Tafuta

Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 32 ya Mwaka A: Kesheni kwa maana hamjui siku ya kufa Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 32 ya Mwaka A: Kesheni kwa maana hamjui siku ya kufa  (ANSA)

Tafakari Dominika 32 ya Mwaka A wa Kanisa: Kesheni Kwani Hamjui Siku Wala Saa!

Tunapoelekea mwisho wa mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa, Mama Kanisa anatuongoza namna na jinsi ya kujiandaa, kujitayarisha na kujiweka tayari kwa maisha yajayo ya uzima wa milele mbinguni. Mwaliko ni huu, kukesha, kuwa tayari wakati wowote kwa ujio wa mjumbe wa Mungu kuja kutuita wakati na mda tusioujua. Basi tuweke matumaini yetu kwa Mungu muweza wa yote na kumwomba kila mara atujalie maandalizi ya kifo chema atuepushe na mabaya yote.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 32 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tunapoelekea mwisho wa mwaka wa Kiliturujia wa Kanisa, Mama Kanisa anatuongoza namna na jinsi ya kujiandaa, kujitayarisha na kujiweka tayari kwa maisha yajayo ya uzima wa milele mbinguni. Mwaliko ni huu, kukesha, kuwa tayari wakati wowote kwa ujio wa mjumbe wa Mungu kuja kutuita wakati na mda tusioujua. Basi tuweke matumaini yetu kwa Mungu muweza wa yote na kumuomba kila mara atujalie maandalizi ya kifo chema atuepushe na mabaya yote kama sala ya mwanzo inavyotuongoza kusali ikisema; “Ee Mungu Mwenyezi Rahimu, utuepushe kwa wema wako na yote yawezayo kutudhuru, tuwe tayari rohoni na mwilini kutimiza mapenzi yako pasipo kizuio”. Nasi tukisali kwa matumaini Yeye daima atasikiliza sala zetu kama mzaburi anavyotufariji katika wimbo wa mwanzo akisema; “Maombi yangu yafike mbele zako, uutegee ukulele wangu sikio lako, ee Bwana” (Zab. 88:2). Somo la kwanza ni la kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek. 6:12-16). Katika somo Sulemani anatueleza kuwa Hekima ya Mungu ina thamani kuliko utajiri na nguvu za mwili, kwani ina uwezo wa kujua siri za nguvu za asili na kufumbua mafumbo ya Mungu kwa ufunuo wake Mungu wenyewe kwa wale wanaofungua mioyo yao na kumruhusu Roho wa Mungu kufanya kazi ndani yao. Hekima hii humpa mtu uvumilivu, umakini na uaminifu kwa maneno na matendo yake, unyenyekevu na kiasi. Hekima hii ya Mungu ndiye Kristo Bwana na mwokozi wa maisha yetu ambaye hung’aa wala hafifii, huonekana upesi kwao wampendao, hupatikana kwao wamtafutao. Hekima hii ya Mungu kila mtu anaweza kuipata kwa njia mbalimbali, lakini zaidi kwa kulipokea na kusadiki Neno lake, ndiye Yesu Kristo.

Kesheni kwani hamjui siku wala saa!
Kesheni kwani hamjui siku wala saa!

Tumtafute basi huyu Hekima hasa katika neno la Mungu, katika sala na Sakramenti za Kanisa ili maisha yetu ya sasa na yajayo yawezekuwa ya furaha na amani tele kama wimbo wa katikati unavyotuhimiza ukisema; “Ee Mungu, Mungu wangu nitakutafuta mapema, nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu wakuonea shauku, katika nchi kame na uchovu isiyo na maji. Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, nizione nguvu zako na utukufu wako. Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai, midomo yangu itakusifu. Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai, kwa jina lako nitainua mikono yangu. Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono, kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha. Ninapokukumbuka kitandani mwangu, nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku. Maana Wewe umekuwa msaada wangu, na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia” (Zab. 63 :1-7). Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike, (1The. 4:13-18). Katika somo hili mtume Paulo anawafariji wakristo Wathesalonike na sisi tusifadhaike juu ya kifo na ufufuko wa wafu maana watu wote, wazima kwa wafu – wanaomwamini Kristo watafufuliwa na kushiriki utukufu wa mbinguni. Hivyo tusibweteke na maisha ya dunia hii bali tukeshe kwani ujio wa Yesu ni muda wowote. Ilitokea kuwa waamini wa kwanza waliamini kwamba Yesu atarudi mapema sana kwa mara ya pili kuwachukua wafuasi wake na kuwapeleka mbinguni. Kwa Wathesalonike hali hii ilisababisha baadhi yao waache kufanya kazi kwa kuona akiba ya chakula walichokuwa nacho kinatosha mpaka Yesu atakapokuja. Muda ukapita na watu wakaanza kukata tamaa, uvumilivu ukawashinda na baadhi yao wakaacha imani yao ya kikristo. Ndipo sasa Paulo anawatia moyo wasikate tamaa waendelee kuchapa kazi huku wakiwa tayari kwa ujio wa Kristo. Ujumbe huu ni wetu sote hata nyakati zetu kuwa tuishi na kufanya kazi kwa bidii kana kwamba tutaishi milele yote hapa duniani huku tukiwa tayari kwa ujio wa ndugu yetu kifo wakati wowote atakapokuja kutuita kila mmoja kwa jina lake na kwa wakati wake kwenda kwa Baba mbinguni kushiriki uzima wa milele pamoja na Kristo na watakatifu wote.

Kesheni katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo ya huruma
Kesheni katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo ya huruma

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 25:1-13). Sehemu hii ya Injili ni simulizi la wanawali kumi walioalikwa harusini, watano wakiwa wapumbavu na watano wenye busara. Mfano huu unatukumbusha wajibu wetu wa kukesha, yaani kudumu katika hali ya neema kama wanawali watano wenye busara na tusibweteke na uzuri wa maisha ya hapa duniani tukajisahau na kuzama katika dhambi tukapewa wasifu wanawali watano wapumbavu. Tukumbuke kuwa hatujui siku wala saa ya kifo chetu. Ili kuulewa vizuri mfano huu, yatubidi tuelewe vitu viwili: mila na desturi za kuoa za Wayahudi kipindi hicho na uhusiano kati ya Mungu na taifa la Israeli ulivyokuwa ukielezwa kama uhusiano wa mume na mke na kazi ya kumkomboa mwanadamu inalinganishwa na kumposa na kumuoa upya mke aliyeasi na kumuacha mume wake kwa uzinzi. Lugha hii anaitumia Mungu anapomwambia Nabii Hosea; “Nenda ukampende tena mwanamke anayependwa na mume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama mimi Mwenyezi ninavyompenda Israeli, ingawa yeye anaigeukia miungu mingine…” (Ho.3:1). Ni lugha ngumu na ni ukweli mgumu kuupokea. Lakini lengo lake hasa ni kuonyesha ukuu wa upendo wa Mungu kwa mwandamu mdhambi anayefananishwa na mwanamke mzinzi kwa kuabudu miungu mingine. Kwa upande mwingine ni kujua mila na desturi za sherehe za arusi nyakati hizo. Sherehe hizi zilianza jioni kwa maandamano kutoka nyumbani kwa wazazi wa bibi arusi na kuishia nyumbani kwa bwana arusi. Kimila bibi arusi aliaalika wanawali, rafiki zake waje kumsindikiza kwenye maandamano wakiwa na taa kuelekea nyumbani kwa mume wake. Kumbe walipaswa kuwa na mafuta kutosha. Injili inasema kuwa bwana arusi alikawia kufika kumchukua bibi-arusi. Alipofika wanawali watano wenye busara walijaza taa zao mafuta ya akiba waliyochukua na watano waliopewa sifa ya upumbavu taa zao zikaanza kuzima kwa kutindikiwa mafuta na hivyo kulazimika kuwaomba wenye busara nao wakawashauri washike njia wakanunue kwa wauzao. Waliporudi walikuta maandamano yamekwishafika kwa Bwana arusi, watu wameingia ndani na milango imefungwa, nao wasiweze kuingia.

Kesheni katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo ya huruma
Kesheni katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti na Matendo ya huruma

Katika sehemu ya kwanza tunaona jinsi upendo wa Mungu ulivyo kwa binadamu mdhambi kuwa daima anatutafuta na kumuita arudi kwake. Naye mdhambi akitubu na kuyaghairi maovu yake Mungu yuko tayari kumsameheme na kumpokea tena. Ndiyo maana alimtoa na kumtuma kwetu mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo kama mshenga kuja kuanza utaratibu mpya wa kurudisha uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu, kutuletea furaha kama furaha za arusi, ishara ya neema na baraka katika maisha ya mwanadamu yaliyopoteza ladha kwa sababu ya dhambi. Na katika sehemu ya pili tunajifunza kuwa sisi tulipobatizwa tulipewa taa inayowaka – neema ya utakaso, ndiyo mafuta ya taa yetu. Dhambi inayafyonza mafuta haya na hivyo tunatindikiwa, tupoteze neema hii ya utakaso. Hivyo tunapaswa kwenda mara kwa wauzao katika sakramenti ya kitubio mara moja tusisubiri mpaka atakapokuja Bwana Arusi. Tusiwe wapumbavu. Kuna hatari nyingi katika maisha zinazosababisha kifo cha ghafla iwe ni kwa ajali au magonjwa ya mlipuko yasiyo na tiba. Kumbe, sasa ndio wakati wa kulia: “Bwana, Bwana tufungulie!” Kilio chetu ni kuishi kwa upendo huku tukimwombe Mungu atujalie Hekima ya kujua mambo ya nyakati za mwisho. Huko ndiko kujua maana ya fumbo la mateso, kifo, na ufufuko wa wazima na wafu kama sala ya kuombea dhabihu inavyosema: “Ee Bwana tunaomba upende kuzitazama dhabihu hizi, ili tujipatie kwa hamu neema za fumbo hili la mateso ya Mwanao tunaloadhimisha”. Hivyo tutakuwa na uwezo wa kumtambua Kristo katika Sakramenti zake hasa Kitubio na Ekaristi kama antifona ya komunyo inavyoimba; “Wafuasi walimtambua Bwana Yesu katika kuumega mkate” (Lk. 24:35). Na hivyo sala baada ya komunyo inayoomba ikisema; “Ee Bwana, sisi tulioburudishwa kwa neema takatifu tunakushukuru na kukuomba sana rehema yako. Nayo neema ya uchaji idumu ndani yetu sisi, tuliopata nguvu ya mbinguni kwa Roho wako”, itafanya kazi ndani mwetu mpaka siku ya uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D32
08 November 2023, 10:48