Tafuta

2023.10.03 UISG Advocacy Forum: watawa  wanaita mitandao yao ya kimataifa kufanya mazungumzo 23-24 Oktoba 2023 jijini Roma. 2023.10.03 UISG Advocacy Forum: watawa wanaita mitandao yao ya kimataifa kufanya mazungumzo 23-24 Oktoba 2023 jijini Roma. 

UISG,watawa ulimwenguni na mitandao ya kimataifa katika mazungumzo ya changamoto za maendeleo

Jukwaa la kwanza la Utetezi la Umoja wa Kimataifa wa Mama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa(UISG)litafanyika kuanzia Oktoba 23 na 24,jijini Roma kwa ajili ya majadiliano na wawakilishi wa serikali,mashirika ya kimataifa,taasisi za Vatican,mashirika ya kiraia na wataalam kutoka ulimwengu wa kitaaluma na waandishi wa habari.

Angella Rwezaula, - Vatican.

Kuainisha mpango wa utekelezaji wa ushirikiano unaolenga kuunda mabadiliko ya kimfumo na kukabiliana na changamoto kuu zinazokabili jamii na sayari. Kuchochea utetezi na mazungumzo yenye mwelekeo wa vitendo ili kukuza na kutekeleza mitindo endelevu ya maisha, mazoea ya kijamii na kiuchumi ambayo yanaheshimu mahitaji ya walio hatarini zaidi, na jamii zinazoongozwa na hali ya kiroho, mshikamano na kutobagua yeyote ndiyo malengo makuu katika  Jukwaa la Kwanza la Utetezi lililoandaliwa na Umoja wa Kimataifa wa Mama  Wakuu wa Mashirikia ya kitawa (UISG) ambao unaoleta pamoja wanachama 1,903 wenye ofisi zao  katika nchi 97, wanaowakilisha zaidi ya watawa elfu 600 duniani kote.

Siku mbili za mikutano na majadiliano

Tukio hilo, lililoandaliwa kwa ushirikiano na Mfuko wa Mshikamano wa Kimataifa, litafanyika  kwa siku mbili  mnamo tarehe 23 na 24 Oktoba 2023 katika Ukumbi Mkuu wa Jumuiya ya Yesu jijini Roma, njia ya  (Borgo Santo Spirito, 4).  Kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wanawake Watawa: Uongozi na Maendeleo,” UISG italeta pamoja mtandao wake wa kimataifa kwa siku hizo  mbili za mikutano na majadiliano, ili kutambua maeneo ya kipaumbele ya utetezi katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa ambayo inaweza kukuza mabadiliko ya kimfumo, kuunganisha ujuzi wa mila na tamaduni  na kiroho kwa jili ya mahitaji mapya yanayotokana na mabadiliko ya haraka ya jamii zetu. Mkutano huo utazingatia baadhi ya changamoto za dharura zaidi za wakati wetu, ambazo kwa hakika huathiri maendeleo ya usawa ya jamii zetu na sayari yetu; kati ya hayo, mabadiliko ya tabianchi na upotevu wa viumbe hai, umaskini, ukosefu wa ajira na usawa wa kijamii, uhamiaji wa kulazimishwa na biashara haramu ya binadamu, migogoro ya afya na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mchango kwa Sinodi

Kama mchango katika mchakato wa sinodi ya Kanisa, UISG na mtandao wake wa kimataifa utakaribisha wawakilishi wa serikali, mashirika ya kimataifa, taasisi za Vatican, mashirika ya kiraia na wataalam kutoka ulimwengu wa kitaaluma na waandishi wa habari jijini  Roma. Kulingana na uzoefu, shuhuda zilizokusanywa na changamoto zinazokabiliwa sehemu mbalimbali za dunia, Watawa hawa na washirika wao watachunguza ni wapi rasilimali zaidi zinapaswa kutengwa na jinsi ya kukuza utetezi na hatua za kupanga programu, ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya ustawi wa watu na sayari.

Sr Murray: yuko mstari wa mbele kwa walio hatarini

"Watawa wako  mstari wa mbele dhidi ya baadhi ya changamoto za haraka zaidi za maendeleo ya kimataifa,” alisema Sista Patricia Murray, katibu wa Umoja huo wa Watawa Kimataifa (UISG). "Kupitia uzoefu wao wa karne nyingi wa kusaidia waliotengwa na walio hatarini zaidi, wakiambatana na maumivu yao na wakishiriki mapambano yao ya uwezeshaji na haki, watawa wameunganisha kielelezo cha kipekee cha ushirikishwaji wa jamii, na kufanya mitandao yao kuwa kipengele muhimu cha fumbo la maendeleo ya kimataifa.” UISG  kwa hiyo inaamini kwamba mitandao kama hii inahitaji kuunganishwa na watoa maamuzi wa kimataifa ili kuelekeza uwezo wao kamili na kuendesha mabadiliko endelevu na ya kimfumo kweli: haya ndiyo maono yanayoongoza kazi yetu ya utetezi na ni msingi wa Jukwaa letu la kwanza la Utetezi.” Alikazia kusema Sr Patricia

Mchakato wa miaka mitatu

Jukwaa la Utetezi linawakilisha kilele cha mchakato ulioanza zaidi ya miaka mitatu iliyopita, mnamo Julai 2020, wakati UISG, kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Mshikamano, walipounda mpango wa Masista Watetezi Kimataifa, unaolenga kuunda mtandao wa watawa wanaojishughulisha na kijumuiya na kijamii kuhusu utetezi wa mazingira, kuhamasisha mawasiliano na ushirikiano na washirika, na kuunda nafasi za kutafakari kwa baadhi ya masuala muhimu ya maendeleo ya kimataifa. Kwa kuzingatia hilo, mnamo 2023, UISG tayari imeandaa hafla mbili: mkutano wa kwanza mnamo mwezi  Aprili ulihusu masuala ya mazingira ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabiachi na upotezaji wa viumbe hai, Mkutano wa Pili ulikuwa  mnamo Julai 2023 ambao, ulizingatia hali ya uhamiaji, kati ya mahitaji, changamoto mpya na uwezo. Kwa njia hiyo "Watawa wako tayari kuchangia mabadiliko ya kimfumo kwa uzoefu wao katika majukumu mbali mbali", alikumbuka hayo Sista Murray. "Wao ni walimu, wauguzi, wahandisi, wa kwanza kuingilia kati hali za dharura, lakini pia ni watafiti, wasomi; watendaji na viongozi wa ngazi zote. Kwa kuunganisha watu wa asili na wenyenyeji na ulimwengu, kupitia mitandao inayoongozwa na watawa, UISG inalenga kuwezesha ulinganisho wa uzoefu tofauti na kubadilishana tafakari, ili kuunda mazungumzo juu ya maendeleo ya kimataifa karibu na mahitaji ya jumuiya mahalia ulimwenguni kote.” alihitimisha.

Kwa maelezo zaidi kuhusu Umoja wa Mama wakuu wa mashirika (UISG): https://www.uisg.org/en/

Na ili kujua zaidi kuhusu Masista Watetezi Kimataifa: https://advocacy.uisg.org/

UISG kufanya Jukwaa la Kimataifa 23-24 Oktoba 2023, Roma
20 October 2023, 10:46