Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka A wa Kanisa: Karama na mapaji ni kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 33 ya Mwaka A wa Kanisa: Karama na mapaji ni kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.  

Tafakari Dominika 33 ya Mwaka A wa Kanisa: Stawisha Karama na Mapaji Yako

Kauli mbiu “Wala usiugeuzie uso wako mbali na mtu maskini” Tob 4:7 ni msaada mkubwa wa kufahamu kiini cha ushuhuda wa upendo unaotolewa na wakristo mintarafu tunu msingi za maisha ya kifamilia zinazofumbatwa katika hofu na wema wa Mungu; Amri za Mungu; Maisha ya sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huu ni ushuhuda makini kutoka kwa Tobit, Mtu wa Mungu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Utangulizi: Mpendwa Msikilizaji wa Radio Vatican, Mama Kanisa anawajibika kimaadili kuwasaidia na kuwahudumia maskini: kiroho na kimwili na ndiyo maana baada ya kufunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, ameanzisha Siku ya Maskini Duniani, ili Jumuiya za Kikristo sehemu mbali mbali za dunia, ziweze kuwa alama wazi ya upendo wa Kristo Yesu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Siku hii ni muhimu sana ili kuonesha na kushuhudia upendeleo wa Kristo Yesu kwa maskini, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasikiliza, kuwahudumia na kuwaonesha maskini upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii kwa kutambua kwamba, hata wao wameumbwa na wanapendwa na Baba wa mbinguni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ikiwa kama watu wa Mungu wanataka kushinda utamaduni wa kifo na kukombolewa kutoka katika udhalimu, wanapaswa kufuata ufukara wa Kristo Yesu, kwa kushiriki na kuambata maisha yanayosimikwa katika upendo, kwa kushirikiana na wengine katika kuumega mkate na kuishi kwa umoja kama ndugu wamoja, kwa kuanzia kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mchakato wa kuwaweka huru maskini wanateswa na baa la umaskini na matajiri wanaokosa furaha na utulivu wa ndani kwa sababu ya ubatili, ili wote kwa pamoja waweze kuwa na matumaini mapya. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia hasa kuhusu umuhimu wa Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini, umuhimu wa ushuhuda wa huruma na mapendo kwa maskini; matendo ya huruma kiroho na kimwili, kielelezo cha huduma kwa Mungu na jirani, mfano wa Injili ya Msamaria mwema; Shukrani kwa Mashuhuda wa huruma na mapendo; Mahitaji msingi ya binadamu pamoja na mifumo mipya ya umaskini duniani hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; huduma kwa maskini ni kiini cha Injili.

Kiwango cha umaskini duniani kinaongezeka kwa kasi ya ajabu.
Kiwango cha umaskini duniani kinaongezeka kwa kasi ya ajabu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani ni wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, waamini wanapokusanyika kuzunguka Meza ya Bwana ili kujipatia zawadi na kujichotea nguvu ya kuweza kuishi kimaskini pamoja na kuwahudumia maskini. Kauli mbiu “Wala usiugeuzie uso wako mbali na mtu maskini” Tob 4:7 ni msaada mkubwa wa kufahamu kiini cha ushuhuda wa upendo unaotolewa na wakristo mintarafu tunu msingi za maisha ya kifamilia zinazofumbatwa katika hofu na wema wa Mungu, tayari kushika na kuishi kwa ukamilifu Amri za Mungu; kwa kujikita katika maisha ya sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Huu ni ushuhuda makini kutoka kwa Tobit, Mtu wa Mungu aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, mwaliko kwa waamini baada ya kushiriki kikamilifu Meza ya Bwana, yaani Fumbo la Ekaristi Takatifu, wawe na ujasiri wa kuwaalika maskini kwa chakula kielelezo makini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, leo ni Dominika ya 33 ya mwaka A. Tunakaribia mwishoni mwa kipindi cha mwaka A. wa Kanisa. Wazo kuu tunalolipata katika Injili ya leo ni kwamba Mwenyezi Mungu ametujalia karama mbalimbali. Je, tunazitambua hizo karama? Je, tunazitumia namna gani? Je, karama hizo zinawasaidia wenzetu tunaoishi nao? Je, zinatusaidiaje katika kumjua Mungu? Inawezekana sizitambui karama nilizojaliwa, Je nimechukua hatua mbalimbali za kuweza kuzitambua karama hizo? Inawezekana sijajaliwa karama nyingi, Je, hiyo ndiyo tiketi ya kutotumia kabisa hata kile nilicho jaliwa? Tutafakari pamoja ili mwishoni uweze kutoa majibu ya maswali hayo.

Maskini wapewe huduma muhimu za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii
Maskini wapewe huduma muhimu za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii

UFAFANUZI. Licha ya Somo la kwanza kuwataja akina mama, haliwaondoi wanaume katika wajibu zao na matumizi bora ya talanta zao. Akina baba “tusifike” kwa wema, utulivu, upole na misimamo imara mintarafu ujenzi na usimamizi wa familia na jamii. Tuombe hekima na maarifa, tumche na tumuogope Mungu, tufanane na Mt. Yosefu katika haki, tukiepa ulevi, nyumba ndogo na marafiki wabaya, tutoe malezi bora kwa wanetu na kuepa mali za udhalimu “kuzilinda mali kwadhoofisha mwili, na kuzisumbukia kwaondoa usingizi” (YbS 31:1, 6). Laiti akina baba tungeota ndoto za maendeleo na kuzitimiza, tungetumia madaraka na mamlaka yetu vema, halafu dunia yetu ingebaki sayari inayong’aa, familia na jumuiya zingekuwa paradiso. Kadiri tulivyoisikia Injili hivi punde, tunaelezwa mfano wa talanta ambayo imegawiwa na Bwana mmoja kwa watumwa wake watatu, kila mmoja amepata kwa kiwango tofauti na mwingine. Mmoja amepata talanta tano, wa pili talanta mbili na wa tatu amepewa talanta mbili. Kila mmoja amepewa kulingana na uwezo wake! Swali la kujiuliza mpendwa msikilizajia Kwa nini maisha yapo hivi? mimi sijui, pasi na shaka sote tupo sawa mbele za Mungu, wote tuna haki sawa mbele ya katiba, akina baba wote ni akina baba tu, hakuna mwenye ubaba wa peke yake, akina mama ni akina mama tu, hakuna mwenye umama wa pekee, wote tuna sura na mfano wa Mungu mwenyewe. Lakini linapokuja suala la uwezo tunatofautiana sana. Mungu hakutujalia kufanana, wapo wenye nguvu za kuhimili talanta 5, wengine 2 na wengine 1 tu. Wapo wenye uwezo wa akili, wana nguvu za kufikiri, kueleza mawazo yao kwa ushawishi na kutenda, wengine hawawezi, hawakujaliwa. Wapo wenye talanta za pekee, vipaji, vipawa, karama, maumbo na sura za kuvutia, sauti tamu za kumleta nyoka toka mafichoni na haiba ya kutosha, wengine hawakujaliwa hayo. Ni siri ya Mungu ili uwezo na utukufu wake vidhihirike, cha muhimu hakuna aliyeachwa bila kitu. Pengine hukupewa 5 lakini umepewa 2, pengine hukupewa 2 ila umepewa 1, kila mtu ana kitu, japo ni kidogo. Tena nionavyo, dunia imejaa watu wa kati, wenye talanta 2 na 1 kuliko 5.

Waamini wanaalikwa kukuza na kudumisha karama zao
Waamini wanaalikwa kukuza na kudumisha karama zao

Tajiri/mwajili ni Kristo, kabla ya kusafiri (kupaa mbinguni) alituachia yote mazuri, matumizi ya vitu hivyo ndio kipindi hiki chote tangu ufufuko wake hadi atakapokuja tena. Watumishi ni wanakanisa, na talanta hizo ni Neno la Mungu, sakramenti, uwezo wa kuponya, kutawala nguvu za giza, elimu, uongozi, uvumbuzi, ibada, kufariji, kupenda na kuongoa. Talanta hizi zinaendana na huduma kila mmoja kwa nafasi yake. kuzitekeleza kwadai sadaka na majitoleo ndio maana Mt. Paulo anatuambia tukeshe, tusilale usingizi. Jamii inakua na mahitaji yanaongezeka, tunahitaji maendeleo na hali nzuri, amani na utulivu, yote yanategemea udumifu wetu... “Sisi si watu wa giza, basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe na kuwa na kiasi.” Huduma ya walimu ni muhimu kama ile ya wauguzi, katekista anapofundisha wakatekumeni wengine wawe na vijana na watoto, wengine wanapowaandaa wanandoa wengine watembelee wagonjwa na masikini, wengine wanapotunga sheria wengine wazisimamie kwa haki na uadilifu...ndio matumizi mema ya talanta zetu. Kristo ametuchagua na kutupa kazi (Yn 15:16). Tuwe faida na baraka tuweze kujibu “Bwana, uliweka kwangu talanta 5, tazama talanta nyingine 5 nilizopata faida.” Kinyume chake ni fedheha na kujitetea kusikopendeza, “ah Bwana unajua, nilitambua wewe u mtu mgumu…” hawa ni wale wanaoficha vipaji vyao, wanaogopa lawama, sio wakweli, hawatumiki ipasavyo, uwepo wao kati yetu hauna faida sababu hawajitokezi, hawatusaidii. “Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.” Mkesha huo ni matumizi mazuri ya talanta/karama tulizojaliwa. Maendeleo ya sayansi, teknolojia, uchumi, siasa na jamii ni mapato ya kutumia vyema talanta tulizojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Karama ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi
Karama ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi

Tunapoendelea kumsubiri Kristo, kila mmoja atumie karama au vipawa alivyojaliwa kwa nguvu zote na awe sehemu ya mabadiliko KIROHO, KIMWILI, na KIJAMII. Vipawa/talanta zetu zitusaidie kumtumikia Mungu na jirani na katika kupambana na umaskini, njaa, ujinga na maradhi. Mama zetu “ninyi si watu wa usiku, wala wa giza basi msilale usingizi, bali mkeshe na kuwa na kiasi.” Somo la Kwanza (Mith 31:10-31) laeleza matumizi mazuri ya talanta mlizojaliwa, labda 5, 2 au 1, kwa kuwa wake wema. “Mke mwema ni nani atakayemwona?” Kaeni vizuri ili Bwna ajapo mseme “Bwana uliweka kwangu talanta 5, tazama nyingine 5 nilizopata faida.” Somo hili linawapa sifa 4…akina mama wote. Mosi, mama ni mke mwema (31:10), furaha ya mumewe. Mtunzaji wa amani, kielelezo cha usafi, weupe wa moyo, na utulivu. Mshabiki wa mapatano, mwenye maono na mtazamo mwema, anajua kumchukulia mumewe, tena ni mvumilivu. Sifa ya pili sio mvivu, hodari wa kazi “huamka kabla haujaisha usiku, kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu, hutia mikono yake katika kusokota...” (31:15-19) hasubiri kuhudumiwa, mchango wake ni dhahiri kwa familia yake na jamii. Sifa ya tatu ya mama ni moyo wa ukarimu “huwakunjulia masikini mikono yake, naam, huwanyooshea wahitaji mikono yake” (31:20) Hafichi mapato ya kazi za mikono yake kwa ajili yake na familia yake tu bali ni mwema kwa watu wote. Halafu sifa ya nne ni “mcha Mungu na kwa sababu hiyo atasifiwa sana” (31:30) Mama unayesoma na kusikiliza tafakari hii, una sifa ngapi kati ya hizi? Tusifukie talanta zetu aridhini bali tuzifanyie kazi kwa utendaji mtukufu. Tusali ili Mungu atujalie neema ya kutumia vizuri talanta zetu ili ifikapo jioni ya maisha yetu kila mmoja wetu asikie maneno haya mazuri kutoka kwa Bwana “vema mtumwa mwema na mwaminifu, ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi, ingia katika furaha ya Bwana wako” (Mt 25:21, 23.)

Liturujia D33
18 November 2023, 09:54