Tafuta

Tarehe 25 Novemba 2023 Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge kimesherehekea Mahafali ya 16 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utafiti na Ubunifu kwa Maendeleo ya Taifa” Tarehe 25 Novemba 2023 Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge kimesherehekea Mahafali ya 16 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utafiti na Ubunifu kwa Maendeleo ya Taifa”  

Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki MWECAU: Utafiti na Ubunifu

Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge yamenogeshwa na kauli mbiu “Utafiti na Ubunifu kwa Maendeleo ya Taifa” na mgeni rasmi alikuwa ni Askofu Flavian Matindi Kassala Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika hotuba yake, amemshukuru Mungu na kutoa pongezi kwa makundi mbalimbali, amegusia kuhusu kauli mbiu ya mahafali ya 16 ya Chuo kikuu cha MWECAU na kwamba, wale waliohitimu sasa ni mwanga wa ulimwengu.

Na Askofu Flavian Matindi Kassala, Moshi, Kilimanjaro

Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge “Mwenge Catholic University” (MWECAU), mbacho zamani kilijulikana kama Chuo Kikuu cha Elimu cha Mwenge (MWUCE), kilianzishwa kunako mwaka 2005. Hiki ni Chuo kikuu ambacho kiko chini ya Baraza la Maaskofu Tanzania na kipo mjini Moshi, Kilimanjaro, Tanzania. Kilianzishwa kama Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Yosefu na baadae kama Chuo Kikuu cha Elimu cha Mwenge, tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania, SAUT. Na tarehe 25 Novemba 2023 kimesherehekea Mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utafiti na Ubunifu kwa Maendeleo ya Taifa” na mgeni rasmi alikuwa ni Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.  Katika hotuba yake, amemshukuru Mungu na kutoa pongezi kwa makundi mbalimbali, amegusia kuhusu kauli mbiu ya mahafali yak umi na sita ya Chuo kikuu cha MWECAU na kwamba, wale waliohitimu katika fani ya ualimu wakumbuke kwamba, wanao wajibu mkubwa kwa Taifa la Tanzania na kwamba, wao kwa sasa ni “Mwanga wa Ulimwengu.” Mhashamu Baba Askofu Ludovick Joseph Minde, Askofu wa Jimbo la Moshi na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge; Mhashamu Baba Askofu Rogath Kimaryo, Askofu wa Jimbo la Same na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge; Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge; Mheshimiwa Sana, Padre. Prof. Philbert Vumilia, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge; Mheshimiwa sana Pd. Athony Makunde, Katibu Mkuu wa AMECEA, Waheshimiwa viongozi wa serikali mliojumuika nasi siku ya leo; Wapendwa Wahadhiri na Wafanyakazi wote wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge; Wapendwa wahitimu wetu wa leo na wanachuo wote kwa ujumla; Wapendwa Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana, itifaki imezingatiwa.

Askofu Flavian Matindi Kassala, Mgeni Rasmi Mahafali ya 16 ya MWECAU
Askofu Flavian Matindi Kassala, Mgeni Rasmi Mahafali ya 16 ya MWECAU

TUMSIFU YESU KRISTU, Leo tumekusanyika kwa tukio hili kubwa la mahafali ya 16 ya Chuo chetu, sio kwa sababu ya uwezo na nguvu zetu au kwa maamuzi yetu bali ni kwa sababu Mungu mwenyewe ametoa kibali cha hili kufanyika. Siku ya leo kama tulivyokwisha kusikia katika hotuba ya Makamu Mkuu wa Chuo, jumla ya wanachuo 1,499 watahitimu katika fani na ngazi mbalimbali ikidhihirisha mafanikio ya kile walichokifuata Chuoni MWECAU. Mafanikio hayo siyo mastahili yao bali ni kwa neema ya Mungu tu. Ni Mungu mwenyewe aliyesimamia mchakato tangu kuchagua fani walizosoma, kujisajili Chuoni, kuelewa namna ya kujifunza na hata leo wanaondoka wakiwa na maarifa na ujuzi mpya tayari kwenda kuwahudumia watu na taifa kwa ujumla kwa kuyaweka katika matendo yale waliyojifunza. Ukweli huu unatufanya tuendelee kuwa na moyo wa shukrani na sifa kwa Mungu. Hivyo basi kila mmoja wetu anayo nafasi ya pekee kabisa na kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa makuu mengi aliyomjalia na kwa mafanikio ya wahitimu wetu wa leo. Pokeeni salamu kutoka kwa Mkuu wa Chuo chetu cha Kikatoliki Mwenge, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya. Baba Askofu Mkuu amenituma siku ya leo kumwakilisha katika mahafali haya. Anawapongeza sana wahitimu wote kwa mafanikio waliyoyafikia. Sambamba na hilo, anatoa shukrani za pekee kabisa kwa Baraza la Chuo na Uongozi kwa ujumla kwa majitoleo yao katika kuhakikisha Chuo chetu kinatoa elimu bora yenye manufaa kwa taifa letu. Pamoja na shukrani kwa Mungu na salamu kutoka kwa Mkuu wa Chuo, napenda kuchukua nafasi hii kwa moyo wa dhati kabisa kulishukuru Baraza la Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge chini ya Mwenyekiti wake Mhashamu Baba Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi kwa kusimamia sera na taratibu mbalimbali zinazotumika kukiendesha Chuo chetu.

MWECAU: Utafiti na Ubunifu kwa maendeleo ya Taifa
MWECAU: Utafiti na Ubunifu kwa maendeleo ya Taifa

Shukrani za pekee kabisa nazielekeza kwa Makamu Mkuu wa Chuo, Mheshimiwa Padri Profesa, Philbert Vumilia na Menejimenti ya Chuo kwa namna wanavyosimamia shughuli kuu zinazofanyika katika Chuo chetu. Leo hii tunashuhudia moja ya matunda ya bidii na majitoleo yao. Kwa hakika wanastahili pongezi kubwa. Mimi binafsi naahidi kuendelea kuwaombea afya njema na mafanikio katika kutekeleza mipango mbalimbali kwa sifa na utukufu wa Mungu. Wahitimu tunaowashuhudia siku ya leo wameandaliwa kwa vipindi tofauti tofauti kuendana na fani au ngazi mbalimbali. Maandalizi hayo yamefanywa na wakufunzi wakishirikiana na wafanyakazi wengine wote wa Chuo. Hivyo basi, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru kwa moyo wa dhati kabisa wafanyakazi wote wa Chuo chetu cha Kikatoliki Mwenge. Hongereni sana wahadhiri na wafanyakazi wote. Kwa hakika, majitoleo yenu ya kila siku yamepelekea kufanikisha malengo ya wahitimu wetu wa leo katika kupata elimu bora itakayowasaidia siyo tu katika kupata ajira, bali kujiajiri na kulitumikia taifa letu la Tanzania katika nyanja mbalimbali. Endeleeni kushirikiana na Uongozi wa Chuo ili wahitimu wetu wakawe mwanga unaong’ara na kuangaza ulimwengu mzima. Ni ukweli usiopingika kwamba, bila wahitimu tusingeweza kuunda mkusanyiko huu. Nichukue nafasi ya kipekee kuwapongeza sana wahitimu wote na kuwashukuru kwa namna walivyoshirikiana nasi muda wote walipokuwa hapa Chuoni. Asanteni sana. Tunawaombea baraka na fanaka katika maisha na katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku. Daima kumbukeni wajibu mlio nao kwa taifa letu. Nyie ni nguvu kazi ya taifa. Tunatambua kwamba kila mmoja amepewa karama mbalimbali na tunashirikishana karama hizo katika kutumikiana. Fani mlizosoma na kuhitimu vyema ni namna ya kupalilia karama mlizonazo na kujiandaa kuzitumia sio tu kwa manufaa yenu bali zaidi sana kwa kuwahudumia wengine kwa sifa na utukufu wa Mungu.  Kamwe msijekuwa na choyo ya kuwashirikisha wengine yale mliyojifunza.

Askofu Kassala akikagua shughuli za wahitimu wa MWECAU
Askofu Kassala akikagua shughuli za wahitimu wa MWECAU

Kwenu wageni waalikwa, mabibi na mabwana, tunatambua mna majukumu mengine na ya msingi kabisa lakini mlipopata mwaliko wa kujumuika nasi hamkusita kuitikia na kufika kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa mafanikio ya wahitimu wetu pamoja na kuwapongeza. Tunawashukuru kwa upendo mnaouonyesha kwa Chuo chetu. Hakika tumefarijika sana kwani bila uwepo wenu Mahafali haya yasingefana. Uwepo wenu pia unatudhihirishia kuwa mnaitambua kazi kubwa inayofanywa na Chuo katika kutoa elimu inayokidhi ubora na viwango ndani na nje ya nchi yetu.   Wapendwa jumuiya ya MWECAU, wahitimu na wageni waalikwa, tunapokusanyika katika mahafali ya 16 ya Chuo chetu tunajivunia kuendelea kuwa sehemu ya kuibua nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi katika kukabiliana na mambo mbalimbali katika jamii. Tumesikia kauli mbiu ya Mahafali ya 16 ya Chuo chetu inayosema, “Utafiti na Ubunifu kwa Maendeleo ya Taifa”. Dhana zinazojenga kauli mbiu hii ni tatu yaani “utafiti”, “ubunifu” na “maendeleo ya taifa”. Tunapozungumzia maendeleo ya taifa hii ni dhana inayoletwa kwa juhudi za pamoja. Kila mwananchi kwa nafasi yake anafanya shughuli zenye kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi na hivyo kupelekea maendeleo ya kila mtanzania. Ndio maana basi tuna ujasiri kusema kwamba, maarifa na ujuzi mlioupata kwa kipindi chote mlichokaa MWECAU yana mchango mkubwa kwa kukuza uchumi na hivyo kupelekea maendeleo ya taifa letu la Tanzania. Tumekwisha kusikia kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo chetu umuhimu na nafasi ya utafiti na ubunifu katika kukuza maendeleo ya nchi. Hivyo basi nami naendelea kuweka mkazo kwa wahitimu kuzingatia mambo hayo na kutambua kwamba wao kama wahitimu wa elimu ya chuo kikuu wana mchango mkubwa katika kufanikisha maendeleo ya nchi yetu. `Tunaendelea kuwaombea ufanisi mnapoendelea kutekeleza jukumu hilo kubwa kwa mustakabadhi wa taifa na jamii yote ya Tanzania. Nitumie nafasi hii pia kutoa changamoto kwa wakufunzi wetu kujitahidi kuibua na kuendeleza bunifu mbalimbali kwa wanafunzi wetu. Pamoja na jitihada nyingi zinazofanyika hapa MWECAU katika kutoa elimu bora, niwaombe wahadhiri wote waongeze jitihada za kuibua na kuendeleza bunifu za wanafunzi. Hii itatusaidia kuongeza umaana na ubora wa elimu ya Chuo kikuu kwa maendeleo yetu.

MWECAU wahitimu kwa mwaka 2023 1, 499 mafanikio makubwa
MWECAU wahitimu kwa mwaka 2023 1, 499 mafanikio makubwa

Tunapofanya mahafali haya ya 16 napenda wahitimu wote watambue pia umuhimu wa “ubunifu” hasa katika kutenda yale tuliyojifunza kwa nadharia darasani. Ni wakati wa kutumia mbinu mbalimbali za ubunifu kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii yetu kama ukosefu wa ajira. Ni muhimu wahitmu wetu watambue kuwa, nyakati hizi sio za kumaliza masomo ya Chuo Kikuu na kusubiria ajira bali kufikiria namna ya kujiajiri. Naelewa kwamba wapo wahitimu waliofundishwa juu ya ujasiriamali na elimu ya biashara kwa ujumla. Ni wakati muafaka kwenda kuweka katika vitendo mbinu za ujasiriamali na biashara katika kujikwamua kutoka katika wimbi la ukosefu wa fursa za   ajira. Wapo wanaohitimu katika fani za sayansi, ni wakati muafaka kutumia elimu yao katika kufanya gunduzi mbalimbali zenye tija. Wapo wanaohitimu katika Shahada ya uzamili (Masters) na 7 uzamivu (Doctorate). Pamoja na mambo mengine waliyojifunza, nina imani kabisa kwamba kundi hili wamefundishwa kwa namna ya pekee kabisa namna ya kufanya tafiti. Kufanya tafiti kunapelekea kutambua chanzo cha tatizo na kuibua mbinu za kukabiliana na tatizo husika. Ni rai yangu kwenu kwamba, mtakwenda kufanya tafiti na kulisaidia taifa katika kuchanganua matatizo, kujua chanzo chake na kupendekeza suluhisho. Kwa wale wahitimu ya fani ya elimu, tunao wajibu mkubwa kwa taifa hili. Tumesomea ualimu ili tukasomeshe au kufundisha wengine. Tutambue kwamba tunaenda kufundisha kundi ambalo ndilo linategemewa kuwa taifa la kesho; likijumuisha vijana wetu wadogo na watoto. Kundi hili kwa kipindi hiki linakubwa na changamoto mbalimbali zinazosababishwa na utandawazi. Mlipotoka huko uariani kuja katika majiundo pengine mliacha dunia ya utandawazi, leo hii mnarudi kama wahitimu mtakutana si tena na dunia ya utandawazi bali dunia ambayo ni utandawazi. Chukuweni hadhari kutambua hali halisi ya dunia na kuiingia kwa umakini. Elimu yenu iwafanye muwe watafiti kwa kila hatua ya maisha mnayotaka kuchukua hali mkishirikia katika kulinda tunu ambazo tumepokea toka kwa Mungu, kama vile heshima kwa uumbaji, kwa viumbe na kwa dunia nzima, ili msije kuwa sababu ya maangamizi ya dunia yetu pendwa.

Askofu Kassala akihutubia katika Ibada ya Misa Takatifu
Askofu Kassala akihutubia katika Ibada ya Misa Takatifu

Ni dhahiri kwamba tunao mchango mkubwa sana wa kusaidia taifa la kesho kujengeka katika misingi bora kwa kujikita katika faida zinazoletwa na utandawazi. Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia wasomi wakishindwa kuwaelekeza vijana na watoto katika maadili na malezi yaliyo mazuri. Swali la kujiuliza siku ya leo, ni je, natumia vipi elimu niliyosoma na maadili niliyopata MWECAU katika kuhamasisha maadili mema na utendaji bora kwa maslahi ya taifa? Je, nifanye tu yale ambayo naona yananipendeza mimi na kuharibu kizazi kijacho? Maswali haya yalete changamoto kwa wahitimu wetu. Tunawatuma kwenda kuwa mfano na kioo cha jamii kwa wengine. Kama ilivyo Kauli Mbinu ya Chuo chetu, “Mwanga wa Ulimwengu”, tunaamini tunawatuma kwenda kumulika maeneo ambayo hayana mwanga kwani nyie ni mwanga kwa wale ambao hawajaweza kufikia hatua mliyoifikia leo. Wapo waliotamani lakini kwa sababu mbalimbali hawakuweza kufanikiwa kuwa kama ninyi mnaohitimu leo. Basi tutambue hilo ni kusudi la Mungu na hivyo basi tukalitumikie taifa na watu wake. Mafanikio ya taifa leo yatapunguza makali ya changamoto mbalimbali za kijamii na hata kiuchumi. Kwa kuhitimisha napenda kutoa shukrani kwa mara nyingine kwa Baraza la Chuo, Seneti, Uongozi na Menejimenti ya Chuo, Wafanyakazi, Wahitimu na wageni wote waalikwa kwa kujumuika nasi na kwa kunisikiliza. Nawatakia kila la heri ninyi wahitimu wetu na wageni wetu waalikwa.  Mwenyezi Mungu awalinde na kuwabariki nyote. Mungu Ibariki MWECAU, Mungu ibariki Tanzania na watu wake wote.

Vigogo wa MWECAU
Vigogo wa MWECAU

Wakati huo huo, Askofu Flavian Matindi Kassala amempongeza Mheshimiwa Padre Dr. Emmanueli M. Wabanhu kutoka Jimbo Katoliki la Geita anayefundisha kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika mashariki na Kati, CUEA kwa kupandishwa hadhi kutoka “Senior Lecturer” "Mhadhiri Mwandamizi" na kuwa “Associate Professor”: "Profesa Mshiriki.” Haya ni matunda ya juhudi binafsi za Profesa Emmanueli M. Wabanhu akisindikizwa na sala za watu wa Mungu Jimboni Geita pamoja na watu wenye mapenzi mema. Pia anakuwa ni Kasisi wa kwanza kutoka Jimbo la Geita kujinyakulia hadhi hii ambayo ni heshima kwa Jimbo na kwa Kanisa la Tanzania. Kwa hakika amefungua mlango ambao vijana: wakleri, walei na watawa watavutwa kuufikia.

+ FLAVIAN MATINDI KASSALA

Askofu wa Geita na Makamu Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

25 Novemba 2023 – MWECAU Moshi - Tanzania.

MWECAU 2023
27 November 2023, 15:49