Tafuta

2023.11.08 Hawa ni washiriki wa uzinduzi wa Uinjilishaji mtandaoni ,Bujumbura Burundi. 2023.11.08 Hawa ni washiriki wa uzinduzi wa Uinjilishaji mtandaoni ,Bujumbura Burundi. 

Burundi,Padre Bideberi:Caritas Taifa na CECAB na kuenzi Siku ya Maskini Duniani

Baraza la Maaskofu Burundi na Caritas Taifa katika afla za Siku ya Maskini duniani huandaa mazingira mazuri ya kuwakumbuka na kuwatembelea Wakimbizi,Wafungwa na kutembelea vituo vya watoto yatima,wajane,wazee,bila kusahau walio katika mazingira magumu na hatarishi kama waathirika wa aina za utumwa mamboleo.

Na Padre Novatus Bideberi, -Burundi na Angella Rwezaula,- Vatican.

"Maskini, sio picha za kuhama bali watu wanaoomba hadhi" ni kutoka katika kifungu cha ujumbe wa Siku ya VII ya  Maskini Duniani itakayaofanyika Dominika tarehe 19 Novemba 2023 ambapo Papa Francisko anatuhimiza tusiwaondoe machoni wale walio katika matatizo kama vile watoto wanaoishi katika mazingira magumu, maeneo ya vita kama vile Mashariki ya Kati, Ukraine, Sudan Kusini na sehemu nyingine nyingi zenye vurugu. Katika Ujumbe wa Baba Mtakatifu wa Siku ya Maskini Duniani unasisitiza wazi juu ya mtazamo hai kwa ajili ya watu wahitaji hasa kwa kuongozwa na kauli mbiu isemayo Usimwondelee mtazamo Maskini (Tb 4,7). Ni katika muktadha huo ambapo Padre Novatus Bideberi Mhudumu katika Kambi za Wahamiaji na Wakimbizi nchini  Burundi amezumgumza kwa kirefu na Vatican News, kuhusiana  na tukio la siku hii,  na maandalizi yake kutokana na kwamba  kitengo chake kinagusa moja kwa moja katika makambi yote ambayo wanakosa kila na kutegemea msaada.  

Papa akishiriki chakula na maskini 2022
Papa akishiriki chakula na maskini 2022

Katika mahojiano hayo na Padre Bideberi anabainisha kuwa:Wapendwa katika Kristo, TUMSIFU YESU KRISTO!

Ninapenda kuungana na Mama Kanisa ambaye tarehe tarehe 19 Novemba itafanywa kumbukizi la mara ya saba, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoanzisha rasmi kumbukizi la Siku ya kuwakumbuka ndugu zetu Maskini na Wahitaji zaidi ya wengine. Mama Kanisa amekuwa kwa namna nyingine akiwajali na kuwatendea kadri ya upendo na huruma ya Mungu, lakini kwa tendo hili la kutenga siku ya adhimisho kwa kuwakumbuka ndugu zetu Maskini linaonesha ni jinsi gani Baba Mtakatifu Francisko  ametaka tulipatie kipaumbele zaidi! Neno la Mungu linalo tuongoza katika sherehe za mwaka huu 2023   kadiri ya dhamira ya Baba Mtakatifu Francisko linatoka katika kifungu cha kitabu cha Tobiti : 4,7;  Neno ambalo linatutaka kuishi upendo na huruma kwa wale wasiojiweza yaani maskini na fukara; tufanye hivyo kwa kuwajali na kuwapunguzia mizigo inayowalemea hasa ya wimbi la Umasikini na ufukara ambao unazidisha kasi ya kuyamomonyoa maisha yao katika jamii zetu!  Baadhi ya Makundi hatarishi yanayoongoza katika wimbi la Umasikini na Ufukara ni pamoja na:- Wahamiaji,Wakimbizi, Wanaodhurumiwa kingono(Wanaohusiana na Biashara Haramu dhidi ya Binadamu), kwa maana ya kununuliwa kama bidhaa, kisingizio kuwapunguzia Umasikini wao..!; Watoto wa mitaani, wajane na wazee, watoto yatima kama matokeo ya vita, nakadhalika.

Baadhi ya maadalizi ya siku ya wakimbizi huko Msumbiji 2022
Baadhi ya maadalizi ya siku ya wakimbizi huko Msumbiji 2022

Katika muktadha wa kauli mbiu ya Baba Mtakatifu kutoka katika Neno la Mungu Tobiti 4,7;  tunashauriwa kuwajali na kuwahudumia wale wanaotuzunguka  na hasa kutofumba macho na masikio yetu yanayozisikia na kuziona shida za wenzetu! Ni katika muktadha  huo ambapo Caritas za Majimbo chini ya uratibu mzuri zimeweza kuratibu vizuri namna iliyo nzuri zaidi  ya maadhimisho au sherehe za kumbukumbu ya siku ya Masikini duniani. Kwa upande wa Kanisa mahalia nchini Burundi, wamekuwa na utaratibu ambao tangia kuanzishwa kwa sherehe hizo 2017, Caritas Burundi ndani ya kivuli cha  Baraza la Maaskofu Burundi(CECAB), limekuwa likifanya matukio mbalimbali katika kuienzi siku hiyo hupokea kwa mikono miwili ujumbe wa Baba Mtakatifu na kuufanyia tafsiri ili kuutajirisha umma wa Wakristo juu ya siku hiyo, na pia kusambaza ujumbe huo kwa jamii nzima, na hii hufanyika kila mwaka. Tafsiri hiyo ya ujumbe wa Baba Mtakatifu hufanyika katika Lugha Mama yaani Kirundi. Na usambazaji huo wa ujumbe wa Baba Mtakatifu huamsha hamasa juu ya uwajibikaji na hivyo kuchukuliwa kama kiini cha mafundisho yasiyoweza kufumbiwa macho kila mwaka.

Chini ya uratibu wa Ofisi ya Caritas Taifa na Caritas majimbo, pamoja na Maaskofu wa Majimbo mahalia huweza kuchagua ni wapi ama katika maparokia au katika makambi ya Wakimbizi, vituo kama viwanja vya ndege, vivuko na hata katika mipaka ambapo panaweza kufanywa  kama Kituo cha kuadhimishia sherehe hizo. Aidha vituo vya Radio na Televisheni kwa mfano Redio Maria Burundi, Radio sauti ya Maridhiano (RVR) Muyinga hutumika kwa kurusha matangazo juu ya maandalizi ya sherehe hizo! Juma moja kabla ya maadhimisho hayo, Caritas Taifa na Baraza la Maaskofu Burundi  (CECAB) huandaa mafundisho juu ya kumbukumbu hiyo ili kuwezesha maandalizi ya mioyo ya watu kulingana na ujumbe na lengo la  Baba Mtakatifu.  Caritas Taifa na Baraza la Maaskofu Burundi husisitiza juu ya ubunifu wa mipango midogo midogo ya maendeleo ili kuinua makundi hatarishi yanayotokomezwa na wimbi la Umasikini na ufukara wa kupindukia kwa (Wakimbizi, Wahamiaji, Waathirika wa biashara ya Ngono, watoto wa mitaani, yatima na wazee...).

Kutembelea wasiojiweza
Kutembelea wasiojiweza

Ofisi yaCaritas Taifa  vile vile ikishirikiana na Ofisi za Caritas Majimbo huandaa mipango mizuri ili kuboresha mazingira ya Masikini  ya kielimu, ki-malazi, kiafya kwa kuwajengea nyumba wasio na makazi, kuwatibisha na kuwatafutia bima ya afya, na hii hufanyika kila mwaka kabla ya adhimisho la Kumbukizi hili la Siku ya Maskini duniani. Vile vile Ofisi za Caritas Taifa kwa uratibu mzuri  huandaa mazingira mazuri ya kuwakumbuka na kuwatembelea Wakimbizi  Wafungwa na kutembelea vituo vya watoto yatima na wajane, wazee, bila kusahau  walio katika hatari ya Biashara haramu dhidi ya Binadamu. Safari hizi huzingatia INJILI kwa njia ya matendo thabiti kama vile (Mavazi, vyakula, madawa).  Katika kuhitimisha sherehe hizi, Ibada ya Misa huadhimishwa na Askofu Jimbo na baadaye kushiriki chakula, neno la siku, na pia kwa wawakilishi wa makundi ya wahitaji zaidi ya wengine kukabidhiwa mahitaji yalazima yaliyokusanywa kutoka katika jamii inayowazunguka kwa uratibu mzuri wa Ofisi za Caritas Taifa na Caritas Majimbo.

Wapendwa Taifa Takatifu la Mungu, kwa utekelezaji wa haya, tunaonesha kuwa tunajali ujumbe wa Mama Kanisa kupitia kwa wakiri wa Kristo yaani Baba Mtakatifu. Ni mara nyingi amesema: "Kanisa lazima litoke nje ya Ngome zake, ili kubaini Umasikini wakupindukia ulioko nje ya Kuta  za Ngome zetu." Na zaidi alisema, "Kanisa ni kambi ambalo linapata kimbilio la watu wake, bila kubagua yeyote na kwa hiyo Kanisa ni kwa watu wote." Na hii tunaweza kutambua ukweli huu kwa kubaini umasikini unaoziponza afya  za hawa Masikini na Fukara; tukawatibisha kwa kuwafanyia vipimo kwa afya zao, kwa kuwachukulia dawa za kinga, kuwalipia madeni mbalimbali kadri ya mahitaji yao. Ndugu wapendwa, tukumbuke tusipotenda haya, hakuna anayetenda badala yetu, maana kama Baba Mtakatifu Francisko asemavyo "Kwa sasa tunaishi nyakati si zakutazama  ndugu mhitaji na kumjali, badala yake tunaishi nyakati za kujijali wenyewe, nyakati za ubinafsi." Mfano wa Msamaria Mwema (rej, Lk 10:25-37) si historia ya wakati uliopita, inatia changamoto wakati wa sasa wa kila mmoja wetu. Kuwakabidhi wengine kazi ni rahisi; kutoa pesa kwa wengine kufanya hisani ni ishara ya ukarimu; Kujihusisha kibinafsi ni wito wa kila Mkristo.

Maskini wengi wanahitaji msaada
Maskini wengi wanahitaji msaada

Na kama Baba Mtakatifu anavyo tukumbusha katika Ujumbe wake kuwa: “Umakini  wetu kwa maskini uwe daima na uhalisia wa kiinjili. Kushirikishana lazima kuendana na mahitaji madhubuti ya mwingine, na sio kujiondolea kwangu yale yaliyo ya ziada. Hapa pia, utambuzi unahitajika, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, ili kutambua mahitaji ya kweli ya ndugu zetu na si matarajio yetu. Wanachohitaji kwa kwa hakika na haraka ni ubinadamu wetu, mioyo yetu iliyo wazi kwa upendo. Tusisahau: “Tumeitwa kumgundua Kristo ndani yao, kuwapa sauti yetu katika sababu zao, lakini pia kuwa marafiki zao, kuwasikiliza, kuwaelewa na kukaribisha fumbo la hekima ya ajabu ambayo Mungu anataka kuwasiliana  nasi kupitia wao”(rej. Evangelium gaudiu,198). Ndugu  Wapendwa yote hayo ni kutimiza kile ambacho Bwana alisema: “Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha; nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.’ (Mt 25, 40)”. Ninawatakia  maandalizi ya Siku ya VII ya Maskini duniani.

Anahitimisha  hivyo Padre Novatus Bideberi Mhudumu wa kichungaji katika Makambi nchini Burundi.

Ushuhuda wa Padre Novatus Bideberi,Mhudumu wa Kichungaji katika kambi za wakimbizi Burundi

 

16 November 2023, 13:35