Tafuta

Askofu Edward Mapunda: Upendo wetu uonekane kwa matendo, iwe chachu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Askofu Edward Mapunda: Upendo wetu uonekane kwa matendo, iwe chachu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. 

Askofu Edward Mapunda: Upendo Uwe ni Chachu ya Uinjilishaji wa Kina Singida

Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida: Upendo miongoni mwa waamini unaomwilishwa katika matendo adili na matakatifu iwe ni chachu ya uinjilishaji ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa mahubiri ya Misa ya kuzindua Grotto ya Mama Bikira Maria, kubariki eneo la shule ya Mt. Maria Josepha na kuweka jiwe la msingi la Kanisa la Mt. Ireneus na Maria Josepha, Kigango cha Kundi, Parokia ya Mt. Yohane Paulo II, Misughaa, Jimbo Katoliki Singida.

Na Padre Deogratias Makuri, - Singida, Tanzania.

Uinjilishaji wa Kina: "Upendo wetu uonekane kwa matendo, iwe chachu ya uinjilishaji," Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa mahubiri ya Misa ya kuzindua Grotto ya Mama Bikira Maria, kubariki eneo la shule ya Mt. Maria Josepha na kuweka jiwe la msingi la Kanisa la Mt. Ireneus na Maria Josepha, Kigango cha Kundi, Parokia ya Mt. Yohane Paulo II, Misughaa, Jimbo Katoliki Singida. Baba Askofu alisisitiza waamini kuwa na moyo wa upendo wao kwa wao na upendo huo uonekane hasa katika namna ya kuishi na watu na katika mahusiano yao na Mungu. Baba Askofu Mapunda amewasititiza waamini kuwa “Hakuna anayeweza kumpenda Mungu kama hampendi jirani yake na ukimpenda Mungu na Jirani, umekamilisha Maandiko, na kwa kufanya hivyo unakamilisha yote aliyoamuru Mungu katika ukamilifu wake, na unakuwa na uhakika wa kuingia katika Ufalme wake na kushiriki uzima wa Milele.”  Askofu ameendelea kukazia kuwa “Tutambue kuwa kumpenda jirani ni njia nyingine ya kumpenda Mungu. Amri hizi mbili ni nguzo na msingi wa sheria zote. Ukivunja moja ya amri hizi mbili umevunja zote. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii yaani maandiko yote matakatifu. Ampendaye Mungu na jirani, rohoni ametulia na ana uhakika wa uzima wa milele. Mwishoni mwa maisha yake hapa duniani, Yesu aliwaalika wafuasi wake kuweka maisha yao katika kiini cha upendo kwa Mungu na jirani.

Upendo kwa Mungu na jirani usimikwe katika uhalisia wa maisha
Upendo kwa Mungu na jirani usimikwe katika uhalisia wa maisha

Baba Askofu pia amesititza kuwa upendo wetu uwe katika kulipenda Kanisa kama jumuiya ya waamini na mwili wa Kristo. Hivyo tunapaswa kushiriki kwa dhati kwa moyo katika maendeleo ya huu mwili wa Kristo kiroho na kimwili. Ushiriki katika ujenzi wa Makanisa na katika maendeleo mbalimbali ya Kanisa. Hivyo mtu atakuwa na amani kamili `pale atakapowajibika kama Mkristo na kutimiza wajibu wake kama mfuasi imara wa Kristo. Baba Askofu akimalizia mahubiri yake yaliyojikita kastika upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani, alisema, Dominika ya 29 ya Mwaka A wa Kanisa tupate nafasi ya kuutafakari upendo kama msingi wa kuishi vema kati yetu sisi kwa sisi lakini pia kama msingi wa kuishi vema katika mahusiano yetu na Mungu kwani ni upendo unaotusaidia kuzishika vema amri zake kwa kuishi kile kilicho kiini cha amri hizo. Baba Askofu pia alitumia nafasi hiyo kusititiza juu ya wamini kusali Rozari na hasa tunapofunga mwezi huu wa Rozari kuwa kusema Dominika hii ni ya mwisho katika mwezi huu wa Oktoba, mwezi ambao Kanisa limeutenga kama mwezi wa Rosari Takatifu na pia mwezi wa kuhamasisha maisha na utume wa Kanisa, yaani mwezi wa kuombea, kukuza ufahamu na kualika majitoleo kwa kazi za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Tuone kuwa Rozari ni sala nyepesi inayotupa nafasi ya kuutafakari upendo wa Mungu kwetu sisi na ukombozi wetu kutoka mikono ya adui shetani.

Rozari Takatifu ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu
Rozari Takatifu ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu

Kanisa hili lililojengwa kwa mwaka mmoja lilianza kujengwa Machi 17,2022 baada ya Kanisa lililokuwa linatumika kuwa kimechakaa na kuchoka kutokana na mbao zake kuliwa na mchwa na kupasuka kutokana na tetemeko la ardhi. Mpaka sasa limetumia Milioni 27,416,000 ikiwa mbali ya nguvu kazi. Leo Baba Askofu alipoweka jiwe la msingi pia ameomba mwakani aje alibariki na kutolea humo Kipaimara. Pia alitumia nafasi hiyo kubarikia Grotto ya Bikira Maria iliyogharimu Tsh. 4,378,000/= ambayo kwa kiasi kikubwa imehamasishwa na walei wakiongozwa na Dada Prisca Ibrahimu. Askofu Edward Mapunda aliwapongeza waamini wa Kigango cha Nkundi kwa majitoleo, sadaka na michango yao katika ujenzi wa Grotto na kuwaasa kuwa watu wa bidii katika Ibada kwa Mama Maria Mama wa Mungu na Mama yetu pia. Waamini wanaalikwa kuwa na utamaduni wa Sala na Ibada kwa Mama Bikira Maria, Mama wa Huruma aliye msaada na makimbilio ya wakosefu. Amewaasa waamini kujibidiisha katika Sala na Ibada kwa Mama Bikira Maria kwa kutenga muda na kufika mara kwa mara kwenye Grotto kusali kwa maombezi ya Mama Bikira Maria. Baba Askofu Edward Mapunda pia alipata nafasi ya kubariki eneo la shule ya Mt. Maria Josepha kigangoni hapo ambayo waamini hao wamejiwekea malengo ya kujenga madarasa mawili kila mwaka ili kuweza kupambana na adui watatu wa maendeleo ambao ni maradhi, ujinga na umaskini kwa kuwapa elimu bora na nzuri watoto wao. Askofu alipongeza juhudi kubwa za waamini hao kwa kuwa vyote hivyo yaani Kanisa, Grotto na shule vimejengewa kwa nguvu za wamini wenyewe wa ndani na nje ya Kigango cha Nkundi chenye waamini 207 na Jumuiya 11 ndani ya miaka miwili tu. Baba Askofu Edward Mapunda `pia alifanya harambee ya kuendeleza ujenzi huo ambapo Mifuko 184 ya saruji ilikusanywa. Mwisho Baba Askofu aligawa zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali ikiwemo soka ambapo kombe liliandaliwa na Ndugu Timothy Kifendi kwa heshima ya Mama Bikira wa Rozari katika kuhamsisha watu kusali na kupenda Rozari Takatifu na kuwaasa vijana kuendelea kuwa nguzo imara ya uinjilishaji na kuipenda imani yao kama Kristo alivyotupenda sisi.

06 November 2023, 11:06