Tafuta

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni, tarehe 22 Oktoba 2023 Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni, tarehe 22 Oktoba 2023   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Oktoba 2023

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni, tarehe 22 Oktoba 2023 linaelezea kwa muhtasari ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, Kardinali Protase Rugambwa, Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu, Jubilei ya Miaka 50 ya JNNK, AMECEA, Jubilei ya Miaka 155 Jimbo kuu la Songea na Miaka 125 Jimbo la Iringa, Mkataba wa Uboreshaji wa Bandari Tanzania.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., - Dar es Salaam

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 97 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa na Mama Kanisa Dominika tarehe 22 Oktoba 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Mioyo inayowaka moto, na miguu inayotembea. (Lk 24:13-35). Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anabainisha jinsi ambavyo katika kazi ya kimisionari Neno la Mungu huangaza na kubadili mioyo ya waamini. Kristo Mfufuka bado anabaki na kutembea na wafuasi wake ili wasikate tamaa. Umuhimu wa kulifahamu Neno la Mungu, Sakramenti ya Sadaka ya Yesu Msalabani, ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wawe tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kwanza kabisa kwa kujikita katika wongofu wa kimisionari tayari kushuhudia upendo wa Kristo kwa waja wake. Waamini wanaalikwa kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa uenezaji wa imani tayari kujikita katika safari ya kisinodi inayonogeshwa na maneno makuu matatu: umoja, ushiriki na utume. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuianza safari hii kwa mioyo inayowaka moto ili kuifanya mioyo mingine iwake kwa Neno la Mungu, ili kuifungua mioyo ya wengine kwa Kristo katika Ekaristi sanjari na kukoleza njia ya amani na wokovu ambao Mwenyezi Mungu, katika Kristo Yesu, amewakirimia binadamu wote. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, tarehe 22 Oktoba 2023 linaelezea kwa muhtasari ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, Kardinali Protase Rugambwa, zawadi ya Mungu kwa familia ya Mungu nchini Tanzania, mwaliko kwa familia ya Mungu kujifunza wito wa umisionari wake mahiri na wa kuigwa. Maaskofu wanazungumzia kuhusu Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu, lililonogeshwa na kauli mbiu “Kongamano la Kondoa: Ushirika na Utunzaji wa Mazingira.

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Siku ya Kimisionari 2023
Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Siku ya Kimisionari 2023

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, JNNK: Miaka 50 ya Kujenga Kanisa kama Familia ya Mungu katika Nchi za AMECEA.” Lengo ni kukuza ufahamu wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo kama ufahamu mpya wa kuwa Kanisa sanjari na kuendelea kukua na kustawi kama wafuasi wamisionari. Maaskofu wanatoa pongezi za dhati kabisa kwa Jimbo kuu la Songea kuadhimisha Jubilei ya Miaka 125 ya uinjilishaji na Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji Jimbo Katoliki Iringa. Maaskofu wanaandika kuhusu kuwekwa wakfu na hatimaye, kusimikwa kwa Askofu Thomas John Kiangio wa Jimbo Katoliki la Tanga. Hatimaye ni tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuhusu Mkataba kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na “Emirate of Dubai” juu ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa maendeleo na uboreshaji wa bandari za Bahari na Maziwa nchini Tanzania. Ni vyema, ni busara na ni hekima Serikali kuwasikiliza wananchi, maana kutowasikiliza ni kujiletea matatizo makubwa zaidi siku za usoni kwani wananchi hawahawa watavitaka vizazi vijavyo kuondokana na unyonywaji huu, kama tunavyoona kwenye kesi nyingi zinazoendelea sasa hivi katika mahakama za kibiashara za kimataifa dhidi ya mikataba iliyovunjwa na Serikali ya Tanzania. Tukumbuke mikataba ya madini miaka ya ’90 viongozi wa dini na asasi za kiraia walipinga uwekezaji wa namna hii, na Serikali ikatumia mamlaka zake kuridhia mikataba hii na sasa hivi tunashuhudia ikivunjwa na nchi kulipa fidia kubwa. Tunasisitiza kwamba SAUTI YA WATU NI SAUTI YA MUNGU, “Vox Populi, Vox Dei” hivyo basi kuwasikiliza wananchi na kufanya maamuzi kadiri wanavyotaka kutailetea serikali heshima kubwa ya kuwa sikivu kwa watu. Kinyume cha haya, Mwenyezi Mungu anatuonya kupitia Nabii Yeremia anaposema: “Kama kapu lililojaa ndege walionaswa, ndivyo nyumba zao zilivyojaa mali za udanganyifu. Ndiyo maana wamekuwa watu wakubwa na matajiri, wamenenepa na kunawiri. Katika kutenda maovu hawana kikomo hawahukumu yatima kwa haki, wapate kufanikiwa, wala hawatetei haki za maskini” (Yeremia 5:27-28). Hivyo tukiwajibika kimaadili, tunaona ni jukumu la serikali kusikiliza wananchi wanaotaka mkataba huu ufutwe. Kwa kuwa tumeonesha kuwa Tanzania tumeshawekeza na kuendeleza bandari, reli na bandari za nchi kavu; ni wajibu miradi hii tuiendeshe Watanzania wenyewe huku tukikaribisha ubia tunaoudhibiti wenyewe. Hiki ndicho wananchi wanachokililia kusudi tujenge uwezo wetu wenyewe. Kwa vile tumegundua mapungufu yetu ya uendeshaji wa bandari, tunaweza kujizatiti kurekebisha mapungufu hayo wakati njia za kiuchumi zikibaki mikononi mwetu. Kwa sababu hizo na maelezo yote ya hapo juu, sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hatuungi mkono Mkataba huu. Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linazidi kuwaalika watu wa Mungu kujibidiisha katika kutoa kwa ukarimu Zaidi kwa ajili ya ufanisi wa shughuli za kimisionari katika Kanisa.

Wanawake Wakatoliki Tanzania wawe wajenzi wa familia ya Kikristo
Wanawake Wakatoliki Tanzania wawe wajenzi wa familia ya Kikristo

Ndugu Wapendwa, Katika Dominika ya Misioni ya mwaka huu, Baba Mtakatifu anatualika kutafakari kwa pamoja wazo hili kuu: "Mioyo inayowaka, miguu katika mwendo". Ni wazo ambalo linazaliwa kutoka katika simulizi juu ya safari ya wafuasi kuelekea Emau, kadiri ya Injili ya Luka 24:13-35. Katika kukutana na Kristo katika Neno na katika kuumega mkate, wafuasi wanapata matumaini mapya, ambayo yanamgusa kila mfuasi mmisionari hata leo hii. Kadiri ya Injili tajwa, mabadiliko hayo yanaelezwa katika taswira hizi: mioyo yao iliwaka ndani yao waliposikia Maandiko yakielezwa na Yesu, macho yao yalifunguliwa walipomtambua, na hatimaye, miguu yao ikashika njia.

1.     Mioyo yetu iliwaka ndani yetu “alipotufafanulia Maandiko”. Katika kazi ya umisionari, Neno la Mungu huangaza na kubadilisha mioyo. Njiani kutoka Yerusalemu kwenda Emau, mioyo ya wafuasi hao wawili ilikuwa imedhoofika kwa sababu ya kifo cha Yesu (rej. aya 17, 21). Bwana Mfufuka anatokea na kutembea pamoja nao (aya 15) kama afanyavyo kwetu hata sasa, licha ya udhaifu na ukosefu wetu wa imani. Hata katika magumu tunayopitia katika uinjilishaji tutambue kuwa utume huu ni wake na tumkimbilie, kwani yeye ni mkuu kuliko shida zetu zote. Sisi ni "watumishi tusio na faida" (taz. Lk 17:10). Ni katika Msingi huu, Baba Mtakatifu anawatia moyo wale wote wanavumilia magumu mbalimbali katika kazi ya umisionari. Daima tukumbuke kuwa Yesu mwenyewe ndiye Neno lililo hai. Hivyo, tujibidishe kumfahamu na kuwa tayari kuambatana naye ili, kwa nguvu na hekima ya ROHO wake aifanye mioyo yetu kuwaka ndani yetu; na atuangazie na kutugeuza, ili tuweze kutangaza fumbo lake la wokovu kwa ulimwengu mzima.

2. Macho yetu “yalifunguliwa na kumtambua” katika kuumega mkate. Yesu katika Ekaristi ndiye chanzo na kilele cha utume. Mioyo ya Wafuasi wa Emau iliwaka kwa ajili ya neno la Mungu, hali kadhalika macho yao yalifumbuliwa na wakamtambua katika kuumega mkate hasa kupitia ishara hizi muhimu sana alizozifanya Yesu: alitwaa mkate, akaubariki, akaumega na kuwapa. Kristo Mfufuka, basi, ndiye anayeumega mkate na, wakati huo huo, ndiye mkate wenyewe, unaomegwa kwa ajili yetu. Hivyo, kila mfuasi mmisionari ameitwa kuwa, kama Yesu na ndani yake, kwa njia ya kazi ya Roho Mtakatifu, mmoja anayeumega mkate na mkate unaomegwa kwa ajili ya ulimwengu. Tunaitwa sio tu kuumega mkate wetu wa vitu halisi kwa masikini, zaidi sana mkate wa Ekaristi ambaye ni Kristo Mwenyewe na hiyo ni kazi ya utume ulio bora zaidi. Hivyo, mioyo yetu na itamani daima ushirika wa Yesu, ikirudia ombi la bidii la wafuasi wawili wa Emau, hasa katika saa za jioni katika kuabudu Ekaristi: “Kaa nasi, Bwana” (Taz. Lk. 24:29).

3. Miguu yetu ikiwa tayari njiani, kwa furaha ya kuwaambia wengine juu ya Kristo Mfufuka. Ujana wa milele wa Kanisa ambalo daima linasonga mbele. Baada ya macho yao kufunguliwa na kumtambua Yesu “katika kuumega mkate”, wafuasi “waliondoka bila kukawia na kurudi Yerusalemu” (taz. Lk 24:33) kuwatangazia wengine furaha ya kukutana na Bwana. Tukumbuke kuwa kila mtu ana haki ya kupokea Injili, zaidi sana katika ulimwengu wetu wa leo unaopitia changamoto nyingi. Sisi sote ni wamisionari na hivyo upendo wa Kristo utubidishe daima kutimiza wajibu huu (2Kor 5:14) unaotudai majitoleo ya kiroho na ukarimu wa vitu halisi. Aidha, tuunge mkono utume wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari yaliyokabidhiwa dhamana ya kukuza ushirikiano wa kimisionari kwa sala na majitoleo (rej. Dominika ya Misioni). Hivyo, sote tunaalikwa kudumisha ushirikiano huu wa kimisionari na kuwa tayari kuanza tena safari (missio ad gentes), tukiangazwa na kukutana kwetu na Bwana Mfufuka na kuchochewa na Roho wake.

Kardinali Protase Rugambwa ameandika historia mpya kwa Kanisa la Tanzania
Kardinali Protase Rugambwa ameandika historia mpya kwa Kanisa la Tanzania

KARDINALI MPYA PROTASE RUGAMBWA – ZAWADI YA MUNGU KWETU. Kanisa la Katoliki nchini Tanzania, tunayo furaha kubwa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi zake mbalimbali anazotukirimia siku hata siku, kwa namna ya pekee wakati huu kwa zawadi kubwa ya Kardinali Mpya. Itakumbukwa kuwa, Dominika ya tarehe 09 Julai, 2023, Baba Mtakatifu Fransisko aliwateua Makardinali wapya 21 miongoni mwao ni Kardinali Protase Rugambwa kutoka nchini kwetu Tanzania. Makardinali wapya wamesimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali uliofanyika tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Hadi wakati wa uteuzi wake, Kardinali Protase ni Askofu Mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Hakika, ahadi ya Bwana inaendelea kutimia kwetu: “Nitawapeni Wachungaji wanaoupendeza moyo wangu” (Yer 15:3). Hivyo, tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kama Mtume Paulo anavyotualika: “Kwa sababu hiyo, sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma…” (1The 2:13).  Ni vema ikakumbukwa kuwa Kardinali Protase Rugambwa, alizaliwa tarehe 31 Mei 1960 huko Bunena-Bukoba nchini Tanzania na kupata Daraja Takatifu ya Upadri kutoka mikononi mwa Baba Mtakatifu - Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Tanzania tarehe 2 Septemba 1990 na kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara. Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatikano. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 18 Januari 2008 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, na tarehe 26 Juni 2012 akateuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Kongregasio ya Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 9 Novemba 2017 Baba Mtakatifu Fransisko akamteuwa kuwa Katibu wa Kongregasio ya Uinjilishaji wa Watu (kwa sasa Dikasteri ya Uinjilishaji), utume alioufanya hadi tarehe 15 Machi 2023. Mnamo tarehe 13 Aprili 2023, Baba Mtakatifu alimteua kuwa Askofu mkuu mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania. Kwetu sisi, Kanisa Katoliki la Tanzania, pamoja na kumshukuru Mungu kwa zawadi hii kubwa na ya pekee, tunawiwa kumpongeza sana Mwadhama Kardinali Mpya kwa utumishi wake uliotukuka katika Kanisa la Mungu hadi sasa. Kwa namna ya pekee sana, tunawiwa kujifunza kwake mengi kuhusiana na wito wa umisionari. Historia ya utume wake ni uthibitisho wa kutosha kwamba amekuwa mmisionari mahiri hivi kwamba kwa nafasi mbalimbali amepewa na Kanisa dhamana kubwa ya kusimamia uratibu wa kazi za kimisionari za Kanisa la kiulimwengu (Universal Church). Utumishi wake katika Dikasteri ya Uinjilishaji (kama inavyotambulika hivi sasa) kwa miaka mingi hivyo, ni udhihirisho kuwa kweli ni mmisionari mahiri na wa kuigwa. Tunaalikwa kujifunza kwake na zaidi sana tumwombee ufanisi zaidi katika utume unaoendelea hususan katika dhamana hiyo kubwa aliyopewa na Mama Kanisa.

Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu, Jimbo Katoliki Kondoa
Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu, Jimbo Katoliki Kondoa

MAADHIMISHO YA KONGAMANO LA KITAIFA LA UTOTO MTAKATIFU. Mnamo tarehe 22 hadi 26 Juni, 2023 Kanisa Katoliki nchini Tanzania liliadhimisha Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu lililofanyika katika Jimbo Katoliki la Kondoa. Kongamano hili liliongozwa na Kauli Mbiu isemayo: “Kongamano Kondoa – Ushirika na Utunzaji wa Mazingira”. Tena, lilihudhuriwa na washiriki wapatao 5,562 kutoka katika majimbo yote 34 ya hapa nchini Tanzania. Miongoni mwa washiriki ni watoto wa Utoto Mtakatifu wapatao 4,707, Walezi wapatao 792, Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa wa Majimbo na Wasaidizi wao wapatao 63 (wakiwemo mapadre, watawa na walei). Tukio hili muhimu sana lilihudhuriwa kwa uwakilishi na Mababa Askofu wapatao kumi, yaani: Mhashamu Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga – Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Askofu Mkuu wa Mbeya, Askofu Mkuu Damian Denis Dallu – Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari Tanzania na Askofu Mkuu wa Songea, Baba Askofu Bernardin Mfumbusa (Askofu wa Kondoa na mwenyeji wetu), Baba Askofu Agapit Ndorobo – Askofu wa Mahenge, Baba Askofu Augustino Shao, CSSp – Askofu wa Zanzibar, Baba Askofu Liberatus Sangu – Askofu wa Shinyanga, Baba Askofu Anthony Lagwen – Askofu wa Mbulu, Baba Askofu Filbert Mhasi – Askofu wa Tunduru Masasi, Baba Askofu Prosper Lyimo  - Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Arusha, Baba Askofu StephanoMusomba – Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Maadhimisho haya ya Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu yalizinduliwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Rais wa Mashirika ya Kipapa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Damian Denis Dallu na tafakari ya siku hiyo ilitolewa na Askofu Mwenyeji – Baba Bernardin Mfumbusa. Katika Homilia yake aliwakaribisha kwanza wageni wote jimboni kwake Kondoa. Kadhalika alitanabahisha nafasi ya Kongamano hilo kuwa ni fursa muhimu sana ya umisionari na malezi ya watoto wetu kote nchini na ulimwenguni kwa ujumla. Kisha, lilifuatia zoezi la kupokea Msalaba kutoka Kanda ya Tabora ambao ndio walikuwa wenyeji wa Kongamano lililotangulia kabla ya hili.

Katika kipindi hiki cha Kongamano, mada mbalimbali ziliwasilishwa hasa kwa makundi makuu mawili, yaani watoto na walezi (wa ngazi zote). Baadhi ya mada hizo ni pamoja na: Ushirika – iliyowasilishwa na Padre Edward Ijengo toka Kondoa, Mazingira (na Ndg. Sulle OFM Cap.), Katekesi juu ya Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu (na Pd. Zefrine Msafiri), Ulinzi na Usalama wa Mtoto (na Pd. Paulino Mligo), Malezi na Makuzi ya Watoto (na Bwana na Bibi Paschal Maziku). Sambamba na mada hizi kulikuwa pia na fursa ya Watoto kushirikishana vipaji vyao kwa njia ya michezo mbalimbali. Hatimaye, Kongamano lilihitimishwa siku ya Dominika ya Tarehe 26 Juni, 2023 kwa Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji, Askofu Mkuu Damian Dallu na homilia katika adhimisho hilo ilitolewa na Askofu Mkuu Gervas M. Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Askofu Mkuu wa Mbeya. Shukrani: Kwa niaba ya Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ninapenda kutoa shukrani za pekee sana kwa wale wote waliofanikisha maadhimisho ya Kongamano hili tangu Mababa Askofu kwa ujumla wao, Jimbo wenyeji (Kondoa), Wazazi, Walezi wa Makundi yote (mapadre, watawa na walei) na zaidi sana watoto wa Utoto Mtakatifu walioshiriki moja kwa moja na wale wote walioungana na watoto wenzao kwa sala na kwa njia ya kimtandao katika kufuatilia maadhimisho hayo. Mungu awabariki nyote na kuwafanikisha katika kazi ya kuwalea Watoto Wamisionari.

Jubilei ya Miaka 50 ya JNNK-AMECEA
Jubilei ya Miaka 50 ya JNNK-AMECEA

MAADHIMISHO YA JUBILEI YA MIAKA 50 YA JUMUIYA NDOGO NDOGO - AMECEA. Hakika ni Neno Jema kumshukuru Mungu (Zab. 92:1), kwa namna ya pekee mwaka huu 2023, ambapo Kanisa Katoliki Ukanda wa AMECEA linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo kama kielelezo chetu cha Kanisa mnamo 1973. Maadhimisho haya yamezinduliwa rasmi tangu mwezi Julai mwaka huu na yatadumu kwa kipindi cha mwaka mzima hadi Julai 2024. ili kuyafanya maadhimisho haya yawe na mguso wa pekee wa kiimani na sio tu kubaki kama tukio la kihistoria, imeandaliwa Kauli Mbiu mahususi ambayo inaonesha dira ya maadhimsho haya inayosema: “Jumuiya Ndogondogo za Kikristo (JNNK): Miaka 50 ya Kujenga Kanisa kama Familia ya Mungu katika Nchi za AMECEA”. Aidha, yameainishwa matukio mengine kwa lengo hilo hilo ambayo yanajumuisha: tathimini ya mafanikio na changamoto zinazozikabili JNNK katika maeneo yetu; kufanya mapitio ya miongozo iliyopo juu ya JNNK kadiri ilivyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania; na kujiwekea mikakati ya uimarishaji na ukuzaji wa JNNK nchini Tanzania baada ya Jubilei, tukitaja kwa uchache. Hima tuungane pamoja katika kuyatimiza malengo haya! Kila mmoja wetu anaalikwa kutambua kuwa maadhimisho haya ni fursa nzuri ya kukuza imani yetu. Tunapomshukuru Mungu kwa zawadi hii ya JNNK – ambazo Mababa Askofu wa Ukanda wetu wa AMECEA walizitambulisha kwetu kama njia mpya ya kuwa Kanisa, ni nafasi pia kwetu ya kukua na kustawi kama wafuasi wamisionari mahiri kama Baba Mtakatifu anavyotuhimiza katika Ujumbe wake wa Dominika ya Kimisionari kwa mwaka huu 2023. Kwa kuzingatia kuwa JNNK ni tunda la Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican (1962-1965), tunaalikwa kuwaombea Mababa wa Mtaguso na zaidi sana Maaskofu-Waasisi wa JNNK ambao miaka takribani nane baada ya Mtaguso, kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, walibuni mfumo huu mpya wa kichungaji ndani ya Kanisa. Nasi tujione kuwa ni zamu yetu sasa kuiendeleza tunu hii njema waliyotuachia. Mungu atubariki na kutuongoza, ili kupitia JNNK tuweze kustawisha roho ya kisinodi inayojisimika katika Ushirika, ushiriki na umisionari. Kwa njia ya JNNK tuendelea kusafiri pamoja kama Familia ya Mungu.

Miaka 155 Jimbo Kuu la Songea na Miaka 125 Jimbo Katoliki la Iringa.
Miaka 155 Jimbo Kuu la Songea na Miaka 125 Jimbo Katoliki la Iringa.

PONGEZI KWA JIMBO LA IRINGA NA JIMBO KUU LA SONGEA KWA KUADHIMISHA JUBILEI YA MIAKA 125 YA UINJILISHAJI MWAKA HUU: Katika Ujumbe wa Dominika ya Misioni mwaka huu 2023, Baba Mtakatifu Francisko anatualika, pamoja na mambo mengine, kukumbuka na kuendelea kuthamini mchango wa wafuasi wamisionari wa nyakati mbalimbali. Kwetu Kanisa la Tanzania, tunawakumbuka wamisionari wa kwanza ambao walituletea Imani Katoliki ambayo imedumu nasi kwa ziadi ya miaka 155 sasa. Kwa namna ya pekee, mwaka huu tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya wamisionari ambao waliinjilisha majimbo ya Iringa na Songea ambao yanafanya jubilee ya miaka 125 tangu kupokea Imani Katoliki. Tunamshukuru Mungu pamoja na Familia ya Mungu katika majimbo haya na tunawapongeza kwa makuu haya ambayo Mwenyezi Mungu amewatendea. Kadiri ya Kalenda ya Mwaka 2023 ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Jimbo Katoliki la Iringa linatazamia kufanya maadhimisho ya Jubilei hiyo tarehe 09 – 10 Septemba, 2023 ilihali Jimbo Kuu la Songea limefanya maadhimisho yake tarehe 30 Septemba – 01 Oktoba 2023. Ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuungana na Familia ya Mungu ya majimbo haya kumshukuru Mungu na kuwaombea Mwanzo Mpya wa maisha yao ya Imani baada ya Jubilei hizo za miaka 125. Pamoja nao tunawaombea Wamisionari – Wabenediktini ambao ndio walipeleka imani katika maeneo haya. Aidha, tunawaombea Mababa Askofu ambao walipewa dhamana ya kuyaongoza majimbo haya kwa vipindi mbalimbali, kwa namna ya pekee maaskofu wa sasa: Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Iringa – tukimtakia pia heri katika maadhimsho yake ya miaka 50 ya Daraja ya Upadre na Baba Askofu Mkuu Damian Dennis Dallu wa Jimbo Kuu la Songea. Tuwaombee mapadre, watawa na waamini walei wote wa majimbo haya ili maadhimisho haya ya Jubilei yawaletee matunda mengi ya kiroho na kimwili. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau (Lk. 24: 13-35), nanyi kwa nafasi mbalimbali mmekutana na Bwana Mfufuka. Hivyo, mioyo yenu ikiwa inawaka ndani yenu na macho yenu yakiwa yamefumbuliwa, hima shikeni njia sasa kuendelea kuitangaza habari njema. Wamisionari wa kwanza wamekwishamaliza ngwe yao, sasa ni zamu yenu. Roho wa Mungu awabariki na kuwaongoza ili muwe kweli wamisionari mahiri wa nyakati zetu. 

Askofu Thomas John Kiangio wa Jimbo Katoliki Tanga
Askofu Thomas John Kiangio wa Jimbo Katoliki Tanga

KUWEKWA WAKFU NA KUSIMIKWA ASKOFU MPYA WA JIMBO KATOLIKI LA TANGA: Familia nzima ya Mungu ya Kanisa Katoliki Tanzania, tunaalikwa kuungana na wanajimbo Katoliki la Tanga kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa aliyowapatia ya Mchungaji Mkuu wa Jimbo, Baba Askofu Thomas John Kiangio. Itakumbukwa kuwa, Jimbo Katoliki la Tanga limekuwa wazi tangu tarehe 20.12.2020 kufuatia kifo cha aliyekuwa askofu wake wakati huo, Mhashamu Baba Askofu Anthony Mathias Banzi. Tangu kipindi hicho, familia ya Mungu ya Jimbo Katoliki la Tanga imedumu katika sala na matumaini makubwa ya kumpata Mchungaji Mkuuu mwingine, hadi tarehe 07 Juni 2023 ambapo Baba Mtakatifu Fransisko alimteua rasmi Mheshimiwa Padre Thomas John Kiangio kuwa Askofu Mpya wa Jimbo hilo na hatimaye kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi siku ya terehe 03 Septemba, 2023 katika Kanisa Kuu la Jimbo la Tanga. Hadi wakati wa uteuzi wake, alikuwa anahudumu kama Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tanga, dhamana ambayo alikabidhiwa rasmi tangu tarehe 24.12.2020. Historia ya Maisha yake hakika imesheheni mengi. Baba Askofu Mpya Thomas John Kiangio alizaliwa tarehe 17 Machi 1965 katika Kijiji cha Mazinde Ngua, Wilaya ya Korogwe katika Mkoa wa Tanga. Wazazi wake ni Baba John Mussa Kiangio na Mama Paulina Ally Suba. Safari yake ya masomo na majiundo ya Kikasisi ilianzia katika Seminari Ndogo ya Mt. Yosefu – Soni (1982), baadaye Seminari Ndogo ya Mt. Petro iliyoko jimboni Morogoro (1987 -1989). Aliendelea na malezi na majiundo yake ya Kikasisi katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Antony, Ntungamo Jimbo Katoliki la Bukoba (1989-1991) na Karoli Lwanga – Segerea, Jimbo Kuu la Dar es Salaam (1991-1997). 

Kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kwa Askofu Kiangio, Jimbo Katoliki la Tanga
Kuwekwa wakfu na hatimaye kusimikwa kwa Askofu Kiangio, Jimbo Katoliki la Tanga

Aidha, Mazoezi ya Mwaka wa Kichungaji aliyafanyia Parokia ya Mlingano, Jimbo Katoliki la Tanga (1994-1995), na ndani ya kipindi hicho alipewa fursa ya kushiriki kozi ya Shughuli za kichungaji, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Mkoani Mwanza. Hatimaye, alipewa Daraja Takatifu ya Ushemasi tarehe 01.01.1997 katika Kanisa Kuu la Mt. Anthony Tanga na baadaye Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 16.07.1997 katika Parokia ya Mama Bikira Maria Mama wa Mateso, Mazinde Ngua.   Kuhusu utume alioufanya kabla ya kuwa Askofu, yako mengi ya kujifunza toka kwake. Baada ya upadrisho wake alihudumu katika nafasi na sehemu mbalimbali katika Kanisa: Paroko Msaidizi katika Parokia ya Ekaristi Takatifu, Lushoto (1997-1998); baadaye akateuliwa kuwa mlezi, mwalimu na Gambera Msaidizi wa Seminari Ndogo ya Mt. Yosefu – Soni, Tanga (1998-1999). Baadaye kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2004 alitumwa kuendelea na masomo ya juu Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko jijini Roma. Baada ya kurejea toka masomoni, aliteuliwa na kutumwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yosefu Soni - Tanga (2005 – 2013). Baadaye kati ya mwaka 2013 hadi mwaka 2020 aliteuliwa kuwa Katibu wa Jimbo na kati ya mwaka 2020 hadi kuteuliwa kwake aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Tanga kufuatia kifo cha Askofu Anthony Mathias Banzi aliyefariki dunia tarehe 20 Desemba 2020. Kwa neema za Mungu, siku ya Dominika ya tarehe 03 Septemba, 2023, Baba Askofu Mpya Thomas John Kiangio aliwekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa tano wa Jimbo Katoliki la Tanga. Tuendelee kumuombea kwa Mungu ili aweze kulichunga na kuliongoza vema kundi alilokabidhiwa na Bwana. Kadhalika, tumuombee ili aweze kuiishi vema dira aliyoichagua katika uaskofu wake: Upendo, Amani na Umoja.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania

TAMKO LA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA (TEC) KUHUSU MKATABA KATI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA “EMIRATE OF DUBAI” JUU YA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA MAENDELEO NA UBORESHAJI WA BANDARI ZA BAHARI NA ZA MAZIWA TANZANIA. “SAUTI YA WATU, SAUTI YA MUNGU”

UTANGULIZI: “Ndugu zangu nawasihi mjihadhari na wote wanaoleta mafarakano na vipingamizi kinyume cha mliyopokea (mapokeo). Waepukeni. Kwa maana watu kama hao … wanatumikia tamaa zao kwa kutumia maneno matamu ya kudanganya kupotosha mioyo ya watu wanyofu” (Warumi 16:17-18).

Sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania,

1.            Tunatambua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo - (a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii; (b) lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; (c) Serikali itawajibika kwa wananchi; (d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba” (Rejea Ibara 8, ibara ndogo 1); hivyo ni lazima Serikali iwasikilize wananchi.

2.            Kwa kutambua kwamba mamlaka ya Serikali yanatoka kwa wananchi, sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Tanzania, tumezisikiliza sauti zao, tumeisikiliza Serikali, na wadau wengine wa maendeleo, tukasali na kutafakari, na hivi tunatamka ifuatavyo:

2.1.          Tukizingatia yaliyojiri na yanayoendelea katika jamii ya Tanzania tangu Mkataba huu uwekwe hadharani, taharuki kutokana na mijadala ya hadharani, mijadala ambayo imeligawa Taifa.

2.2.          Na tukizingatia kuwa si mara yetu ya kwanza kutoa matamko kama hili kuhusu masuala yanayohusu jamii yetu;

2.3.          Na kwa kurejea ibara za Mkataba tajwa hapo juu ambazo zina utata kwa uwekezaji wenye tija kwa Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo;

2.4.          Na tukiwa tunayashuhudia mashinikizo ya marekebisho ya sheria yanayokusudiwa kufanywa ili kuulinda Mkataba huu ambao Bunge la Tanzania limeuridhia hali tukiona ukiukwaji wa utawala wa sheria.

Maaskofu Katoliki Tanzania hawakubaliani na Mkataba wa Bandari Tanzania
Maaskofu Katoliki Tanzania hawakubaliani na Mkataba wa Bandari Tanzania

KWA HIYO:

3.            Tukisukumwa na dhamiri iliyo na lengo la kulinda rasilimali, mshikamano, amani, uhuru, na umoja wa kitaifa; tunathubutu kusema kuwa baada ya miaka 63 ya uhuru wa nchi hii, wananchi hawajapenda kuiachia bandari ya Dar es Salaam apewe mwekezaji mmoja aiendeshe, kwa vile Watanzania wenyewe wana uzoefu wa kuiendesha.

4.            Tunaona kuwa ni muhimu sasa kuendelea kujenga uwezo wa KITAIFA, kwa sekta zetu za umma na binafsi za Kitanzania tukiweka ubia na makampuni yenye ubobezi wa kiteknolojia kutoka sehemu mbalimbali duniani, na siyo ubia wa kutoka nchi moja, tukitumia mikataba yenye tija tuliyoandaa wenyewe juu ya mashirika yetu ya kibiashara.

5.            Tunakiri kuwa utaratibu wa Serikali kuweka wawekezaji kutoka nje tu katika njia kuu za uchumi umetukosesha uendelevu wa vitega uchumi vyetu hasa pale wawekezaji wanapoondoka. Hivyo, bandari ikiwa ni moja ya njia kuu na ya asili ya uchumi inayotuwezesha kufanya biashara kubwa na mataifa mbalimbali, ni lazima iendelee kuwa biashara ya Watanzania wenyewe na ibaki mikononi mwetu hata kama tunaingia ubia wenye tija.

6.            Kwa kurejea jitihada tulizofanya kuelewa Mkataba huu na kutoa ushauri wetu ambao haujazaa matunda mpaka sasa, na tukirejea mikutano yetu na Serikali katika ngazi za juu, ya tarehe 12 na 26 Juni mwaka huu 2023:

6.1.       Tumefuatilia kwa umakini mijadala, maoni, mapendekezo na vilio vya wananchi walio wengi, ambao ni wamiliki wa bandari na rasilimali zote, na tumetambua kuwa wananchi walio wengi hawautaki Mkataba huu ambao unampa mwekezaji wa nje mamlaka na haki ya kumiliki njia kuu za uchumi kama zilivyobainishwa kwenye Mkataba huu.

6.2.       Tumebaini kuwa kama nchi tumeshawekeza na kuendeleza bandari, reli, na bandari kavu huku tukiziendesha wenyewe. Hii ndiyo shauku ya wananchi, kusudi tuendelee kujenga uwezo wetu. Hali kadhalika, tumegundua mapungufu yetu ya uendeshaji wa bandari; vile vile tunao uwezo wa kuendelea kujizatiti kurekebisha mapungufu yanayojitokeza, wakati njia za kiuchumi zikibaki mikononi mwetu.

6.3.       Kuna mifano tosha jinsi Watanzania tulivyoweza kujenga uwezo katika kuendesha mabenki kama vile NMB na CRDB, taasisi nyeti za umma na za binafsi na kadhalika.

7.            Sasa kwa vile wananchi walio wengi hawataki uwekezaji wenye masharti mabovu kama haya katika bandari zetu zote; na kwa kuwa Serikali inawajibika kwa wananchi, lazima viongozi wasikilize   sauti ya watu, kwani sauti yao ni sauti ya Mungu.

8.            Historia imetufundisha kuwa kupuuza sauti ya wananchi kuhusu mikataba kwa siku za nyuma, kumeisababishia nchi hasara kubwa za kiuchumi, ukosefu wa ajira, na mapato ya kuendeshea huduma muhimu kama vile afya, maji na elimu. Tunashuhudia sasa Serikali kutokuwa na uwezo wa kuajiri na kulipa wafanyakazi wa kutosha katika sekta za elimu na afya ijapokuwa wahitimu wa fani hizo wako mitaani bila ajira. Hii ni kwa sababu vyanzo vikubwa vya mapato, mathalani migodi ya madini, vimemilikiwa na kuendeshwa na wawekezaji kutoka nje kwa mikataba mibovu.

9.            Kupuuza sauti ya wananchi juu ya uwekezaji usiosikia sauti yao kumewaletea pia wananchi wa maeneo wanayoishi mateso, kama inavyoonekana kwa jamii za Wamasai wa Loliondo, ambao haki zao za kiutamaduni na kijamii zimekiukwa. Uwekezaji umepewa kipaumbele kisicho na tija na raia wa Kimasai wameachwa wakiteseka.

10.        Tumeutafakari kwa makini Mkataba huu. Mkataba huu umechochea mgawanyiko wa wananchi katika kupambana na ukiukwaji mkubwa wa utawala wa sheria, kutozingatiwa uhuru wa taasisi za kidemokrasia na mwingiliano wa mihimili ya dola hasa Serikali na Bunge na sasa Mahakama inanyemelewa. Kama Watanzania tunapenda kusema kwamba bila uhuru wa taasisi hizi na utawala wa sheria tutaliangamiza Taifa.

11.        Ikumbukwe kwamba, kutokana na mjadala mpana wa suala hili la mwekezaji mmoja kwenye bandari za Tanzania, wananchi wenye mawazo tofauti hawajui wamwendee nani ili misimamo yao iweze kusikilizwa na kuzingatiwa; kwani Wabunge ambao ni wawakilishi wao wamewatelekeza kwa kufungamana na mwekezaji mmoja, kutokana na Bunge kuridhia Mkataba huu mnamo tarehe 10 mwezi Juni, 2023.

12.        Hivyo, sisi Maaskofu Katoliki Tanzania wenye jukumu la kusimamia ustawi wa kila mwanadamu tunamwomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mamlaka aliyo nayo asitishe wasilisho la ridhio hili kwa upande wa pili, na vile vile Bunge nalo lifute ridhio la Mkataba huu unaolalamikiwa.

13.        Makubaliano haya ya Kiserikali (Inter-Governmental Agreement - IGA) yana hatari zifuatazo kwa nchi yetu:

13.1.      Kuharibu umoja na amani ya nchi yetu. Tukumbuke amani ikivunjika, yaweza kurudi tena baada ya jitihada ya vizazi vingi. Nchi jirani kadhaa zimethibitisha hili.

13.2.      Rasilimali za nchi zinazolindwa kwa pamoja kuwanufaisha baadhi ya raia na hivyo kuleta ubaguzi wa kiuchumi kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 27 Ibara ndogo ya 1, inayosema “Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi …”

14.        Ibara zifuatazo za Mkataba huu zina matatizo yatakayosababisha nchi kutofikia uhuru wa kiuchumi (economic independence):

14.1.      Ibara ya 2 (1): inayohusu lengo la Mkataba huu ambalo ni kuweka utaratibu unaoibana Tanzania kisheria katika kuendeleza, kuboresha na kuendesha bandari zote za bahari na maziwa, maeneo maalum ya uwekezaji, maeneo ya usafirishaji wa mizigo, na maeneo mengine ya kiuchumi.

14.2.      Ibara ya 4: inayohusu wigo wa Mahusiano na Utekelezaji unaoitaka Serikali ya Tanzania kuwajibika kuijulisha Dubai kila fursa ya uwekezaji inapojitokeza. Hii    inakinzana na baadhi ya sheria za nchi yetu, kwa mfano sheria ya ushindani na ile ya manunuzi.

14.3.      Ibara ya 5: ambapo DP World imepewa haki ya kuendeleza, kusimamia na kuendesha miradi pekee yake, wakati Tanzania inabaki na wajibu wa kumwezesha kufurahia haki hiyo.

14.4.      Ibara ya 6: inayoitaka Tanzania kuwajibika kuipatia DP World vibali na vivutio vya kutekeleza miradi yake kama Serikali. Hii inapingana na baadhi ya sheria za kiutaratibu.

14.5.      Ibara ya 7: inayoitaka Serikali kuwajibika kutoa mamlaka yanayotakiwa na mwekezaji bila ucheleweshaji.

14.6.      Ibara ya 8:  Haki ya kutumia ardhi ambapo Mkataba unasababisha uvunjifu wa sheria za ardhi na sheria zinazohusu masuala ya ardhi.

14.7.      Ibara ya 10: Usiri wa Mkataba ambapo Mkataba unazuia mamlaka nyingine kama TAKUKURU /BUNGE kufuatilia mikataba.

14.8.      Ibara za 23 na 24: zenye ugumu wa kujitoa kwenye Mkataba.

Sauti ya watu, Sauti ya Mungu
Sauti ya watu, Sauti ya Mungu

HITIMISHO: Ni vyema, ni busara na ni hekima Serikali kuwasikiliza wananchi, maana kutowasikiliza ni kujiletea matatizo makubwa zaidi siku za usoni kwani wananchi hawahawa watavitaka vizazi vijavyo kuondokana na unyonywaji huu, kama tunavyoona kwenye kesi nyingi zinazoendelea sasa hivi katika mahakama za kibiashara za kimataifa dhidi ya mikataba iliyovunjwa na Serikali ya Tanzania. Tukumbuke mikataba ya madini miaka ya ’90 viongozi wa dini na asasi za kiraia walipinga uwekezaji wa namna hii, na Serikali ikatumia mamlaka zake kuridhia mikataba hii na sasa hivi tunashuhudia ikivunjwa na nchi kulipa fidia kubwa.  Tunasisitiza kwamba SAUTI YA WATU NI SAUTI YA MUNGU, hivyo basi kuwasikiliza wananchi na kufanya maamuzi kadiri wanavyotaka kutailetea serikali heshima kubwa ya kuwa sikivu kwa watu. Kinyume cha haya, Mwenyezi Mungu anatuonya kupitia Nabii Yeremia anaposema: “Kama kapu lililojaa ndege walionaswa, ndivyo nyumba zao zilivyojaa mali za udanganyifu. Ndiyo maana wamekuwa watu wakubwa na matajiri, wamenenepa na kunawiri. Katika kutenda maovu hawana kikomo hawahukumu yatima kwa haki, wapate kufanikiwa, wala hawatetei haki za maskini” (Yeremia 5:27-28). Hivyo tukiwajibika kimaadili, tunaona ni jukumu la serikali kusikiliza wananchi wanaotaka mkataba huu ufutwe. Kwa kuwa tumeonesha kuwa Tanzania tumeshawekeza na kuendeleza bandari, reli na bandari za nchi kavu; ni wajibu miradi hii tuiendeshe Watanzania wenyewe huku tukikaribisha ubia tunaoudhibiti wenyewe. Hiki ndicho wananchi wanachokililia kusudi tujenge uwezo wetu wenyewe. Kwa vile tumegundua mapungufu yetu ya uendeshaji wa bandari, tunaweza kujizatiti kurekebisha mapungufu hayo wakati njia za kiuchumi zikibaki mikononi mwetu. Kwa sababu hizo na maelezo yote ya hapo juu, sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hatuungi mkono Mkataba huu. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Oktoba 2023
Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Oktoba 2023

SHUKRANI KWA UKARIMU WA MWAKA 2022 NA MWALIKO KWA UKARIMU ZAIDI: Ni ukweli usiopingika kuwa Imani yetu ya Kikristo ina msingi wake katika UKARIMU, hasa kwa kumtazama Kristo ambaye ni kielelezo chetu kama Maandiko Matakatifu yanashuhudia: “…kama vile, Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Mt. 20:28). Kwa kifo chake msalabani, Kristo anabaki kwetu kuwa ndiye kielelezo cha ukarimu huu, tena ukarimu wa kutoa uhai wake kwa ajili ya wokovu wetu. Ni katika msingi huu, Kanisa kwa nyakati zote linahimiza juu ya umuhimu wa UKARIMU kwa Mungu mwenyewe na kadhalika na kwa jirani. Ukarimu huu huwa na sura mbalimbali, mojawapo ikiwa ni Ukarimu wa Kimisionari (Missionary Cooperation) wa kuwa tayari kufanya majitoleo kwa ajili ya kuifikisha Injili katika maeneo mengine hasa yaliyo magumu. Ili kufikia lengo hili, Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ndio yamepewa dhamana ya kuratibu ukarimu wa aina hii kila mwaka kokote ulimwenguni. Kwa mwaka 2022 Kanisa la Tanzania lilifanikiwa kutoa ukarimu mkubwa kwa Mfuko wa Pamoja wa Baba Mtakatifu (Universal Solidarity Fund). Mwaka 2021 tulitoa ukarimu wa TZS 610,641,745 na mwaka 2022 tulitoa ukarimu wa TZS 651,612,482. Mchango wetu umeongezeka mwaka 2022 kwa TZS 40,970,737 ambalo ni ongezeko la 6.21%. Hivyo, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kwa niaba yangu, natoa shukrani za dhati kabisa kwa ukarimu wenu huo mkubwa. Aidha, ninatoa shukrani za dhati kwa majimbo, watawa wa kike na kiume, mapadre, Seminari zetu Kuu na Ndogo, taasisi za Elimu ya Juu, shule, maparoko na Marafiki wa Baba Mtakatifu (watu binafsi na jumuiya) kwa sala na majitoleo yenu. Mwenyezi Mungu awabariki, awazidishie mema yake bila kipimo na kuwastawisha katika Upendo wa kweli “…maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2Kor 9:7-8). Mwisho, ninazidi kuwaalika muendelee kujibidisha katika kutoa ukarimu zaidi kwa ajili ya ufanisi wa kazi za kimisionari katika Kanisa. Tuendelee kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Mwezi wa Kumi ambao ni Mwezi wa Umisionari. Kwa namna ya pekee tujiandae vema kwa ajili ya maadhimisho ya Dominika ya Misioni ambayo kwa mwaka huu itaadhimishwa tarehe 22 Oktoba, 2023. Hali tukitambua kuwa SALA ndio moyo wa umisionari, tujiandae vema kwa ajili ya SALA YA NOVENA (siku tisa kabla ya Dominika hii) kadhalika na MAJITOLEO yetu kwa siku hiyo kwa ajili ya kazi ya Uinjilishaji inayoendelea.

Asanteni Sana na Mungu awabariki.

Maaskofu Katoliki Tanzania
20 October 2023, 11:03