Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 31 ya Mwaka A wa Kanisa: Uaminifu na uadilifu ni ushuhuda muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 31 ya Mwaka A wa Kanisa: Uaminifu na uadilifu ni ushuhuda muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika 31 ya Mwaka A wa Kanisa: Uaminifu na Uadilifu Ni Ushuhuda wa Uinjilishaji

Basi katika Dominika hii ninawaalikeni tutafakari wazo hili, Uaminifu ni ushuhuda wazi wa uinjlishaji kila wakati. Sisi sote kwa ubatizo wetu tumepewa uwezo wa kutawala na kuwaelekeza wenzetu katika njia sahihi ili waweze kufika mbinguni kwa Baba yaliko makao yetu sote kwani duniani hapa tunapita tu. Hivyo tunapaswa kudhihirisha hilo kwa maneno na matendo yetu kama mwalimu wetu wa pekee yaani Yesu Kristo mwenyewe alivyofanya! Ushuhuda Amini.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Maingilio: Mpendwa katika Kristo, leo Mama Kanisa mtakatifu anaadhimisha Dominika ya 31 ya mwaka A. Basi katika Dominika hii ninawaalikeni tutafakari wazo hili, Uaminifu ni ushuhuda wazi wa uinjlishaji kila wakati. Sisi sote kwa ubatizo wetu tumepewa uwezo wa kutawala na kuwaelekeza wenzetu katika njia sahihi ili waweze kufika mbinguni kwa Baba yaliko makao yetu sote kwani duniani hapa tunapita tu. Hivyo tunapaswa kudhihirisha hilo kwa maneno na matendo yetu kama mwalimu wetu wa pekee yaani Yesu Kristo mwenyewe alivyofanya. Ufafanuzi: Ndugu yangu, katika somo la kwanza Mungu ambaye ni mfalme mkuu anatambulishwa na mjumbe wake yaani nabii Malaki kama Bwana wa majeshi anayaona maovu yanayotendwa na Makuhani katika Hekalu jipya. Makuhani hawa wamegeuka na kuiacha njia sahihi ya kumtumikia Mungu na wanawakwaza watu wengi katika sheria. Hii ni kwasababu wanafanya kinyume na maagizo ya Mungu aliyowapa wakati akiweka Agano na mtumishi wake mwaminifu Lawi, aliyempendeza Mungu kwa utumishi wake mtakatifu na safi. Nabii Malaki kwa maongozi ya Mungu anawaonya na kuwakemea tena kwa maneno makali, hawa Makuhani ambao wamekosa uaminifu mbele ya Mungu kawa kujitangaza wenyewe badala ya kumtangaza Mungu. Hivyo Mungu anachukizwa na tabia yao hiyo na kuapa kuwalaani na kuwafanya wadharaulike mbele ya watu wote. Zaidi ya hapo Nabii Malaki anamtambulisha Mungu kuwa ndiye pekee anayepaswa kuabudiwa na kutumikiwa na watu wote kwani binadamu wote ni ndugu na watoto wake.

Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa
Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa

Katika Injili tunaona Yesu anawaonya wanafunzi na wafuasi wake wote, wasifuate matendo ya Waandishi na Mafarisayo bali wafuate mafundisho yao na kuyatendea kazi kwani ndivyo mafundisho ya torati na manabii. Mafarisayo kwa kutoelewa wayatendayo wanajiona kuwa wao ni wenye haki na watakatifu, lakini Yesu anawalaumu kwa matendo yao kwani wanafanya tofauti na wanavyo fundisha. Hapa Yesu anaonyesha kuwa imani bila matendo yanayoendana nayo imani hiyo imekwisha na ni unafiki na fedheha tu. Pia Yesu anawaonesha wanafunzi wake, jinsi gani waandishi na mafarisayo wanavyofanya tofauti na mafundisho yao, kwa kuwafunga mizigo mizito ya sheria na kuwatwisha watu mabegani wakati wao wenyewe wasitake hata kuigusa hata kwa vidole vyao. Sambamba na hilo Yesu anawaonya wafuasi wake wasipende sifa na heshima za nje kama wafarisao wanavyo fanya, kwa kupendelea viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika Masinagogi na kusalimiwa masokoni na kuitwa walimu. Bali anawatake wafuasi wake wawe waadilifu katika kumtumikia Mungu kwa kuonyesha matendo ya huruma kwa watu wote. Zaidi ya hayo Yesu anawaeleza ukweli wafuasi wake kuwa hakuna mwalimu mwingine duniani ila ni yeye (Yesu) tu, na pia hakuna Baba mwingine ila ni Mungu mwenyezi pekee, na katika yeye sisi sote ni ndugu na watoto wake, kwani sote tumeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu.

Uaminifu na uadilifu ni nyenzo msingi za uinjilishaji mpya
Uaminifu na uadilifu ni nyenzo msingi za uinjilishaji mpya

Na katika somo la pili, Mtume Paulo anaelezea maisha yake huko Thesolonike, na namna alivyowatunza na kuwapenda Wakristo wa huko. Paulo anaeleza jinsi gani alitangaza habari njema kwa upendo mwingi na alivyowatumikia wakristo katika mambo ya roho na mwili. Zaidi anasema jinsi wakristo wa Thesolonike walivyolipokea neno lake si kama neno la binadamu bali kama neno la Mungu. Mtume Paulo anasema, yeye na wafuasi wake wanamshukuru Mungu kwa kuwafanya wakristo walipokee vema neno la Mungu na kuwa ndugu zao na mwisho anawaasa kudumu katika imani ili neno la Mungu liendelee kutenda kazi yake ndani yao. Katika maisha ya kila siku ya kujifunza ni mengi machache kutaja. Kama nilivyokwisha sema kwa ubatizo wetu sisi sote ni watumishi wa Mungu katika nafasi ya ukuhani kwa wote (common priesthood) na hivyo tunapaswa kuvitumia vipaji vyetu mbalimbali tulivyozawadiwa na Mungu, kama ualimu, udaktari, uongozi serikalini, au kada mbalimbali ambazo kila mmoja amajaliwa, nakadhalika. Na hivyo tutumikiana kidugu kama watoto wa Baba mmoja kwa maneno na matendo kuelekea kwenye wito wetu wa utakatifu yaani ukamilifu. Zaidi katika kufanikiwa tuache kulewa madaraka na kujitafutia sifa za nje. Kwa mfano eti mimi nahubiri vizuri, ninamali sana, hivi Kanisa linanitegemea nisipo kuwepo tu, hakuna lolote!

Tufanye kazi, kwa uadilifu na uaminifu kama kielelezo cha uinjilishaji mpya
Tufanye kazi, kwa uadilifu na uaminifu kama kielelezo cha uinjilishaji mpya

Tusibweteke na mambo ya mwili tu, tutafute ya roho na kuwa wajasili katika kujishikiza kwa Mungu. Ulimwengu wa leo ambao unaumizwa na kukosa famidhila ya uminifu ni uwazi usipingika kila binadamu wengi leo hii, wamejeruhiwa na kubaki na makovu yatokanayo na ukosefu wa uaminifu, hiyo wengi wanaishi kwa kutokuwa na amani ya nafsi, akili, mwili, mazingira, utawala, uchumi, katika familia na ulimwengu mzima. Mataendo na maneno vinakinzana, hapa ndipo mtume yakao anatukumbusha juu ya utendaji nausemi wetu “Basi muwe watendaji wa Neno na wala msiwe wasikilizaji tu, ambao wanajidanganya wenyewe” Yakobo 1:22-27. Ulimwengu wa matukio na kupenda kusifiwa sana badala ya kuwa watumishi wenye kutenda zaidi tukimuiga Kristo Bwana na mwalimu wetu. Waliopewa dhaman ya uongozi na utumishi leo hawatofautiani na Mafarisayo ambao Kristo anawakemea katika injili ya leo na anatuonya tabia hiyo, ni wakati sasa wa kubadilika na kuwa na sifa ya uaminifu wa utendaji wetu uwe sawa sawa na maneno yetu. Lolote tulifanyalo kwa hatua ndogo tu na kwa uaminfu na upendo, linaweza kusababisha matokeo makubwa sana ya maana katika maisha yetu kila siku mintarafu uijilishaji mpya katika mwanga wa injili ya furaha. Yesu anasema, basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili aiyejenga nyumba yake juu ya mwamba (Luka 7:24). Nae mtume Paulo anatuhusia kuwa, “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote mkifundishana na kuonyana kwa Zaburi na nyimbo na tenzi za Rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu” (Wakolosai 3:16). Ninakutakia dominika njema ya kujenga tabi ana fadhila ya uaminifu kwani ni hadhina bora yenye kukulipa mara dufu na kulinda ut una hadhi yako na kubakia kuwa mtoto wa Mungu na kanisa. Pamoja tuseme uaminfu wa Kristo uaminifu wangu…Uaminifu wangu uaminifu wa Kristo.

Liturujia D 31

04 November 2023, 08:59