Tafuta

Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 31 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Tuhudumiane kidugu kwa ajili ya maisha na uzima wa milele. Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya 31 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa: Tuhudumiane kidugu kwa ajili ya maisha na uzima wa milele.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika 31 ya Mwaka A wa Kanisa: Huduma ya Upendo

Tunakumbushwa kuwa, kutumikiana kuliko kwema ni njia ya kufika mbinguni kwa Baba. Hili ndilo jukumu tulilopewa tulipobatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu kwa njia ya sakramenti ya Kipaimara tukaimarishwa ili kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu mema. Nasi tukifanya hivyo upendo na huruma ya Mungu vitajidhihirisha kwetu maana Mungu atakuwa nasi daima hatatuacha kamwe kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Wewe Bwana usiniache,.."

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 31 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Katika Dominika hii tunakumbushwa kuwa, kutumikiana kuliko kwema ni njia ya kufika mbinguni kwa Baba. Hili ndilo jukumu tulilopewa tulipobatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu kwa njia ya sakramenti ya Kipaimara tukaimarishwa ili kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu mema. Nasi tukifanya hivyo upendo na huruma ya Mungu vitajidhihirisha kwetu maana Mungu atakuwa nasi daima hatatuacha kamwe kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Wewe Bwana usiniache, Mungu wangu usijitenge nami, ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana, wokovu wangu” (Zab. 38:21-22) na sala ya mwanzo inakaza kusema; “Ee Mungu Mwenyezi na mwenye huruma, wawajalia waamini wako neema ya kukutumikia vema na kwa uchaji. Tunakuomba utuwezeshe kukimbilia ahadi zako pasipo kukwaa.” Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Malaki (Mal. 1:14-2: 8-10). Hiki ni kitabu cha mwisho katika agano la kale na maana ya jina Malaki ni mjumbe wangu aliyeishi miaka 450 kabla ya Kristo. Kitabu hiki kiliandikwaa baada ya wayahudi kurudi kutoka uhamishoni Babeli kikielezea sababu za ubaridi wa imani ya wana wa Israeli kwa Mungu wao. Katika sehemu hii ya somo la kwanza Nabii Malaki anatoa maonyo kutoka kwa Mungu, Bwana wa majeshi na Mfalme mkuu kwa maovu yaliyotendwa na Makuhani katika Hekalu jipya lililojengwa Yerusalemu baada ya kutoka uhamishoni Babeli. Kipindi hiki ibada zilizofanyika katika hekalu hili jipya hazikuwa na heshima mbele ya Mungu na mafundisho ya makuhani yaliuwa kikwazo kwa watu. Hivyo Nabii Malaki anawakaripia makuhani kwa kushindwa kuwaongoza watu katika sheria ya Musa ambapo matokeo yake ni watu kupoteza mizani ya maadili hivyo kupelekea maskini, wajane, yatima na wageni kuteseka kwa kunyimwa haki zao.

Huduma ya udugu na upendo ni njia ya kwenda mbinguni
Huduma ya udugu na upendo ni njia ya kwenda mbinguni

Nabii Malaki anatangaza matokea ya hali hii kwa makuhani kuwa Mungu atawapelekea laana na kuzilaani baraka zao na kuwa siku inakuja wakati ibada inayompendeza Mungu itaadhimishwa tena ambapo watashiriki watu wa mataifa yote na jina la Mungu litatukuzwa kila mahali na sadaka safi itatolewa kwa ajili yake na kati ya mataifa. Sadaka hii itatolewa na kuhani mkuu mmoja ambaye ni mtakatifu, asiye na doa, aliye safi, aliyejitenga na dhambi. Huyu kuhani ndiye Masiya, Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe ambapo sadaka yake msalabani imechukua nafasi ya sadaka zote zilizowahi kutolewa na mwanadamu kwa Mungu na kwa sasa sadaka hii inatolewa katika kila adhimisho la Misa Takatifu. Yeye kuhani mkuu hakuwa na makuu bali alijinyenyekeza na kufanya mapenzi ya Mungu. Mzaburi alivyomtafakari aliimba kwa maneno haya ya wimbo wa katikati akisema; “Bwana, moyo wangu hauna kiburi, wala macho yangu hayainuki, wala sijishughulishi na mambo makuu yashindayo nguvu zangu. Hakika nimeituliza nafsi yangu, na kuinyamazisha, kama mtoto aliyeachishwa kifuani mwa mama yake, ndivyo roho yangu ilivyo kwangu. Ee Bwana, uilinde nafsi yangu katika amani yako” (Zab. 131). Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa wathesalonike (1The. 2 :7-9, 13). Katika somo hili mtume Paulo anaeleza jinsi alivyowatunza na kuwapenda wakristo wa Thesalonike. Kwa mikono yake alifanya kazi ili asiwasumbue kumtegemeza. Kwa bidii yake ya kufanya kazi na matendo yake mema aliwatangazia habari njema kwa upendo mwingi watu wa Thesolonike na kuwaongoza vyema katika mambo ya roho na mwili na hivyo kuwafanya walipokee neno lake si kama neno la binadamu bali kama neno la Mungu. Hivyo mtume Paulo pamoja na wafuasi wake wanamshukuru Mungu kwa kuwafanya wao walipokee vema neno lake na kuwa ndugu zao na mwisho anawaasa kudumu katika imani ili neno la Mungu liendelee kutenda kazi yake ndani yao. Kumbe tunapaswa kulipokea kila mara neno la Mungu kwa moyo wa imani na matumaini kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba ili kwalo tuweze kutakatifunzwa na kustahilishwa kuushiriki uzima wa milele.

Nabii Malaki anawakaripia Makuhani kwa kushindwa kuwaongoza watu katika Sheria
Nabii Malaki anawakaripia Makuhani kwa kushindwa kuwaongoza watu katika Sheria

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 23:1-12). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anaweka wazi mambo mawaili. Kwanza kabisa anatoa karipio kali kwa walimu wa dini wasiofaa. Nyakati za Yesu, kazi ya makuhani na walawi ilikuwa kuongoza ibada hekaluni na kazi ya kuwafundisha watu sheria ya Musa ilikuwa kazi ya waandishi na mafarisayo ambao walikuwa ni walei. Ndiyo maana Yesu anasema kuwa “waandishi na mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa”. Katika hili Yesu anawaonya kwa mambo manne. Kwanza ni kuongeza sheria ambazo hazikuwekwa na Mungu na hivyo kufanya maisha ya watu kuwa magumu. Pili ni kutokushika yale waliyoyafundisha na hivyo kutokuwa mfano bora wa maisha ya imani na maadili kwa watu. Tatu ni kuwa na majivuno, kutafuta sifa mbele za watu na kuchukua nafasi ya Mungu. Nne ni kujaa kwao unafiki, uchoyo na ubinafsi. Itakumbukwa kuwa unafiki ni dhambi mbaya sana ndiyo maana Yesu aliikemea waziwazi. Hii ni dhambi ya mtu kufanya matendo ili aonekane na watu kwa nje tu, lakini ndani mwake amejaa uozo mtupu. Kwa waandishi na mafarisayo majivuno yao yaliendana na unafiki wao; walitaka waonekane wenye hekima na watu watakatifu ndiyo maana walipanua matamvua yao na kuongeza hirizi zao. Haya matamvua yalikuwa ni vyombo vidogo vya ngozi vyenye kurasa zilizoandikwa sheria ya Musa. Kila myahudi mkereketwa, alizivaa kwa kujifunga juu ya paji la uso na mkono wa kushoto wakati wa sala na wakati wa kwenda katika sinagogi. Lakini wao waliongeza ukubwa wake na kuzivaa wakati wote kumaanisha kuwa walifuata vyema na kwa uaminifu sheria na amari za Mungu kuliko watu wengine. Vivyo hivyo kwa hirizi walizovaa kwenye upindo wa vazi ambazo zilifungwa katika pande nne za kanzu zilizoning’inia.

Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha
Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha

Tukumbuke kuwa mambo haya Mungu kwa njia ya Musa aliwaamuru wayafanye kama ishara ya uteule wao kwake na iwasaidie kuzikumbuka daima amri za Mungu na kuziishi. Tunasoma hivi katika kitabu cha Hesabu 15:38-39; “Bwana akamwambia Musa; Sema na Waisraeli uwaambie: kwa vizazi vyote vijavyo jifanyieni vifundo katika pindo za mavazi yenu vikiwa na uzi wa buluu kwenye kila kifundo. Mtakuwa mkivitazama vifundo hivyo ili mpate kukumbuka amri zote za Bwana, ili mpate kuzitii msije mkajitia uzinzi wenyewe kwa kuzifuata tamaa za mioyo yenu na za macho yenu. Ndipo mtakumbuka kuzitii amri zangu zote nanyi mtawekwa wakfu kwa Mungu wenu” (rejea Kumb. 22:12). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anawaonya wafuasi wake na kuwatahadharisha kuwa wasipende sifa na heshima za nje kama Mafarisao wanavyopendelea viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika Masinagogi, kusimama masokoni ili wasalimiwe na watu na kuitwa walimu bali wao wawe waadilifu katika kumtumikia Mungu kwa kuonyesha matendo ya huruma kwa watu wote hasa walio wanyonge kwani sisi sote ni ndugu na watoto wa Mungu mmoja, sote tumeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu. Sisi nasi kwa sakramenti ya ubatizo tumeshirikishwa unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo. Hivyo tunaitwa na kutumwa kutangaza habari njema ya wokovu kwa mataifa yote na kuwafanya kuwa wafuasi wa Yesu (Mt. 28:19-20). Kumbe mafundisho haya ya Yesu yanatuhusu na sisi. Basi tujitahidi kufanya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu ili kwayo sisi tupate huruma yake kama sala ya kuombea dhabihu; “Ee Bwana, sadaka hii tunayokutolea iwe dhabihu safi mbele yako, ituletee na sisi huruma yako”. Hivyo tutapata uzima wa milele kama antifona ya komunyo inavyosema; “Bwana asema: Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yn. 6:57). Tukifanya hivi sala baada ya komunyo inayosema; “Ee Bwana, tunaomba neema yako izidi kutenda kazi ndani yetu, na tena ituweke tayari kupokea ahadi za sakramenti hizi zilizotuburudisha”, itatimizwa kwa sisi kuingia katika uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D31

 

02 November 2023, 14:08