Tafuta

Tafakari ya Dominika ya 23 ya Mwaka A wa Kanisa: Sifa kuu za mwanamke mwadilifu. Tafakari ya Dominika ya 23 ya Mwaka A wa Kanisa: Sifa kuu za mwanamke mwadilifu.  (ANSA)

Tafakari Dominika 33 ya Mwaka A wa Kanisa: Sifa Kuu za Mwanamke Mwadilifu

Wasifu wa mke mwema na mwadilifu ana sifa zifuatazo: (1) anaaminiwa na mumewe (2) Hutenda mema kwa mumewe (3) Ni mchapakazi, hujishughulisha kwa bidii bila kujali muda (4) Huwasaidia maskini na wahitaji. Hafanyi mambo kwa kujifaidisha mwenyewe bali hutazama pia mahitaji ya watu wengine (5) Mcha- Mungu. Kila mwanamke ambaye ni mke wa mtu (na hata mwanaume ambaye ni mume wa mtu) ajipime kama ana sifa hizo, tayari kuzimwilisha katika utume.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Jimbo Kuu la Mwanza

Visingizio vinavyotawaliwa na ubinafsi na kujitazama wenyewe kuliko kutazama mafaa ya wengi husababisha “kufukia” fadhila za kimungu na kiutu. Tunu, karama na vipaji mbalimbali tulivyonavyo vinapaswa kuleta faida katika hija yetu hapa duniani, ili Mungu atukuzwe na mwanadamu atakatifuzwe. Tunapaswa kuwa tayari kutoka hesabu ya talanta tulizopewa na Mungu. Somo letu la kwanza (Mit. 31:10-13, 19-20, 30-31) linatueleza “wasifu wa mke mwema.” Kwa kadiri ya somo letu la leo mke mwema ana sifa zifuatazo: (1) anaaminiwa na mumewe (2) Hutenda mema kwa mumewe (3) Ni mchapakazi, hujishughulisha kwa bidii bila kujali muda (4) Huwasaidia maskini na wahitaji. Hafanyi mambo kwa kujifaidisha mwenyewe bali hutazama pia mahitaji ya watu wengine (5) Mcha- Mungu. Kila mwanamke ambaye ni mke wa mtu (na hata mwanaume ambaye ni mume wa mtu) ajipime kama ana sifa hizo. Somo letu la leo halisemi kuwa mke mwema hapatikani kabisa bali ni kazi ngumu sana kumpata maana ana sifa za pekee. Na tukumbuke kuwa “siyo kila mwanamke ni mke” na “siyo kila mke ni mke mwema.” Ingawa katika uhalisia somo linamhusu “mke” kwa maana ya mwanamke aliyeolewa, tusisahau kuwa sisi sote kwa ubatizo wetu tumeingia katika mahusiano na Mungu, na hivyo tunapaswa kuwa na sifa za mke mwema: (i) kumcha Bwana na kujitahidi kwa kila hali kumpendeza mume wetu, yaani kumpendeza Mungu (ii) kuwatendea mema wahitaji na maskini (iii) taa zetu “matendo yetu mema” zisizimike. Je, sisi wakristo ambao tumeungana na Mungu (kama muungano wa mume na mke) tunazo sifa za mke mwema?

Sifa kuu za mwanamke mwema na mwadilifu
Sifa kuu za mwanamke mwema na mwadilifu

Leo hii wanawake wengi hawaaminiwi katika ndoa zao kutokana na maneno mengi ya ulaghai kwa waume zao na kutokana na matendo yao yasiyozingatia wito wao wa ndoa. Leo hii wapo wanawake wanaowanyanyasa waume zao, hasa wakifukuzwa kazi au kufilisika. Wanawake wengine wanadiriki hata kuua waume zao ili kurithi mali. Lakini wapo pia wanawake ambao mpaka leo hawataki kujishughulisha- hawafanyi kazi zozote bali wameajiri mabinti wa kazi (housegirls) ambao hufanya kazi ambazo kimsingi zilipaswa kufanywa na mke. Mke ambaye hajishughulishi anashindwa hata kulea watoto na kutimiza wajibu kama mama, mke na mlezi na badala yake anakalia kupiga umbea na “mashosti”, starehe na kusubiri kuletewa kila kitu na mumewe. Hata hivyo, wapo wanawake wachapakazi na wenye kujishughulisha bila kujali uthamani au uduni wa kazi wanazofanya. Mwanamke amka, chapa kazi ili mjenge pamoja familia na taifa. Mwisho, mke ni lazima awe mcha-Mungu: mcha-Mungu anaogopa kuvunja maagano na ahadi za ndoa, hutimiza wajibu wake kwa Mungu, kwa mume na kwa watoto na  humtegemea Mungu nyakati za raha na shida. Mke mwema ni sifa kwa mumewe. Sifa hizi za mke mwema zapaswa kuwa sifa za mume mwema.

Kesheni katika maadili na utu wema
Kesheni katika maadili na utu wema

Katika somo la pili (1 Thes. 5:1-6) Paulo anawakumbusha Wakristo wa Thesalonike na sisi sote kuwa jambo la muhimu katika ufuasi wetu ni “kuwa tayari kwa siku ya hukumu, siku ya Bwana” na wala siyo kufahamu ni lini siku hiyo itafika. Hatupaswi kuridhika kupita kiasi kwa kuona kuwa tuna amani na usalama. Kipindi ambacho tunabweteka kwa kudhani tuna amani na usalama ndipo watu hujisahau na kufanya anasa na machukizo mengi. Tuwe macho nyakati hizi. Paulo anahimiza juu ya “kukesha.” Kwa Paulo “kukesha” siyo kuacha mume/mke na watoto majumbani na kwenda makanisani au viwanjani kuimba nyimbo za mapambio na kutoa vilio vya kelele za maombi kana kwamba Mungu ni kiziwi. Tukikesha namna hii tutavunja hata ndoa zetu na kushindwa kuhudumia familia zetu. Paulo anaposema “tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe” anamaanisha “kukesha katika imani na maadili” (spiritual and moral vigilance) ambao msingi wake ni kumcha Mungu kama afanyavyo mke mwema kwenye somo la kwanza. Tukeshe katika sala, tukeshe katika matendo ya kiibada, tukeshe katika kupendana kutoka moyoni pasipo unafiki, tukeshe katika kutimiza wajibu wetu kwa familia zetu na kwa ndoa zetu, tukeshe katika muunganiko na Kristo tukikumbuka kuwa sisi ni wana wa nuru na wala siyo wana wa giza.

Wanawake wawe ni mifano bora ya kuigwa katika maisha
Wanawake wawe ni mifano bora ya kuigwa katika maisha

Katika Injili yetu ya ya Dominika ya 33 ya Mwaka A wa Kanisa (Mt. 25:14-30) Yesu anatupa mfano wa “watumwa watatu waliopewa talanta na baadaye kutakiwa kutoa hesabu.” Msisitizo wa Injili ya leo ni jukumu la kila mmoja wetu kutoa hesabu ya kile alichopewa na Mungu kama talanta (zawadi). Wakati wa Yesu kulikuwa na aina nyingi za fedha kama vile talanta na dinari. Katika mfano wa leo tunasikia juu ya “talanta walizopewa watumwa watatu.” Kwa thamani talanta ilikuwa ni kubwa kuliko dinari. Talanta moja ilikuwa ni sawa na ujira wa kibarua uliokusanywa kwa miaka 15. Kumbe hata mtumwa ambaye tunadhani alipewa talanta chache kwa uhalisia alipewa kiasi kikubwa sana. Watumwa hawakupewa talanta ili kukaa nazo tu, bali wazizalishe na mwisho watoe hesabu, hasa faida waliyopata. Lakini pia watumwa hawakupewa kiasi sawa cha talanta, kila mmoja alipewa kiasi tofauti na mwenzake. Watumwa wawili wa kwanza walileta talanta walizopewa pamoja na faida walizozalisha. Mtumwa wa tatu alirudisha talanta bila faida na kutoa visingizio. Mtumwa wa tatu alifanya makosa makubwa mawili: (1) Hakuwa na ujasiri wa kuthubutu kuizalisha talanta kwa kuhofia kupata hasara. Kwa maneno mengine mtumwa wa tatu hakuwa “risk-taker” (2) Alikuwa mbinafsi kwa kuwa hakutaka bwana wake apate faida na hivyo kuizika talanta yake: “wavuna usikopanda, wakusanya usipotawanya”. Kauli hii inaashiria kuwa hakutaka bwana wake afaidike. Swali lake kubwa moyoni lilikuwa hili: “Yaani mimi nisumbuke, faida apate mwingine? Siwezi kufanya biashara kichaa mimi.” Haya ni mawazo ya ubinafsi.

Wanawake watumie vyema karama na mapaji yao ustawi wa wengi
Wanawake watumie vyema karama na mapaji yao ustawi wa wengi

Kutoka katika Injili tunajifunza yafuatayo: (1) Tutawajibika kutoa ya hesabu ya vyote tulivyokabidhiwa na Mungu ili kuona kama vimetuletea faida ama la. Injili imetueleza kuwa watumwa “walipewa mali za bwana wao,” mathalani talanta. Hata sisi leo tumepewa mali/talanta nyingi na za thamani sana ambazo baadaye tutapaswa kutoa hesabu yake. Tumepewa talanta nyingi na za thamani sana: maisha, imani, afya, nguvu, fursa, mali, pesa na vipawa mbalimbali kama vile uwezo wa kiakili, uongozi, mvuto kwa watu, nguvu ya ushawishi, umahiri wa kuhubiri, uwezo wa kujenga hoja, karama ya uandishi n.k. Je, tutakuwa kama wale watumwa wawili waliozizalisha au kama yule mmoja aliyeizika ardhini? Kila kitu tulichonacho ni zawadi- ni talanta kutoka kwa Mungu. Vyote tulivyonavyo ni mali za Bwana wetu ambaye ametupa sisi tuzitumie kwa faida. Mungu hatupatii talanta sawa kwa kila mmoja bali hutupatia talanta tofauti tofauti kwa ajili ya kumtumikia Yeye na jirani zetu. Je, tunavitumia kumtumikia Mungu na watu? Tunavitumia kwa mafaa ya yote au tunavikumbatia kwa sababu ya ubinafsi na hofu? Je, tunaviendeleza au kunavificha? Imani tuliyopewa tuizalishe ili itupatie wokovu, tusiizike kwa matendo yetu mabaya; mali na karama nyingine zitumike kuleta faida kiroho na kimwili. (2) Tusipotumia talanta zetu tutapoteza hata kidogo tulichonacho. Nini madhara ya kuvicha/kutotumia talanta? Yesu anatupatia jibu la swali hili: hata kile alichonacho atanyang’anywa. Kwa maneno mengine ni kwamba tusipotumia talanta kuleta faida basi tutazidi kupoteza. Mtumwa aliyepewa talanta moja alibweteka/aliridhika (hakujihusisha na chochote) na ndiyo maana alinyang’anywa hata ile moja aliyokuwa nayo.

Wanawake ni amana na utajiri wa Kanisa
Wanawake ni amana na utajiri wa Kanisa

Nini maana yake? It is simply by doing nothing we lose everything (usipofanya kitu utapoteza kila kitu): ukipewa zawadi ya imani halafu huizalishi/huikuzi basi ujue wazi itapotea kabisa; ukipewa karama halafu huitumii basi hiyo karama itapotea kabisa. Katika ulimwengu wa leo wapo watu ambao wanadhani kuwa watapata hasara au wataonekana wa kawaida tu endapo watatumia talanta zao kwa ajili ya wengine. Kuna watu hawataki kutumia talanta zao za uongozi ndani na nje ya Kanisa mpaka wabembelezwe au kuabudiwa kama miungu. Kuna wanaotumia talanta zao pale tu wanapoona kuwa watapata mafaa binafsi. Kwa kufanya hivyo talanta zao hazitazaa. Tunapaswa kujua kuwa Mungu atatuhoji juu ya namna tulivyotumia talanta ambazo ametupatia. Tukizitumia vizuri tutaongezewa (tutapata baraka tele). (3) Hatupaswi kuwa watu wa visingizio katika uwajibikaji wetu kiimani au kijamii. Mtumwa aliyepewa talanta moja anatoa visingizio vingi: “Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; bali nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi.” Watu wengi huwa tunatoa visingizio vingi tunaposhindwa kutimiza wajibu wetu. Tusitafute visingizio: “yule kapendelewa kuliko mimi”; “mimi nina karama chache tu”; “sina muda” “nina majukumu mengi” “nitazidiwa” “nitapata hasara” “kwa nini niwape mapadre shukrani ya mavuno ilihali niliyesumbuka kulima ni mimi?”. Kwa Mungu hakuna upendeleo, hakuna vichache, hakuna hasara. Mungu humpa kila mtu kwa kadiri ya Hekima yake na kwa malengo anayoyajua Yeye. Dominika njema

18 November 2023, 08:53