dogo la asili ya Madhabahu ya Mama Yetu wa Arabia ambapo sanamu kubwa iliyoletwa na Wakarmeli imehifadhiwa ambayo mwaka huu itaadhimisha miaka 75 ya uwepo wake. Kwa miaka mingi tuliomba ardhi ya kujenga Kanisa katika eneo hilo lakini mwishowe mikataba na serikali ilishindikana. Ingehitaji makanisa mengi zaidi kuweza kukaribisha kila mtu!” Askofu Berardi anaongeza kusema kuwa nchini Kuwait kuna shule tatu: moja inaendeshwa na watawa wa Wakarmeli, moja na Wasalesia na nyingine na watawa wa Lebanon wa Rozari. “Haziitwi shule za Kikatoliki, dini ya Kikristo haiwezi kufundishwa hapa. Ni shule za kibinafsi mchanganyiko zilizofunguliwa kwa wote, Waislamu na Wakristo. Hata hivyo, inajulikana kwamba hizo ni shule za Kikristo kwa kuwa watawa wana mazoea ya kidini."