Tafuta

Waamini wa Suda Kusini wakati wa ziara ya Papa Francisko Februari 2023. Waamini wa Suda Kusini wakati wa ziara ya Papa Francisko Februari 2023.  (AFP or licensors)

Sudan Kusini:Askofu Taban wa kwanza wa Torit ameacha ishara ya matumaini na uponyaji

Askofu Paride Taban wa Torit,nchini Sudan Kusini amefariki dunia Mosi Novemba akiwa na miaka87.Katika utume aliwahi kufungwa 1965 na serikali ya Khartoum,tena 1989 na SPLA harakati lililopigania uhuru wa Sudan Kusini.Alistaafu mnamo 2004 na 2005 akaanzisha Jumuiya huko Kuron,kijiji cha amani cha Utatu Mtakatifu.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Mchungaji aliyefanya amani na upatanisho kuwa kitovu cha maisha yake ya huduma kwa watu wa Mungu, ndivyo walivyoweza kuelezea muhtasari wa sura ya Paride Taban, ambaye alikuwa ni Askofu wa kwanza wa jimbo la Torit nchini Sudan Kusini, aliyefariki dunia mnamo tarehe 1 Novemba 2023 akiwa na umri wa miaka 87 ambapo alikuwa amelazwa katika hospitali ya Nairobi, Kenya. Alizaliwa mnamo mwaka wa 1936, na akapewa Daraja la Upadre mnamo mwaka 1964, wakati wa kipindi cha kufukuzwa kwa wamisionari kutoka Sudan. Mnamo Januari 1980 aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu  Katoliki la Juba na kupewa wakfu wa kiaskofu mnamo tarehe 4 Mei 1980 mikononi mwa  Mtakatifu Yohane Paulo II. Mnamo Julai 1983 aliteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Torit.

Majaribio ya vita nchini Sudan

Majaribio ya vita hivyo nchini Sudan Kusini yalimlazimisha Askofu Taban kwenda uhamishoni nchini Uganda, Kenya na Jamhuri ya Afrika ya Kati mnamo mwaka 1984. "Nilifurahi kuwa askofu wakati wa vita kwa sababu nilikuwepo kuwafariji na kuwatia moyo watu na kushiriki mateso yao," marehemu Askofu alisema hayo katika mahojiano yaliyotolewa mnamo Julai 2022 katika Radio Tamazuj, kituo cha radio cha Sudan Kusini, katika kuadhimisha miaka 11 ya uhuru wa Sudan Kusini. Nchi ambayo ilipata uhuru mnmo mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kujitenga na maeneo mengine ya Sudan.

Kufungwa gerezani na kuanzisha kwa Baraza la Makanisa NSCC

Askofu Taban pia alikumbuka pia kwamba alifungwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1965 na serikali ya Khartoum na kisha tena mwaka 1989 na SPLA (Sudan's People Liberation Army, harakati lililopigania uhuru wa Sudan Kusini). Kwa hiyo "Niliwekwa gerezani na watu wangu, na SPLA," alikumbuka hayo  kwa tabasamu. "Waasi walinifunga gerezani kwa sababu waliponichukua Torit nilibaki pale na watu na walidhani mimi ni wakala wa serikali. Lakini nilibaki tu kuwa karibu na watu." Ili kuhimiza mazungumzo kati ya hali halisi ya Sudan mnamo mwaka 1990 Askofu Taban alikuwa miongoni mwa waanzilishi na rais wa kwanza wa Baraza Jipya la Makanisa  ya Sudan (NSCC), linalojumuisha Kanisa Katoliki, Kanisa la Maaskofu la Sudan, Kanisa la Kipresbyterian la Sudan, African Inland Church, Kanisa la Kipentekoste la Sudan na Kanisa la Sudan Interior.

Mazungumzo ya amani wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe

Kwa njia hiyo chini ya uongozi wake, Askofu Paride Tabani, Baraza hili la NSCC lilifanya kazi kama mwezeshaji katika mazungumzo ya amani wakati wa Vita vya Pili vya wenyewe kwa wenyewe  nchini Sudan na kama mtetezi wa haki za binadamu. Katika kutafuta kwake amani mara kwa mara, Askofu Paride Taban kwa niaba ya AMECEA (Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki) alikwenda nchini Rwanda mwaka 1994, mwaka wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa dhidi ya Watutsi.  Askofu Taban alistaafu uongozi wa jimbo la Torit mnamo mwaka 2004 na mwaka 2005 akaanzisha Jumuiya huko Kuron, kijiji cha amani cha Utatu Mtakatifu nchini Sudan Kusini, kinachopokea watu wa asili tofauti za makabila ambao ni wahanga wa migogoro. Kijiji hiki kimekuwa ishara ya matumaini na uponyaji.

03 November 2023, 14:31